Dar es Salaam. Siku moja baada ya mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kusimama kwa mara ya kwanza tangu Septemba 7, amesema huenda akakaa hospitalini kwa miezi sita zaidi.
Juzi, Lissu anayepata matibabu katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya alisimama kwa msaada wa madaktari.
Akijibu swali ni lini atarejea nchini na kama atasafiri nje ya Afrika kwa matibabu zaidi aliloulizwa jana na mwandishi wetu, Lissu alisema, “Ndio kwanza nimesimama jana (juzi), kuna miezi sita ya ‘rehabilitation’ (kumrudisha katika hali ya kawaida). Madaktari waliniambia kuna miezi sita au tisa.”
“Kwanza nimesimama kwa mara ya kwanza uamuzi wa je, nitamalizia hapa au nitakwenda bado, itategemea ushauri wa madaktari na kisha majadiliano na familia kwa sasa bado sijajua.”
Tangu mwanasheria huyo mkuu wa Chadema aliposhambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi akiwa katika makazi yake Area D mjini Dodoma Septemba 7, hakuwahi kusimama na wakati wote alikuwa akionekana amelala au amekaa hadi juzi.
Katika picha iliyomwonyesha Lissu akiwa amesimama, madaktari wawili walimshika huku mmoja akiurekebisha mguu wake wa kulia.
Lissu alituma ujumbe kwa wapigakura wa Singida Kaskazini akisema; “Wajiandae kwa mapambano makubwa ya kisiasa… kila mmoja atimize wajibu wake na kuacha visingizio.”
Akizungumzia hatua ya Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) kusimama, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema, “Ni jambo la kumshukuru Mungu, tulikuwa tunapigania mwenzetu asimame, tunamshukuru Mungu kwa hatua hii.
“Itachukua muda kidogo ili aweze kurejea katika hali yake, lakini tumshukuru sana Mungu kwa kutupa Lissu, lakini tuwashukuru sana madaktari waliomuuguza na hili ni funzo kwetu,” alisema.
Alipoulizwa iwapo wanamkumbuka Lissu katika harakati zake, Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni alisema, “Kila kiongozi ana wajibu wake wa kiharakati, uongozi si shule unakwenda kujifunza, kila mmoja ana vipawa vyake, wengine ni wazuri katika kuhoji, wengine katika mikutano ya hadhara, wengine mikakati na kila mmoja ana wajibu wake.
“Lissu ni moja ya wanasiasa makini na mahiri hasa linapokuja suala la kuhoji, amekuwa msaada mkubwa katika kambi ya upinzani bungeni na zaidi katika masuala ya sheria na Mahakama, kila mmoja anajua hivyo, kwa hiyo ni kweli tunaposema ‘tumemmisi’ ni kweli tumemmisi sana,” alisema.
Mbowe alisema, “Tunawashukuru Watanzania walio wengi walioshiriki kumuuguza Lissu, kumwombea, kutoa michango na salamu zao hadi amefikia hatua ile ambayo wengi hawakutegemea.Tunawashukuru viongozi wa dini na watu waliomwombea kamanda wetu aweze kupona.”
No comments:
Post a Comment