Wednesday, 22 November 2017

Wizara yataka madai ya wavuvi kuchunguzwa


Mafia. Naibu Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Abdallah Ulega amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Shaibu Anunduma kuunda kamati kuchunguza madai ya wavuvi watatu kupokwa mtumbwi, leseni, simu na kisha kutoswa baharini.

Tukio hilo linadaiwa kutokea Agosti 2,2017 saa tano asubuhi baada ya kuvua samaki katika Kisiwa cha Mbarakuni kilichopo ndani ya Hifadhi ya Bahari (Marine Park) kinyume cha sheria.

Ulega ameagiza kuundwa kamati baada ya kutokea mvutano kati ya maofisa wa Hifadhi ya Bahari na wananchi wa Kijiji cha Jojo-Mafia wanaojishughulisha na uvuvi  wanaolalamika kwamba wananyanyaswa na maofisa hao.

Katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana Jumanne Novemba 21,2017 katika Kijiji cha Jojo, mwenyekiti wa kijiji hicho, Mussa  Hassan alisema wavuvi Hamis Athuman, Hamad Faki na Issa Shali walitoswa baharini na waliokolewa na mvuvi wa kijiji kingine saa tisa alasiri ikiwa ni saa nne tangu walipotoswa.

Mwenyekiti huyo amesema wanakijiji  wanategemea shughuli za uvuvi katika Kisiwa cha Mbarakuni kuendesha maisha yao lakini wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Waziri Ulega amesema ni kosa la jinai kuwatosa baharini  wavuvi wanaokiuka sheria za uvuvi.

“Nchi inaendeshwa kwa mujibu wa sheria, utaratibu na kanuni. Wavuvi wakikamatwa wanatakiwa kuletwa kwenye kamati ya kijiji na ikishindikana wanapaswa kupelekwa polisi. Mhalifu yeyote anapelekwa polisi,” amesema.

Amesema kamati itakayoundwa kuchunguza tukio hilo inapaswa kuwa huru ili itende haki.

Ulega amesema wanachotaka ni uhusiano mwema kati ya wahifadhi na wananchi na kwamba, maofisa watakaobainika kuwatosa baharini wavuvi hao watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Pia, ameagiza wavuvi kufuata sheria akisema kisiwani hicho na vingine vya Shungimbili na Nyororo vimehifadhiwa kisheria hivyo hawapaswi kufanya shughuli za kibinadamu.

Mkurugenzi wa Hifadhi za Bahari, Dk Milali Machumu amekanusha wavuvi hao kutoswa baharini.

Amesema kabla ya tukio hilo, wavuvi hao waliwateka maofisa wao na kuwapeleka kijijini.


Meli ya wachina yaibua Matapeli



WAKATI upimaji wa afya bure ukiendelea katika meli maalumu kutoka China, baadhi ya wananchi jijini Dar es Salaam wamegeuza shughuli hiyo kuwa mtaji baada ya kuanza kuuza namba za kadi wanazopatiwa.

Aidha, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk Grace Maghembe amesema tayari watu 6,000 wamepata namba kuwawezesha kuwaona madaktari hao kwa utaratibu unaofaa.

Dk Maghembe alitoa mwito kwa wananchi ambao hawajapewa namba, kusubiri hadi waliopata namba hizo watakapohudumiwa. “Tunawaomba msiendelee kusongana; tumeshagawa namba hadi 6,000, hivyo subirini hawa wapate huduma ndipo tutaangalia kama tutaendelea kugawa namba nyingine kulingana na uwezo wa madaktari hawa,”alisema Maghembe.

Meli hiyo yenye madaktari na wataalamu wa afya zaidi ya 380 iliwasili nchini Novemba 19 na inatarajiwa kutoa huduma hiyo kwa siku tano kwa wagonjwa 600 kwa siku. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisema amepata taarifa juu ya uwepo wa watu hao wanaofika kwenye meli hiyo kama wagonjwa wanaotaka kuhudumiwa, lakini wakipatiwa namba hizo hugeuka na kuziuza kwa Sh 5,000 hadi Sh 50,000, jambo ambalo ni kosa na kinyume na makusudio.

“Upimaji huo tulisema ni bure na ni makosa kwa mtu kununua au kuuza namba,” alisema. Alibainisha kuwa, baadhi ya wagonjwa wamebainika kutakiwa kusafirishwa kwenda China kupatiwa huduma zaidi hivyo ofisi yake itaandaa utaratibu wa kuwawezesha kusafiri.

Akaongeza, “wagonjwa hawa wanaotakiwa kusafirishwa tutaangalia utaratibu wa kuwasaidia baada ya kupata idadi kamili tutawasaidia kupata hati za kusafiria pamoja na kuangalia utaratibu wa kuwawezesha wakiwa huko kwa matibabu.”

Msajili wa Vyama vya Siasa apelekwa Mahakamani na Chama cha ‘Mtikila’

Msajili wa Vyama vya Siasa apelekwa Mahakamani na Chama cha ‘Mtikila’


   Msajili wa Vyama vya Siasa nchini,Jaji Francis Mutungi.  

       Dar es Salaam. Chama cha Democratic (DP), kimeomba kibali cha kumfungulia mashtaka msajili wa Vyama vya Siasa nchini.

Chama hicho ambacho kiliasisiwa na Mchungaji Christopher Mtikila ambaye sasa ni marehemu kimewasilisha maombi Mahakama Kuu, kikiomba kibali cha kumfungulia kesi msajili wa Vyama vya Siasa kikimtuhumu pamoja na mambo mengine kuingilia mambo yake ya ndani.

Maombi hayo yaliyofunguliwa na Bodi ya Wadhamini wa chama hicho katika Mahakama Kuu, Masjala Kuu Dar es Salaam dhidi ya Msajili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) yamepangwa kusikilizwa na Jaji Kiongozi, Ferdinand Wambali, Jumatatu ijayo.

Kwa mujibu wa hati ya maombi ya faragha yaliyowasilishwa mahakamani hapo chama hicho kimefikia uamuzi huo baada ya msajili kukiandikia barua mbalimbali ikiwemo ya kubatilisha mkutano mkuu wa chama uliofanyika Mei 26.

Pia, chama hicho kinapinga hatua ya msajili kutowatambua viongozi wa chama hicho waliochaguliwa katika mkutano huo na badala yake kuwatambua wasio viongozi na wasio wanachama.

Chama hicho kinawakilishwa na mawakili Daimu Halfan na Juma Nassoro.

Kwa kujibu wa hati ya kiapo cha mwenyekiti wa chama hicho, Georgia Mkitila, Aprili 6, msajili alikiandikia barua chama hicho kukikumbusha kuwa uongozi wake ulikuwa unafikia mwisho wake Mei 26, mwaka huu.

Katika barua hiyo, msajili pia alikumbushia chama hicho kufanya mkutano mkuu tarehe hiyo na si vinginevyo.

Georgia, ambaye ni mke wa marehemu Mtikila anaeleza kuwa kutokana na maelekezo hayo ya msajili, chama hicho kiliandaa mkutano mkuu na kikamwandikia msajili barua ya mwaliko.

Anaeleza kuwa msajili alijibu kuwa mkutano huo utakuwa ni batili isipokuwa tu malalamiko yaliyowasilishwa kwake kuhusu uchaguzi wa Mkoa wa Dar es Salaam yatakuwa yamepatiwa ufumbuzi.

Georgia anaeleza kuwa Mei 25, chama hicho kilimwandikia barua msajili kutoa maelezo na kusisitiza kuwa mkutano huo utakuwa halali.

Alisema kuwa walifanya mkutano mkuu Mei 26 kwa mujibu wa katiba yao ya mwaka 2002 na kwamba licha ya kumwalika, msajili hakuhudhuria yeye wala ofisa yeyote kutoka ofisi yake.

Alibainisha kuwa baada ya mkutano huo waliwasilisha kwa msajili taarifa zote na mwenendo wa mkutano, ikiwemo orodha ya wajumbe waliohudhuria.

Alifafanua kuwa msajili katika barua yake ya Juni 16, alikiri kupokea taarifa za mkutano mkuu wa chama hicho na kwamba angezitafakari pamoja na malalamiko kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho ili kujiridhisha.

Georgia alidai kuwa Julai 3, msajili alitangaza kuwa mkutano huo ulikuwa batili na akaamuru chama hicho kiandae mkutano mwingine.

Alisema chama hicho kupitia mamlaka yake ya ndani ya nidhamu kilishamvua wadhifa wa ukatibu mkuu,  Feruzi Msimbachaka na kumjulisha msajili,ambaye alikataa kutambua mamlaka hayo ya kinidhamu ya chama.

Alisema msajili amekataa kuwatambua viongozi waliochaguliwa ama kuteuliwa na chama, badala yake anawatambua na kukubali kila kitu kutoka kwa watu walioondolewa madarakani.   

BAVICHA wafunguka baada ya Mwenyekiti wao kuhamia CCM





Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Chadema (BAVICHA), Patrick Ole Sosopi amesema kwamba kuondoka kwa Mwenyekiti wa baraza hilo Patrobas Katambi ndani ya Chama hicho hakijawateteresha na kudai kwamba Katambi hakuwa mkubwa kuliko Chama chao.

Akizungumza jana muda mfupi baada ya Mwenenyekiti wa Baraza hilo kuhamia CCM, Ole Sosopi alisema kwamba Patrobasi hakuwa Bavicha kwani aliingia ndani ya chama hicho akiwa hana umaarufu hivyo kuondoka kwake kusiwavunje moyo vijana vingine na kusisitiza kwamba bado baraza hilo la vijana lipo imara.

"Patrobas siyo Bavicha, ila yeye alikuwa sehemu ya Bavicha. Bavicha ipo imara na hii ni taasisi.

"Na Patrobasi kuondoka Chadema siyo jambo geni, ni jambo la kawaida kama jinsi viongozi wengine wavyotoka chama kimoja kwenda kikingine.

"Tunamtakia kila la kheri huko alipokwenda. Vijana wetu waendelee kuiwa busy kufanya kampeni kwa ajili ya uchaguzi na wasihangaike na habari za Patrobas". Alisema Ole Sosopi na kuongeza;

"Ndani ya Chadema hakuna mtu maarufu isipokuwa Patrobas alipata umaarufu alipokuwa ndani ya Chama na ameondoka, hivyo Chama kitaendelea kuwa imara siyo kwa ajili ya mtu mmoja. Kupitia uchaguzi huu mdogo tunapaswa kutuma meseji kwa CCM na yeye Katambi  hivyo vijana msihamishwe na hili jambo mkaacha kuendeleza kampeni".

Aidha aliongeza kwamba kitendo cha Patrobas kuhamia CCM ni usaliti ambao ameudhihirisha kwa watanzania na wanachama kuungana na watu au serikali ambayo imeshindwa kumbaini nani aliyempiga risasi mwanasheria mwenzake Tundu Lissu.

Aliongeza kwamba kinachofanywa na CCM siyo siasa bali ni 'Project' inayofanyika kushawishi watu waone kwamba CCM imebadilika lakini ukweli ni kwamba "CCM ni ileile na madudu yake ni yaleyale kwa zaidi ya mika 50 nawashauri wafanye siasa zinazohgusa wananchi"

Madereva walevi kufanya kazi mochwari

Mamlaka ya Usalama wa Uchukuzi nchini Kenya NTSA imependekeza adhabu mpya miongoni mwa madereva walevi.



Madereva walevi sasa watalazimika kufanya kazi katika vyumba vya kuhifadhia maiti ili kupunguza idadi kuu ya ajali za barabarani.

”Hatuwezi kuwa na madereva wengi walevi wanaofanya ajali na wanapofikishwa mahakamani wanapewa adhabu hafifu.Tutakapokamilisha kutengeza sera hiyo mpya tutahakikisha kuwa inakuwa sheria”, alisema mkurugenzi wa mamlaka hiyo Francis Meja.

Na Wakenya wengi katika mitandao ya kijamii waliunga mkono mpango huo na kusema kuwa utawafanya madereva kuwa makini.

Je una hisi sheria hii ikija Tanzania itasaidia kupambana na madereva walevi?.

Hizi ndizo sababu za mke wa Mugabe kuchukiwa




Grace Mugabe

Wakati mwisho wa utawala wa miaka 37 wa mume wake Aliyekuwa Rais Robart Mugabe wa Zimbabwe ukiwa wa aibu, sababu tano za wananchi wa taifa hilo kumchukia Grace Mugabe zimeanikwa.

Kwa mujibu wa mitandao mbalimbali ya kijamii na magazeti ya nchi hiyo, Grace Mugabe alisababisha watu kumchukia kutokana na tabia yake ya kupenda kufanya manunuzi ya gharama ambayo yalisababisha kupewa jina la utani la First Shopper, badala ya first Lady. Manunuzi hayo yanadhaniwa kutumia fedha za umma.

Sababu nyingine inayotajwa kumfanya achukiwe ni ubabe, ambao aliounyesha katika matukio mbalimbali ya hadhara, alipokuwa akiongozana na mume wake katika shughuli za kisiasa. Katika hafla nyingi, Grace aliweza kuwafokea maofisa wa serikali hadharani na kumfanya kuogopwa kupita kiasi.

Licha ya sifa hizo, pia mwanamke huyo aliyezaa na Mugabe akiwa bado kwenye ndoa yake, anadaiwa kuwa mgomvi, kwani mara kadhaa ameripotiwa kuwapiga watu, wakiwemo waandishi wa habari na watu wa kawaida, kama ilivyokuwa mapema mwaka huu, alipompiga na kumuumiza msichana mmoja wa miaka 20 nchini Afrika Kusini, baada ya kumkuta akiwa na watoto wake wa kiume hotelini.

Jambo lingine lililomfanya kuchukiwa na wananchi wengi wa nchi hiyo ni tamaa yake ya madaraka, kwani licha ya kuwa kiongozi wa Jumuia ya wanawake wa Zanu PF, pia kwa nyakati tofauti alionyesha kutamani kuchukua nafasi ya mume wake, kitu kilichofanya wananchi wake kuona kama nchi inataka kuendeshwa kifamilia.

Inadaiwa hata kuondolewa kwa Makamu wa Rais Emmerson Mnangangwa, kulifanywa na Mugabe kwa shinikizo lake. Kitu kingine kinachowaudhi wananchi wa nchi hiyo ambayo fedha yake haina thamani kutokana na vikwazo kutoka nchi za Magharibi, ni kitendo chake cha kukosa heshima za kike, hasa tabia yake ya kuropoka hovyo katika hafla mbalimbali zinazohitaji staha kwa wanawake.

Hadi wakati gazeti hili likienda mtaani, bado haikujulikana alipo mwanamke huyo mzaliwa wa Afrika Kusini, baadhi ya habari zikisema amekimbilia Namibia, lakini wengine wakisema amedhibitiwa nchini Zimbabwe

Wazee, bodaboda kutokomeza mimba za utotoni Tarime


Changamoto ya mimba na ndoa za utotoni katika Wilaya ya Tarime ni sawa na maeneo mengine nchini, lakini huenda ikawa historia baada ya wazee wa kimila na madereva wa bodaboda kusema sasa inatosha na wapo tayari kuunga mkono juhudi za Serikali za kupinga vitendo hivyo.

Wilaya ya Tarime ipo ndani ya Mkoa wa Mara ambao ni kati ya mikoa mitano inayoongoza kuwa na tatizo la mimba za utotoni linalokatisha ndoto za watoto wa kike kufikia malengo yao.

Takwimu za Wizara ya Afya, Maendeleo Jinsia, Watoto na Wazee zinaonyesha Mkoa wa Katavi unaongoza kwa mimba za utotoni kwa asilimia 45 ukifuatiwa Tabora (43), Dodoma (39), Mara (37) na Shinyanga (34).

Kiongozi wa wazee wa kimila wa kabila  la Kikulya kutoka koo 13 za wilaya hiyo, Elias Maganya hivi karibuni  ameeleza msimamo walioufikia kuhusu mimba za utotoni ikiwa ni sehemu kusaidia kampeni ya Serikali, wadau na watetezi wa haki za watoto kuhakikisha tatizo  hilo linakwisha  kwa kuwajengea uelewa wananchi umuhimu wa mtoto wa kike.

Msimamo huo wa wazee wa kimila ulikuja baada ya  Mkuu wa Wilaya  ya Tarime, Glorious Luoga kuwaomba viongozi hao kushirikiana nao katika kutetea haki za mtoto wa kike ikiwamo kupambana na kupinga ndoa za utotoni, mimba na ukeketaji kunakodaiwa kuchangiwa na mila na desturi za wakazi wa wilaya hiyo.

Luoga alitoa ombi hilo wakati wa kongamano la kujadili utoaji wa haki za msingi kwa mtoto wa kike ikiwamo ulinzi wake lililoandaliwa na masharika mbalimbali ya kutetea haki za watoto likiwamo la Plan International na lilihudhuriwa na wazee wa kimila na wanafunzi kutoka shule mbalimbali pamoja na watendaji wa Serikali kutoka Wizara ya Afya na Halmashauri ya Tarime.



Serikali inasemaje?



Maganya anasema wanaunga mkono juhudi za mtoto katika kufikia malengo yake na hawana shida kushirikiana na Serikali na wadau na watetezi wa watoto.

“Napenda kumhakikishia mkuu wa wilaya na Watanzania kwa ujumla suala la mimba na ndoa za utotoni litakuwa historia katika wilaya hii wazee wa kimila tumeshaamua kuunga mkono juhudu za wadau,” anasema na kuongeza:

“Kama tuliweza kusitisha mapigano ya kikoo huko nyuma hili halitashindika na uzuri wenyewe tunajuana  kupitia koo zetu.”

“Msituone hivi, sisi wenyewe tunatambua  umuhimu wa  mtoto wa kike tunaishukuru sana  Serikali  kwa  kutukutanisha na masharika ya kutetea haki za watoto ambayo yametujengea uwezo wa kutambua thamani na haki za watoto hawa.”

Maganya anasema katika kuhakikisha wanafanikiwa mchakato huo wataanza kufanya mkutano na wazazi kuwaelimisha namna ya haki za mtoto wa kike, pia watawapa mikakati ya kuwadhibiti watoto na kutowaruhusu kwenda sehemu zenye uvunjifu wa maadili.

Kiongozi huyo, anasisitiza kuwa ikitokea kijana au mtu ameoa au kumpa mimba mwanafunzi ataitwa katika mabaraza ya kimila kisha kujadiliwa na kulipa faini ya ng’ombe watakaohitajika kulingana na makubaliano ya baraza.

 “Tumedhamiria  kumaliza tatizo hili na hatutakuwa na mlolongo mrefu kwa atakayebainika kutenda vitendo hivi dhidi ya mtoto wa kike, akibainika hatutasubiri vyombo vya dola  tutaanza naye kisha tutamkabidhi vyombo hivyo kwa hatua za  kimahakama na tutahakikisha anafungwa,” anasema Maganya.



Madereva bodaboda

Wakati wazee wakieleza hayo, Umoja wa Madereva wa Bodaboda wa Wilaya ya Tarime Mjini (Uwamitamo), umesema wakati umekwisha kwa wanachama wao kunyooshewa vidole dhidi ya uhalifu kwa watoto wa kike na atakayebainika atachukuliwa hatua za kinidhamu  ikiwamo  kufukuzwa na kutozwa faini ya papo papo.

Madereva wa bodaboda  wa Tarime wanadaiwa kufanya uhalifu kwa watoto wa kike  kwa kuwapa ujauzito kutumia mbinu ya kuwapa lifti wakati wa kwenda na kurudi shule pia wanawarubuni hata wale wasiobahatika kwenda shule.

Lakini katika kuunga mkono juhudi za Serikali na wadau katika kupiga vita dhidi ya ndoa na mimba za utotoni umoja huo kupitia vijiwe vya maegesho wamejiwekea mikakati thabiti ya kuhakikisha haki ya mtoto wa kike inalindwa.

Mwenyekiti wa kamati ya nidhamu wa kituo cha  pikipiki cha Juminta, Steve Nashon, wilayani Tarime  anasema katika kuhakikisha wanawadhitibiti  madereva wenye vitendo vya utovu wa nidhamu kwa mtoto wa kike kituo chao kimeweka  faini ya Sh5,000 papo hapo kwa dereva atakayebainika kumshikashika mtoto wa kike.

Anasema watahakikisha faini hiyo inatekelezwa kwa ufanisi  ili iwe fundisho kwa madereva wenye tabia ya kuwashikashika watoto wa kike ambao baadhi yao ni rahisi kurubuniwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kipato kidogo  cha fedha.

“Kijiweni wananiogopa ndiyo maana wakaamua kunipa cheo hiki na sina haya na tutahakisha jambo hili linafanikiwa ingawa nitajenga chuki na madereva wengine kutokana na msimamo wangu kwa mtoto wa kike na tunatoa onyo kwa madereva bodaboda kubadilika,” anasema Nashon.

Wakati Nashon akieleza hayo, mjumbe mkuu wa Umitamo, Kulwa Joseph anasema  kwa kipindi kirefu wamekuwa madereva wa bodaboda wa wilaya hiyo wakionyoshewa vidole  dhidi ya vitendo vya kihalifu  kwa mtoto wa kike kwa kuwarubuni na kusababisha ndoto zao kutokamilika.

“Tunanyooshewa vidole na jamii ya Wanatarime kwa sababu sisi ndiyo tupo karibu nao kutokana na shughuli zetu zinatufanya kufika sehemu yoyote na huwa tunawapakiza wakituomba msaada wa usafiri. Lakini madereva wasiowaaminifu wanatumia mwaya huo wa msaada kufanya uhalifu dhidi ya watoto hawa ambao kwa kiasi kikubwa watakuwa na mchango mkubwa kwa siku za baadaye,” anasema Joseph.

Joseph anasema mwanachama akibainika anapewa onyo kwanza kisha wanatafuta ushahidi kuhusu uhalali wa kosa alilotenda na ukipatikana anaondolewa eneo hilo ili iwe fundisho kwa wanachama wengine.

Amesisistiza kuwa umoja huo umejipanga kisawasawa katika kuhakikisha wanatetea haki za watoto hao na kwamba hawatakubali kuwa sehemu ya watuhumiwa wa kukatisha ndoto za watoto hao.

“Tayari kuna wanachama watatu walishakumbana na adhabu hii. Sasa tunawatangazia kiama wale wenye mchezo huu kuacha mara moja kama wanataka kuendelea kuishi Tarime mjini,” anasema Joseph.



Serikali inasemaje?

Katika kuhakikisha  haki ya mtoto wa kike inaendelea kulindwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jinsia na Watoto na Wazee,  Ummy Mwalimu anatoa miezi sita kwa  shule za msingi na sekondari kuanzisha madawati  ya ulinzi na usalama ili kuzuia mimba za utotoni.

Ametoa agizo hilo wakati wa maadhimisho ya kimataifa ya siku ya mtoto wa kike duniani yaliyofanyika kitaifa uwanja wa TCC wilayani Tarime yaliyokuwa na kaulimbiu ya ‘Tokomeza Mimba za Utotoni Tufikie Uchumi wa Viwanda’.

Mwalimu anasema bado ana imani ndani ya miezi hiyo mchakato huo utakamilika kwa kiasi ili kuwaokoa watoto wa kike waliopo kwenye hatari mbalimbali  kuondokana na mimba za utotoni na hatimaye kuendelea na masomo na ili kutimiza ndoto zao.

“Mimba za utotoni bado ni tatizo katika mikoa mbalimbali. Madawati haya yatasaidia kufanikisha kuzuia kwa kuwa yatapokea matatizo yanayowakabili hasa kutoka kwa wazazi na mazingira yanayowazunguka kisha kufanyiwa kazi,” alisema Mwalimu.

Serikali imeadhimisha siku hiyo kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali zaidi ya 10 yanayotetea haki za watoto ikiwamo Umoja wa Ulaya kupitia taasisi za Plan International, Save the Children na Unicef.



Kauli ya wanafunzi 

Rehema Amos mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari ya Nyamisangura anasema baadhi ya watoto wa kike wameingia  kwenye matatizo kutokana na wazazi wao kutowasikiliza hasa mahitaji yao jambo linalosababisha kudanganyika.

Mwakilishi wa shirika la Unicef nchini, Maniza Zaman ameipongeza Serikali kwa kuona umuhimu wa kuanzisha siku hiyo kwa kutumia kaulimbiu ya ‘Tokomeza mimba za utotoni tufikie uchumi wa viwanda’.

“Napenda kusisitiza umuhimu wa mtoto wa kike katika kuifanya Tanzania iwe nchi imara na yenye maendeleo ya kiuchumi. Umri wa kubarehe ni kipindi muhimu cha kuelekea katika utu uzima. Watoto wa kike wakiandaliwa na kuweza kuvuka kipindi hiki kwa usalama, wana fursa ya kuja kuwa wananchi watakaochangia maendeleo ya jamii na taifa,” anasema Zamani.

Zamani anasema binti mmoja kati ya wanne wenye umri wa miaka 15 hadi 19 wana watoto na kwamba Tanzania ni moja kati ya nchi yenye kiwango kikubwa cha ndoa za utotoni.

Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano wa Taasisi ya Plan International, Martha Lazaro anasema shirika hilo linatambua ndoa za utotoni, mimba na ajira hatarishi ni vikwazo kwa mtoto katika kutimizi ndoto zake ndiyo maana limeamua kuungana na Serikali katika kuhakikisha mtoto wa kike anapata haki yake.

“Mikakati yetu ni kuhakikisha mtoto wa kike anatambulika, ikiwamo kushiriki kikamilifu katika kufanya uamuzi sahihi kwake.Mtoto wa kike asipopata nafasi ya kufanya uamuzi hawezi kutimiza ndoto zake.

“Pia, Plan imejiwekea mkakati wa kumjengea uwezo mtoto wa kike ya kuweza kujitambua, kujiamini na kujua ni wapi anaweza kupata haki za msingi,” anasema Lazaro.


TANGAZO: CHUO CHA TUMAINI JIPYA MAFINGA KINATANGAZA NAFASI ZA MASOMO




MKUU WA CHUO CHA AFYA CHA  TUMAINI JIPYA MAFINGA ANA FURAHA KUWATANGAZIA KUWA CHUO KIMEANZA KUPOKEA MAOMBI YA MASOMO KWA MWAKA WA MASOMO 2017/18 KATIKA KOZI ZIFUATAZO.
                                                    
1. CERTIFICATE IN CLINICAL MEDICINE YAANI TABIBU MSAIDIZI KWA MIAKA MIWILI

Sifa za mwombaji: Awe na ufaulu wa kidato cha nne kwa angalau alama D nne yakiwemo masomo ya sayansi yaani Fizikia (Physics), Kemia (Chemistry) na Baolojia (Biology)

2. CERTIFICATE IN COMMUNITY HEALTH (Uhudumu wa afya ngazi ya jamii) MWAKA MMOJA

Sifa za mwombaji: Awe na ufaulu wa kidato cha nne kwa angalau D nne likiwemo somo la Baolojia (Biology)


MUHULA MPYA UTAANZA MWEZI HUU WA SEPTEMBA, 2017.

YOTE HAYO YANAZINGATIA MWONGOZO WA WIZARA YA AFYA NA NACTE.

CHUO KIMESAJILIWA KWA USAJILI WA KUDUMU KWA NAMBA 144.

ADA ZETU NI NAFUU NA ZINALIPWA KWA AWAMU.

FOMU ZINAPATIKANA CHUONI TUMAINI JIPYA MAFINGA – IRINGA AU KWENYE WEBSITE YA CHUO.www.tumainijipya.ac.tz

Kwa maulizo tafadhali wasiliana na chuo kwa namba 0755 535 301 AU 0625 716 530 AU 0754 444 151.




Makonda atinga Clouds Media kuwapa pole



Makonda akiongea na maofisa wa vikosi vya usalama.

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam,  Paul Makonda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Dar es Salaam mapema leo ametembelea Ofisi za Clouds Media Group kutoa pole ikiwa ni siku moja baada ya ofisi hizo kukumbwa na janga la moto uliotokea hapo jana majira ya saa nne asubuhi.

Viongozi wengine wa serikali waliofika ofisini hapo ni Mkuu wa Wilaya wa Kinondoni, Ally Hapi na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta.

Hata hivyo, tayari matangazo ya vituo vya Clouds FM na Clouds TV yamerejea hewani baada ya kupotea siku nzima  jana kutokana na hitilafu ya iliyosababishwa na moto huo ambao chanzo chake hadi sasa hakijajulikana.

Wema Sepetu ; Sitarudi CCM



Wema amesema hayo baada ya kuona ujumbe wa Steve Nyerere kumpongeza Alberto Msando kwa uamuzi wake wa kukihama chama cha ACT Wazalendo ya kwenda Chama Cha Mapinduzi, CCM.



“HAHAHAHAHAHAHAHAHAHA SASA UTAKUWA MZALENDO WA KWELI , MSANDO NAESHIMU MAAMUZI YAKO MAANA NI MAAMUZI SAHIHI, KWAKO PAMOJA NA FAMILY YAKO , RAFIKI ZAKO NASI TUPO PAMOJA NAWE, SOON NA YULEEEEEEEEE RAFIKI YETU , DADA ETU , MSANII MWENZETU , NAYE YUPO NJIANI KURUDI NYUMBANI, COMING BACK TIVU , WELCOME MSANDO,” aliandika Steve Nyerere.

Baada ya kauli hiyo, Wema Sepetu aliamua kuweka mambo sawa juu ya kauli hiyo huku akidai kwamba hana mpango wa kuhama Chadema na kurudi CCM.

“I hope hauniongelei mimi… Maana mawazo hayo sina,” aliandika Wema Sepetu.

Muigizaji huyo alikihama chama hicho baada ya kudai kuna mambo ambayo hayaendi sana ndani ya chama hicho

TANESCO yapewa onyo na Serikali


Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewaagiza watendaji wa Tanesco kuhakikisha kuwa hawakati Umeme bila sababu maalum na hivyo kuwaondolea wananchi adha ya kukosa nishati hiyo.

Naibu Waziri aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa TEDAP unaohusu upanuzi na ujenzi wa vituo vya kupozea Umeme na njia za Umeme ambapo vituo vya kupozea Umeme alivyovitembelea ni Mbagala, Gongo la Mboto, Kipawa na City Centre.

“Umeme ukatike pale inapostahili tu, na endapo tatizo linatokea mfano kwenye mifumo ya Umeme ni muhimu mkatoa taarifa mapema kwa wananchi,” alisema Subira Mgalu.

Aliongeza kuwa ukatikaji wa Umeme unasababisha malalamiko kutoka kwa Wananchi kwani kukosekana kwa nishati hiyo kunaathiri shughuli nyingi hasa za kimaendeleo na kiuchumi zinazowaingizia kipato.

Aidha Naibu Waziri aliwaagiza watendaji wa TANESCO wanaosimamia mradi huo wa TEDAP jijini Dar es Salaam, kuhakikisha kuwa kazi hiyo inakamilika tarehe 15 Desemba, 2017.

Vilevile alieleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea vizuri na kwamba kukamilika kwake kutaboresha hali ya upatikanaji wa Umeme katika jiji la Dar es Salaam.

“Nawaomba watanzania wawe na matumaini na Serikali ya Awamu ya Tano kwani inajitahidi katika Ujenzi wa miundombinu ya Umeme, nia ikiwa ni nishati ya Umeme kupatikana muda wote,” alisema Naibu Waziri.

kwa upande wake, Meneja Mradi wa Usafirishaji na Usambazaji Umeme kutoka TANESCO, Mhandisi Emmanuel Manirabona alisema kuwa Shirika hilo linafanya juhudi mbalimbali ili utekelezaji wa mradi huo ukamilike ndani ya muda ulioelekezwa.

Mradi wa TEDAP unahusisha upanuzi na ujenzi wa Vituo Vipya 19 vya kupoza Umeme wa Msongo wa kV 132/33 na kV 33/11 pamoja na ujenzi wa njia za Umeme wenye Msongo wa kV 132, kV 33 na kV 11 katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Kilimanjaro.

Gharama za utekelezaji wa mradi husika ni Dola za Marekani milioni 43, ambazo zimetolewa na Benki ya Dunia (WB) kupitia Mradi huo.

Mwanafunzi wa Chuo Akutwa Amejinyonga



MWANACHUO mmoja Chuo cha Utumishi wa Umma –Tawi la Tabora kinachojulikana kama Uhazili  Raphael Kadesha (22)  amefariki dunia baada ya kujinyonga kwa kutumia tai ya kuvaa shingoni.

Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora Graifton Mushi tukio hilo limetokea jana saa 4 asubuhi ambapo marehemu alifunga tai juu ya kitanda chake.

Alisema kuwa marehemu alikuwa akisoma kozi cha Cheti cha Awali cha Utawala katika Chuo hicho.

Mushi aliongeza kuwa chanzo cha kifo hicho hakijulikani na Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kujua nini kilimfanya mwanachuo huyo kuchukua maamuzi hayo yaliyoacha simanzi katika jamii yake na Chuo kwa ujumla.

Alitoa wito kwa wanachuoni kuomba ushauri kwa viongozi wao Chuo au wa kiroho pindi wanapokuwa na matatizo binafisi kwani kujiua sio suluhisho la matatizo bali ni kuwaongezea walezi wao shida na majonzi zaidi.

Mushi alisema kuwa mwili wa marehemu umehifahiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete.

Naye Mkurugenzi wa  Chuo hicho Dkt. Ramadhani Marijani alitoa wito kwa wanachuo kuwa watulivu wakati Jeshi la Polisi likiendelea na uchunguzi wa sababu zilizopelekea mwanachuo huyo kuchukua maamuzi yaliyoacha simamazi sio tu kwa familia yake bali hata kwa Jumuiya nzima ya Uhazili.

Alisema kuwa ni vema kama kuna mwanachuo yoyote anakuwa na tatizo au msongo wa mawazo kuwaeleza viongozi wake wawe wa Serikali ya Wanafunzi, Mama Mlenzi, Mshauri wa Wanachuo au Mkurugenzi mwenye ili waweze kusaidia katika ushauri utakaowapa ufumbuzi kuliko kuchukua maamuzi ya haraka.

Mugabe hatokumbukwa kwa jema lolote



Wengi miongoni mwa watu walidhani kwamba njia pekee ya Robert Mugabe kukata tamaa ya kuwa rais ni kifo cha kawaida .

Huenda alifikiri hivyo pia.

Kama kiongozi mkongwe mwenye sera za viongozi wa miaka ya ukombozi ya 1970 na 80 wengi wasingelitarajia aachie madaraka kwa maandishi. Pengine hilo linamaanisha kitu fulani juu ya namna dunia imebadilika katika karne 21.

Kasri la rais halikushambuliwa, hakuna kumaliza mamlaka vibaya mikononi mwa umati wa watu kama ilivyokuwa kwa Kanali Gaddafi, hakuna mauaji kwa kufyatuliwa risasi kama rais Ceausescu wa Romania, hakunyongwa kama Saddam Hussein.

Licha ya yote Robert Mugabe aliyoyatenda ,zimbabwe ni taifa la amani na utulivu. Na licha ya uhalifu wote ambao anawajibika nao, amekuwa mtu mwenye akili kuliko mwizi katili.

Atakumbukwa kwa mauaji mabaya ya eneo la Matabeleland katika miaka ya 1980 , kwa uvamizi wa mashamba ya wazungu miaka ya 90 na baadae , na kwa mateso ya kikatili dhidi ya wapinzani wake wa chama cha Movement for Democratic Change (MDC) wakati walipoonekana kuelekea kushinda katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2008.

Mtu ambaye alionekana kukaribia kuchukua wadfa wake , makamu wa rais wa zamani nt Emmerson Mnangagwe, alihusika katika uhalifu huo kwa kiasi kikubwa , na bado watu nchini Zimbabwe - sawa na kwingineko duniani - bado wanahisi vema kumona mugabe akiondoka na watajaribu kusahau yote.

Wote wamesahau mambo yoote mazuru ambayo Robert Mugabe aliyafanya. Kwa mfano Zimbabwe ina kiwango cha juu zaidi cha wasomi kwasababu yake.

Lakini kwa bahati mbaya hilo halitakumbukwa.