Sunday, 21 January 2018

Wakazi wa Kilimanjaro waiomba Serikali kuweka matuta kuepusha ajali



WAKAZI wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, wameiomba serikali  kupitia Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), kuweka matuta katika barabara ya Sanya Juu- Bomang’ombe, ili kuzuia ajali ambazo zimekuwa zikitokea na kusababisha watu kupoteza maisha.

WAKAZI wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, wameiomba serikali  kupitia Wakala wa Barabara nchini (Tanroads), kuweka matuta katika barabara ya Sanya Juu- Bomang’ombe, ili kuzuia ajali ambazo zimekuwa zikitokea na kusababisha watu kupoteza maisha.

Wakazi hao wamesema barabara hiyo kwa muda mrefu imekuwa na ajali nyingi za watu kugongwa na magari na kupoteza maisha papo hapo na hakuna jitihada zozote ambazo zimekuwa zikichukuliwa na serikali kuzuia ajali hizo.

Mmoja wa wakazi wa Majengo Sanya Juu, Idrisa Mndeme, alisema serikali kupitia Tanroads inapaswa  kuwawekea matuta katika barabara hiyo kwenye maeneo ya kuanzia Standi Kuu ya Sanya hadi Fuka, kwa kuwa madereva wa magari wamekuwa wakiendesha kwa mwendo kasi bila kujali watembea kwa miguu.

“Ndani ya mwezi huu kuna ajali mbili zimetokea. Mtu mmoja aligongwa na gari na kupoteza maisha na mwingine ambaye ni mwendesha pikipiki aligongwa na gari na kufariki papo hapo,”alisema.

Yassin Kimaro kwa upande wake aliwatupia lawama madereva wenye magari makubwa kwa kuendesha kwa mwendokasi na mara nyingine hudharau alama za pundamilia kwa kupitisha magari bila kujali watu wanaovuka.

“Madereva wa magari huendesha magari kwa kasi mno, hali ambayo imekuwa ikichangia sana ajali ambazo zinaweza kuepukika iwapo matuta yangekuwa yamewekwa,”alisema.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Siha, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Onesmo Busweru, alikiri kuwapo kwa baadhi ya madereva ambao wamekuwa wakiendesha kwa kasi, hivyo kusababisha ajali ambazo zingeweza kuepukika

Kutokana na hali hiyo aliagiza Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani  kuweka kidhibiti mwendo (tochi) katika maeneo hayo ili kuwadhibiti madereva ambao wamekuwa akiendesha kwa kasi.
 

Joyce Kiria amwaga siri za mumewe hadharani

Mwanaharakati na mwanamke shujaa nchini Tanzania, Joyce Kiria ameweka hadharani kuwa mahusiano yake kwa sasa na mumewe Henry Kileo ambaye alishawahi kushika nyadhifa mbalimbali CHADEMA.

Joyce Kiria amesema kuwa kwasasa mahusiano yake hayapo sawa kwani yeye amekuwa ndiye baba na mama wa familia kwa kila kitu yaani kuhudumia familia nzima pamoja na mumewe.

Akitoa taarifa hiyo kwa umma kupitia ukurasa wake wa Instagram huku akibubujikwa na majozi, Kiria amesema huwa anamshauri mumewe atafute japo kazi itakayowaingizia kipato ili kusaidiana kutunza familia lakini mumewe anakuwa mkali na kumpiga.

“Sikutegemea kama ipo siku kwa mkono wako ungeunyanyua kunipiga (@kilewo2020mwanga) ukasahau kabisa! ukasahau yooote. Nimeharibu career yangu kupigania ndoto yako kwa kugawa watu wangu kwenye biashara zangu, nimepoteza ndugu jamaa na marafiki, umeniachia nimebeba mzigo wa familia kwa muda wote, Malipo yako ni kunipiga/ kunidhalilisha na kunitoa machozi, umenipiga kwa sababu Mimi ni mnyonge siyo! sina nguvu, kwa sababu ni MWANAMKE Sina nguvu za kupigana na MWANAUME. Umeniumiza mwili wangu unauma kila mahali, ukanigongesha kwenye gari, ili iweje? Nia yako ilikuwa ni nini? kuniua??,“ameandika Kiria huku akielezea jinsi alivyompigania mumewe hadi kwenye kampeni za uchaguzi mkuu mwaka 2015 hadi akaingiza deni kubwa na kufungiwa kipindi chake cha Wanawake Live kilichokuwa kinaruka EATV.

“Haya MACHOZI yangu namlilia Mungu wangu aliye juu, yeye ndo ataamua, kama ni mimi niliandamana na watoto, nikakufanyia kampeni na deni kubwa nikaingia mpaka nikafungiwa Kipindi hewami, ninakutunza wewe na Watoto wako kwa miaka yote Mungu yupo. Leo umenipiga (@kilewo2020mwanga)?? Sawa watakusifia hao wanaokusifu ujinga, wanaokuambiaga Mimi sikuheshimu, badala wakwambie ufanye kazi utunze familia, Leo watakuona wewe ni mwanaume kwa kunipiga.“amemaliza Kiria.

Mumewe na Joyce Kiria ni moja ya vigogo wa CHADEMA na kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 aligombea nafasi ya Ubunge katika jimbo la Mwanga, Kilimanjaro lakini kwa bahati mbaya alishindwa kupata nafasi hiyo.

Jafari Maganga: Watanzania wameanza kukubali falsafa ya Azam FC


Kuelekea mchezo wa leo wa ligi kuu soka Tanzania Bara kati ya Tanzania Prisons dhidi ya Azam FC, msemaji wa wa Azam FC Jafar Idd Maganga amesema watanzania wameanza kukubali falsafa ya timu hiyo ya kutumia vijana.

Jaffar amesema kocha mkuu wa timu hiyo Aristica Cioaba, amekuwa muumini wa kutumia vijana kitu ambacho awali kilionekana kupingwa na mashabiki wengi wa soka wakiamini kuwa timu hiyo haitafanya vizuri.

''Watanzania wengi wameshaanza kukubali na wanaunga mkono uongozi wa Azam FC kuwatumia vijana na kocha huyu (Cioaba) amekuwa akiwaamini zaidi vijana tofauti na makocha wetu waliopita'', amesema Jaffar.

Kuhusu mchezo wa leo jioni, Jaffar amesema benchi la ufundi limejipanga kuhakikisha linapanga wachezaji ambao wataendana na timu ya Tanzania Prisons pamoja na hali ya uwanja wa Sokoine ili kuhakikisha timu yao inapata matokeo mazuri.

Azam inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 27 huku vinara wa ligi Simba SC, wakiwa na alama 29. Mabingwa watetezi Yanga SC watakuwa dimbani pia kucheza na Ruvu Shooting.

Kocha wa Simba afunguka kuhusu Nicholas Gyan

Kocha msaidizi wa vinara wa ligi kuu soka Tanzania Bara Simba SC Masoud Djuma, ameweka wazi kuwa pamoja na kumpatia nafasi ya kucheza hivi sasa nyota wa timu hiyo kutoka Ghana Nicholas Gyan, lakini aliwahi kumwambia hajui kucheza.

Masoud  amesema baada ya kujiunga na Simba alimkuta Gyan na baada ya kumtazama kwenye mazoezi alimtamkia kuwa hawezi kucheza soka wala hafananii kuwa mchezaji lakini kwasasa Gyan amemjibu kwa vitendo.

"Nilimwita Gyan na kuzungumza naye na nikamwambia wewe si mchezaji, inakuwaje haupigi pasi, wala hautulizi mpira vizuri, kwa sababu haiwezekani mchezaji awe anakosa vitu hivyo, lakini kumbe mwenyewe kichwani alikuwa anafikiria kuwa  anarogwa," ameeleza Masoud.

Kocha huyo raia wa Burundi ameongeza kuwa baada ya kugundua kuwa Gyan anawaza hivyo alikaa naye na kumshauri kisha akampa nafasi ya kucheza na mwisho wa siku ameonesha kiwango kikubwa na amekuwa msaada kwa timu.

Masoud amekuwa akimtumia Gyan upande wa kulia kutokana na kasi yake ili kusaidia mfumo wake wa 4-4-2 ambao huwa unabadilika na kuwa 3-5-2 timu ikiwa inacheza hivyo Gyan mara nyingi husaidia kurudi kama mlinzi wa kulia na baadae kupanda kama winga.

Kiwanda cha Dangote chapewa siku 14


Naibu Waziri wa Madini, Doto Biteko ametoa siku 14 kwa uongozi wa kiwanda cha saruji cha Dangonte mkoa wa Mtwara kuingia mkataba na wachimbaji wadogo wa gypsum.

Biteko ametoa kauli hiyo leo Januari 21, 2018 baada ya kutembelea kiwanda hicho na kuzungumza na viongozi wake.

Amesema mikataba hiyo inapaswa kuwa na kipengele cha kuwalipa ndani ya siku 30 baada ya kiwanda kukusanya gypsum kutoka kwa wachimbaji hao, lengo likiwa ni kuleta ufanisi na tija katika biashara zao.

“Nimekubaliana hapa kamishna wa kanda atasimamia hili la mikataba kati ya kiwanda na wachimbaji wa gypsum. Sehemu ya malipo itakuwa ndani ya mkataba na watalipa ndani ya siku 30,” amesema.

Amesema wachimbaji hao wamekuwa wakilalamikia kucheleweshewa malipo yao baada ya kupeleka kiwandani bidhaa zao.

“Nimeambiwa wachimbaji hawa walikuwa wanalipwa baada ya miezi mitatu lakini kwa mkataba huu ambao wataingia na kiwanda sasa watakuwa wanalipwa ndani ya siku 30,” amesema Biteko.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inalenga kuwasaidia wachimbaji wadogo sambamba na wawekezaji ambao wanapaswa kufanya kazi bila kusumbuliwa.

 “Uwepo wa kiwanda hiki unawasaidia wachimbaji wetu waweze kupata bei nzuri pamoja na kupata soko la uhakika la kuuza bidhaa zao. Dangonte wameniahidi kwamba ndani ya muda mfupi watatekeleza agizo hili,” amesema.

Biteko amesema lengo la ziara yake ni kuwasaidia wachimbaji wa gypsum ambao hawana mikataba na kujikuta wakibanwa katika uuzaji wa bidhaa zao.


Snura: Mwanamke anayelea watoto mwenyewe ni elimu tosha Duniani


MWANAMUZIKI anayefanya vizuri kwenye miondoko ya mduara, Snura Mushi, ameibuka na kudai kuwa mwanamke anayelea watoto mwenyewe ni elimu tosha duniani.

Akizungumza na Mikito Nusunusu, Snura alisema kuwa, amepata changamoto nyingi sana kwenye kulea watoto wake lakini anashukuru amesimama vyema kama mwanamke shujaa na amejifunza mengi ikiwa ni pamoja na kuwa jasiri ambapo anaweza kusimama popote sasa na kujiamini.

“Yaani kulea watoto mwenyewe kama mwanamke ni elimu tosha ya duniani na mimi najivunia hilo sana, mwanzo ilikuwa ni ngumu sana na sisi wanawake tumekuwa tukiwategemea sana wanaume wakiwepo lakini ukiyajaribu maisha ya ulezi peke yako na kuyashinda unajikuta jasiri ambaye unaweza

Waziri Ummy asikitishwa na kifo cha mtoto akiyekuwa na uvimbe



Maria Amrima (17) mkazi wa Mtwara, aliyekuwa akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) kutokana na uvimbe mkubwa begani, amefariki dunia.

Mkurugenzi wa ORCI, Julius Mwaiselage alisema mgonjwa huyo alifariki dunia jana alfajiri wakati akiendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

Maria ambaye alitakiwa kufanyiwa upasuaji Muhimbili mwaka mmoja uliopita wakati uvimbe huo ukiwa mdogo, alitoweka na kwenda katika tiba za asili kabla ya kurejea hospitalini hapo Januari 3 akiwa katika hali mbaya na kuhamishwa ORCI.

Kuhusu kifo hicho, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema mwili wa marehemu ulisafirishwa jana mchana kwenda mkoani Mtwara kwa maziko.

“Inasikitisha kwani wamejitokeza dakika ya mwisho, msaada wetu haukuweza kuokoa maisha yake, tutaongeza jitihada zaidi kuwaelimisha wananchi juu ya umuhimu wa kuwahi hospitalini kufanyiwa uchunguzi,” alisema.

Waziri huyo ambaye alimtembelea Mariam wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) alisema, “Wananchi wanapaswa kufuata maelekezo ya madaktari ikiwamo kuanza matibabu mara moja na si kwenda kukaa nyumbani na mgonjwa.”

Awali, jopo la madaktari bingwa kutoka vitengo vitatu vya Muhimbili na Ocean Road, walikutana kujadili namna ya kumtibu mtoto huyo aliyekuwa na umri wa miaka 17 baada ya tiba ya upasuaji kushindikana.

Vyuo vya ufundi vyatakiwa kutoa upendeleo kwa wasichana


Naibu waziri wa elimu sayansi na Teknolojia William Ole Nasha ameviagiza vyuo vya ufundi kote nchini kuondoa vikwazo na kutoa upendeleo maalum kwa wanafunzi wa kike wenye sifa wanaojiunga na elimu ya ufundi kwakuwa  idadi kubwa wanafunzi wa kike wanaichukia elimu ya ufundi kutokana na vikwazo vilivyopo kwenye vyuo hivyo dhidi yao.

Naibu waziri Ole Nasha ametoa kauli hiyo alipokuwa anazungumza na wahitimu wa fani mbalimbali za ufundi kwenye chuo cha ufundi Arusha ATC.

Kaimu mkuu wa chuo cha ufundi Arusha Dkt. Masud Senzia amesema chuo hicho kimetekeleza kwa vitendo adhima ya serikali ya viwanda kwani kimeanza kufanya majaribio ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji.

Mkurugenzi wa elimu ya ufundi Thomas Katebalirwe akaelza mikakati ya serikali katika kuboresha elimu ya ufundi.

Dili la wa Mkhitaryan, Sanchez lakaribia kukamilika


Baada ya michezo yao ya  jana kauli za makocha wa timu za Arsenal, Arsene Wenger na Manchester United, Jose Mourinho zilionesha kuwa usajili wa wachezaji Alexis Sanchez na Henrikhi Mkhitaryan uko mbioni kukamilika.

"Sanchez hakucheza kwa sababu huwezi kusafiri kwenda Kaskazini na kucheza mpira wa miguu wakati huo huo," alisema Wenger wakati akijibu swali alipoulizwa kwanini Sanchez hakucheza kwenye ushindi wa 4-1 iliopata Arsenal dhidi ya Crystal Palace.

Kocha wa Man United Jose Mourinho yeye alipoulizwa kuhusu usajili wa Sanchez, alijibu kwa kifupi ''upo karibu kukamilika''. Jibu hilo la Mourinho lilionesha wazi kuwa makubaliano kati ya pande hizo mbili yamekamilka ambapo Henrikh Mkhitaryan wa United atakwenda Arsenal.

Katika msimu mmoja na nusu ambao Mkhitryan ameichezea Man United amefanikiwa kufunga mabao matano na kusaidia mengine sita huku Sanchez akifunga mabao 60 na kusaidia mengine 25 katika misimu mitatu na nusu aliyoicheza Arsenal.

Ripoti mbalimbali kutoka nchini England leo zinaripoti kuwa huenda nyota hao wawili Mkhitaryan raia wa Armenia na Sanchez raia wa Chile watafanyiwa vipimo ili kukamilisha taratibu za kujiunga na klabu zao mpya.

Mama wa Askofu Gwajima afariki Dunia

Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima leo Januari 21, 2018 amepata pigo kwa kuondokewa na mama yake mzazi Ruth Basondole Gwajima ambaye amefariki asubuhi ya leo.

Gwajima amesema kuwa mama yake mzazi amefariki akiwa na umri wa miaka 84 na kuwa mazishi ya mama yake mpendwa yatafanyika siku ya Alhamisi ya Januari 25, 2018 Salasala jijini Dar es Salaama.

"Leo Saa mbili asubuhi mama yangu Mzazi, Bi Ruth Basondole Gwajima ametwaliwa na Bwana. Karudi Mbinguni akiwa na Umri wa Miaka 84. Kuna Furaha ya Ajabu Shujaa Wangu Amerudi kwao. Kwasababu katika maisha yake alimtumikia Mungu. Mazishi yatafanyika Alhamis Tarehe 25/01/2018; Salasala Dar es Salaam" alisema Gwajima.

EATV
.

Wizara ya Afya yatoa tahadhari juu ya homa ya CHIKUNGUNYA


Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto imetoa tahadhari kwa umma kuhusu ugonjwa wa homa ya CHIKUNGUNYA ambao umeripotiwa na vyombo vya habari kutokea Mombasa nchini Kenya lakini bado Shirika la Afya Duniani (WHO) halijatoa taarifa rasmi.

Wizara ya Afya imetoa tahadhari ya ugonjwa wa CHIKUNGUNYA kutokana na muingiliano mkubwa uliopo kati ya nchi ya Kenya na Tanzania.

Dalili za ugonjwa huo ni pamoja na homa kali na maumivu ya viungo, misuli, kichefuchefu na uchovu.

Ripoti za awali kabisa za kuwepo ugonjwa huo wa CHIKUNGUNYA zilipatikana katikati ya mwezi uliopita ambapo kilichofuatia kilikuwa ni kukusanya sampuli za damu na kuziwasilisha kwenye maabara kwa ajili ya uchunguzi.

Ugonjwa wa CHIKUNGUNYA unaweza kupunguzwa kwa kuchukua hatua kadhaa ikiwemo kuhakikisha mazingira ni masafi ili kuepusha mazalia ya mbu.

ACT yaendeleza msimamo wake Siha, Kinondoni


Chama cha ACT-Wazalendo kimesema hakitashiriki uchaguzi katika majimbo ya Kinondoni na Siha kwa kuwa sababu zilizowafanya wasusie uchaguzi mdogo uliopita,  bado hazijafanyiwa kazi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 21, 2018 Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho-Bara, Msafiri Mtemelwa amesema changamoto walizozilalamikia katika uchaguzi wa Januari 13 katika majimbo ya Singida Kaskazini, Songea Mjini na Longido bado hazijafanyiwa kazi.

Amesema bado chama hicho kitaendelea kushinikiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufanya mageuzi katika mchakato wa uchaguzi.

Amesema malalamiko ya chama hicho kwa NEC ni matumizi ya nguvu ya vyombo vya dola dhidi ya vyama vya upinzani kwa lengo la kukisaidia chama tawala CCM.

Uchaguzi wa Siha na Kinondoni unafanyika baada ya waliokuwa wabunge wa majimbo hayo kuhamia CCM Desemba mwaka jana.

Breaking News: ACT Wazalendo wametangaza kujitoa kwenye Marudio ya Uchaguzi

 Chama cha ACT Wazalendo kupitia kwa Naibu Katibu Mkuu wake Bara Msafiri Mtemelwa kimetangaza kutoshiriki Uchaguzi mdogo wa marudio katika Majimbo ya Kinondoni na Siha.

 Mtemelwa alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuona mazingira ya Uchaguzi ambayo waliyalalamikia kwa Tume ya Uchaguzi hayajafanyiwa marekebisho.