Naomba pia nitumie wasaha huu kuweza kukaribisha katika makala yetu ya leo ili tuweze kujifunza juu ya mafanikio. Naamini unajua kujifunza hakuna mwisho, hivyo unatakiwa kila siku kuweka maarifa ya kukusaidia, ukishindwa kufanya hivyo utakwama.
Katika makala yetu ya leo nitaomba tu nikukumbushe mambo ambayo unatakiwa uyakumbuke kila wakati kwenye maisha yako . Ni mambo ya msingi kwani yatakusaidia kuweza kuwa na mtazamo chanya na kubadili mambo mengi sana kwako.
1. Mambo yaliyopita hayawezi kubadilishwa tena.
Unatakiwa kuelewa kama kuna mambo ambayo yameshapita huwezi kuyabadilisha tena hata kama yalikuumiza au ulifanya makosa kiasi gani. Kwa sasa unatakiwa kuganga yajayo, habari ya mambo yaliyopita yatumie kama fundisho tu kwako, lakini ndio yameshapita, usiumize kichwa na kujilaumu sana.
2. Maoni ya watu hayaamui hatima ya maisha yako.
Hata siku moja usije ukakaa ukafikiri kwamba maoni ya watu wengine wanayosema juu ya wewe ndiyo yanaamua maisha yako yawe vipi. Maisha yako yanabaki hivyo yalivyo kwa sababu wewe umeamua yawe hivyo. Lakini usikubali hata siku moja maoni ya watu yakurudishe nyuma na usiyatumie kama kisingizio.
3. Maisha yako yatakuwa mazuri tu ukijipa muda.
Ukiamua siku zote kubadilisha maisha yako unaweza. Kikubwa jipe muda wa kutosha kubadilisha maisha yako hatua kwa hatua na kila kitu kitabadalika. Haijalishi unaona maisha yako ni magumu kiasi gani, lakini muda ndio kila kitu. Muda unaweza kusawazisha mambo mabaya na yakawa mazuri kabisa. Tumia muda wako vizuri.
4. Utashindwa tu, kama utakata tamaa.
Ndoto yoyote ile uliyonayo au ambayo unatamani kuifikia una uwezo mkubwa wa kuifikia. Ila hautaweza kuifikia ndoto yako hiyo ikiwa utafika mahali wewe mwenyewe utaamua kukata tamaa. Moja ya sumu kubwa ya kimafanikio ni kukata tamaa, ukikata tamaa ujue kila kitu kwako kimeishia hapo na hutaweza kusogea tena.
5. Furaha ya kweli inapatikana ndani mwako.
Ukweli huu hautakaa ubadilike kamwe kwamba furaha ya kweli inapatikana ndani mwako na wala si nje yako. Unaweza ukakazana sana kutafuta furaha nje kwa kufanya vitu ambavyo unaamini vitakupa furaha, lakini ukivipata vitu hivyo unashangaa ile furaha tena bado huna. Hivyo jifunze kutafuta furaha ya kweli ndani mwako.
6. Mawazo chanya, ni njia ya mabadiliko chanya pia.
Mbinu mojawapo ya kuwa na maisha bora. Ni kwa wewe kuwa na mawazo chanya. Unapokuwa na mawazo chanya ni rahisi sana kwa wewe kuweza kuleta mabadiliko chanya pia. Watu wengi wanashindwa kwa sababu ya kuwa na mlundikano wa mawazo mengi ambayo kwao ni hasi. Kuwa na mawazo chanya ubadili maisha yako.
Yapo mambo mengi ya kukumbuka kila unapoelekea kwenye mafanikio yako. Kwa leo hii nimekukumbusha mambo haya machache. Kwa kuyafanyia kazi itakuwa sehemu kubwa ya mabadiliko kwenye maisha yako.