Mshambuliaji wa zamani wa Barcelona Ronaldo Luís Nazário de Lima, amesema uhamisho wa nyota wa sasa wa Brazil Neymar Jr kutoka Barcelona kwenda PSG ni kama amepiga hatua moja nyuma.
Ronaldo ameyasema hayo kwenye mahojiano na chaneli ya 'Youtube' ya mchezaji wa zamani wa Brazil Arthur Antunes Coimbra maarufu kama Zico, alipoulizwa juu ya hatua alizopiga Neymar baada ya kuondoka Barcelona.
"Kwangu mimi uamzi huo ni kama kapiga hatua kurudi nyuma, lakini kila mtu huwa anatafuta changamoto mpya kama ilivyokuwa kwangu nilipoondoka Barcelona wakati huo nikajiunga na Inter Milan lakini ligi ya Italia ilikuwa na ushindani zaidi kuliko ilivyosasa ligi ya Ufaransa'', amesema Ronaldo.
Neymar aliondoka Barcelona kwenye majira ya kiangazi 2017 na kuhamia Paris Saint-Germain ya Ufaransa kwa dau la rekodi ya dunia € 222, zaidi ya shilingi bilioni 600. Neymar ameshaifungia PSG jumla ya mabao 20 katika michuano yote msimu huu ikiwemo 11 katika ligi kuu ya Ufaransa Ligue 1.
Hatua hii ya Ronaldo imekuja ikiwa ni siku mbili tu tangu Neymar mwenye miaka 25 aachwe kwenye kikosi cha UEFA mwaka 2017, huku nyota wawili Lionel Messi na Cristiano Ronaldo wakijumuishwa.