Timu ya Real Madrid inaripotiwa wamefikia makubaliano na staa wa Paris Saint-Germains, Neymar, ili akajiunge nayo ifikapo mwishoni mwa msimu ujao.
Mbrazili huyo amekuwa mchezaji ghali zaidi duniani majira ya joto msimu huu baada ya kuhamia PSG akitokea Barcelona kwa uhamisho wa pauni milioni 200.
Licha ya kuanza vizuri msimu huu akiwa na PSG baada ya kufunga mabao 15 na kutoa pasi zilizozaa mengine 11 katika mechi 18 tu, tetesi zimeibuka zikidai kuwa Neymar hana furaha kamili katika mazingira yake mapya.
Ripoti kutoka kwenye chanzo cha habari nchini Hispania Diario Gol, zinadai kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amekubaliana na Real Madrid na anatarajiwa kutua Bernabeu mwishoni mwa msimu wa 2018-19.
“Neymar anatamani sana kushinda tuzo ya Ballon d’Or na anaamini kuwa atakuwa na nafasi nzuri kutimiza ndoto zake akiwa katika Jiji Kuu la Hispania,” kilieleza chanzo hicho.
Manchester United na Manchester City pia zinasemekana zinavutiwa na mchezaji huyo, ambaye mkataba wake Parc des Princes utafika ukomo mwaka 2022.
No comments:
Post a Comment