Saturday, 20 January 2018

Man Fongo Amvaa Sholo Mwamba

Msanii wa miondoko ya singeli Man Fongo amesema hawezi kukaa na kumzungumzia Sholo Mwamba kwa madai yeye ni mfa maji ndiyo maana haishi kutapa tapa kila uchao kumtaja.

 Man Fongo ameeleza hayo baada ya masaa machache kupita tokea kuonekana kwa 'video' ya Sholo iliyorushwa na EATV katika kipindi cha 'FRIDAY NIGHT LIVE' (FNL) usiku wa kuamkia leo, ikiwa imemuonyesha akimlaumu msanii mwenzake kuwa hana kipaji cha kuendelea kufanya muziki mzuri ndani ya mwaka 2018 huku akimtaka arejee katika fani yake ya awali ya 'DJ'.

"Mimi kwa sasa siwezi kumzungumzia mtu yeyote kwa maana naangalia muziki wangu kwa sababu ndiyo unaonifanya nieleweke kwa wadau wangu, pia unasababisha familia yangu ipate kula. Kwa hiyo mtu akitaka kutoka kwa kutumia kiki na kupitia mgongo wangu nakuwa bado simuelewi. Hivyo siwezi kumtumikia Sholo Mwamba 'eti aniambie mimi nirudi katika fani yangu ya 'DJ' wakati yeye hayupo katika 'manegement' yangu na yeye ni msanii kama mimi", alisema Man Fongo wakati alipofanyiwa mahojiano maalum.

Pamoja na hayo, Man Fongo ameendelea kwa kusema "ninachopenda kumshauri Sholo Mwamba ni kwamba atoe ngoma mpya ili aweze kusikilizwa na raia anachokifanya, apambanie muziki wake aweze kufika mbali na asiangalie muziki wangu mimi", alisisitiza Man Fongo.

Kwa upande mwingine Man Fongo amesema mwaka 2018 amejiandaa vizuri katika ufanyaji kazi wake na wala haiwezi kuwa kama alivyosema mpinzani wake huyo ambae kwa muda mrefu wamekuwa wakitoleana mapovu katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii.

"Kazi mpya nimeangusha juzi tu na mpaka sasa ninapo kwambia inafanya vizuri hivyo Sholo Mwamba ni mfa maji tu kama mtu ambae anatapa tapa yaani mfa maji haishi kutapa tapa. Kwa hiyo ameona bora apate kiki kwa mgongo wangu ili aweze kutoka", alisema Man Fongo.

Viongozi CCM Moshi Waaswa Kubadilika

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amewataka viongozi wa chama hicho Manispaa ya Moshi, kuacha kutembea na watu mifukoni na kutengeneza kofia za ubaguzi ndani ya chama kwa kuwa hali hiyo imekuwa ikikigharimu chama wakati wa uchaguzi.

Polepole amesema chama hicho kimekuwa kikijikuta katika wakati mgumu wakati wa uchaguzi kutokana na baadhi ya viongozi ndani ya chama kupenda ubinafsi na kuweka mbele uheshimiwa badala ya utumishi.

Ametoa rai hiyo leo Jumamosi wakati akizungumza  kwenye kikao cha ndani cha Halmashauri Kuu ya CCM Manispaa ya Moshi kilichofanyika mjini Moshi katika ukumbi ulioko kwenye ofisi za chama hicho mkoa ambapo amesema sasa ni wakati wa kujiimarisha ili kuweza kushika hatamu kila ngazi.

Amesema kumekuwepo na baadhi ya viongozi ndani ya chama ambao wamekuwa wakitengeneza makundi ya walionacho na wasio nacho wakati wa uchaguzi hali ambayo imekuwa ikikifanya  chama kushindwa kila mwaka wa uchaguzi katika majimbo mbalimbali likiwemo jimbo la Moshi Mjini.

"Kushindwa kwa CCM  katika majimbo mengi Kilimanjaro hasa hili la Moshi Mjini, kulisababishwa na viongozi, kutembea na majina yao mifukoni na kuweka uheshimiwa mbele badala ya utumishi,  hali hii ilijenga makundi, sasa ni lazima  tubadilike," amesema Polepole

VIDEO: CHADEMA Watoa Kauli Nzito Uchaguzi Kinondoni


Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Zanzibar, Salum Mwalimu amefanikiwa kurudisha fomu ya kugombea Ubunge jimbo la Kinondoni huku akiwataka wanachama wa chama hicho kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha muda mfupi.

TAZAMA FULL VIDEO HAPO CHINI.......USISAHAU KUSUBSCRIBE

Mkurugenzi wa Maji Musoma atumbuliwa

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Isaack Kamwelwe , ametengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa Mji wa Musoma, Gantala Said (pichani kushoto) ambaye anachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa tuhuma za ubadhirifu wa fedha kwenye Mradi wa Maji Bunda na akizivunja Bodi za Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira za Mikoa ya Arusha na Mara (Musoma) baada ya kujiridhisha kuwa utendaji wao siyo mzuri.

Kamwele amefikia uamuzi huo leo baada kubaini kuwa kumekuwepo na uzembe wa utekelezaji wa miradi ya serikali ya maji kwa baadhi ya watendaji katika idara hizo.

“Kufuatia ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majliwa mkoani Mara, imebainika kuwa kumekuwepo na matatizo ya huyo Mkurugenzi Gantala ambaye Waziri Mkuu ameagiza Mkurugenzi huyu watendaji wengine wachunguzwe na TAKUKURU.

“Hivyo kuanzia leo Januari 20, 2017 ninatengua uteuzi wa Mkurugenzi wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira wa Mji wa Musoma, Gantala Said na nafasi yake itakaimiwa na Eng. Robert Petro Mponya wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUASA), ninamuagiza aisaidie Musoma ili waweze kufanya kazi inayotakiwa,” alisema Kamwele.

Wolper awafunda mabinti

Msanii wa filamu bongo ambaye sasa amegeukia ujasiriamli, Jackline Wolper, amewapa somo mabinti na kuwafunda juu ya kujishughulisha ili kujipatia kipato chao, na hatimaye waweze kuheshimika.

Akizungumza kwenye Friday Night Live ya East Africa Television, Jackline Wolper amesema ni wakati sasa mabinti kuacha kutegemea pesa wanazopewa na wanaume, na badala yake wajishughulishe ili kutengeneza pesa yako mwenyewe.

“Wadogo zangu wa kike 2018 mi ntaendelea kuwatia hasira, na kuendelea kuwaambia kwamba hela ya mwanaume sio ya kwako, ukishachukua hela ya mwanaume fanya kitu chako, iwe hela yako, usikubali kunyanyasika, kwa hela ya mtu, kwa hiyo wadogo zangu nitaendelea kuwaisipire ili mfanye kazi ili utambe na hela yako, usitambe kwa hela ya kuhongwa”, amesema Wolper.

Hivi sasa Wolper anamiliki biashara yake ya mavazi ambayo ana buni na kushona mwenyewe, ambayo aliwahi kusikika akisema inamuingizia pesa nyingi ingawa watu wengi wakimdharau kwa kumuita 'fundi cherehani'.


Waziri Mkuu ataka Watumishi Na Madiwani kushirikiana

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa Halmashauri na Mji wa Bunda pamoja na Madiwani washirikiane katika utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya maendeleo.

Pia amewaagiza watumishi wa umma katika halmashauri ya wilaya na mji wa Bunda wafanye kazi kwa bidii na wawahudumie wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote.

Waziri Mkuu aliyasema hayo jana (Ijumaa, Januari 19, 2018) wakati akizungumza na watumishi na Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya na wa Halmashauri Mji wa Bunda, katika ukumbi wa Halmashauri ya Bunda.

“Watumishi wa umma  acheni kukaa sana maofisini tengeni muda wa kuwatembelea wananchi katika maeneo yao na shirikianneni nao katika kutatua kero zinazowakabili. Madiwani na watumishi lazima mshirikiane ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Alisema watumishi na madiwani wakishirikiana katika usimamizi wa utekelezaji wa miradi mbalimbali  ya maendeleo, wilaya itafanikiwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Pia Waziri Mkuu aliwasisitiza watumishi hao kufanya kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za utumishi  na wajiepushe na vitendo vya rushwa, wizi , ufisadi na uzembe kwa sababu vinarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Awali, Waziri Mkuu alikagua mradi wa maji wa Bunda na baadae alizindua kikundi cha Ushirika cha Igembe Sabo na kukagua skimu ya umwagiliaji wa zao la mpunga ya Nyatwali wilayani Bunda.

Waziri Mkuu alihitimisha ziara yake wilayani Bunda kwa kuhutubia mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Stendi Mpya katika mji mdogo wa Bunda.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Sheria kali yaandaliwa kulinda misitu nchini

SERIKALI kwa kushirikiana na wadau wa uhifadhi wa misitu na bayoanui, inakamilisha taratibu za kutungwa sheria mpya pamoja na kanuni zake ili kudhibiti uharibifu wa misitu nchini.

Hatua hiyo inakuja kutokana na sheria zilizokuwepo kupitwa na wakati na kuchangia kuharibika kwa misitu kila mwaka.

Maamuzi ya kuanzisha sheria hiyo mpya yamekuja kutoka na sekta ya misitu na nyuki hapa nchini kuwa katika hatari ya kutoweka hali inayochangiwa kwa asilimia kubwa na vitendo vya uchomaji wa mkaa pamoja na ukataji kuni.

Akizindua mchakato wa kuhakiki rasimu ya taifa ya misitu, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, alisema maamuzi ya kutunga sheria mpya yanatokana na ile iliyopo ya mwaka 1998 kutokuendana na mabadiliko ya jamii ya sasa ambayo yanatishia kwa kasi uhai wa sekta hiyo ya misitu.

Naibu Waziri alisema sekta ya misitu na nyuki ni mtambuka kwani inashirikisha wizara mbalimbali kama Nishati, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi),Afya, Viwanda na Biashara hivyo kulingana na sheria mpya kazi ya kulinda misitu itakuwa ikifanywa kwa pamoja.

Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania(TFS),Profesa Dos Santos Silayo, alisema kuanzishwa kwa sheria hiyo mpya itakuwa mkombozi wa misitu nchini kwa kuwa iliyopo ilitoa mwanya kwa baadhi ya watu kufanya uharibifu.

Alisema kuwa rasilimali za misitu zipo za kutosha kulingana na ikolojia mbalimbali za kila eneo kama kuweka sheria kali za kuhifadhi kuna hatari ya vizazi vijavyo vikashindwa kuzitumia rasilimali hizo.

Mtalaam wa misitu, Dk. Felician Kilahama,alisema kuwa sekta ya misitu inakabiliwa na changamoto kubwa ya usimamizi,ukataji wa miti ambapo katika kipindi cha miaka mitatu iliopita hekta 582 zilifanyiwa uharibifu kwa ajili ya shughuli za uchomaji wa mikaa na ukataji wa kuni.

Alisema kuwa kuanzishwa kwa sheria hiyo mpya ya misitu na kusimamiwa kwa pamoja , serikali pamoja na wadau kutawezesha kurudisha misitu ya asili kwa haraka ambayo imeanza kutoweka kutokana na uharibifu mkubwa wa mazingira.

Agizo la Waziri Mwigulu kwa Polisi kuhusu kukamata wazururaji

January 20, 2018 Waziri wa Mambo ya Ndani, Dr. Mwigulu Nchemba amelitaka Jeshi la Polisi nchini kutafuta namna ya kupunguza wahalifu wanaokamatwa kwa makosa kama uzururaji ili kupunguza mrundikano kwenye mahabusu.

Ameeleza kuwa suala hili pia litaepusha watuhumiwa wanaopelekwa mahabusu kwa makosa ya uzururaji kupata nafasi ya kuzungumzia masuala ya uhalifu na watuhumiwa waliozoea.

Kwa upande mwingine Dr. Mwigulu ameagiza wananchi kushirikiana na serikali katika ujenzi wa vituo vya polisi kwa kuwa suala la ulinzi ni ajenda ya kila Mtanzania na linapaswa kupewa kipaumbele.

Akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Dr. Mwigulu amesema kuwa mkakati wa Halmashauri hiyo kujenga kituo cha kisasa cha polisi ni kitendo cha kupongezwa kwani wanalenga kukomesha uhalifu wa aina zote.

VIDEO: Le Mutuz, Awataka watumia mitandao waitumie kwa manufaa

Mtoto wa aliekuwa waziri mkuu mstaafu, William malecela 'Le Mutuz' amewataka watumia mitandao ya kijamii kuitumia vizuri kwa manufaa ili kujitengenezea kipato, ameyasema hayo leo akiwa katika chuo cha T I A kilichopo uhasibu ambapo alialikwa kama mgeni na kikundi cha Victorious Women Empowerment Ili kuelezana machache juu ya namna ya kumkomboa mwanamke.

vile vile amesisitiza na kuwataka kusoma kwa bidii wanafunzi ambao bado wako mashuleni wanasoma na kusema kuwa elimu ndio mafanikio yao na itawafanya kufikia leo, vile vile akawaeleza baadhi ya changamoto alizopitia hadi alipofikia hapo alipo kuwa alianza kulala stendi ya magari na kuchoma kuku KFC na hakujali kama baba yake alikuwa waziri mkuu.

TAZAMA FULL VIDEO HAPA...... USISAHAU KUSUBSCRIBE.....

Waziri arudi CCM atwae jimbo 2020

Mwanasiasa  wa upinzani na aliyekuwa Naibu Waziri katika serikali ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete, Goodluck Ole Medeye, ametangaza kurejea Chama Cha Mapinduzi huku akidai kuwa ameamua kufanya hivyo kwa kuwa vitendo vya rushwa,-Hususan nyakati za uchaguzi, vimemalizwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Dk. John Magufuli.

 Ole Medeye juzi alisema kilichomkimbiza CCM mwaka 2015 na kujiunga na Chadema ni vitendo vya rushwa katika mchakato wa kupata wagombea wa chama hicho tawala.

Alisema anafurahi kuona sasa vitendo hivyo havipo ndani ya CCM baada ya kudhibitiwa na Rais Magufuli.Ole Medeye alikuwa mmoja wa wabunge watano wa CCM waliojiunga na Chadema Agosti 12, 2015 wakiongozwa na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (Monduli).

Ole Medeye aliteuliwa na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuwania nafasi ya Uspika wa Bunge baada ya Uchaguzi Mkuu.

Wengine waliohama pamoja na Lowassa ni Makongoro Mahanga (Segerea), James Lembeli (Kahama) na mbunge wa viti maalum, Esther Bulaya ambaye sasa ni mwakilishi wa wananchi wa Bunda Mjini (Chadema).

Hata hivyo, Ole Medeye alihama Chadema kabla ya mwaka kumalizika na kujiunga na UDP kinachoongozwa na John Cheyo Juni 12, 2016.

Medeye alisema alihamia UDP kwa kuwa inasimamia haki na demokrasia na kwamba yeye alikuwa akitaka demokrasia ya kweli na jukwaa la haki katika kuleta haki na maendeleo kwa Watanzania.

Alisema  kuwa alikaa chama hicho cha 'Bwana Mapesa' kwa miezi mitatu tu hata hivyo, kwa kuwa "nilikwenda kufanya kazi maalum."

Na sasa, Ole Medeye amesema ameamua kurejea CCM kwa kuwa kila mwanachama anayo fursa kushiriki uchaguzi, ikiwamo kugombea nafasi yoyote bila kutoa rushwa na akashinda.

"Mimi sijawahi kuwahonga watu ili wanichague," alisema Ole Mideye na "wakati huo CCM kulikuwa na rushwa sana; ndiyo maana nikaamua kukimbia.

"Lakini kwa sasa hakuna tena kitu kama hicho, hivyo nimeamua kurejea CCM."

Ole Medeye alisema katika Uchaguzi Mkuu ujao, mwaka 2020, anataka kurudi na kuwatumikia wananchi kupitia nafasi ya ubunge.

Maseneta wakwamisha serikali ya Trump

Bunge la Seneti nchini Marekani limeshindwa kuidhinisha mswada ambao ungeongeza ufadhili wa serikali ya kitaifa kwa mwezi mmoja.

Kufuatia hatua hiyo huduma nyingi za serikali zitakwama, hata hivyo athari kamili itaanza kuonekana siku ya Jumatatu, wakati wafanyakazi wa serikali watarejea kazini.

Mara ya mwisho shughuli za serikali zilikwama nchini Marekani ni mwaka wa elfu mbili na kumi na tatu, na ilidumu kwa muda wa siku kumi na sita wakati ambapo wafanyakazi wengi wa serikali walishurutishwa kwenda likizo ya lazima.

Ni mara ya kwanza kwa huduma za serikali kukwama huku chama cha Republican kudhibiti mabunge yote na ikulu ya White house.

Ikulu ya whitehouse imewalaumu wabunge wa Democrats kwa kuweka siasa juu ya maswala ya kiusalama , familia za wanajeshi, watoto walio katika mazingira magumu, na uwezo wa taifa hilo kuwahudumia raia wa Marekani.

Lakini kiongozi wa wabunge wa Democrats Chuch Schumer, alisema kuwa rais Trump alikataa makubaliano yasiopendelea upande wowote na hakukishinikza chama chake katika bunge la Congress.

Mkwamo wa huduma za serikali nchini Marekani ulifanyika mara ya mwisho 2013 na ukachukua muda wa siku 16.

Republicans waliutaja muswada huo kwa jina la ''Schumer Shutdown' na hawakukosea.

Chuck Schumer na wabunge wenzake wa Democrats kupitia usaidizi wa wabunge wachache wa Republican walizuia muswada ambao ungesaidia serikali kuendelea na shughuli zake, hata ijapokuwa kwa muda.

Hatahivyo kuchukua jukumu na kutoa lawama ni vitu viwili tofauti.

Democrats watasema kuwa walikuwa wamekubaliana na rais kupitisha muswada usiopendelea upande wowote kuhusu mabadiliko ya sheria ya uhamiaji, kabla ya kukiuka makubaliano hayo wakati wa mkutano katika afisi ya Oval wiki iliopita.

Swala la kurushiana lawama lilianza saa sita usiku na mshindi bado hajatangazwa.

Hatahivyo atakayeshindwa katika mkwamo huu ni chama kitakachoingia katika vita na idadi ndogo ya wabunge ikiwa ni habari mbaya kwa rais Trump na chama cha Republicans.

Habari njema ni kwamba , pande zote mbili na ngome zao za kisiasa zitafurahishwa kwa kufanya mambo kuwa magumu.

Kwa nini pande hizo mbili zisikubaliane?

Swala linalogombaniwa ni lile la Democrats kutaka zaidi ya wahamiaji wasio na vibali walioingia nchini Marekani kutofurushwa.

Wahamiaji hao walipatiwa vibali vya kuwa nchini humo kwa muda chini ya mradi ulioanzishwa na rais wa zamani Barrack Obama.

Mnamo mwezi Septemba, bwana Trump alitangaza alikuwa anasitisha mpango huo huku akilipatia bunge la Congress hadi mwezi Machi kuwa na mpango mbadala.

Waziri Ndalichako awapa wiki moja TBA

Waziri wa elimu,sayansi,na teknolojia na ufundi Profesa Joyce Ndalichako amewapa wiki moja Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kuonyesha maendeleo ya mradi wa ujenzi wa madarasa, hostel na ofisi kwa ajili ya chuo kikuu cha Muhimbili Kampasi ya Mloganzil

Waziri Ndalichako ametoa agizo hilo leo alipokuwa kwenye ziara ya kutembelea mradi huo na kutoridhishwa nao, baada ya kukuta hauna maendeleo yoyote huku serikali ikiwa imeshalipa gharama za ujenzi.

“Ninawapa wiki moja, nataka hapa nione vifaa vyote vya ujenzi viwe vimemwagwa vywa kutosha, nataka nione mafundi wa kutosha, haiwezekani site kubwa kama hii mafundi hawafiki hata 40, kweli kazi itaenda!? Niliwaambia muongeze mafundi mwezi wa 11 lakini kwa sababu mlizozijua wenyewe hamjaongeza, sasa ndani ya wiki moja wasipoongeza mafundi, hatuwezi kuwa na mkandarasi ambaye haendani na matakwa ya mteja, nimekwisha wapatia bilioni 3 na milioni 900,  nikiangalia fedha nimezitoa tangu mwezi wa 8 sioni kazi ambayo inafanana na kiwango cha fedha ambayo nimewapatia, ndani ya wiki moja wasipotimiza angalieni namna ya kuvunja huo mkataba.”, amesema Waziri Ndalichako.

Waziri Ndalichako ameendelea kwa kulalamika kuwa wakandarasi hao wamekuwa wakiaminiwa na serikali na kuwapa miradi mingi, lakini wamekuwa wakisua kukamilisha miradi kwa muda.

New VIDEO: Mr. Blue – Mbwa Koko

New VIDEO: Mr. Blue – Mbwa Koko

New VIDEO: Mr. Blue – Mbwa Koko

DOWNLOAD VIDEO