Sunday, 19 November 2017

Mbowe kumnadi mgombea aliye mahabusu

Mbowe kumnadi mgombea aliye mahabusu



Wakati Mwenyekiti wa Chadema,  Freeman Mbowe akitarajiwa kuwahutubia wakazi wa Kata ya Mhandu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani, mgombea wa chama hicho, Godfrey Misana yupo mahabusu kutokana na kukabiliwa na shitaka la kujeruhi.

Katibu wa Chadema Mkoa wa Mwanza, Boniphace Nkobe  amesema Mbowe ameambatana na aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu.

Amesema mkutano huo pia utahudhuriwa na aliyekuwa mbuge wa Nyamagana, Ezekia Wenje na utafanyika saa kumi jioni.

Misana (46), mgombea udiwani wa Chadema katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Novemba 26,2017 na kampeni meneja wake, Charles Chinjibela (37) Ijumaa Novemba 17,2017 walipandishwa kizimbani wakidaiwa kumjeruhi meneja wa kampeni za CCM katika kata hiyo, Thomas Warioba.

Katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mwanza, mbele ya hakimu Ainawe Moshi wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 14,2017.

Akisoma mashtaka katika shauri hilo namba 540/2017, mwendesha mashtaka wa Jamhuri, Elizaberth Barabara alidai washtakiwa walitumia visu na mawe kumjeruhi Warioba.

Upande wa Jamhuri uliomba Mahakama kuzuia dhamana ya washtakiwa kwa kile ilichoeleza ni kwa usalama wao.

Ombi hilo la Jamhuri limepingwa na wakili wa utetezi, Gasper Mwanaliela.

Wakili Mwanaliela alisema dhamana ni haki ya wateja wake na kwamba, kuwanyima kutawazuia kushiriki kikamilifu katika kampeni za uchaguzi mdogo wa udiwani unaotarajiwa kufanyika Novemba 26,2017.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu Moshi alisema Mahakama itatoa uamuzi kuhusu dhamana Novemba 21,2017. Washtakiwa walipelekwa mahabusu


Profesa Lumumba awakingia kifua JPM, Kagame


MWANAZUONI maarufu barani Afrika, Profesa Patrick Lumumba, amesema Rais Dk. John Magufuli na Rais wa Rwanda, Paul Kagame si madikteta bali wanachokifanya ni kuhakikisha kunakuwa na siasa za miiko na maadili.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana katika Mkutano wa Pan African Humanitarian wa mwaka huu ulioandaliwa na Asasi ya Vijana ya Umoja wa Mataifa (Yuna) uliokuwa na kaulimbiu ya “amani inawezekana jana, sasa na kesho” na kuwakutanisha vijana kujadili nafasi zao katika kuleta amani barani Afrika.

Profesa Lumumba ambaye ni raia wa Kenya, alisema katika miaka ya hivi karibuni, wamekuja viongozi wenye mwelekeo na uchungu wa kuhakikisha mataifa yao yanaendelea, lakini baadhi ya wanasiasa wamekuwa wakiwaita madikteta.

“Tunapaswa kujua hawa watu tunaowaita madikteta ni akina nani, kwa sababu kuna viongozi wameibuka katika miaka mitatu hadi 20 iliyopita, wakiwa na mwelekeo na kuona uchungu wa kuhakikisha mataifa yao yanaendelea, lakini baadhi ya watu wengine wanawaita eti ni madikteta,” alisema na kuongeza:

“Lakini viongozi hao ni watu wazalendo na wakereketwa wa maendeleo endelevu, hivyo watu kama hawa lazima tujiulize mienendo yao ni ya kidikteta? Au ni ya kuhakikisha mataifa yao yanapiga hatua za haja na hoja. Mfano wengine wanasema Kagame, Dk. Magufuli ni dikteta, sikubaliani nao kwa sababu kile ambacho wanakifanya, wanajaribu kusema kwamba lazima kuwe na siasa za miiko na maadili.

“Nakubali kwamba udikteta ni jambo ambalo halistahili, lakini ni muhimu kuhoji kwamba uhuni ndiyo demokrasia? Kwa sababu kumeibuka wimbi la watu ambao ni wababaishaji hata sio wapinzani, kila kitu anachokifanya (rais) wao kazi yao ni kupinga.”

Akizungumzia suala la amani, hasa katika vipindi vya uchaguzi, alisema ni wakati wa kujiuliza ni aina gani ya uongozi inahitajika barani Afrika ili kuwe na njia ya kubadilisha uongozi isiyoleta vurugu tofauti na ilivyo sasa.

“Pia tunapaswa kuangalia hivi vitu tunavyoviita vyama, ni vyama kweli au ni vikundi tu, genge tu la vibarua waliokuja kujitafutia nyadhifa ili kupora mali za Waafrika. Vijana ndio wataibua hoja hii na kutathimini kuwa mataifa yetu tunayaandaa kwa minajili ya kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo,” alisema.

Pia alisema anaamini Afrika itakuja kuwa na amani na utulivu kwa sababu jitihada mahsusi zimeshaanza kufanywa na viongozi wake na tayari wamekwisha kutoa tamko kwamba kufikia mwaka 2020, lazima vitu vinavyoleta migogoro vitolewe na kila mtu anatakiwa kushiriki kwa nafasi yake.

Mtanzania


Zimbabwe: Chama cha Zanu-PF kimemfuta Mugabe kama kiongozi wake

Zimbabwe: Chama cha Zanu-PF kimemfuta Mugabe kama kiongozi wake


Chama tawala nchini Zimbabwe Zanu-PF kimefuta Robert Mugabe kama kiongozi wake.

Kimemtua aliyekuwa makamu wa rais Emmerson Mnangagwa ambaye alifutwa wiki mbili zilizopita kama kiongozi wake.

Kufutwa kwa Bw. Mnangawa kumezua mambo mengi huku jeshi likitwaa madaraka na kumzuia Mugabe 93, kumteua mke wake Grace kama makam wa rais.

Maelfu ya watu nchini Zimbabwe waliingia barabarani siku ya Ijumaa kuandamana kumpinga Bw. Mugabe.

Bw. Mugabe anatarajiwa kukutana na makanda wa jeshi na msafara wa magari umeonekana ukiondoka makao ya rais.

Mkuu wa chama chenye nguvu cha wale waliopigania uhuru Chris Mutsvangwa, aliiambia Reuters kuwa chama kilikuwa kinaanza mchakato wa kumuondoa Mugabe madarakani kama rais

Bifu la Ronaldo na Ramos lafikia mwisho

Bifu la Ronaldo na Ramos lafikia mwisho


KOCHA wa klabu ya mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Real Madrid, Zinedine Zidane, ameweka wazi kuwa nyota wake, Cristiano Ronaldo na nahodha Sergio Ramos, wamemaliza tofauti zao.

Uongozi wa klabu hiyo uliwakutanisha wachezaji hao juzi, kabla ya kuelekea katika mchezo wao dhidi ya Atletico Madrid kwenye Ligi Kuu nchini Hispania.

Sababu za wawili hao kuwa kwenye mgogoro ni baada ya Real Madrid kukubali kichapo cha mabao 3-1 dhidi ya Tottenham kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, Novemba 1, kwenye Uwanja wa Wembley, hivyo Ronaldo akatupia lawama kwa uongozi wa klabu hiyo kwa kudai kwamba, walifanya makosa makubwa kuwauza wachezaji wao, James Rodriguez na Alvaro Morata.

Kauli hiyo ya Ronaldo ilionekana kumchukiza sana Ramos na ndipo nahodha huyo alisema kuwa, Ronaldo ni mchezaji mbinafsi sana na hakupaswa kuongea kauli kama hiyo na alitakiwa kushirikiana na wenzake ili kuisaidia timu.

Hata hivyo, baada ya mgogoro huo kuwa mkubwa, Ronaldo aliweka wazi kuwa, hana mpango tena wa kuendelea kuwa na timu hiyo mara baada ya kumaliza mkataba wake.

“Ni wazi kwamba Sergio Ramos ni miongoni mwa wachezaji wenye akili sana ndani na nje ya uwanja, anaweza kumwambia kitu mchezaji yeyote hata kama ni Cristiano Ronaldo, isitoshe wachezaji hao wamekuwa pamoja kwa muda mrefu na wamezoeana.

“Mchezaji huyo alistahili kumwambia hivyo Ronaldo kutokana na kauli yake, lakini ukweli ni kwamba kila kitu kipo sawa kwa sasa, uongozi wa klabu uliamua kukaa pamoja na wachezaji hao kwa ajili ya kumaliza tofauti zao na kila kitu kinakwenda sawa sasa.

“Kwa pamoja naweza kusema nina wachezaji wawili kwenye kikosi ambao wanatengeneza historia ndani ya timu hii, wamekubali kumaliza tofauti zao ili kuweza kuipigania timu yao katika michezo inayofuata,” alisema Zidane.

Wababe hao wa soka barani Ulaya, msimu huu wanaonekana kuwa wameuanza vibaya kutokana na kiwango chao na ushindi wanaoupata, huku baadhi ya mshabiki wakidai kuwa, mshambuliaji wao huyo ambaye ana tuzo nne za Ballon d’Or, amekuwa kwenye kiwango cha chin

Diego Simeone: Griezmann anaweza kuondoka baada ya kuzomewa Jana



KOCHA Diego Simeone amedokeza kwamba Antoine Griezmann anayetakiwa na Manchester United, anaweza kuondoka Atletico Madrid.

Simeone amesema hayo baada ya kuulizwa mustakabali wa Griezmann kufuatia kuzomewa wakati Atletico Madrid ikilazimishwa sare ya 0-0 na Real Madrid jana katika La Liga.

Kocha huyo wa Atletico alimpumzisha mshambuliaji wake huyo Mfaransa kwa mara ya pili mfululizo kwenye mechi ya ligi na akazomewa kipindi cha pili wakati anakwenda benchi.

Simeone alisema: "Nyumbani nilifundishwa kwamba wakati mmoja wenu anapokuwa sehemu ya familia unapaswa kuwasimamia hadi kifo,".

Na kwa sababu mashabiki wa Atletico Madrid wamekwishaanza kuhisi siki za Griezmann zinahesabika kutokana na kutakiwa na United waliokaribia kumsajili msimu huu na Barcelona wanamtaka pia kwa mwakani.

Griezmann amefunga mabao mawili tu msimu huu katika mechi 10 alizocheza na Simeone amerudia mara mbili kusema katika mkutano na Waandishi wa Habari.

"Unamsapoti mtu hadi kifo hadi atakapokuwa si sehemu ya familia yako tena,".

Kiungo Saul amesema: "People wanatakiwa kumtetea. Greizman ni mchezaji wetu muhimu na tunatakiwa kumsapoti wakati wote,".

Dau la kumnunua Griezmann lilikuwa Euro Milioni 200 January mwaka huu, lakini litapungua hadi Milioni 100 msimu ujao.

Manchester United ilikaribia kumsajili msimu huu, lakini ikashindwa kutokana na Atletico Madrid kufungiwa kusajli mchezaji mpya hadi mwaka 2018.

Nyota ya Sane yazidi kung'aa Epl


Mshambuliaji wa klabu ya Manchester City, Leroy Sane, amefanikiwa kuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu nchini England wa Oktoba, baada ya kuisaidia timu hiyo kushinda michezo mitatu mfululizo mwezi huo.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21, amekuwa tegemeo kwenye kikosi cha kocha Pep Guardiola na amekuwa akipachika mabao mengi pamoja na kupiga pasi za mwisho katika michezo mbalimbali. Katika michezo mitatu ya Oktoba, ameweza kufunga kila mchezo na kutoa pasi ya mwisho.

Kutokana na mabao sita aliyoyafunga mchezaji huyo na kutoa pasi tano za mwisho ndani ya Ligi Kuu, mchezaji huyo ameingia kwenye orodha ya wachezaji wanaotengeneza nafasi nyingi msimu huu akiungna na mshambuliaji wake Sergio Aguero ambaye ana mabao nane na pasi tatu za mwisho.

Katika ushindi wa mabao 7-2 dhidi ya Stoke City, alifunga bao moja na kutoa pasi moja ya mwisho, huku ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Burnley, alifunga bao moja na kutoa pasi moja ya mwisho, sawa na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya West Brom.

Sane anakuwa mchezaji wa pili kutoka nchini Ujerumani kuchukua tuzo hiyo, huku mchezaji wa kwanza akiwa Jurgen Klinsmann, ambaye aliwahi kuichukua wakati anakipiga katika kikosi cha Tottenham, Agosti 1994.

Katika tuzo hiyo, Sane alikuwa anashindana na wachezaji watano ambao ni pamoja na mchezaji mwenzake wa timu hiyo, kiungo Kevin De Bruyne, beki wa klabu ya Arsenal, Nacho Monreal, Glenn Murray kutoka Brighton, kipa wa klabu ya Burnley, Nick Pope na nyota wa klabu ya Crystal Palace, Wilfried Zaha.

“Ninashukuru sana kwa ushirikiano ninaoupata kutoka kwa wachezaji wenzangu, ninaamini kwa hali hii tunaweza kufanya makubwa msimu huu, nawashukuru wote kwa sapoti,” alisema Sane.

Hata hivyo, kutokana na mchango wa Sane ndani ya Man City, amemfanya kocha wake, Guardiola na yeye kuchukua tuzo ya kocha bora wa Oktoba nchini England

Saturday, 18 November 2017

Video | Memo _ Hallelujah (COVER) DIAMOND PLATNUMZ FT MORGAN HERITAGE

Video | Memo _ Hallelujah (COVER) DIAMOND PLATNUMZ FT MORGAN HERITAGE



Irene Uwoya atua Rwanda kuhani msiba wa aliyekuwa mumewake

Irene Uwoya atua Rwanda kuhani msiba wa aliyekuwa mumewake


Mrembo wa zamani wa taji la Miss Chang’ombe na mwigizaji maarufu nchini, Irene Uwoya amewasili jijini Kigali, Rwanda kuhani msiba wa aliyekuwa mumewe, Ndikumana Hamad.

Ndikumana aliyekuwa akijulikana kama Katatut, alifariki dunia ghafla siku chache zilizopita na kuzikwa juzi jijini Kigali.

Uwoya hakuwa jijini Kigali wakati wa mazishi na usiku wa kuamkia leo ametua jijini Kigali akiongozana na mwanaye, Klishy ambaye alizaa na marehemu. Pia aliongozana na mama yake mzazi.

Uwoya alijifunika sura muda wote wakati akiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kanombe jijini Kigali.

Wakati anatua, ndugu wakiwemo mashabiki wa michezo na burudani, walijitokeza uwanjani hapo.

Kataut ambaye alicheza soka katika nchi kadhaa za Ulaya, mauti yalimkuta akiwa kocha msaidizi wa Rayon Sports na siku moja kabla ya kifo chake alikuwa mazoezini.

Kwa hapa nchini, Kataut aliwahi kuichezea Stand United kabla ya Kocha Patrick Liewig raia wa Ufaransa, kupendekeza aachwe

Mr Nice amvaa Dudud Baya


Msanii Mr Nice ambaye kwa sasa ameachia kazi yake mpya ya Yaya, amejibu tuhuma za msanii mwenzake Dubu Baya aliposema kwamba maisha yamemshinda na kukimbilia Kenya, na kumjibu kuwa Dudu Baya ni msanii asiyejielewa, ndio maana hana mahali pa kuishi.

Akizungumza na mwandishi wa East Africa Teleivison, Mr.Nice amesema ni wakati sasa Dudu Baya akomae na game kama anavyofanya yeye, kwani muda wa malumbano na kuchafuana hautamsaidia chochote, na hastahili kufanya hayo kwakuwa umri umeshamucha.

Mr. Nice ameendelea kwa kusema kwamba Dudu Baya ni mlevi na anaishi maisha ya kuigiza, hivyo kabla hajaanza kumuongelea vibaya ni vyema akaanza kujilinganisha naye kama wanafanana kimaisha.

Serikali yakarabati vyuo 10 vya ualimu



Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa 

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imetumia Sh11.9 bilioni kukarabati miundombinu ya kufundishia, kujifunzia na mabweni katika vyuo 10 vya ualimu nchini.

Amevitaja vyuo hivyo kuwa ni Morogoro, Mpwapwa, Butimba, Kasulu, Songea, Tukuyu, Marangu, Kleruu, Korogwe na Tabora.

“Ukarabati huu umewezesha wanachuo 5,920 waliokuwa wanasoma Stashahada maalumu ya Sayansi, Hisabati na Tehama katika Chuo Kikuu cha Dodoma -Udom kuhamishiwa katika vyuo hivyo,” amesema.

Waziri Mkuu Majaliwa alitoa kauli hiyo jana Ijumaa, Novemba 17,2017 bungeni mjini Dodoma wakati akitoa hoja ya kuahirisha mkutano wa tisa wa Bunge la 11 ambalo limeahirishwa hadi Januari 30, 2018.

Amesema ili kuongeza fursa za wanafunzi kusomea ualimu, Serikali imepanga kujenga na kukarabati vyuo vya ualimu vya Kitangali, Ndala, Mpuguso na Shinyanga kwa thamani ya Sh36.47 bilioni.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema mradi huo ambao utatekelezwa kwa miaka mitatu kuanzia 2016/17 hadi 2018/19, unalenga kuongeza fursa kwa wanafunzi wenye sifa kupata nafasi ya kujiunga na elimu ya ualimu.

“Ujenzi na ukarabati huu utasaidia kuongeza udahili katika vyuo vya ualimu vya Serikali kutoka wanachuo 20,535 katika mwaka 2017 hadi kufikia wanachuo 23,835 katika mwaka 2019, ikiwa ni ongezeko la wanachuo 3,300,” amesema.

Wakati huohuo, waziri mkuu amesema Serikali imeanza maandalizi ya awamu ya pili ya ukarabati wa vyuo saba vya ualimu vya Serikali.

Amevitaja vyuo hivyo kuwa ni Tandala, Nachingwea, Tarime, Kinampanda, Mandaka, Patandi na Ilonga.

Amesema vyuo vya ualimu vya Murutunguru, Kabanga na Mhonda vitalazimika kujengwa upya baada ya wahandisi kubaini kuwa vyuo hivyo havifai kukarabatiwa kutokana na uchakavu mkubwa wa majengo yake.

Afande Sele awapa makavu Bongo Movie


Msanii mkongwe wa muzuki wa kizazi kipya, Selemani Msindi marufu kwa jina la Afande Sele, ameweka wazi juu ya chuki aliyonayo kwa tasnia ya filamu bongo (bongo movie).

Akiongea na Planet Bongo ya East Africa Radio, Afande Sele amesema hawachukii wasanii wa bongo movie, bali huchukia tabia zao chafu ambazo zinaharibu Tasnia.

Afande Sele ameendelea kwa kusema kwamba wasanii wa bongo movie wana tabia chafu hasa za kuwanyanyasa wanawake kwa kuwatumikisha kingono, huku akimtolea mfano muigizaji Elizabeth Michael (Lulu) ambaye amefungwa.

Waziri Mkuu Canada Aijibu Serikali ya Tanzania Sakata la B



Wakati katibu mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano akiwa nchini Canada kushughulikia suala la ndege ya Bombardier, waziri mkuu wa nchi hiyo, Justin Trudeau amesema hawezi kuingilia uhuru wa mahakama ambayo anaamini itatenda haki.

Hivi karibuni Rais John Magufuli alisema amemwandikia barua waziri huyo mkuu wa Canada ili kujua hatima ya ndege hiyo.

Hata hivyo naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alisema jana kuwa hawezi kuzungumzia jambo hilo kwa sababu waziri mkuu yupo na wao hawajapata taarifa rasmi.

“Lakini kingine naomba utambue kuwa katibu mkuu bado yupo Canada, kwa hiyo mambo mengi mimi sijayapata hadi atakaporudi aje kutu-breaf kilichojiri huko,” alisema Nditiye.

Akizindua uwanja wa ndege mjini Bukoba, Novemba 6, Rais Magufuli alisema amemwandikia barua waziri mkuu wa Canada kumuomba kuachiwa kwa ndege hiyo na amemtuma mwanasheria mkuu wa Serikali, George Masaju kwenda nchini humo kushughulikia suala hilo.

Kwenye barua yake ya majibu ambayo yameripotiwa na gazeti la National Post la nchini humo, waziri mkuu wa Canada Trudeau amesema hana cha kufanya kwa kuwa shauri hilo lipo mahakamani.

“Ni bahati mbaya kwamba suala hili limechelewesha kuwasili kwa ndege hii. Serikali ya Canada haina uwezo wa kuingilia, ila tuna imani mahakama itaamua kwa weledi na haki,” amekaririwa akisema Trudeau katika gazeti hilo.

Ndege hiyo, Bombardier Q400-8 inashikiliwa kwa amri ya mahakama nchini humo kutokana na shauri lililopo kati ya Serikali na kampuni ya Stirling Civil Engineering.

Kampuni hiyo ilikuwa na mkataba wa ujenzi wa Barabara ya Wazo Hill – Bagamoyo ambao ulivunjika kabla haujakamilika, hivyo ikaamua kukimbilia kwenye Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa ambako ilishinda kesi. Baada ya kushinda kampuni hiyo ilipewa kibali cha kukamata mali za Tanzania katika nchi za Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ubelgiji, Uganda na Canada.

Kwa miezi mitatu sasa, mahakama nchini Canada inaendelea kuishikilia ndege hiyo iliyonunuliwa kwa Dola 32 milioni za Marekani (zaidi ya Sh70.4 bilioni) kwa niaba ya kampuni ya Stirling inayoidai Serikali Dola 28 milioni (zaidi ya Sh61.6 bilioni) ambazo ni thamani ya mkataba uliovunjwa pamoja na riba.

Ndege hiyo ni miongoni mwa zile ambazo Rais Magufuli aliahidi kununua ikiwa ni mikakati ya kulifufua Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Awali, ndege hiyo litarajiwa kuwasili nchini mwezi Julai, lakini hilo halikufanyika na Agosti 18, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, mwanasheria mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alisema ndege hiyo imekamatwa nchini Canada na inaweza kupigwa mnada kutokana na deni ambalo Serikali inadaiwa na kampuni hiyo yenye makao yake Montreal, Canada.

Agosti 19, Serikali ilifanya mkutano na wanahabari kukanusha taarifa hizo, lakini ilikiri kuwapo mgogoro na kampuni hiyo.

Aliyekuwa kaimu mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Zamaradi Kawawa alisema mgogoro kuhusu ndege hiyo upo na kimsingi umetengenezwa na Watanzania ambao kwa bahati mbaya wameweka masilahi ya kisiasa na ya binafsi mbele zaidi ya masilahi ya Taifa.

Alisema Serikali ilikuwa imeanza majadiliano ya kidiplomasia kwa ajili ya kulimaliza suala hilo. Kwa sasa, ATCL inamiliki ndege mbili mpya aina ya bombardier zilizoingia nchini Septemba 2016, na imeagiza ndege nyingine tatu za aina hiyo na Boeing Dreamliner moja.

Akizungumzia mafanikio ya miaka miwili ya Rais John Magufuli hivi karibuni msemaji mkuu wa Serikali, Hassan Abbasi alisema mpaka Juni mwakani ndege zote zitakuwa zimewasili nchini.

Mbowe Awataka Viongozi wa Dini Wasione Aibu Kuikosoa Serikali




Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewataka viongozi wa dini kupaza sauti kukemea maovu ili kuiokoa nchi katika kilio.

Mbowe  alisema hayo jana wakati wa ibada ya kumuaga marehemu mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Hai, Looka Mushi iliyofanyika katika Usharika wa Nkwarungo.

“Dunia yetu imejaa uovu, sisi ambao tuko kwenye siasa tunatambua nguvu ya viongozi wa kiroho, kauli yao moja kukemea uovu inatingisha nchi nzima,” alisema Mbowe. “Semeni tunatambua tangu enzi mmekuwa mkikemea maovu na ‘kui-shape’ nchi, msione aibu kuwakemea viongozi waovu.

“Viongozi wa dini msiingize roho ya uoga, mtaiponya nchi, mkikaa kimya nchi itakufa, nchi inateketea, nchi inaangamia viongozi msikae kimya watu wanauawa.

“Itafika kipindi kwa kiburi cha madaraka wataamrisha baba askofu alale rumande kwa mfano, Mungu akunusuru sana Baba Askofu Dk Frederick Shoo atakapoambiwa alale ndani ndiyo utakuwa ukombozi wa Taifa letu Bwana Yesu asifiwe,” alisema Mbowe.

Kwa upande wake, Askofu Shoo alisema viongozi wa dini waache unafiki na waige mwenendo wa Mchungaji Mushi.

“Watumishi wengi ni wanafiki, hivyo waache unafiki na kuwa na rangi mbilimbili muige mwenendo wa mchungaji Mushi,” alisema Dk Shoo.

Askofu mstaafu Erasto Kweka alisema matendo mema yaliyotangauliza neno la Mungu ndiyo silaha ya kweli ya kila binadamu.

Alisema jambo muhimu ni kuishi kwa kuangalia waliofanikiwa katika imani walifanya nini.

“Leo tunamuaga mpendwa wetu, anayesifiwa na kila mmoja kutokana na kutukuka kwa matendo yake mema, tutafakari na kutenda kwa kumpendeza Mungu kama alivyofanya Mchungaji Mushi,” alisema Kweka.

Muhubiri katika ibada hiyo, Mchungaji Lewis Hiza alisema watu wanashangaa kwa nini alikuwa na urafiki na Mchungaji Mushi.

“Jibu ni kuwa wazee wanaozeeka vizuri, huwa na urafiki na vijana ili kuwaachia yaliyo mema na neno alilokuwa akiniambia kila siku nishike neno kwa sababu litaniweka pazuri na litakuwa majibu ya kila swali,” alisema Hiza.

Akisoma wasifu wa marehemu, katibu mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Arthur Shoo alisema Mchungaji Mushi alipata tatizo la mapafu mwaka 2008 na kupata matibabu katika hospitali mbalimbali.

Alisema mwaka 2014 aliugua na kufanyiwa upasuaji na kutolewa uvimbe tumboni katika Hospitali ya Manipal Bangalore nchini India.

“Pia mwaka huohuo alifanyiwa upasuaji wa kuondoa tezi dume. Mwaka 2015 alirudi tena India kwa uchunguzi, alionekana anaendelea vizuri japokuwa aliendelea kusumbuliwa na tatizo la mapafu ambalo mzizi wa tatizo ulianza kwenye ugonjwa wa pafu mpaka alipofariki Ijumaa iliyopita,”alisema Shoo