Monday, 25 December 2017

Wizi Wa Miundombinu Ya Umeme, Wananchi Waiomba Tanesco Kukamilisha Fidia



Wananchi wa Kijiji cha Misigiri, Tarafa ya Ndago,Wilayani Iramba,Mkoani Singida wameliomba shirika la ugavi umeme Tanzania (TANESCO) kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi 17 wa Kijiji hicho ambao maeneo yao yamepitiwa na njia kuu ya umeme wa KV 400 kutoka Mkoani Iringa hadi Shinyanga ili waweze kuondoa chuki kati yao na shirika hilo na hivyo kuwa walinzi wakubwa wa miundombinu iliyowekwa kwenye njia hiyo.
Wananchi hao, Kanasi Peter, Boniface Nzenga, Mwita Wilson Makanga na Helena Yuda wamesema vitendo vya uharibifu na wizi wa miundombinu ya shirika hilo vinasababishwa na shirika hilo kutowalipa wananchi hao madai yao ya fidia kutokana na njia kubwa ya umeme kupita kwenye maeneo waliyokuwa wakilima na hivyo kuwafanya waendelee kufanya shughuli za uzalishajimali zilizokuwa zikiwaingizia kipato.
Malalamiko hayo yametolewa na wananchi wa Kijiji cha Misigiri,Tarafa ya Ndago wakati uongozi wa shirika la TANESCO ulipokwenda kutoa elimu kwa wananchi hao juu ya kushirikiana na shirika hilo kulinda wizi pamoja na uharibifu wa miundombinu ya shirika hilo.

Waziri Mpina aagiza kuvvunjwa mkataba Kati ya Ranchi ya Mzeri na Overland



Waziri wa mifugo na uvuvi Luhaga Mpina ameagiza kuvunjwa kwa mkataba kati ya ranchi ya Mzeri na Kampuni ya Overland ambayo ilianzisha kampuni ya OVENCO kutokana na kasoro mbalimbali zilizojitokeza na kutengenezwa mkataba mpya utakaozingatia maslahi ya taifa.
Agizo hilo amelitoa wakati wa ziara yake katika ranchi Mzeri iliyopo wilayani Handeni ambapo baada ya kupokea taarifa amebaini kutokamilika kwa uundwaji wa bodi kampuni OVENCO na kuiacha kampuni ya overland yenye 70% ya hisa kufanya shughuli zake bila usimamizi wa pamoja.
Anesena Mkataba uliopo ambao umedumu kwa zaidi ya miaka miwil uvunjwe ifikapo disemba 31 mwaka huu na kutengeneza mpya ambao utaainisha thamani ya uwekezaji na ukubwa wa eneo kulingana na mahitaji badala ya kuhodhi ardhi kubwa bila ya kuendelezwa
Aidha Waziri Mpina amesema pamoja na kasoro zilizopo kwenye mkataba wa uanzishwaji wa Ovenco ameridhishwa na juhudi za mwekezaji katika kuinua sekta ya mifugo na kwamba wakati mkataba mpya ukiandaliwa maslahi ya uwekezaji huyo yatalindwa
Akizungumzia hatua hiyo ya waziri meneja uzalishaji uendeshaji ranchi za taifa Bwire Kafumu amesema Narco itafanya uhakiki wa thamani halisi wa mali zilizopo na kuishauri serikali.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni ya overland Feisal edha amesema ameridhishwa na hatua ya waziri ambayoitatoa fursa na haki kwa pande zote

Muuza bangi aingia kimakosa ndani ya gari la polisi akidhani ni teksi



Mtu anayeshukiwa kuwa muuza madawa ya kulevya alijipa krismasi asiyoitaka wakati aliingia kwenye teksi akiwa na karibu misokoto 1000 ya bangi na kugundua kuwa alikuwa ameingi kwenye gari la polisi nchini Denmark.
Polisi nchini Denmak walisema kuwa mwanamume huyo alikuwa akirudi nyumbani wakati alifanya makosa hayo mabaya.
Makosa hayo yalitokea katika eneo la Christiana, wilaya moja ya mji mkuu Copenhagen iliyo maarfu kwa biashara ya madawa ya kulevya.
Polisi wanasema kuwa mwanamume huyo atafunguliwa mashtaka, Polisi walisema kuwa walifurahi kumuona, kwani alikuwa amebeba misokoto 1,000 ya bangi.
Bangi ni haramu nchini Denmark.
Polisi wamefanya uvamizi mara kadhaa katika wilaya ya Christiana miezi ya hivi karibuni waliwatafuta wauza madawa ya kulevya .

Yanga yavuka kizingiti kombe la FA



Klabu ya Soka ya Yanga imeweza kuibuka na ushindi wa bao 2-0 dhidi Reha FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la FA mzunguko wa pili mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mchezo huo ambao timu ya Reha ilianza kwa kushambulia upande wa wapinzani wao na kuwashika vilivyo kwani hadi dakika 45 zinamalizika hakuna timu ailiyofunga katika kipindi cha pili timu ya Yanga ikabadilika na kuanza kujaribu kupiga mashuti ambapo dakika ya 82 mchezaji Pius Buswita aliwapatia Yanga bao la kwanza lilodumu kwa dakika tatu na Amiss Tambwe aliweza kuongeza bao lingine lilowafanya kusonga mbele katika michuano hiyo.

Nuh Mziwanda Akanusha Kurudiana na Shilole



Staa wa Bongo fleva Naftal Mlawa ‘Nuh Mziwanda’, amefungukia tetesi za kurudiana na msanii mwenzake wa ambaye pia alikuwa mepenzi wake wa zamani kabla ya kila mtu kushika hamsini zake Zuwena Mohamed ‘Shilole’ kwa kuweka wazi kwamba hana wazo wala hisia zozote za kurudiana na msanii huyo kwa siku za hivi karibuni.
Akizungumzia stori hizo Nuh mziwanda alisema kwamba amekuwa akizisikia tetesi za uwepo wa penzi la chinichini kati yake na Shilole licha ya kwamba mwanamke huyo ni mke wa mtu.
“Siwezi kurudiana na Shilole hata iweje, mimi kurudiana na shilole ni stori tu ambazo watu wanazusha,ukweli siwezi kumrudia mtu huyo. Na sivutiwi kuzungumzia habari zake kwa sasa kwakuwa anamaisha yake ya ndoa takatifu, si vizuri kumwongelea kwa sasa. Siwezi kurudiana na Shishi” alisema Nuh Mziwanda

Misingi ya Uvumilivu kwenye Ndoa



Ni wazi kuwa migogoro kwenye uhusiano wowote ule ipo, hasa pale wenza hao wasipopeana nafasi ya kusikilizana.
Kila siku narejea hii hoja kuwa, hata kwenye uhusiano wa mapenzi lazima kutakuwepo na mikwaruzano ya hapa na pale jambo la msingi ni namna ya kushughulikia misuguano hiyo bila kuibua chuki na hatimaye kuvunja uhusiano.
Hata katika uhusiano wa kawaida, mikwaruzano na misuguano ni kama kukanyaga bomu, bila kuchukua tahadhari na kutegua bomu lenyewe, ukiondoa mguu mtu bomu hilo linalipuka na kuharibu kila kitu.
Uvumilivu ndio jibu kubwa kwa wenza endapo itatokea kukwaruzana au kutoelewana.
Endapo mwenza wako amekuudhi na kukupandisha hasira jambo la msingi kabisa ni kuhakikisha unadhibiti hasira hizo. Jaribu kuelewa kwanza tatizo kabla hasira hazijakuathiri na kukutawala.
Kumbuka kuwa hasira hasara na siku zote mtu mwenye hasira huzungumza na kufanya mambo ambayo baadaye hujikuta akijilaumu. Lakini pia watalamu wa masula ya mahusiano wanasema ya kwamba siku zote epuka kuchukua maamuzi ukiwa na hasira.
Unapotokea msuguano katika mapenzi epuka kuwa mzungumzaji na mlalamishi, kuwa mtulivu na tanguliza busara mbele kabla ya kutamka chochote kinywani kwako.
Huo ndio msingi wa uvumilivu.
Katika hili, vitabu vingi vya uhusiano vinashauri kuwa endapo mwenza anaona hali na mazingira ya mazungumzo hairidhishi kutokana na ugomvi wenyewe ni bora kuahirisha mazungumzo hayo na kupanga muda mwingine wakati wote wawili wakiwa wametulia.

Sunday, 24 December 2017

Jeshi la Polisi Lawaonya Wavunjifu Wa amani



Jeshi la Polisi Kanda Maalum jijini Dar es salaam, limewaonya na kuwatahadharisha watu wenye tabia za uhalifu kutovunja sheria katika siku hizi za sikuu, kwani limekaa macho na kujipanga kuwadhibiti.
Taarifa hiyo imetolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es salaam Lazaro Mambosasa alipokuwa akizungumza na mwandishi wa East Africa Television, ambapo amesema kwamba hapo kesho jiji litazingirwa na askari wa kutosha kuhakikisha wakazi wake wanakuwa salama dhidi ya vitendo viovu.
"Kwanza nimepiga marufuku disco toto kwa ajili ya usalama, lakini pia kwenye fukwe polisi watakuwepo kuangalia usalama, wale wanaovizia mikoba na vitu vingine niwaambie tu hawatakuwa salama, kwani askari wetu wamejipanga kukabiliana nao, kutakuwa na ulinzi wa kutosha, askari wa jeshi la polisi, tumeomba ushirikiano kutoka kwa askari wa makampuni binafsi, walinzi shirikishi, hivyo hawataweza kwenda hatua tatu bila kudakwa", amesema Mambosasa.
Sambamba na hilo Kamanda Mambo sasa amewataka wananchi kusherehekea sikukuu hizo kwa amani wakiwa majumbani kwao na familia zao, ili kuhakikisha watoto wanakuwa salama, huku akiwaonya wale watumia vyombo vya moto kuwa makini na kufuata sheria za barabara.
"Tunaelekeza watu watii sheria, tunajua watu wakishakunywa wanapoteza ufahamu, wito ni kwamba watii sheria za barabarani na washerehekee na familia zao majumbani mwao, ili watoto waendelee kuwa salama, wasiwaache wenyewe", amesema Kamanda Mambosasa.
Kamanda Mambosasa amesema ulinzi huo mkubwa na wa hali juu utaendelea mpaka sikukuu za mwaka mpya, ili kudhibiti matukio ya uhalifu yanayotokea siku za sikukuu.

Sherehe za Mapinduzi Kugharimu 1.2 bilioni



Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema itatumia zaidi ya Sh1.2 bilioni kwa maadhimisho ya miaka 54 ya Mapinduzi ya Zanzibar ambayo kilele chake kitakuwa Januari 12 mwakani.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed amesema hayo leo Jumapili Desemba 24,2017 ofisini kwake Vuga mjini Unguja alipotoa taarifa ya maandalizi ya sherehe hizo.
Amesema fedha hizo zinatarajiwa kutumika katika maandalizi ya siku ya kilele, ufunguzi wa miradi 49 ya maendeleo ya kiuchumi, miradi ya maji, majengo ya shule, umeme na barabara.
Waziri amesema miradi 33 itazinduliwa baada ya kukamilika na 16 itawekwa mawe ya msingi. Miradi hiyo ni ya taasisi za umma, jamii na ya wawekezaji.
Waziri Mohamed amesema Serikali imepiga hatua katika kufanikisha huduma za kijamii na maendeleo sambamba na lengo la Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.
Amesema wananchi wanapaswa kujitokeza kuunga mkono jitihada za Serikali katika kufanikisha maadhimisho hayo ambayo yatazinduliwa Desemba 30,2017 kwa kufanya usafi wa mazingira.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Dk Idriss Muslim Hijja amesema miradi iliyopendekezwa kuingizwa katika maadhimisho imefuatiliwa na kutolewa taarifa kwa sekretarieti ya halmashauri ya sherehe na maadhimisho ya kitaifa.
Amesema katika uzinduzi na uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi, viongozi wa kitaifa wa Serikali zote mbili wamejumuishwa wakiwemo marais, mawaziri na wastaafu wa pande zote mbili.
Kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa Januari 12,2018 katika Uwanja wa Amani mjini Unguja ambako Rais Ali Mohammed Shein atakuwa mgeni ra

Mabasi ya Kwenda Mikoani Kufanya kazi masaa 24



Mkurugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra), Johansen Kahatano amesema kuanzia mwakani wataandaa mkakati wa mabasi kufanya kazi saa 24 na kupandisha nauli wakati wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka.
Kahatano amesema hayo leo Jumapili Desemba 24,2017 alipozungumza na waandishi wa habari eneo la Ubungo kuhusu hali ya usafiri.
Amesema kumekuwa na changamoto ya usafiri takriban kila mwisho wa mwaka na kusababisha kero kwa abiria.
“Tumeliona hilo na sisi Sumatra tumeandaa mpango ambao tunafikiri unaweza ukawa suluhisho la adha ya usafiri hapa Ubungo; kwanza tunafikiria kuruhusu mabasi kufanya kazi saa 24 wakati wa sikukuu za mwishoni mwa mwaka,” amesema.
Amesema pia wataweka nauli kubwa wakati wa msimu wa sikukuu ili abiria wasafiri kipindi ambacho nauli itakuwa ndogo.
Kahatano amesema mpango huo utaanza kufanyiwa kazi mwakani kwa kukaa na wadau wa usafiri na wananchi kuujadili.
Akizungumzia hali ya usafiri kituoni Ubungo amesema iko shwari kulinganisha na jana ambapo abiria walikuwa wengi na mabasi yalikuwa machache.
“Tumejitahidi kusaidia kupunguza adha hii kwa leo baada ya kuruhusu watu wenye magari yenye uwezo wa kupakia abiria kuja na kupatiwa vibali hapa Ubungo,” amesema.

VIDEO:Mtoto wa Babu SEYA afunguka kauli ya Magufuli, Lowasa



Mtoto wa Babu Seya aitwaye, Mbangu Nguza amesema kuwa wao kama familia wanamshukuru Rais Dk John Magufuli kutokana na kuwaachia kwa msamaha Baba yake, Nguza Viking 'Babu Seya' na mdogo wake Papii Kocha waliokuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela katika gereza la Ukonga, siku ya Uhuru Desemba 9 mwaka huu.
Pia amefunguka kuhusiana na kauli ya aliyekuwa mgombea wa Urais wa UKAWA, Edward Lowasa ambaye aliahidi kuwaachia huru endapo angeshinda urais mwaka 2015.
TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI....USISAHAU KUSUBSCRIBE


Mwanamke Amfungia mumewe Ndani na Kisha Kumchoma moto - Mtwara



Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara linamsaka mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Zuhura Ismail (29) kwa tuhuma za kumuua mume wake baada ya kumfungia ndani na kisha kuichoma nyumba kwa petroli.
Taarifa hizo zimetolewa na Kamanda wa Polisi mkoani humo Lucas Mkondya, ambapo amesema kwamba chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi, baada ya mwanamke huyo kugundua kuwa aliyekuwa mume wake anaishi na mke mwingine, na kuamua kumvizia nyumbani kwake kisha kuichoma moto na kusababisha kifo chake.
"Ni kweli Jeshi la Polisi Mkoani Mtwara linamsaka mwanamke mmoja ayefahamika kwa jina la Zuhura Ismail kwa tuhuma za kuichoma nyumba aliyokuwa anaishi mume wake na mwanamke mwingine, kutokana na wivu wa kimapenzi baada ya Zuhura kugundua kuwa mumewe anaishi na mke mwingine, na kuamua kwenda kuchoma nyumba hiyo moto na kuwasababishia majeraha makubwa, ambapo mumewe alipelekwa hospitali lakini kutokana na majereha hayo makubwa alifariki dunia, lakini mwanamke aliyekuwa nae anaendelea vizuri", amesema Kamanda Mkondya.
Aidha Kamanda Mkondya amesema mara baada ya tukio hilo mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Zuhura Ismail alitoroka na kwenda kusikojulikana, na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka na pindi atakapopatikana watatoa taarifa.

Rose Muhando Awafungukia wanaomsema kuhusu kujiunga CCM



Msanii wa muziki wa Injili nchini Tanzania, Rose Muhando ameamua kufunguka ya moyoni baada ya kupokea maoni mengi ya watu wakimponda kuhusu maamuzi yake ya kujiunga na Chama cha Mapinduzi.
Rose Muhando amesema wanaomponda na kumkebehi anawachukulia ni watu wa kawaida kwani hawezi kujifunza kwa watu walioshindwa huku akidai ameshazoea kusemwa.
“Watu wengine hawaelewagi nini wanachoongea, wanaongea ili waonekane nao wanaongea. Mimi ni mtu ambaye ninayejitambua sawa eehhh!! mimi hata sijali, nimeshazoea kutukanwa kwahiyo hata sihangaikagi na maneno yao. Mimi ni funzi kwa walioshindwa na nimeondoka kwa walioshinda, walioshindwa wana maneno mengi kutokana na nilishaimba uoga wako ndio umasikini wako, Mimi siwezi kuishi kwa uoga kwenye nchi yangu kwani ni maamuzi yangu na sijavunja sheria ya nchi na ningeogopa zaidi kama ingekuwa ni dhambi.”amesema Rose Muhando kwenye mahojiano yake na E-Gospel ya Radio E-FM.
Mapema mwezi huu kwenye Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi mjini Dodoma, Rose Muhando alialikwa kutumbuiza kwenye mkutano huo na kabla ya kukaribishwa Jukwaani, Katibu Mwenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema Rose na Kundi lake wamekuja na maombi mawili likiwemo la kujiunga CCM na kutumbuiza huku akisema kuwa vyote vimekubaliwa.
Awali Rose Muhando hakuwa kwenye upande wowote wa vyama vya kisiasa na amesema kujiunga CCM au Chama chochote ni maamuzi yake na sio dhambi wala kosa kisheria.

RC Gambo ashiliki Kwenye Ujenzi Wa Hospitali ya Wilaya



Mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amezindua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Arusha mjini katika eneo la Njiro kontena. Shughuli ambayo ilihidhuriwa na mamia ya wakazi wa Jiji hilo.
Akizungumza na wananchi hao Gambo alisema “Nina furaha sana kushuhudia tukio hili litakaloacha alama katika maisha ya watu wetu wa Arusha,kwani wakati wa kampeni Mhe Rais Magufuli aliahidi na tunatekeleza kwa vitendo.”
Hospitali hiyo inatarajiwa kuhudumia wakazi zaidi ya laki nne kutoka wilayani humo na maeneo ya jirani ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanasababisha hospitali ya mkoa ya Mount Meru kuelemewa.
 Vile vile Gambo anasema kwa sasa mapato yanayokusanywa na Jiji la Arusha kwa mwaka bado hayatoshelezi hata kulipa mishahara ya watumishi wake na kwa maana hiyo ni muhimu kuweka mifumo thabiti ya ukusanyaji wa mapato jijini humo.
“Jiji la Arusha mapato yake ya ndani kwa mwaka hayazidi bilioni 12 na mishahara pekee ya watumishi wa halmashauri ni zaidi ya bilioni 40, sasa hapo ukilipa tu mishahara hela yote inakwisha na bado unakua na deni, sasa hata fedha za maendeleo zitatoka wapi zaidi ya kutegemea hela zinazoletwa na Magufuli?? Gambo alihoji.
Ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Arusha kwa awamu ya kwanza unafanyika katika moja ya maeneo ya wazi yaliyo kuwa yakimilikiwa kinyemelela na baadhi ya wajanja wachache na kwa sasa ujenzi umeanza ambao utagharimu kiasi cha shilingi milioni 500 hii ikiwa ni jengo la Ghorofa moja kwa ajili ya wagonjwa wa nje.
Naye mkurugenzi wa Jiji la Arusha Athuman Kihamia alimshukuru Mhe Gambo kwa kuweza kulipigania eneo hilo mpaka limeweza kurudi kwenye mikono ya wananchi.
“Kwakweli kama sio jitihada zako eneo hili lilishaondoka mikononi mwetu hivyo kwa niaba ya wananchi wa Arusha ninakushukuru sana, pia nikuahidi tutazingatia ushauri wako wa kulitumia eneo hili vizuri kwa kujenga majengo ya ghorofa kuanzia tano ili kulitumia eneo hili vizuri” alisema Kihamia. Ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajiwa kukamilika June mwaka 2018 ambapo zaidi ya wakazi laki 4 watapata huduma ya afya karibu na