Saturday, 16 December 2017

Zitto Kabwe ahoji kuhama kwa makada Wa ACT



Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ametumia hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha Kamati Kuu kuzungumzia wimbi la kuhama kwa makada wa chama hicho, akihoji iwapo kimeanza kupoteza mwelekeo.
Katika hotuba yake leo Jumamosi Desemba 16,2017, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini amewataka wajumbe wa kamati hiyo kujiuliza maswali magumu, likiwemo la kwa nini hali hiyo inakikumba chama chao.
Makada wa chama hicho waliojiunga na CCM ni Profesa Kitila Mkumbo aliyeachia nafasi ya ushauri wa ACT –Wazalendo baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho; wakili Albert Msando, Samson Mwigamba na Edna Sunga.
Katika hotuba hiyo, Zitto amesema hamahama hiyo imezua taharuki kwenye chama hicho na kuacha maswali juu ya kinachoendelea katika siasa za Tanzania.
“Ni lazima tujiulize maswali magumu sisi wenyewe na kuzungumza tukitazamana machoni, je hakuna sababu za ndani sisi wenyewe zinazokimbiza wanachama wetu? Kama zipo ni zipi? Je ni sababu ambazo tunaweza kurekebisha na kukiimarisha chama," amehoji Zitto.
Amesema, "Kama ni sababu zilizo nje ya uwezo wetu tunafanya nini ili kuzikabili, je bado sisi tunaamini katika misingi ya chama kwa mujibu wa Azimio la Tabora? Tulikuwa kundi tu tulioumizwa na vyama tulivyokuwamo na tukaamua kuunda chama kupoza hasira zetu tu na sasa hasira zimeisha hakuna sababu ya chama kuwapo."
Amesema kati ya waanzilishi watatu wa ACT, wawili wamekikimbia na kujiunga na CCM na kwamba, jambo hilo huenda likarutubisha hoja kuwa chama hicho kilikuwa mradi wa chama tawala, kwamba sasa hauna maana tena.

No comments:

Post a Comment