Baada ya kuhojiwa na Idara ya Uhamiaji kuhusu uhalali wa uraia wake Askofu wa Jimbo la Ngara - Rulenge, Severine Niwemugizi ameeleza kwamba amezungumza na Rais John Magufuli.
Askofu Niwemugizi akizungumza na Mwananchi kwa simu jana kujua kile walichozungumza na Rais Magufuli hasa baada ya kuandika ujumbe wa kumpongeza Rais kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Facebook, kiongozi huyo wa kiroho alisema, “Ni kweli leo (jana) nilizungumza na Rais Magufuli, alinipigia simu na tumekuwa tukiwasiliana kujuliana hali.”
Jana, askofu huyo alikaririwa akisema amehojiwa mara mbili na Uhamiaji katika kile kinachoelezwa ni utata wa uraia wake huku akieleza kuwa amezaliwa wilayani Biharamulo mkoani Kagera.
Alipoulizwa kama mazungumzo hayo ni baada ya taarifa za kuhojiwa na Uhamiaji, Askofu Niwemugizi alijibu huku akianza kwa kucheka, “Hahahahaha!! Ni kweli Rais kataka kujua hasa kuna nini, yeye amesema atalifuatilia na kukiwa na... nitamfahamisha.”
Askofu huyo ambaye Septemba mwaka huu aliibua mjadala wa Katiba Mpya na kusema kuwa yuko tayari kuitwa mchochezi endapo kundi la watetezi wa haki za binadamu watachukuliwa kama wachochezi alisema kuhojiwa huko hakutamrudisha nyuma katika misimamo yake, “Siwezi kurudi nyuma, nimetumwa na Kristo, Nabii anaweza kupendwa au kuchukiwa na mimi siwezi kunyamaza.”
Askofu Niwemugizi aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) alisema, “Mimi nazungumza lakini kuna Watanzania wengine wanazungumza sana. Lakini mimi kuhojiwa mara mbili hakutaninyamazisha.”
Ujumbe aliouweka Facebook, unasema, “Nasali Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo haki, uniokoe na mtu wa hila asiye haki. Kwa kuwa wewe ndiwe Mungu uliye nguvu zangu; kwa nini umenitupa?
Kwa nini ninakwenda nikihuzunika, adui wakinionea? ...Nafsi yangu, kwa nini kuinama, na kufadhaika ndani yangu? Umtumaini Mungu; kwa maana nitakuja kumsifu, aliye afya ya uso wangu na Mungu wangu” (Zab 43:1-2,5). Asante Rais wangu JPM kwa faraja uliyonipa.”
Wakichangia ujumbe huo, Deusdedit Mwombeki alisema “Amina Baba Askofu Severine Niwemugizi kwa ujumbe wako wa faraja nami umenigusa. Pole sana na hongera kwa faraja uliyopewa na Rais Magufuli.”
Prosper Mallya alisema, “Kweli humuweka mtu huru, kiongozi hukutana na misukosuko ila kwa kuwa wewe unawasemea wanyonge na Roho wa Bwana yu nawe, hutaogopa wala hutarudi nyuma. Mwenyezi akutie Roho wa hekima na akili uendelee kunena yale unayoona ni kwa manufaa na ustawi wa taifa letu.”
Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania, Askofu David Mwasota akizungumzia kitendo cha Uhamiaji kumhoji askofu huyo alisema kila nyakati na utendaji wake kikubwa ni kuliombea Taifa.
“Serikali ina macho na taarifa nyingi na labda inajua kwa nini inamhoji, lakini kwa heshima ilibidi hata taarifa zake zisijulikane...” alisema Askofu Mwasota na kuongeza:
“Tunawapa pole wenzetu wa Kanisa la Katoliki na tunawaomba kila mtu kwa nafasi yake tuliombee Taifa… lakini tuelewe kipindi hiki ni tofauti na kile cha Jakaya Kikwete.”
Mwananchi lilipomtafuta Rais wa TEC, Askofu Tarcisius Ngalalekumta kujua hatua ambazo baraza lake imechukua alisema “Kwanza ndiyo nasikia kutoka kwako, lakini kanisa linajiongoza, Serikali kama kuna kitu inakitafuta hatuwezi kuizuia.”
Ngalalekumtwa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Iringa alisema “Hilo sisi halina tatizo, Kanisa Katoliki halina mipaka, kuna maaskofu kutoka nchi mbalimbali.”
Source: Mwananchi
No comments:
Post a Comment