Thursday, 28 December 2017

Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB atangaza kujiuzulu


MTENDAJI Mkuu wa CRDB Bank, Dr Charles Kimeo, leo ametangaza kustaaafu ifikapo Mei 2019. Dkt. Kimei aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kwamba hatua hiyo ni kwa ajili ya kuanzisha mchakato wa Bodi ya Wakurugenzi wa benki hiyo kupata mtu atakayeshika nafasi yake kwa mujibu wa taratibu na kanuni zilizopo.

Kabla ya kujiunga na benki hiyo, Dk Kimei alifanya kazi Benki Kuu ya Tanzania kama Mkurugenzi Mfawidhi wa Shughuli za Benki, Mkurugenzi wa Sera, Uchumi na Utafiti, Meneja wa Idara ya Utafiti wa Uchumi na Sera na nyadhifa nyingine mbalimbali katika Idara ya Utafiti. Hivi sasa ni Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki Mabenki nchini.

Amewahi pia kufanya kazi katika bodi mbalimbali ikiwemo ya Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi na Kijamii (ESRF), Mamlaka ya Elimu nchini, Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kampuni ya Huduma za Mikopo Midogo ya CRDB na tawi la CRDB nchini Burundi.

Dkt. Kimei ana Shahada ya Uzamivu katika Uchumi aliyoipata Chuo Kikuu cha Uppsala cha Sweden, Shahada ya Uzamili katika Uchumi aliyoipata Chuo cha Uchumi cha Stockholm na Shahada ya Sayansi (Uchumi) aliyoipata Chuo Kikuu cha Taifa cha Moscow.


Baada ya kuwashuku wachezaji kuiba blanketi, shirika la Ndege lawaomba radhi


Shirika la American Airlines limewaomba msamaha wachezaji wawili wa mpira wa kikapu ambao walifukuzwa kutoka kwa ndege kwa kuwashuku kuiba.

Marquis Teague na Trahson Burrell waliabiri ndege hiyo siku moja kabla ya krismasi wakielekea kucheza mechi.

Lakini kabla ya ndeye kuondoka uwanjani, mhudumu mmoja wa ndege alidai kuwa wanaume hao walikuwa mablanketi kutoka upande wa kifahari wa ndege ambapo walilazimishwa kushuka kutoka kwe ndege hiyo.

Baadaye ilibainika kuwa ni abiria walikuwa wamewapa mablanketi hayo.

Wachezaji hao wote walikuwa wa asilia ya Afrika akiwemo mhudumu wa ndege.

Hakuna mchezaji kati ya hao wanaochezea timu ya Memphis Hustle amezungumzia kisa hicho.

Laiki naibu kocha wa Hustle, Darnell Lazere aliandika katika twitter kuwa kitendo hicho kilichochewa na ubaguzi wa rangi.

Wachezaji walikuwa wakisafiri kutoka uwanja wa Dallas-Fort Worth kwenda Sioux Falls, South Dakota wakitumia ndege ya Envoy Air iliyo sehemu ya American Airlines.




Nikki wa Pili atupa dongo hili



 Msanii Nikki wa Pili ambaye ni miongoni mwa wasanii wachache wanaofanya uchambuzi wa masuala mbali mbali ikiwemo uchumi wa taifa, ametupa jiwe gizani kuhusu sera mpya ya viwanda.

Kupitia ukurasa wake wa twitter Nikki wa Pili ameandika ujumbe kuhusu sera mpya ya Tanzania ya viwanda inayotekelezwa na serikali ya awamu ya tano, na kusema kwamba ni vyema tukajitafakari kwa hili kwani nchi ambazo zimefanikiwa, zilitumia mfumo wa ruzuku na sio wawekezaji pekee.

"Kupitia ruzuku ya serikali, na ulinzi dhidi ya ushindani wa kisoko kwa miaka 40 ndipo Japan wakafanikiwa kuisimamisha secta ya viwanda vya magari, sasa tunao hubiri Tanzania ya viwanda kupitia wawekezaji na ushindani wa kisoko tujitafakari",ameandika Niki wa Pili.

Sasa hivi Tanzania inapambana kuleta mapinduzi ya viwanda ili nchi iweze kuzalisha vitu vingi yenyewe bila kuagiza nje, huku ikitoa fursa kwa wawekezaji mbali mbali kuja nchini kuwekeza kwenye sekta ya viwanda.




Lissu huenda akakaa hospitali miezi sita zaidi


Dar es Salaam. Siku moja baada ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kusimama kwa mara ya kwanza tangu Septemba 7, amesema huenda akakaa hospitalini kwa miezi sita zaidi.

Juzi, Lissu anayepata matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alisimama kwa msaada wa madaktari.

Akijibu swali ni lini atarejea nchini na kama atasafiri nje ya Afrika kwa matibabu zaidi aliloulizwa jana na mwandishi wetu, Lissu alisema, “Ndio kwanza nimesimama jana (juzi), kuna miezi sita ya ‘rehabilitation’ (kumrudisha katika hali ya kawaida). Madaktari waliniambia kuna miezi sita au tisa.”

“Kwanza nimesimama kwa mara ya kwanza uamuzi wa je, nitamalizia hapa au nitakwenda bado, itategemea ushauri wa madaktari na kisha majadiliano na familia kwa sasa bado sijajua.”

Tangu mwanasheria huyo mkuu wa Chadema aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi akiwa katika makazi yake Area D mjini Dodoma Septemba 7, hakuwahi kusimama na wakati wote alikuwa akionekana amelala au amekaa hadi juzi.

Katika picha iliyomwonyesha Lissu akiwa amesimama, madaktari wawili walimshika huku mmoja akiurekebisha mguu wake wa kulia.

Lissu alituma ujumbe kwa wapigakura wa Singida Kaskazini akisema; “Wajiandae kwa mapambano makubwa ya kisiasa… kila mmoja atimize wajibu wake na kuacha visingizio.”

Akizungumzia hatua ya Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kusimama, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema, “Ni jambo la kumshukuru Mungu, tulikuwa tunapigania mwenzetu asimame, tunamshukuru Mungu kwa hatua hii.

“Itachukua muda kidogo ili aweze kurejea katika hali yake, lakini tumshukuru sana Mungu kwa kutupa Lissu, lakini tuwashukuru sana madaktari waliomuuguza na hili ni funzo kwetu,” alisema.

Alipoulizwa iwapo wanamkumbuka Lissu katika harakati zake, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema, “Kila kiongozi ana wajibu wake wa kiharakati, uongozi si shule unakwenda kujifunza, kila mmoja ana vipawa vyake, wengine ni wazuri katika kuhoji, wengine katika mikutano ya hadhara, wengine mikakati na kila mmoja ana wajibu wake.

“Lissu ni moja ya wanasiasa makini na mahiri hasa linapokuja suala la kuhoji, amekuwa msaada mkubwa katika kambi ya upinzani bungeni na zaidi katika masuala ya sheria na Mahakama, kila mmoja anajua hivyo, kwa hiyo ni kweli tunaposema ‘tumemmisi’ ni kweli tumemmisi sana,” alisema.

Mbowe alisema, “Tunawashukuru Watanzania walio wengi walioshiriki kumuuguza Lissu, kumwombea, kutoa michango na salamu zao hadi amefikia hatua ile ambayo wengi hawakutegemea.Tunawashukuru viongozi wa dini na watu waliomwombea kamanda wetu aweze kupona.”



Sakata la Airtel, Wafanyakazi TTCL wajitosa


Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Huduma za Mtandao wa Mawasiliano Tanzania (Tewuta) kimepongeza hatua ya Rais John Magufuli kumtaka Waziri wa Fedha kuanza uchunguzi kubaini ukweli kuhusu ubinafsishwaji wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL).

Katibu Mkuu wa Tewuta, Junus Ndaro amesema chama hicho kinatambua fika kuwepo mchezo mchafu uliosababishwa na Watanzania wachache wenye uchu wa fedha wakisaidiana na wawekezaji kupora rasilimali hiyo ya Taifa.

Ndaro amesema leo Alhamisi Desemba 28,2017 kuwa, kwa muda mrefu chama hicho kimekuwa kikitoa malalamiko kuhusu ufisadi huo serikalini lakini hakikusikilizwa.

“Tunampongeza Rais Magufuli kwa kuthubutu kutamka pasipo shaka kuwa taarifa alizonazo zinaonyesha kampuni ya Airtel ni mali ya TTCL, jambo hili tulilipigia kelele kwa muda mrefu,” amesema.

Ndaro amesema mara zote hawakusita kutamka kuwa Celtel ambayo sasa ni Airtel ni mali ya TTCL iliyoporwa pasipo kulipwa chochote.

“Wafanyakazi tunatambua kuwa TTCL haikuporwa Celtel pekee bali ilinyang’anywa pia Chuo cha Posta na Simu hali iliyosababisha tukose mahali pa kupata mafunzo,” amesema Ndaro.

Kutokana na kuanza uchunguzi wa sakata hilo, Ndaro amesema viongozi wa Tewuta wako tayari kutoa kila aina ya ushirikiano kuhakikisha Serikali inashinda na kuirudisha Airtel mikononi mwa TTCL.

JPM aagiza TCRA kuzifuta kampuni za simu zitakazoshindwa kujiunga na soko la hisa

“Tuna ushahidi wa kutosha na tuko tayari kutoa ushirikiano kwa Serikali katika hatua zote kuleta haki iliyopotea ya Kampuni ya Simu Tanzania,” amesema.




Askofu wa KKKT ahoji mipaka ya dini na siasa



Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza amehoji mipaka ya kuzungumzia masuala ya siasa na dini, huku akitaka wananchi kutojengewa hofu ya kutoa maoni yao.

Kauli ya askofu huyo inafanana na iliyotolewa na Mkuu wa Kanisa hilo, Askofu Fredrick Shoo katika ibada ya Krismasi Jumatatu iliyopita kwamba kuna baadhi ya watu wanawajengea wananchi hofu ili wasiweze kutumia uhuru wao kutoa mawazo.

Askofu Bagonza alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumza na mwandishi wetu, ikiwa ni muda mfupi baada ya kuweka ujumbe katika ukurasa wake wa Facebook, akihoji sababu za watu kuwasakama viongozi wa dini wanaojadili masuala ya siasa.

Alipotakiwa kuthibitisha kama ujumbe huo ni wa wake, Askofu Bagonza alisema “Ni kweli ni wa kwangu na kama huuoni, vijana watakuwa wamechezea mtandao.”

Ujumbe huo unasema, “Wakijenga shule hawaingilii wizara ya elimu, wakijenga hospitali hawaingilii wizara ya afya, wakijenga kisima cha maji hawaingilii wizara ya maji. Wakiombea mvua hawaingilii mamlaka ya hali ya hewa.

“Wakihimiza kilimo hawaingilii wizara ya kilimo, wakitoa msaada wa dawa kwa mgonjwa, wanapongezwa, wakihoji kwa nini hakuna dawa hospitali, wanaambiwa wanachanganya dini na siasa na wakikosoa mfumo wa kisiasa, wanaambiwa wanaingilia siasa! Kuna kitu hakiendi sawa.”

Akifafanua kuhusu ujumbe huo alisema, “Tujenge utamaduni wa kujenga hoja na kutotukanana matusi. Kuna watu wengine wanaamini uhuru wa kusema umetoweka. Nasema, kuwapa uhuru watu kusema na kutoa mawazo yao kunajenga kuliko kuwazuia au kuwajengea hofu.”

Askofu Bagonza pia alizungumzia madai kwamba viongozi wa dini wamekuwa wakimya sasa, “Si kama huko nyuma tulikuwa tunasema na sasa hatusemi hapana, Krismasi hii tumeanza kusema, lakini tukisema mnasema tunasema sana, tukikaa kimya mnasema tunakaa kimya.”

Alisema haki huliinua Taifa na mlinzi mkubwa wa amani ni haki.

“Vyombo vya dola wanahitaji haki, kila mtu anahitaji haki na silaha pekee ya amani ni haki. Tuwape uhuru watu waseme bila kuwazuia, tujenge utamaduni wa kujenga hoja,” alisema.

Askofu Shoo akihubiri katika ibada Krismasi kwenye Usharika wa Moshi Mjini wa Dayosisi ya Kaskazini ya kanisa hilo alisema watu wanajazwa hofu ili wasiseme ukweli wa kile wanachokiamini.

“Kuna watu wanajaribu kuwajaza watu hofu ili watu wasiseme ukweli na wasikae katika kweli. Watu wanajazwa hofu ili wasitetee kile wanachokiona ni cha haki,” alisema Dk Shoo ambaye pia ni Askofu wa dayosisi hiyo.

Alisema, “Watu wanajazwa hofu ili wasiwe huru kutoa mawazo wanayojisikia kuhusu Kristo, nchi yao na imani yao. Tukidumu katika kweli inatupa nguvu na uhuru wa kusema na kutembea bila woga.”

“Yesu amezaliwa si kutuletea tu neema lakini anatuletea kweli kuhusu maisha ya hapa duniani. Mafundisho yanatufundisha tumpokee ili atawale maisha yetu. Tudumu katika ukweli huu na daima tusimame katika kweli hiyo, wala tusione aibu wala tusione woga wa kusimama katika kweli hiyo. Wala tusione woga wa kutetea kweli hiyo,” alisema.

Jeshi la Polisi lasema wahalifu wamehamia Digitali



Msemaji wa Jeshi la Polisi Kamishina Msaidizi wa Polisi (ACP), Barnabas Mwakalukwa amedai kwamba pamoja na kwamba sikukuu ya Krismas kupita kwa amani pasipo matukio ya uhalifu, anaamini kwamba hali ya maisha imebadilika hali inayowafanya wahalifukuachana na uhalifu wa analogia na kwenda digitali.

Akizungumza na Mtangazaji wa East Africa Drive ya EA Radio Bi Scola Kisanga, Kamanda Mwakalukwa amesema kwamba wizi wa analogia umepungua kabisa na wahalifu hao wamebadili mbinu za kufanya na ndiyo asababu watu wengi bado wanalalamika kutapeliwa kwa njia ya simu.

"Uhalifu umehama na hakuna ule wa kizamani. Zamani walikuwa wanadanganya labda muonane ndo wanafanya uhalifu lakini sasa hivi wamejificha nyuma ya mitandao lakini hata huko pia tunafanya doria. Wananchi wasisite kutoa taarifa polisi wanapokumbwa na matatizo hayo".

Akizungumzia kuhusu vyombo vya usalama nchini kujipanga kwenye sikukuu za mwaka mpya, Mwakalukwa amesema kwamba kila Mkoa unampango kazi wake wa kusimamia hiyo siku na kuongeza kuwa wao kama jeshi la polisi wamekataza kupiga fataki, kuchoma matairi na vitendo vyote ambavyo vitavunja sheria.

Mwanaume auwa watoto wake wawili kwa sumu



KIAMBU, KENYA: Jeshi la Polisi linamshikilia Mwanaume mmoja aliyewaua Watoto wake wawil 2 na yeye kunywa sumu ambayo haikumuua.

Watoto hao waliouawa mmoja alikuwa na miaka 7 na mwingine miaka 3

Inadaiwa kuwa siku moja kabla ya Sherehe ya Christmas familia hiyo ilisafiri hadi Narumoru ambako Mama wa Watoto hao alibakia huko kwasababu ambazo hazijajulikana.

VIDEO: TEWUTA wawataja Wahujumu wa TTCL



Chama cha wafanyakazi wa sekta ya Huduma za mtandao wa mawasiliano Tanzania (TEWUTA), wawataja wahujumu wa TTCL ambao walihusika katika kuihujumu shirika hilo kongwe, na pia kutaja baadhi mali ambazo zilikuwa zikimilikiwa na shirika hilo ikiwemo eneo la standi kuu ya mabasi la ubungo.

ANGALIA FULL VIDEO ..............HAPA USISAHAU KU SUBSCRIBE........


Ndalichako asema Wizara yake haina urasimu


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Wizara yake haina urasimu wowote katika usajili wa shule zinazoanzishwa ikiwa tu zimetimiza vigezo vinavyozingatiwa.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo alipotembelea shule ya Sekondari Chegeni inayoendelea kujengwa Kijiji cha Bulima wilayani Busega pamoja na Shule ya Msingi Njalu iliyopo Wilayani Itilima zote zikiwa mkoani Simiyu zinajengwa kwa nguvu ya wananchi.

“Lengo la Serikali ni kuwa na shule nyingi lakini ni lazima vigezo na masharti yaliyowekwa na Wizara yazingatiwe, kuna watu ambao siyo waaminifu, zamani ilikuwa hata mtu akiwa na madarasa matatu akiomba usajili anaruhusiwa na shule inasajiliwa lakini wakisharuhusiwa wanabweteka na matokeo yake wanaleta shida kwa watoto wetu” amesema Profesa Ndalichako.

Kwa upande mwingine Waziri Ndalichako ameahidi kuchangia ujenzi wa shule hizo kwa kutoa saruji mifuko 100 kwa Shule ya Njalu(Itilima) na Mifuko 150 kwa Shule ya Chegeni (Busega) huku akiwataka Wakurugenzi wa Halmashauri hizo kuhakikisha kuwa wanatafuta vifaa vingine ili kukamilisha miundombinu inayotakiwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali ya Mkoa na Wilaya ya Itilima itachangia  saruji mifuko 100 kwa shule ya Msingi Njalu na Serikali ya Mkoa na Wilaya ya Busega itachangia mifuko 50 kwa Shule ya Sekondari Chegeni.


Zari aendeleza bifu lake na Mobeto


Baada ya mwanamitindo Hamisa Mobetto kumtibua upya mama watoto wa Diamond, Zari The Boss Lady ikiwemo kumuita mcheza picha chafu, Zari ajibu mapigo tena.

Mobetto ambaye alikuwa nchini Uganda weekend iliyopita kwaajili ya show ya Girls Power, alimtupia dongo Zari na kumuita mcheza picha za uchi.

Alhamisi hii Zari ameamua kumtolea uvivu Mobetto kwa kuandika ujumbe mkali mfululizo kupitia mtandao wa snapchat.

“Bora mimi changudoa mzee niliye na mafanikio na bado ananipenda kuliko kijana wa miaka 20+ mama uliyeachwa solemba mara mbili na tuzo juu #MchepukoUsioNaAKili #MweweWaMwaka,” , aliandika Zari Snapchat.

“Kijana, kijana kila siku kijana, kijana na mzuri lakini huwezi kutafuta mwanaume wa kwako mwenyewe….namna chan**doa usivyojiamini, Kama unajiamini na uzuri na akili basi acha tuone mwanaume gani atakutaka baada ya drama hizi, baby daddy 3 loading ukiwa na miaka 20+ atakuwa mjinga pia,” alisema Zari kupitia ujumbe huo.

Zari akaongeza “sio wewe cha***doa uliyelia social media ukidai Lulu kakuibia bwana’ko lakini umegeuka kufanya hicho hicho ulicholilia wakati unajua inavyouma, Mungu hawezi kubariki furaha yako juu ya maumivu ya mwanamke mwingine…ng’oo!!!”
“Unaweza kupost picha zote za nyuma ukiwa nae, lakini tayari nimekwisha msamehe makosa yake yaliyopita. Siwezi kubadilisha historia….nimechukulia kawaida naendelea kujenga maisha yangu ya kesho. Uchawi wote unaisha nguvu na sasa anarudi kwa akili zake kumrudia,” amesema Zari na kusisitiza.



Pretyy Kind aingizwa mjini na muhuni


Kisura wa filamu Bongo, Suzan Michael ‘Pretty Kind’ amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuibiwa hela kiasi cha shilingi milioni moja alizokuwa ameweka kwenye gari lake pamoja na kadi ya benki, baada ya kumpa mtu funguo ili asogeze gari lake ambalo lilikuwa limeziba njia.

Kwa mujibu wa shuhuda wa tukio hilo, ishu hiyo ilijiri siku chache zilizopita, ambapo msanii huyo alikuwa studio moja maeneo ya Sinza, ndipo kijana mmoja ambaye si mwenyeji wa studio hiyo akamuomba funguo akamsogezee gari yake ambayo ilikuwa imezuia njia, akampa. Baadaye wakati anaondoka, mrembo huyo alibaini kuwa amelizwa fedha hizo.

Kutokana na sekeseke hilo Pretty alipotafutwa alisema; “Nimekoma kuwapa watu hovyo gari langu, maana bora kaiba hivyo tu, angeiba gari sijui ingekuwaje, nilimuweka ndani mtu wa studio amuonyeshe huyo mwizi alipo, eti anadai ni mtoto wa mkubwa hawezi kupatikana, nimeumia sana,”alisema bishosti huyo ambaye amefungua jalada la kesi Kituo cha Polisi Kijitonyama KJN/RB/12224 WIZI.



OMG kufunga mwaka na kolabo ya Kimataifa


Kundi la muziki la OMG limesema linatarajia kuachia kolabo kubwa na msanii mkubwa kutoka Afrika.

Member wa kundi hilo Young Lunya ameiambia The Playlist ya Times Fm kuwa pia katika kolabo hiyo kuna msanii mwingine kutoka nje ya Afrika.

“Na kabla mwaka hajaisha kuna zawadi moja kubwa sana naona tuiachie, kuna kolabo kubwa sana tumefanya na msanii wa Afrika ila kuna mmoja ni nje ya Afrika,” amesema.

Kwa upande wake Con Boi amezungumzia utendaji kazi wao kwa mwaka huu, 2017 kwa kusema; “Mwaka huu hatukuachia kazi nyingi lakini tunafanya kazi, zipo zinafanyika, 2018 utakuwa ni mwaka wa ku-release, tutaachia sana nyimbo kuanzia mwezi wa kwanza hadi wa 12 ni mauaji kutoka OMG,”.