Wednesday, 20 December 2017

Vyama Vya Upinzani Vyamkosoa Mzee Makamba



Baadhi ya vyama vya upinzani vimekosoa kauli iliyotolewa juzi na aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba vikisema imelenga kudhoofisha upinzani nchini.
Juzi, akihutubia Mkutano wa Mkuu wa CCM, Makamba alisema Rais mstaafu Jakaya Kikwete alikuwa ‘anabatiza’ kwa maji, lakini Rais John Magufuli anafanya hivyo kwa moto na mfano mzuri ni uchaguzi wa marudio wa kata 43 ambao CCM ilizoa viti 42.
“Huu si ubatizo wa moto? Kazi tunayoifanya leo ni kuchagua kocha ambaye ni wewe (Rais Magufuli), kocha msaidizi Mangula (Philip) na Dk Shein (Ali Mohamed). Kama haitoshi unatakiwa uchague dawati la ufundi Kamati Kuu, sasa wenzangu wajue nimlisikia rafiki mmoja alikwenda kwa jimbo la Mnyika (John) na kusema 2020 njia nyeupe,” alisema mwanasiasa huyo.
“Njia nyeupe kwa utaratibu huu, kwa matokeo haya na ubatizo huu wa moto 2020 mshindi ni CCM we’ lala. Naomba mniruhusu niwaambie kina Mrema (Lyatonga), ubatizo ni uleule na leo sitaki kutabiri.Natabiri 2020 mheshimiwa Lowassa (Edward), Mbowe (Freeman) na Mapesa (John Cheyo ), John Shibuda wajue njia si nyepesi.”
Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema hakutarajia kama Makamba angetoa kauli hiyo kutokana na alichodai kuwa ni kuminywa kwa demokrasia nchini.
Alisema kinachofanyika sasa dhidi ya wapinzani ni sawa na refa anayechezesha mpira wa miguu kuwapa kadi nyekundu wachezaji wote wa timu husika, halafu timu nyingine inaendelea kucheza.
Naibu Katibu wa CUF (Bara), Magdalena Sakaya alisema kauli hiyo haileti picha nzuri kwa siasa.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema Makamba yupo sahihi na upinzani unabidi kufanya kazi ya ziada kama wanataka kushinda 2020.
“Tulikosea na tulichelewa kuunda upinzani, mwaka 1995 tulikuwa na nafasi nzuri sana ya kuungana kwa sababu hakukuwa na rais kama Magufuli, lakini sasa hivi yupo na sisi wapinzani tusipobadilika na siasa zetu za kususa watatuchapa kweli 2020,” alisema Mrema.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen-Kijo Bisimba alisema Makamba alisema ukweli kutokana na hali na mazingira ya siasa nchini.

Wanaochakachua Pesa Za Tasaf waonywa



KAIMU Katibu Tawala Mkoa wa Tabora, Natalis Linuma, ameiomba serikali kusaidia vijiji ambavyo havijaingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini katika mkoa na vijiji.
Aliyasema hayo wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tasaf III kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Mkuchika.
Linuma alisema vijiji vingi ambavyo havijaingizwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini, watu wake wana hali duni na baadhi wameachwa na watoto yatima.
Aidha, alisema kutokana na kaya hizo kutoingizwa katika mpango huo, kumesababisha malalamiko.Linuma alimwambia Waziri Mkuchika kuwa kaya 953ziliondolewa wakati wa uhakiki wa kubaini kaya zisizokuwa nasifa.
Alisema, Mkoa wa Tabora una jumla ya wilaya saba na tarafa 19, kata 174 na vijiji 696, mitaa148 ambayo mpango huo unatekeleza uhawilishaji katika kaya zenye sifa.
Lengo lilikuwa ni utambuzi na uandikishwaji wa kaya 52,558 na kaya 47,805 ziliandikishwa, kuanzia mwezi Agosti 2017.
Aidha, jumla ya Sh. 20,038,121.000 zilihawilishwa kwa walengwa 39,293.
Katika halmashauri zote za mkoa wa Tabora, mpango wa kunusuru kaya maskini umesaidia kuwapatia elimu watoto wenye wazazi wasio na uwezo.
Waziri Mkuchika alisema amepokea taarifa hiyo, lakini alipata fununu kuwa kuna baadhi ya viongozi wasio waaminifu.
Mkuchika alisema kuwa taarifa alizozipata ni baadhi ya viongozi kuomba rushwa na kuwaonya wakiendelea na tabia hiyo watakiona cha mtemakuni.

Hamisa Mobeto Anasa kwenye mtego Wa Zari



Mwanamitindo Hamisa Mobeto.
Mwanamitindo Hamisa Mobeto anadaiwa kunasa mtegoni baada ya ‘kuuvaa mkenge’ ulioratibiwa na hasimu wake wa siku za hivi karibuni, Zarinah Hassan ‘Zari’.
Kwa mujibu wa chanzo kilicho karibu na Zari, inadaiwa kuwa mjasiriamali huyo alimtumia mtu aitwaye William Bugeme ambaye pia ana ukaribu naye wa damu, ili aweze kumchukua mwanamitindo huyo, ambaye amezaa na baba wa watoto wake wawili.
Inadaiwa lengo la Zari ni kuona wawili hao wakiwa karibu, basi ni dhahiri kuwa ukaribu kati ya Hamisa na baba watoto wake utaisha, kwani uhusiano wa kimapenzi na William hauwezi kukubalika.
“Mnajua kuwa huyo Hamisa amenasa kwa Bugeme lakini hajui kuwa huo ni mpango wa Zari ili amtoe kwa baba mtoto wake, asipoangalia atatumika tu kisha atabwagwa kwani jamaa yupo kimaslahi zaidi kwa ajili ya kuokoa penzi la dada yake,” alisema Sosi huyo.
Kwa mujibu wa sosi huyo, picha za wawili hao wakiwa katika pozi tofauti zilinaswa hivi karibuni zikiwa zimerushwa mtandaoni.
Zarinah Hassan ‘Zari’
Sosi huyo alikwenda mbali zaidi na kuvujisha siri ya Zari kuwa ndiye anayemtuma ndugu yake huyo ili akifanikisha kuwa naye kimapenzi itakuwa rahisi kuachana na baba wa watoto wake.
Hata hivyo sosi huyo alidai fungu kubwa na zuri limeandaliwa kuhakikisha Hamisa hakwepi mtego huo.
“Mwanamke ni mjanja sana sana haongei ni pesa ndio inaongea, Bugeme toka zamani anafahamiana na Hamisa sasa ameamua kumtumia huyo huyo ili kuumaliza mchezo wake kabisa, unadhani mzazi mwenzake akiona ameingia kwenye penzi na Bugeme ataendelea naye, amecheza kwelikweli,” kilitiririka chanzo.
Risasi Jumatano lilimtafuta hewani Hamisa ili azungumzie sakata hilo kama ameshalifahamu au anajipanga vipi, lakini pia kuzungumzia picha zake zinazomuonesha akiwa na kaka huyo, lakini alipopokea simu yake alisikiliza madai yote kisha akakata simu.

Video | Rayvanny ft Maphorisa x Dj Buckz – Makulusa | Mp4 Download

Video | Rayvanny ft Maphorisa x Dj Buckz – Makulusa | Mp4 Download



DOWNLOAD

Audio | Rayvanny ft Maphorisa x Dj Buckz – Makulusa | Mp3 Download


Audio | Rayvanny ft Maphorisa x Dj Buckz – Makulusa | Mp3 Download






Dalili Tano za Tezi Dume



Ugonjwa wa tezi tume imeelezwa ya kwamba ni miongoni mwa magonjwa ambayo yanasumbua jamii yetu kwa kiwango kikubwa sana na hata kupelekea kusababisha vifo.
Hata hivyo tafiti mbalimbali zinazidi kuonesha ya kwamba wanaume ambao wanatumia pombe kali kwa kiwango kikubwa wapo hatarini kupata ugonjwa huo. Licha ya wanywaji wa pombe kali lakini inasadikika ya kwamba wanaume ambao wanafanya kazi za viwandani, husasani viwanda vya rangi au wanaofanya kazi ya kupaka rangi wapo hatarini kupata ugonjwa huo.
Lakini pia wanaume ambao wapo hatarini kupata ugonjwa huo ni pamoja na wanaume wenye historia ya tatizo hili wenye familia zao, yaani wale ambao mmoja wa ndugu zake (kaka au mdogo wa kiume) au baba kama amewahi ugua ugonjwa huu.
Lakini pia watalamu mbalimbali wa masuala ya afya, wanazidi kueleza ya kwamba wanaume wenye umri wa kati ya miaka 40-70 wapo hatarini kupata ugonjwa huu wa tezi dumi.
Lakini licha ya kuendelea kusambaa kwa kasi kwa ugonjwa huu watalamu wa afya wanaeleza ya kwamba endapo ugonjwa huu wa tezi tume utaweza kutambulika mapema unaweza kutibika.
Dalili za ugonjwa wa saratani dume.
Katika hatua zake za awali, dalili za saratani ya tezi dum hazitofautiani na zile za kuvimba kwa tezi dume (BPH). Dalili hizo ni pamoja na
1. Kukojoa mkojo uliochnanganyika na damu.
2. Kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku.
3. Kukojoa mkojo wenye mtiririko mchafu.
4. Kutirirka kwa mkojo baada ya kumaliza kukojoa.
5. Kupata maamuvu wakati unapoanza kukojoa.

Faida zingine za Maji Mwilini



Moja kati ya kauli mbiu ambayo ipo katika matumizi ya maji wanasema ya kwamba, maji ni uhai. Huo ni ukweli usiopingika juu ya kauli hiyo ijapokua watu wengi huwa hawatumii maji hayo.
Hivyo kama wewe ni miongoni mwa watu hao Makala haya yatakufaa kwani utakwenda kujua ukweli kuhusu faida za maji mwilini.
Faida za maji mwilini ni kama ifuatavyo;
1. Unywaji wa maji husaidia kuifanya ngozi yako kuwa nyororo na nadhifu.
2. Maji husaidia kwa kiwango kikubwa katika mfumo wa kuchanganya chakula katika mwili wa mwanadamu. Lakini pia maji husaidia kupunguza uwezekano wa kuapata saratani ya colonikwa asilimia 45.
3. Maji husaidia kupunguza calories mwilini, yaani badala ya kunywa vimininika vingine kama vile soda, juisi na bia ambavyo vina calories, hivyo unashauriwa utumie maji kwani yenyewe hayana calories. Lakini pia unashauriwa ya kwamba kila wakati uendelee kutumia maji kwani yenyewe hayana mafuta, sukari ambavyo husababisha athari mbaya katika mwili wa binadamu.
4. Kwa wale ambao hushambuliwa na maumivu ya kichwa, tunaambiwa ya kwamba maji husaidia kutibu maamivu ya kichwa, kwani inasdikia ya kwamba upungufu wa maji mwilini husababisha kichwa kuuma, hivyo kila wakati ni vyema ukatumia maji ili ujitibu.
5. Utumiaji wa maji kwa kiwango kikubwa kila wakati humsaidia mtu kuweza kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya moyo, hivyo unashauriwa kwa siku tunywe zaidi walau bilau nane kwa siku

Tuesday, 19 December 2017

Mwenyekiti Sau Kuzikwa Disember 22



Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Dk Paul Kyara aliyefariki dunia jana anatarajiwa kuzikwa Desemba 22,2017 kijijini Legho, Kilema mkoani Kilimanjaro.
Dk Kyara alifariki dunia jana asubuhi Jumatatu Desemba 18,2017 akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam.
Katibu wa chama hicho, Johnson Mwangosi amesema Desemba 21,2017 saa tano asubuhi wanatarajia kuwa na ibada na kuaga mwili wa marehemu nyumbani kwake Madale.
Mwangosi amesema baada ya shughuli hiyo mwili wa Kyara utasafirishwa kwenda kijijini Legho.
Majaliwa, mtoto wa marehemu Kyara amesema baba yake alikuwa akisumbuliwa na figo tangu mwaka 2012.
Amesema Ijumaa Desemba 15,2017 alipata tatizo la shinikizo la damu na sukari ilipanda.
Majaliwa amesema alipelekwa hospitali alikopatiwa matibabu na aliruhusiwa kurejea nyumbani.
Amesema Jumamosi Desemba 16,2017 alizidiwa na saa tatu usiku walimpeleka katika Hospitali ya Regency kwa matibabu.
Amesema madaktari walijitahidi kuokoa maisha yake lakini shinikizo la damu na kisukari hakikushuka hivyo kusababisha kifo chake.
“Nitamkumbuka baba, wakati amelazwa neno alilokuwa akisisitiza ni upendo na umoja," amesema Majaliwa.

Airtel yaja na ofa kabambe msimu huu Wa sikukuu



Kampuni ya Simu za Mkononi nchini Airtel imezidi kuonesha ukomavu wake katika kuwaletea wateja wake huduma bomba baada ya sasa kuja na kifurushi cha Smatika ambacho kinaanzia Sh 2,00 hadi Laki moja.
Vifurushi hivyo vimekuja mahususi kwa lengo la kukata kiu ya bando la intaneti kwa watumiaji wa Airtel huku wakiboresha vifurushi hivyo katika msimu huu wa Sikukuu ambapo kifurushi cha MB 50 kwa Sh 250 sasa kitakujia kwa Sh 2,00 ili kwenda sawa na vocha za 2,00 zilizopo lakini kikikupatia bando la MB 40 kwa siku.
Airtel pia imekuja na bando jipya kabisa la Sh 2,000 ambalo litakua na kifurushi chenye ujazo wa GB 3 kwa siku tatu kulinganisha na awali ambapo Sh 2,000 mteja alikuwa akipata kifurushi cha GB 1.3 kwa siku.
Akizungumzia lawama ambazo zimekuwa zikitolewa na wateja wa mtandao huo kuhusu kupunguzwa kwa vifurushi vya mtandao huo, Meneja Masoko Airtel, Aneth Muga alisema wateja wengi wamekuwa wakilalamika kuhusu kuondolewa kwa vifurushi vya UNI lakini wamesahau kuwa vifurushi hivyo vilikuwa maalumu kwa ajili ya wanafunzi wa vyuo.
“ Ndugu zangu wanahabari Airtel imeendelea kukata kiu ya watumiaji wa mtandao wetu, watu wengi wanalalamika kuwa tumepunguza vifurushi vyetu bila kuangalia kwa undani, mathalani kifurushi cha 250 kilikuwa kikimpatia mteja MB 50 lakini sasa tunatoa MB 40 kwa Sh 200.
“ Ukiangalia hapo huoni utofauti wowote lakini pia kuwa na kifurushi cha Sh 200 kunampa unafuu mteja ambaye ananunua vocha za Sh 200,” alisema Aneth.

Rais Magufuli amwaga Neema Ruvuma



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kupitia wizara ya Nishati, ametoa kiasi cha shilingi bilioni 210 kwaajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa Umeme unaojengwa mkoani Ruvuma.
Akiongea katika ziara yake ya siku tatu mkoani Ruvuma Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amesema Rais Magufuli ametoa fedha hizo kwa kushirikiana na wahisani wengine.
“Mheshimiwa Rais ndio ametoa fedha hizi bilioni 210 kwa kushirikiana na wahisani ambapo bilioni 104 ni kwaajili ya kusambaza umeme katika wilaya zote za mikoa ya Ruvuma na Songea”, amesema Waziri Kalemani.
Mradi huo wa umeme unatarajiwa kuwafikia wananchi zaidi ya 32,000 katika vijiji 120 vya mikoa hiyo. Waziri ameongeza kuwa mradi huo utawawezesha wananchi kuingiza fedha nyingi kutokana na fursa zitakazojitokeza baada ya kukamilika.
Kalemani amewataka Wakandarasi kumaliza kwa wakati mradi huo kwani tayari wameshapewa fedha zao bila kucheleweshewa. Mradi unatarajiwa kukamilika mwezi Agosti 2018.

Mtulia Kurudi tena Kinondoni



Aliyekuwa Mbunge Kinondoni (CUF), Maulid Mtulia ambaye amehamia CCM ametangaza nia ya kugombea tena ubunge katika jimbo hilo kwa tiketi ya chama hicho tawala.
Desemba 2 Mtulia amejiuzulu nafasi ya ubunge, huku akisema amefikia uamuzi huo bila kushawishiwa mtu yeyote na amebaini Serikali ya CCM inafanya kazi kubwa ya kutekeleza Ilani na imefanya vizuri katika mambo mengi ambayo upinzani iliahidi kuyatekeleza.
Baada ya hatua hiyo, chama cha CUF upande wa Profesa Ibrahim Lipumba ametangaza kuwaomba radhi wapiga kura wa Kinondoni kwa Mtulia kujiuzulu uanachama kisha ubunge.
Lakini leo Jumanne Desemba 19, 2017 kupitia andiko lake alilolituma kwa vyombo vya habari, Mtulia amesema atachukua fomu ya kuomba ridhaa ya kuteuliwa ndani ya CCM ili agombee tena nafasi hiyo.
“Chama changu kikiridhia nitakwenda mbele ya Wanakinondoni kuomba ridhaa ya kuwatumikia katika nafasi ya ubunge kupitia CCM. Pia nawapa pole sana kwa maumivu mliyoyapata kutokana na uamuzi wangu wa kujiuzulu ubunge wa Kinondoni,” amesema Mtulia.
Hata hivyo, Mtulia amewahakikishia wakazi wa Kinondoni kuwa bado anawapenda na yupo tayari kutumikia tena kwa lengo la kuleta maendeleo ya jimbo hilo ambalo awali lilikuwa likishirikiliwa na CCM kwa kipindi cha muda mrefu.

Mambo ya kukumbukwa aliyoyafanya Rais Magufuli Mwaka 2017



RAIS Dk. John Magufuli amefanya mambo mengi ndani ya mwaka huu, lakini haya 10 yatazidi kukumbukwa na Watanzania.
BABU SEYA, PAPII KOCHA
Tukio la kuachiwa kwa wanamuziki Nguza Mbangu Viking (Babu Seya) na Johnson Nguza (Papii Kocha) lilitangazwa na Rais Magufuli wakati wa maadhimisho ya uhuru, Desemba 9, mwaka huu.
Rais alipotangaza msamaha kwa wanamuziki hao maarufu kuliamsha nderemo na vifijo kutoka kwa mashabiki wa muziki wa dansi nchini.
Familia hiyo ilianza kutumikia kifungo cha maisha jela tangu Juni mwaka 2004 kwa kosa la kuwalati wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, jijini Dar es Salaam.
RELI YA KISASA
Tukio la ujenzi wa reli ya kisasa lilikuwa la kipekee kwa nchi yetu kwani Rais Magufuli alizindua rasmi ujenzi wake akasema itasafiri kwa mwendo wa kilomita 160 kwa saa.
Rais alisema Tanzania ndiyo nchi pekee barani Afrika ambayo imeweza kujenga mradi wa reli kama hiyo kwa fedha zake za ndani.
Ujenzi wake umeanzia Dar es Salaam kwenda Morogoro na utagharimu dola za Marekani bilioni 1.29 na shughuli za ujenzi wa reli hiyo zinaendelea.
TANESCO, WIZARA ZIVUNJWE
Mwaka huu pia, Rais Magufuli alitembelea mradi wa ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo na kuagiza majengo ya makao makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Wizara ya Maji yavunjwe.
Alitoa maagizo hayo kutokana na majengo hayo kujengwa ndani ya hifadhi ya barabara ya Morogoro.
Majengo ya wizara tayari yamevunjwa na Tanesco inaendelea na mchakato wa ubomoaji.
MABWENI YA UDSM
Jambo jingine ambalo Rais Magufuli atakumbukwa nalo kwa mwaka huu, ni uzinduzi wa majengo mapya ya mabweni ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM).
Mabweni hayo yana uwezo wa kuchukua wanafunzi 3,840 na yalijengwa chini ya mwaka mmoja na kugharimu sh. bilioni 10.
Hivi karibuni majengo hayo yaliripotiwa kuwa na nyufa, lakini Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) uliwatoa hofu wanafunzi kuwa hayana tatizo.
KUVUNJA BARAZA LA MAWAZIRI
Oktoba mwaka huu, Rais Magufuli alivunja Baraza la Mawaziri na kufanya mabadiliko kadhaa.
Katika mabadiliko hayo, aliongeza wizara na mawaziri kutoka 19 hadi 21. Nafasi za manaibu mawaziri ziliongezwa kutoka 16 hadi 21.
Lengo la mabadiliko hayo ilielezwa ni kuleta ufanisi wa kiutendaji serikalini.
DAWA ZA KULEVYA
Alipoingia madarakani alitangaza kiama cha wauzaji na watumiaji wa dawa za kulevya na vigogo kadhaa walikamatwa kujihusisha nazo.
Februari mwaka huu, rais alimteua Rogers Sianga kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA).
Baada ya uteuzi huo, Sianga alimhakikishia rais kuwa atapambana na dawa hizo hadi ushindi upatikane.
Agosti, mwaka huu, Rais Magufuli alimteua pia Luteni Kanali Frederick Felix Milanzi kuwa Kamishna wa Operesheni wa mamlaka hiyo ili kukoleza vizuri moto wa kukabiliana na dawa hizo nchini.
BANDARINI
Mwaka huu rais alifanya pia ziara ya kushtukiza bandarini na kukuta tena madudu mengine, ikiwa ni mwendelezo wa ziara zake bandarini hapo.
Safari hii alikuta magari 50 yaliyoagizwa nchini na watu wasiojulikana kwa jina la Ofisi ya Rais.
Rais Magufuli alisema magari hayo siri yake ni kubwa kwani yamekaa bandarini tangu Juni mwaka 2015 na yaliletwa pamoja na magari ya serikali.
Akahoji,“inakuwaje rais nipate taarifa za magari kufichwa lakini waziri, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) msijue?”
MADENI YA WALIMU
Desemba mwaka huu, rais alirejesha matumani ya walimu ambao kwa muda mrefu wanasumbukia madai yao bila ufumbuzi.
Akizungumza na mamia ya wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Desemba 14, mwaka huu, mjini Dodoma, aliahidi kulipa takriban sh. bilioni 25 za madeni ya walimu.
“Ninawaahidi walimu wenzangu, mara baada ya uhakiki kuisha wale walimu ambao wanadai malipo halali watalipwa,”alisema.
Alisema kabla hajawa rais alikuwa mwalimu hivyo anazifahamu vizuri shida za walimu hivyo walimu wajisikie wana mwakilishi mzuri.
MADINI
Rais Magufuli aliunda tume mbili kuchunguza madai ya wizi na ufisadi unaodaiwa kufanywa na wawekezaji tangu walipoanza uzalishaji wa dhahabu nchini.
Ripoti ya kamati ya kwanza ilipotoka ikiongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma ilibaini kasoro za usimamiaji, hivyo rais alimfuta kazi Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na kuvunja Bodi ya Uwakala wa Ukaguzi wa Madini Tanzania (TMAA).
Ripoti ya kamati ya pili iliongozwa na Profesa Nehemia Ossoro ilibaini usafirishaji wa mchanga umepotezea taifa fedha nyingi.
Profesa Ossoro alisema fedha zilizopotea tangu mwaka 1998 ni kati ya sh. trilioni 132 hadi trilioni 380.
BOMBA LA MAFUTA
Mwaka huu ulikuwa pia na tukio la aina yake. Ni uzinduzi wa ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima Uganda hadi Bandari ya Tanga.
Bomba litapita mikoa nane, wilaya 24 na vijiji 124 na wakandarasi watatu kutoka nje wanasimamia mradi huo na kutoa fursa mbalimbali za ajira kwa wananchi wa pande hizo mbili.

Wananchi washerehekea kuuawa kwa Fisi 15



MAMIA ya wakazi wa Kijiji cha Buzanaki kata ya Nyamarimbe katika mkoa wa Geita, wamesherehekea kuuawa kwa fisi 15 hadi jana, katika matukio tofauti wiki moja baada ya mtoto wa miaka sita kuliwa na wanyama hao na wengine watatu kujeruhiwa.
Kwa mujibu wa wazazi wa mtoto huyo aliyejulikana kwa jina la Yusufu, Martha Musa na Simon Balele walidai marehemu alikamatwa na fisi saa moja jioni Desemba akiwa na watoto wengine wanne ambao baada ya tukio walikimbia na kutoa taarifa.
Desemba 2 mabaki ya mwili wa mtoto Yusufu yalipatikana kijijini hapo yakiwa yamebakia utumbo na mfupa mmoja wa paja ambavyo ndivyo vilivyozikwa kwa heshima ya familia.
Kutokana na tukio hilo, wanakijiji chini ya Mwenyekiti wa Kijiji Robert Maholosha, Ofisa Mtendaji, Rose Paul walitangaza msako wa fisi ulioongozwa na kuratibiwa na Musese Kabulizina ambaye ni ofisa wanyamapori wilaya ya Geita.
Hadi jana fisi 15 walikuwa wameuawa katika matukio tofauti katika kijiji cha Buzanaki fisi 6 na katika kijiji cha Idoselo fisi 9 wameuawa ambako nako wanakijiji watatu walijeruhiwa.
Kwa mujibu wa ofisi ya wanyamapori wilaya ya Geita mwaka 2010 hadi 2014 watu saba waliuawa na fisi huku mwaka 2017 ameuawa mtoto mmoja na wengine watatu kujeruhiwa.
Hata hivyo, tukio la Mei 7 mwaka 2012 lililotokea katika kijiji cha Luezera ndilo lililotisha zaidi kwani baada ya fisi kumkamata mtoto mwenye umri wa miaka 8 saa moja jioni wakati akitoka dukani kununua mafuta ya taa na kutoweka naye kuliibuka sintofahamu kubwa.
Katika tukio hilo, wanakijiji kadhaa walihamasishanana kuwaua watu watatu kwa marungu, mapanga na fimbo wakiwatuhumukuwafuga fisi hao kwa ajili ya ushirikina.
Katika tukio hilo pia wanakijiji hao waliteketeza nyumba 5 za familia tofauti kwa moto huku mzee mwenye umri wa zaidi ya miaka 70 akijinyonga kwa kuhofia naye kuuawa kwa kipigo na wananchi baada ya kutuhumiwa kuwa miongoni mwa watuhumiwa.
Hata hivyo, Musese Kabulizina, Ofisa Wanyamapori wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita ameionya jamii kutoyahusisha matukio ya fisi na imani za kishirikina na badala yake anasema kuwapo kwa fisi wengi katika makazi ya watu ni matokeo ya uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kwa wanyamapori wakiwamo fisi kuanza kuvamia makazi ya binadamu kusaka mahitaji kikiwamo chakula.