Thursday, 28 December 2017

Ndalichako asema Wizara yake haina urasimu


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako amesema Wizara yake haina urasimu wowote katika usajili wa shule zinazoanzishwa ikiwa tu zimetimiza vigezo vinavyozingatiwa.

Waziri Ndalichako ameyasema hayo alipotembelea shule ya Sekondari Chegeni inayoendelea kujengwa Kijiji cha Bulima wilayani Busega pamoja na Shule ya Msingi Njalu iliyopo Wilayani Itilima zote zikiwa mkoani Simiyu zinajengwa kwa nguvu ya wananchi.

“Lengo la Serikali ni kuwa na shule nyingi lakini ni lazima vigezo na masharti yaliyowekwa na Wizara yazingatiwe, kuna watu ambao siyo waaminifu, zamani ilikuwa hata mtu akiwa na madarasa matatu akiomba usajili anaruhusiwa na shule inasajiliwa lakini wakisharuhusiwa wanabweteka na matokeo yake wanaleta shida kwa watoto wetu” amesema Profesa Ndalichako.

Kwa upande mwingine Waziri Ndalichako ameahidi kuchangia ujenzi wa shule hizo kwa kutoa saruji mifuko 100 kwa Shule ya Njalu(Itilima) na Mifuko 150 kwa Shule ya Chegeni (Busega) huku akiwataka Wakurugenzi wa Halmashauri hizo kuhakikisha kuwa wanatafuta vifaa vingine ili kukamilisha miundombinu inayotakiwa.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka amesema Serikali ya Mkoa na Wilaya ya Itilima itachangia  saruji mifuko 100 kwa shule ya Msingi Njalu na Serikali ya Mkoa na Wilaya ya Busega itachangia mifuko 50 kwa Shule ya Sekondari Chegeni.


No comments:

Post a Comment