Tuesday, 19 December 2017

Mwenyekiti Sau Kuzikwa Disember 22



Mwenyekiti wa Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Dk Paul Kyara aliyefariki dunia jana anatarajiwa kuzikwa Desemba 22,2017 kijijini Legho, Kilema mkoani Kilimanjaro.
Dk Kyara alifariki dunia jana asubuhi Jumatatu Desemba 18,2017 akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Regency jijini Dar es Salaam.
Katibu wa chama hicho, Johnson Mwangosi amesema Desemba 21,2017 saa tano asubuhi wanatarajia kuwa na ibada na kuaga mwili wa marehemu nyumbani kwake Madale.
Mwangosi amesema baada ya shughuli hiyo mwili wa Kyara utasafirishwa kwenda kijijini Legho.
Majaliwa, mtoto wa marehemu Kyara amesema baba yake alikuwa akisumbuliwa na figo tangu mwaka 2012.
Amesema Ijumaa Desemba 15,2017 alipata tatizo la shinikizo la damu na sukari ilipanda.
Majaliwa amesema alipelekwa hospitali alikopatiwa matibabu na aliruhusiwa kurejea nyumbani.
Amesema Jumamosi Desemba 16,2017 alizidiwa na saa tatu usiku walimpeleka katika Hospitali ya Regency kwa matibabu.
Amesema madaktari walijitahidi kuokoa maisha yake lakini shinikizo la damu na kisukari hakikushuka hivyo kusababisha kifo chake.
“Nitamkumbuka baba, wakati amelazwa neno alilokuwa akisisitiza ni upendo na umoja," amesema Majaliwa.

No comments:

Post a Comment