Na. Ahmad Mmow. WAZIRI wa nishati, Merdard Kalemani jana aliwajia juu watendaji wa TANESCO kanda ya kusini. Huku akikataa kupokea taarifa ya meneja wa wakala wa umeme vijijini(REA), mkoani Lindi, Jackson Lawuo, nakumtaka naibu mkurugenzi mkuu wa TANESCO amchukulie hatua meneja wa TANESCO mkoa wa Lindi.
Kalemani alifikia uamuzi huo kutokana na kutoridhirishwa na hali ya mambo na utendaji wa shirika hilo katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Miongoni mwa sababu zilizosababisha akatae kupokea taarifa ya meneja wa wakala wa umeme vijijini ni kuchelewa kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijijini katika awamu ya tatu mkoani humu.
Kuhusu meneja wa TANESCO mkoa wa Lindi, Johnson Mwigune, waziri Kalemani amemuagiza naibu mkurugenzi mkuu wa TANESCO amchukulie hatua meneja huyo kutokana na kutoridhirishwa na utendaji wake. Hasa kwakushindwa kutoa taarifa kwa wakati kwa waziri mwenye dhamana ya nishati kuhusu hali ya umeme na kuchelewa kuanza utekelezaji wa mradi wa usambazaji umeme vijiji awamu ya tatu.
Waziri huyo licha ya kumuagiza naibu mkurugenzi huyo, lakini pia alimtaka meneja huyo ahakikishe anamsimamia mkandarasi wa usambazaji umeme vijijini aharakishe zoezi la usambazaji. Huku akiagiza utekelezaji wa mradi huo uanze ndani ya mwezi huu katika vijiji Vilivyopo kwenye mpango huo.
Waziri Kalemani aliyetoa maagizo hayo jimboni Mtama wilaya ya Lindi ameutaka pia uongozi wa TANESCO kanda ya kusini uhakikishe unarekebisha miundombinu ya umeme ndani ya siku tatu. Ikiwamo nguzo za umeme. Akibainisha kuwa tatizo la nguzo linachangia kukosekana upatikanaji umeme kwa uhakika katika baadhi ya maeneo. Japokuwa mashine zakufua umeme zimetengenezwa.
"Umeme unakatika mara kwa mara licha ya mashine kukarabatiwa nakuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 15.8 ambazo zingekidhi mahitaji ya mikoa hii ya Lindi na Mtwara, "alisema Kalemani.
Awali mkuu wa mkoa Lindi, Godfrey Zambi katika taarifa yake kwa waziri huyo alieleza kutoridhishwa na utoaji taarifa sahihi za hali ya upatikanaji umeme mkoani humu. Huku tatizo la umeme likiendelea kuwaathiri wananchi, taasisi za umma nakukwamisha shuguli za maendeleo na kiuchumi mkoani humu.
No comments:
Post a Comment