Saturday, 16 December 2017

Balozi alnajem amkabidhi diwani bharwani wa vigwaza vifaa vya mil. 4.5



Na Omary Mngindo, Vigwaza
BALOZI wa Kuwait nchini Tanzania Jasem Alnajem amemkabidhi Diwani wa Kata ya Vigwaza Halmashauri ya Chalinze Alhaj Mohsin Bharwani mabeseni 100 yenye thamani ya sh. Mil. 4.5 yatayotumika kwa wajawazito wataofika kujifungulia kwenye Zahanati iliyopo Kijiji cha Vigwaza.
Mabeseni hayo yenye sabuni, poda na vifaa vyote muhimu kwa ajili ya matumizi ya mtoto anayezaliwa ni sehemu ya vifaa ambavyo mpango wake ulizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Hassani Suluu kwa kushirikiana na Ubalozi huyo wa Kuwait.
Akizungumza na wananchi hao, Balozi Alnajem kwanza alielezea furaha yake ya kufika Vigwaza kukutana na wakazi hao, pia ameangalia madhari ya eneo hilo huku akisema kuwa kufika kwake Vigwaza kumetokana na juhudi za Diwani huyo kumtafuta ofisini kwake kisha kumwelezea changamoto zinazowakabiri wananchi waishio Kijiji cha Vigwaza na Kata hiyo kwa ujumla.
Aliongeza kuwa amefika Vigwaza lengo kusaidia Mama na mtoto na wananchi si kujitangaza na kuwa hatua hiyo imetokana na kuguswa na changamoto alizoelezwa na Diwani wao, pia ataendelea kusaidi sekta ya afya na elimu huku akisisitiza misaada iwafikie walengwa wa mpango huo na kuwa uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Kuwait utaendelezwa kwa maslahi ya nchi na watu wake.
Kwa upande wake akizungumza baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo, Bharwani alianza kwa kumsukuru Balozi kwa msaada huo unaolenga kuwasaidia mama wajawazito wanaojifungulia katika Zahanati hiyo huku akisema utakuwa msaada walengwa wanaofika kwa ajili ya kupata huduma hiyo na kwamba anaimani vitatumika kama malengo yalivyokusudiwa.
"Mabeseni haya mabeseni 100 yatawasaidia wajawazito kabla ya kujifungua na baada ya kujifungua vyote vinagharimu kiasi cha sh. Mil. 4.5, hii ni sehemu ya mpango uliozinduliwa na Makamu wa Rais Mama Samia Hassan Suluu kwa kushirikiana na Ubalozi wa Kuwait hapa nchini nasi Vigwaza tumeambulia msaada huu" alisema Bharwani.
Aidha Diwani huyo aliongeza kuwa mbali ya vifaa hivyo pia Balozi kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu amezindua mpango mwingine unayogusa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), miguu, mikono pamoja na wasioona ambapo amekabidhi miwani, magongo, baskeli yenye mataili manne pamoja na mafuta kwa wenye ulemavu wa ngozi vyote vikiwa na thamani ya sh. Mil. 13.
"Nilipokutana na Balozi nilimgusia mambo mbalimbali yakiwemo sekta za maji, afya pamoja na elimu ambazo sisi wana-Vigwaza bado tunauhitaji mkubwa wa huduma hizo kutoka kwa wadau, katika kufanikisha hili la leo namshukuru sana ndugu yangu Muna amenipatia ushirikiano mkubwa, asingekuwa yeye nisingeonana na Balozi," alisema Diwani huyo.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo Thomas Mollel alielezea shukrani zake kwa Balozi huyo kwa kuona umuhimu wa kufika ndani ya wilaya hiyo huku akisema misaada hiyo itatumika kama ilivyokusudiwa huku akiwaomba wataosimamia zoezi hilo kuhakikisha wanalitekeleza kwa walengwa na si vinginevyo.

No comments:

Post a Comment