Saturday, 18 November 2017

Mbowe Awataka Viongozi wa Dini Wasione Aibu Kuikosoa Serikali




Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amewataka viongozi wa dini kupaza sauti kukemea maovu ili kuiokoa nchi katika kilio.

Mbowe  alisema hayo jana wakati wa ibada ya kumuaga marehemu mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Hai, Looka Mushi iliyofanyika katika Usharika wa Nkwarungo.

“Dunia yetu imejaa uovu, sisi ambao tuko kwenye siasa tunatambua nguvu ya viongozi wa kiroho, kauli yao moja kukemea uovu inatingisha nchi nzima,” alisema Mbowe. “Semeni tunatambua tangu enzi mmekuwa mkikemea maovu na ‘kui-shape’ nchi, msione aibu kuwakemea viongozi waovu.

“Viongozi wa dini msiingize roho ya uoga, mtaiponya nchi, mkikaa kimya nchi itakufa, nchi inateketea, nchi inaangamia viongozi msikae kimya watu wanauawa.

“Itafika kipindi kwa kiburi cha madaraka wataamrisha baba askofu alale rumande kwa mfano, Mungu akunusuru sana Baba Askofu Dk Frederick Shoo atakapoambiwa alale ndani ndiyo utakuwa ukombozi wa Taifa letu Bwana Yesu asifiwe,” alisema Mbowe.

Kwa upande wake, Askofu Shoo alisema viongozi wa dini waache unafiki na waige mwenendo wa Mchungaji Mushi.

“Watumishi wengi ni wanafiki, hivyo waache unafiki na kuwa na rangi mbilimbili muige mwenendo wa mchungaji Mushi,” alisema Dk Shoo.

Askofu mstaafu Erasto Kweka alisema matendo mema yaliyotangauliza neno la Mungu ndiyo silaha ya kweli ya kila binadamu.

Alisema jambo muhimu ni kuishi kwa kuangalia waliofanikiwa katika imani walifanya nini.

“Leo tunamuaga mpendwa wetu, anayesifiwa na kila mmoja kutokana na kutukuka kwa matendo yake mema, tutafakari na kutenda kwa kumpendeza Mungu kama alivyofanya Mchungaji Mushi,” alisema Kweka.

Muhubiri katika ibada hiyo, Mchungaji Lewis Hiza alisema watu wanashangaa kwa nini alikuwa na urafiki na Mchungaji Mushi.

“Jibu ni kuwa wazee wanaozeeka vizuri, huwa na urafiki na vijana ili kuwaachia yaliyo mema na neno alilokuwa akiniambia kila siku nishike neno kwa sababu litaniweka pazuri na litakuwa majibu ya kila swali,” alisema Hiza.

Akisoma wasifu wa marehemu, katibu mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini, Arthur Shoo alisema Mchungaji Mushi alipata tatizo la mapafu mwaka 2008 na kupata matibabu katika hospitali mbalimbali.

Alisema mwaka 2014 aliugua na kufanyiwa upasuaji na kutolewa uvimbe tumboni katika Hospitali ya Manipal Bangalore nchini India.

“Pia mwaka huohuo alifanyiwa upasuaji wa kuondoa tezi dume. Mwaka 2015 alirudi tena India kwa uchunguzi, alionekana anaendelea vizuri japokuwa aliendelea kusumbuliwa na tatizo la mapafu ambalo mzizi wa tatizo ulianza kwenye ugonjwa wa pafu mpaka alipofariki Ijumaa iliyopita,”alisema Shoo

No comments:

Post a Comment