Monday, 11 December 2017

Watoto sita wapelekwa Israel kwaajili ya Matibabu



Watoto sita wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi  miaka kumi na tatu wamepelekwa nchini Israel kwa ajili ya matibabu ya moyo.

Watoto hao wamepelekwa chini ya ushirikiano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s  Heart – SACH) ya nchini Israel. Safari hiyo ya matibabu imejumuisha wauguzi pamoja na wazazi wa watoto ambao kwa pamoja wameondoka nchini Disemba 10 mwaka huu.

Baada ya matibabu ya watoto kukamilika, Maafisa Wauguzi wawili watabaki kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo ya mwaka mmoja ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa waliopo katika wodi ya uangalizi maalum (ICU) na chumba cha upasuaji.

Aidha kundi hilo limekuwa ni kundi la tano la watoto kwenda kutibiwa magonjwa ya moyo nchini Israel tangu mwaka 2015 ambapo Taasisi ya Moyo ilianza ushirikiano  na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart –SACH) ya kuwapeleka wagonjwa nchini humo. Hadi sasa watoto 46 wameshatibiwa nchini humo na wanaendelea vizuri.


Amber Lulu afunguka mafanikio aliyoyapata mwaka huu


Msanii wa muziki Bongo, Amber Lulu amefunguka mafanikio aliyoyapata kwa mwaka huu.

Muimbaji huyo amesema cha kwanza kabisa ni uhai wake na mambo mengine yanabaki kuwa binafsi na hata mipango ya kujenga pia.

“Maisha yangu siwezi nikayaweka hadharani, sijui nimeingiza au nimetoa shilingi ngapi lakini namshukuru Mungu mwaka huu umekua wa bahati sana” Amber Lulu ameiambia Bongo5.

“Hiyo ni siri yangu, ukifika wakati nitawaambia nimejenga nakadhalika lakini sasa hivi am not ready” amesema.


Msanii Gilad amesema Cinderella ya Ali Kiba ilimfunza kuimba Kiswahili



Msanii wa muziki toka nchini Kenya mwenye asili ya Israel, Gilad amesema wimbo wa Alikiba Cinderella ndio uliomfunza kuimba Kiswahili.

Muimbaji huyo ameiambia FNL ya EATV kuwa ngoma hiyo ndio ya kwanza kuimba kwa lugha ya Kiswahili ndipo na nyingine zikafuata.

“Cinderella ni wimbo wa kwanza kujifunza kuimba, ni wimbo wa kwanza kuinba kwa Kiswahili. Nilikuwa naimba na bendi jukwaani, kwa hiyo ni wimbo wa kwanza kuimba kwa Kiswahili na nilikuwa natumbuiza kila wiki, nikaja nikaimba Kidumu ‘Haturudi Nyuma’, pia Juliana ‘Tawala’ amesema.

Miongoni mwa ngoma alizoimba kwa Kiswahili Gilad ni pamoja na Nakuhaidi, Sema Milele, Unajua na Mapenzi. Pia mwaka huu ameweza kushinda tuzo mbili za Afrima.

Gilad kwa sasa anasikika Bongo kupitia ngoma mpya ya rapper Azma ‘Shubiliga’.

Mwana FA asema hatujaombana msamaha na Jide




Msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye hivi karibuni amemaliza tofauti zake na msanii mwenzake Lady Jaydee baada ya kutokuwa na maelewano mazuri kwa muda mrefu, amesema hakuna mtu aliyemuomba msamaha mwenzake kati yao ili kuyamaliza.

Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Mwana FA amesema ugomvi wake na Jaydee hakuna mtu aliyewakalisha kujaribu kuwapatanisha au wenyewe kuombana msamaha, bali waliumaliza kwa yeye kumpigia simu, na kuzungumza kama ambavyo wengine wanazungumza,

"Hakuna aliyemuomba msamaha mwenzake, mi ndio nilianza, nilimtumia meseji oya vipi, akajibu fresh, nikamwambia FA hapa usiku nilikutafuta, akajibu mimi siku hizi nimezeeka nalala mapema, ndo hivyo tukayamaliza hivyo", amesema Mwana FA.

Mwana FA ambaye kwa sasa ameachia kazi mpya aliyomshirikisha Maua Sama, amesema licha ya kumaliza tofauti zao na Jaydee, watu wasitarajie sana kazi ya pamoja kwani kibinadamu itaonekana wamemaliza tofauti hizo kwa ajili ya kazi.

Askari JWTZ waliouawa na waasi, miili yao kuwasili leo



Dar es Salaam. Miili ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliouawa na waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inarejeshwa nchini leo.

Taarifa ya ofisi ya habari ya JWTZ imesema miili ya askari hao itawasili nchini leo Jumatatu Desemba 11,2017 saa kumi na mbili jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Awali, akizungumzia na waandishi wa habari jana Jumapili Desemba 10, 2017 Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali James Mwakibolwa alisema miili ya askari hao ingerejeshwa nchini kati ya Jumanne Desemba 12, au Jumatano Desemba 13,2017 kwa ushirikiano kati ya Serikali na Umoja wa Mataifa (UN).

Mwakibolwa alisema askari hao walivamiwa kambini na waasi wa ADF na mapigano yalidumu kwa takriban saa 13. Alisema askari 14 wa JWTZ waliuawa, 44 wamejeruhiwa na wengine wawili  hawajulikani walipo.

Alisema tukio hilo lililotokea Desemba 7,2017 katika kambi ndogo iliyopo katika daraja la Mto Simulike, kaskazini mashariki mwa Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu nchini DRC.

Tundu Lissu: Madaktari wamesema nitasimama na kutembea


Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Tundu Lissu amefunguka na kusema kuwa ameambiwa na madaktari wake kuwa atasimama, atatembea na kurudi tena Tanzania kuendelea na majukumu yake kama kawaida.

Tundu Lissu amesema hayo leo alipofanya mahojiano na DW na kusema kuwa kwa sasa anaendelea vizuri kiafya na kuwa madaktari wamemweleza kuwa atasimama na kutembea tena kama zamani na kurudi nyumbani kwake Tanzania.

Aidha Tundu Lissu amesema hajapoteza matumaini ya kuwapata na kuwatambua watu ambao walishambulia kwa risasi kwa kuwa anaamini sehemu ambayo tukio hilo lilitokea kulikuwa na ulinzi na walinzi wa serikali.

"Matumaini hayajapotea kwa vile nakaa kwenye nyumba za serikali hizi nyumba zinalindwa masaa 24, Je, siku hizo napigwa risasi walinzi walikuwa wapi? Walinzi wa geti kubwa nao walikuwa wapi? Ile sehemu yote tunayoishi imezungushwa ukuta na kuna geti kuu lenye ulinzi masaa 24 nao walikuwa wapi? alihoji Tundu Lissu

Mbali na hilo Tundu Lissu ameelezea jinsi ambavyo tukio hilo lilitokea mnamo Septemba 7, 2017 pale Dodoma msikilize hapa chini akitolea maelezo hilo.

Hii ndio droo ya hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya



Droo ya Hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya maarufu kwa jina la Champions League imepangwa na kuna michezo mitatu ambayo imeonekana kuwavutia watu wengi.

Juventus wanatarajia kukutana na Tottenham Hotspur wakati ambapo wababe wa Hispania Real Madrid wao watakula sahani moja na wababe wa Ufaransa, Paris Saint-Germain.

Ratiba hiyo inamaanisha kuwa staa wa PSG, Neyamr atakutana na Real Madrid kwa mara nyingine baada ya mchezaji huyo kukuna nao mara kadhaa lipokuwa akiitumikia Barcelona.

Gumzo zito ni juu ya  Chelsea wanaonolewa Kocha Antonio Conte ambapo wanatarajiwa kukutana na Barcelona.

Manchester City wao wataanzia ugenini ambapo huko watakipiga dhidi ya Basle wakati Porto wataikaribisha timu nyingine ya England, Liverpool katika hatua hiyo.

Sevilla wao wataanza nyumban I kuikaribisha Manchester United kabla ya timu hizo kurudiana wiki moja baadaye.

Michezo ya hatua hiyo itachezwa Februari, mwakani.

Ratiba kamili ya hatua hiyo ni hii hapa:
Juventus vs Tottenham Hotspur

Basle vs Manchester City

Porto vs Liverpool

Sevilla vs Manchester United

Real Madrid vs Paris Saint-Germain

Shakhtar Donetsk vs Roma

Chelsea vs Barcelona

Bayern Munich vs Besiktas

Pole Pole Amchana Lowassa



Humphrey Polepole ameibuka na kusema kuwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa serikali ya awamu ya nne Edward Lowassa alishindwa kuzuia Babu Seya asifungwe na kudai pia alishindwa mshawishi Mhe. Jakaya Kikwete ili awatoe watu hao.

Polepole amesema hayo baada ya watu kuanza kusema kuwa jambo alilofanya Rais Magufuli kuwatoa Babu Seya na mwanaye Papi Kocha ni jambo ambalo Lowassa aliahidi katika kampeni zake za 2015 kuwa endapo angechaguliwa kuwa Rais wa Tanzania angewaachia huru watu hao.

"Huyu mzee ambaye amezungumza kwamba hii ilikuwa ahadi yake kipindi cha kampeni ni mzee ambaye amehudumu kwenye serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kipindi ambacho Babu Seya anafungwa huyu mzee alikuwa Waziri Mkuu mwenye nguvu sana, kama alijua Babu Seya labda hakutendewa haki kwa namna yoyote kwa fikra zake angaliweza kumshauri Rais wake kipindi hicho kwamba huyu mtu hastahili kufungwa asamehewe" alisema Polepole

Polepole aliendelea kusisitiza kuwa Lowassa alishindwa kuzuia Babu Seya na watoto wake wasifungwe "Kashindwa kuzuia Babu Seya asifungwe, kashindwa mwaka wa kwanza kumshawishi Rais wake amsamehe Babu Seya, ameshindwa kufanya hivyo kwa miaka mingi iliyopita.

"Magufuli hakuwa kwenye nafasi ya uamuzi kipindi hicho alikuwa Waziri wa kawaida kabisa baada ya tafakuri ya kina ya miaka miwili akaona katika watu ambao wamejirudi huyu anastahili msamaha, huyo mzee anaibuka oohh nilifanya mimi, huyu mzee aache hizi tabia za kinafiki, kizandiki kwani Watanzania wanataka upinzani unaojenga hoja" alimalizia Polepole.

Babu Seya na mtoto wake Papii Kocha waliachiwa huru katika kifungo cha maisha jela baada ya Rais John Pombe Magufuli kuwapa msamaha katika siku ya Uhuru wa Tanzania bara, ambapo kila mwaka Disemba 9 zinafanyika sherehe za kumbukumbu.

Rais Kenyatta amuandikia barua Rais Magufuli



Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amemuandikia barua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kupinga kitendo cha mauaji ya askari wake 15 waliokuwa wakilinda amani nchini Kongo, na kumpa pole kufuatia msiba huo mkubwa.

Katika barua hiyo, Rais Kenyatta amesema kushambuliwa kwa askari, ambao walikuwa wakihudumia kwa sababu nzuri ya kuanzisha amani ya kudumu nchini DRC ilikuwa mbaya, huku akiwapa pole watanzania na ndugu wa marehemu, na kuwaombea wale waliojeruhiwa waweze kupona haraka.

Uhuru Kenyatta ameendelea kwa kusema kwamba Kenya itaendelea kushirikiana na watu na serikali ya Tanzania katika kulinda amani ya Kongo na maeneo ya maziwa makuu, na kuangalia kesho bora ya maeneo hayo.

Rais Kenyatta amesema Kenya inathamini jukumu muhimu lililofanywa na watunza amani tangu imehusika katika mipango mingi ya kulinda amani.

Mwishoni mwa wiki iliyopita askari 15 wa Tanzania waliokuwa wakilinda amani nchini Kongo waliuawa na askari waasi wanaoendesha ampigano nchini humo, huku 44 wakijeruhiwa, 8 wakiwa mahututi na wawili hawajulikani walipo.


Babu wa Loliondo aoteshwa tena kikombe



Ngorongoro. Mchungaji Ambilikile Mwasapile maarufu Babu wa Loliondo aliyehudumia maelfu ya watu ndani na nje ya nchi kwa dawa aliyoitoa kwa kipimo cha kikombe amedai ameoteshwa kuwa umati utarudi kijijini Samunge kupata dawa.

Amesema ana uhakika wa jambo hilo kwa kuwa hata mwaka 2011 kabla ya maelfu ya watu kufika nyumbani kwake alioteshwa, hivyo amejiandaa kuweka miundombinu bora zaidi na hasa ujenzi wa vibanda atakavyovitumia kutoa huduma.

Mchungaji Mwasapile alisema hayo jana Jumapili Desemba 10,2017 mbele ya ujumbe wa Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tamisemi, Joseph Kakunda aliyekuwa mkoani Arusha kukagua miradi ya maendeleo, ikiwemo ya kuwawezesha wananchi kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Miongoni mwa waliofika kupata ‘kikombe’ kwa gharama ya Sh500 mwaka 2011 walikuwemo wafanyabiashara maarufu, wanasiasa na viongozi waandamizi serikalini.

Akizungumzia dawa yake anayodai inatibu maradhi mengi amesema kwa sasa anaitoa kwa watu wachache wanaofika kijijini hapo.

Miongoni mwao amesema ni watalii wanaofika kutembelea vivutio vya kitalii vilivyopo katika Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.

"Huwa nawauliza watalii namna walivyoifahamu dawa yangu wanasema habari za ‘kikombe cha Babu’ imeenea katika nchi zao za Ulaya na Amerika," amesema Mwasapile.

Naibu Waziri wa Tamisemi, Kakunda akiwa na ujumbe wake baada ya kupata kikombe alimshukuru Mchungaji Mwasapile kwa alivyolifanya Taifa kujulikana na kusababisha maendeleo ya kijamii katika Kijiji cha Samunge.

Ametoa mfano wa barabara ya kutoka wilayani Longido na Kigongoni wilayani Monduli ambazo zimeboreshwa kutokana na idadi kubwa ya watu waliokuwa wakifika kupata huduma ya dawa.

Amesema hata huduma ya mitandao ya mawasiliano ya simu ilifika eneo hilo kwa haraka kutoka na watu wengi waliohitaji kuwasiliana na ndugu zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro, Raphael Siumbu amesema Mwasapile amechangia shughuli za maendeleo kutokana na idadi kubwa ya waliokwenda kijijini hapo na kusababisha mzunguko wa fedha kuwa mkubwa.

Amesema watu wengi kijijini Samunge  wamepanda miti inayotumika kutengenezea dawa hivyo kuchangia utunzaji wa mazingira na huduma za kijamii kuongezeka.

Takukuru yamfikisha Mahakamani Sadifa kwa makosa mawili


Dodoma. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Dodoma imemfikisha mahakamani aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Sadifa Juma Khamis.

Sadifa ambaye pia ni mbunge wa Donge, Zanzibar amefikishwa leo Jumatatu Desemba 11,2017 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma kwa makosa mawili.

Kamanda wa Takukuru mkoani Dodoma, Emma Kuhanga alisema jana Jumapili Desemba 10,2017 kuwa Sadifa angefikishwa mahakamani leo.

Alisema kiongozi huyo alikamatwa nyumbani kwake akituhumiwa kwa kuwapa soda wajumbe wa UVCCM kutoka Mkoa wa Kagera kitendo ambacho ni kinyume cha maadili.

Kuhanga akithibitisha kukamatwa kwa Sadifa alisema alikamatwa Jumamosi Desemba 9,2017.


VIDEO: Tanroad yasaini mikataba nane



Makampuni nane ya kichina yamesaini mikataba ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita 402.97.

Kampuni hizo zimesaini mikataba hiyo na Wakala wa Barabarani TANROADS mbele ya Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof Makame Mbarawa.

TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI........USISAHAU KUSUBSCRIBE

VIDEO: UKAWA yafunguka kuhusu Serikali ya awamu ya tano



Umoja wa katiba ya wananchi UKAWA umesema kuwa umejiridhisha kuwa Serikali ya awamu ya Tano sio serikali ambayo inafuata utawala bora,  kuzingatia haki za binadamu huku ikivunja katiba.

TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI......USISAHAU KUSBUSCRIBE

Akizungumza na  waandishi wa habari, Mwenyekiti mwenza wa Umoja huo,  Freeman Mbowe amesema vipo viashiria vingi vinavyoonesha kuwa uongozi wa awamu ya Tano hauzingatii katiba ikiwemo kuzuia mikutano ya kisiasa Pamoja na kushambulia Kwa viongozi wa vyama vya upinzani.

" Serikali inabana wazi  kuzungumzia na kuikosoa,  hata nyinyi wandishi hampo Salama, ndio maana mwenzenu azory Mpaka sasa hajapatikana na serikali haijatoa tamko lolote" amesema Mbowe.

Mbowe pia alizungumzia uchaguzi mdogo wa madiwani ambapo Kata 43 zilifanya uchaguzi huku ccm ikishinda Kata 42 na Chadema walishinda moja.

Alisema viongozi  wao wakiwemo wabunge, madiwani na wagombea wa upinzani walikua wakikamatwa na kuwekwa ndani huku wasimamizi wao wakitolewa nje ya vyumba vya Kura jambo ambalo ni kinyume na katiba ya nchini.