Mwalimu mbaroni akidaiwa kubaka wanafunzi wake tisa
MWALIMU wa Shule ya Msingi Itiryo, Samweli Bisendo (29), amekamatwa na jeshi la polisi akituhumiwa kubaka wanafunzi tisa wa shule yake iliyopo wilayani Tarime.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi wa Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe, alisema kuwa mwalimu huyo anadaiwa kutenda unyama huo kwa nyakati tofauti hadi alipobainika.
"Jeshi la polisi limefanikiwa kumkamata mwalimu wa shule ya msingi Itiryo, Samweli Mariba Bisendo (29) kwa tuhuma ya kubaka watoto wapatao tisa ambao ni wanafunzi wa shule ya msingi Itiryo,” alisema Kamanda Mwaibambe na kuongeza kuwa matukio hayo yalifanyika kati ya Novemba 30 na Desemba 6,mwaka huu.
“Alikamatwa wakati akiwa anajiandaa kutorokea nchi jirani ya Kenya," alisema Mwaibambe.
Aidha, Mwaibambe alipongeza ushirikiano kutoka kwa wananchi ambao ndiyo waliowezesha jitihada za polisi kuzaa matunda katika kumkamata mwalimu huyo.
"Pia mwalimu huyo, bila aibu, aliwafanyia matukio ya unyanyasaji wa kijinsia wanafunzi wengine watatu wa shule ya msingi Itiryo," alisema Mwaibambe.
Kamanda huyo alitoa wito kwa jamii kuendelea kutoa taarifa kwa vyombo vya dola pale wanapobaini kuwapo kwa uvunjaji wa hseria za nchi ili watuhumiwa wakamatwe na sheria kutwaa mkondo wake.
No comments:
Post a Comment