Wednesday, 13 December 2017

Mama Mjamzito ajifungulia kichakani


MKAZI wa Kijiji cha Ibondo, Kata ya Ludete, wilayani Geita, Ester Balele, amelazimika kujifungulia kwenye kichaka hatua chache kutoka kwenye nyumba anayoishi mkunga wa zahanati ya Ibondo, baada ya kukosa huduma kwa wakati.


Akizungumza na gazeti hili kijijini hapo, Balele alisema alikutwa na hali hiyo Novemba 29, majira ya saa 12.30 alfajiri alipo kwenda katika zahanati hiyo kujifungua na mkunga kugoma kufungua mlango.

Alisema kuwa siku hiyo majira ya saa tisa usiku akiwa amelala nyumbani kwake alipata dalili ya uchungu na kuamua kwenda kumuamsha mama mkwe na shemeji yake ili wampeleke zahanati akajifungue,  lakini baada ya kufika kwenye zahanati hiyo mkunga huyo aligoma kufungua licha ya kugongewa mlango mara kadhaa.

Alisema waliamua kumgongea mkunga huyo kwenye nyumba anayolala baada ya kukuta zahanati imefungwa.

Alisema ilipofika majira ya saa 12.30 alfajiri wakati wanaendelea kumgongea, hali ya uchungu ilizidi akalazimika kusogea kwenye kichaka ili ajifungue na alipomaliza mkunga huyo alitoka nje na kuwahoji kwa nini wanamsumbua usiku na kudai wanataka kumvamia.

Mkunga wa zahana hiyo, Aloyce Emmauel katika mahojiano na gazeti hili, amekiri kugoma kufungua mlango akihofia usalama wake huku akionyesha waandishi wa habari eneo la kichaka alipojifungulia mwanamke huyo .“Ni kweli nilisikia watu wanagonga mlango sikuweza kufungua kwa wakati huo, ilipofika majira ya saa 12.30 nilifungua mlango nikawakuta watu watatu nje wakiwa na mwanamkemmoja akihangaika kujifungua wakati narudi ndani kuchukua vifaa ghafla akawa amejifungua mtoto wa kiume,” alisema mkunga huyo.

Hata hivyo, zahanati hiyo kwa muda mrefu imekuwa ikilalamikiwa na wananchi kwa lugha chafu kwa wagonjwa, kufanya kazi kwa mazoea na huku wakidaiwa kujihusisha na rushwa.

Wakati mkunga akikiri kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Geita, Solomon Shati, amekanusha kuwapo kwa mwanamke aliyejifungulia nje.

“Sijafika eneo la tukio, lakini nimewasiliana na mkuu wa zahanati ya Ibondo, Asteria Chekanabo, amesema hakuna mwanamke mjamzito aliyejifungulia kichakani,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mwalimu Hermani Kapufi, alipotafutwa kuelezea tukio hilo, ofisi yake imedai kuwa yuko safarini kikazi.

Source: Nipashe


No comments:

Post a Comment