Siku 6 kabla ya kufunga mwaka 2017, wasomaji na wafuatiliaji wa habari kupitia mitandao ya kijamii ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), wametoa maoni wakiwataja mawaziri watano wa Serikali waliofanya vizuri katika maeneo wanayoyasimamia.
Wametoa maoni hayo takriban wiki moja baada ya gazeti hili kufanya tathmini ya utendaji wa mawaziri watano. Katika orodha hiyo, mawaziri wawili wameingia katika makundi yote mawili ambao ni William Lukuvi wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ummy Mwalimu anayeisimamia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto.
Wananchi wametoa maoni hayo kupitia swali lililoulizwa kwenye akaunti za MCL za mitandao ya kijamii za Instagram, Facebook na Twitter.
Swali hilo lililoambatana na picha ya Rais John Magufuli akiongoza kikao cha Baraza la Mawaziri lililisema, “Ni waziri gani katika Serikali ya Rais Magufuli ambaye amekuvutia kwa utendaji wake mwaka huu? Kwa nini? Toa maoni yako.”
Mbali ya Lukuvi na Ummy, mawaziri wengine waliotajwa kufanya vizuri kwa maoni ya wasomaji hao ni; Selemani Jafo (Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa); Dk Hamisi Kigwangalla (Maliasili na Utalii) na Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano).
Kwa maoni yao, Lukuvi ndiye anayeongoza akifuatiwa na Jafo, Dk Kigwangalla, Ummy na Profesa Makame.
Hadi jana jioni, Lukuvi alikuwa akiongoza katika mitandao yote ya Instagram, Facebook na Twitter akimwagiwa sifa na wasomaji zaidi ya 100.
Katika gazeti hili toleo la Desemba 16, mawaziri waliotajwa mbali ya Lukuvi na Ummy walikuwa, Angellah Kairuki wakati huo akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora na Utumishi), Profesa Palamagamba Kabudi (Katiba na Sheria) na Profesa Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi na Teknolojia).
Ingawa waliotoa maoni kupitia mitandao ya kijamii ya MCL waliwataja mawaziri hao watano, wapo ambao walisema hawakufanya vyema.
Wengine waliwataja mawaziri vivuli kutoka kambi ya upinzani akiwamo Tundu Lissu wa Katiba na Sheria huku baadhi wakimtaja aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliyeng’olewa katika wadhifa huo Machi 23.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pia ametajwa kama kiongozi anayemudu nafasi yake vyema kwa kuwasimamia watendaji walio chini yake, wakiwamo mawaziri akielezewa kuwa mwaka huu ametimiza majukumu yake vyema.
Akichangia swali hilo, angwisa137 alisema, “Kuanzia mwakani tunatarajia makubwa mno kutoka kwa mawaziri. Watakuwa wamezijua wizara zao vizuri. Ila Lukuvi yuko vizuri mno. Hamisi Kigwangalla namkubali. Ila mawaziri waache kufanya kazi kwa mazoea tunahitaji mabadiliko ya kweli.”
Mwingine alikuwa maseleizengo ambaye alisema, “Waziri Lukuvi ni pekee amefanya kazi ya wanyonge... ameokoa viwanja vingi sana vya wanyonge vilivyokuwa vimeibwa na wenye fedha. utapeli wa ardhi umepungua sana.”
Mtoa maoni mwingine, mikeuswege alisema, “Lukuvi na Jafo ni wahalisia wengine walio wengi wanafanya kwa pressure.’’
Kwa maoni yake, Isaya Wa Yesu alisema, “Majaliwa ni Waziri Mkuu ambaye anajua kuyatumia mamlaka yake vizuri, Lukuvi amerudisha nidhamu kwa maofisa ardhi pia amewapa watu uhuru na amani ya kumiliki ardhi.”
Kareemgriff alisema, “Majaliwa, kubwa kabisa alivyotenganisha utendaji wake na masuala ya kichama, amekuwa si mwongeaji bali mtendaji.”
Katika maoni yake Julius S. Bugarika alisema, “Sauti ya watu wengi ni sauti ya Mungu. Lukuvi comment (maoni) nyingi zinaukubali utendaji wake. Waziri aliyefanya vizuri kiutendaji mwaka 2017 ni William Lukuvi.”
Mtoa maoni mwingine, witnessselestin alisema, “Mh. Lukuvi sababu ametafuna mifupa mingi na migumu iliyowashinda watangulizi wake na waheshimiwa wengine waige kutoka kwake huku edo_de__best akisema ‘’Makame Mbarawa naona anasimamia vizuri taaluma yake.”
Mwingine alikuwa meshackkwila ambaye alisema, “Mh Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu ni mtu mwenye busara anaongea kwa kufikiri sana naweza kusema ni kiongozi bora wa kuigwa.”
France Kavishe alisema, “Dah kwangu waziri aliyefanya vizuri na anayefanya vizuri awamu hii kwangu ni Mh. Dr @HKigwangalla.”
Mchangiaji mwingine, festosimkwayi_sr alisema, “Mheshimiwa Ummy Mwalimu anafanya mambo yake katika kulitumikia Taifa kwa uhakika bila papara wala mbwembwe. Hakika ni waziri wa afya anayetumia elimu na dhamana aliyopewa vyema.”
Akizungumzia maoni hayo ya wasomaji wa MCL, Lukuvi alisema, “Nimefurahi kuona wameridhika na utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Ardhi, tutaendeleza ushirikiano huo.”
Waziri Lukuvi alisema moja ya jukumu alilopewa na Rais John Magufuli ni kuhakikisha anamaliza migogoro ya ardhi.
Alisema anafanikiwa kutokana na juhudi zake na ushirikiano anaoupata kutoka kwa watendaji wa wizara.
“Tuliacha watendaji wa Serikali huko nyuma wakatengeneza migogoro, hakuna mgogoro wa ardhi ambao hauhusiki na watendaji au viongozi wa Serikali. Nimeambiwa na Rais ndani ya miaka mitano hii jukumu kubwa liwe ni kutatua migogoro ya ardhi,” alisema Lukuvi.
Akizungumzia hilo, Waziri Ummy alianza kwa pongezi akisema, “Nashukuru kwa ‘feedback’ kutoka kwenu na kutoka kwa wananchi, nawashukuru sana! Hakika mnanitia moyo katika utendaji wangu.”
Alisema sekta ya afya bado inakabiliwa na changamoto nyingi lakini anachopenda kuwaahidi Watanzania ni kuendelea kupambana usiku na mchana ili kutatua changamoto kadhaa.
Waziri Ummy alizitaja changamoto hizo kuwa ni kuendelea kuboresha huduma za mama na mtoto ili kupunguza vifo vya wajawazito na uzazi na kuimarisha upatikanaji wa dawa muhimu katika ngazi zote za kutoa huduma na hasa ngazi ya msingi yaani zahanati na vituo vya afya.
Alitaja mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuimarisha hospitali za rufaa za mikoa ili kuziwezesha kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa kuzipatia madaktari bingwa, vifaa na vifaa tiba lengo likiwa ni kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Jambo lingine ambalo alisema wizara yake itahakikisha inalifanya ni, “Kuongeza idadi ya Watanzania wanaojiunga katika mifuko ya bima ya afya ili kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha pindi wakiugua. Hivi sasa ni asilimia 32 tu ya Watanzania wamejiunga na mifuko ya bima ya afya. Ninaamini kwa mwaka 2018, sekta ya afya tutapata mafanikio makubwa,” alisema waziri Ummy.
Waziri Mbarawa akichangia swali hilo kwenye ukurasa wetu wa Twitter alindika ‘’Shukrani kwa wote tuendelee kushirikiana kwa maendeleo ya wananchi wote.”
Juhudi za kuwapata mawaziri wengine waliotajwa na wasomaji ambao ni Dk Kigwangalla na Jafo ziligonga mwamba kwa kuwa simu zao za mikononi ziliita pasipo kupokewa na wengine hazikupatika kabisa.