Sunday, 17 December 2017

Njia 10 Za Kupunguza Magonjwa Ya Mlipuko Wa Kuku



Mlipuko wa magonjwa ni moja ya sababu za hasara kubwa kwa wafugaji na vifo vinavyotokea kwa wakati mmoja. Pindi mfugaji anapokumbwa na janga la vifo vya ndege, kabla ya kufikia mwisho wa mzunguko wa uzalishaji hivyo basi asitarajie kupata faida nzuri mara baada ya mauzo.
Hasara itokanayo na vifo inaweza kuepukika au kupunguzwa na kutokea kwa kiasi kidogo.
Hili linawezekana, ifuatayo ni namna ya kufanikisha hilo;-
1. Osha vyombo vya maji kila wakati na mwaga maji yaliyobaki.
Hakikisha unamwaga maji yaliyosalia mbali na kuosha chombo na sabuni kila siku, weka maji safi yasiyo na dawa na wala usitumie maji ya mto au yale usiyoyajua chanzo chake. Kama utaweka maji dawa basi tumia ‘vitamini’ muhimu kama ‘vitalyte’ ambazo zinasaidia kuua vijidudu.
2. Wape maji kabla ya chakula.
Ndege wapo tofauti na binadamu au wanyama wengine. Hakikisha unawapa maji kabla ya chakula hasa kama unatumia maranda, hii ni kuhakikisha hawakanyagani wanapogombania chakula sehemu moja.
3. Usiwape chakula chenye uvundo.
Ni hatari sana kuwapa ndege/kuku wako chakula chenye ukungu, ni kama kuwalisha sumu. Ukungu au uvundo huwafanya kuku waugue kirahisi sana au kuwasababishia madhara mengine kiafya.
4. Fuatilia kwa makini ratiba za chanjo na tiba.
Mfugaji unatakiwa kupata tiba na chanjo sahihi kwa ndege unaowafuga. Kuchanja ndege kutasaidia sana kuimarisha kinga yao dhidi ya magonjwa hatari kama kideri, ndui, gumboro na mareksi. Dawa kama vile za minyoo na antibayotiki ni muhimu sana kwenye afya ya kuku na ndege wengine.
5. Nunua na fuga vifaranga wenye afya njema.
Matatizo mengi ya afya ya ndege au kuku ni matokeo ya maisha duni ya awali ya kuku hao au huwa wanarithi. Itambulike hivi, baadhi ya ndege/kuku hurithi afya mbovu kutoka kwa wazazi wao. Hata hivyo baadhi ya watotoleshaji pia wanafuga kuku ambao wana afya mbovu na hivyo huuza vifaranga au mayai dhaifu na waathirika na hivyo mnunuzi anajikuta ananunua matatizo.
6. Zuia mkusanyiko wa hewa ya ammonia.
Maranda yakikaa muda mrefu bandani, hufanya hewa ya ammonia kuzalishwa kwa wingi, hewa hii hufanya ndege wapaliwe hadi kufa. Kila mara ondoa maranda mabichi au yaliyovunda na weka mengine haraka iwezekanavyo ili kuepuka vifo vitokanavyo na kupaliwa au magonjwa ya mfumo wa hewa.
7. Zuia panya na vicheche.
Banda la ndege linatakiwa lisiruhusu panya au wanyama wadogo jamii ya kicheche kuingia ndani, na ndege wa mwituni kwa kuweka nyavu au kupulizia dawa, ikiwa watapata upenyo wataua na kula ndege/kuku wako na kuacha vimelea vya magonjwa wanapokula vyakula au kunywa maji ya ndege wako.
8. Zingatia usafi na usalama.
Kipengele hiki cha usafi na usalama ni kipana ila unachotakiwa kufanya ni kuzingatia usafi nje na ndani ya banda. Unatakiwa ukamilishe usalama wa afya ya ndege/kuku wako kila wakati, jambo ambalo wafugaji wengi hutekeleza pindi wanapo shitukizwa na mlipuko wa magonjwa.
9. Wape chakula cha kutosha.
Ndege kama walivyo wanyama wengine, hawawezi kukua na kuzalisha vizuri endapo wanapewa chakula duni na kidogo. Chakula bora ni msingi imara na ni kinga kwani chakula duni hupelekea uzito kupungua na kinga kuwa chini na hivyo hufa mapema. Jitahidi wape kuku chakula cha kutosha ila usiwazidishie.
10. Wakinge dhidi ya baridi kali.
Baridi kali ni adui kwa afya ya wanyama, ndege na binadamu. Jaribu kila uwezavyo kuwakinga kuwakinga ndege wako na baridi kali kwani inaua haraka sana kama sumu. Wawekee chanzo cha joto wakati wa baridi au jenga banda ambalo halipitishi baridi kali.
Hizo ndizo njia muhimu ambazo ukiwa mfagaji unazoweza kuzitumia ili kukinga magonjwa yanatokanayo na kuku.

Mambo 5 Ya Kuzingatia, Kama Wewe Ni Mjasiriamali Unayetaka Mafanikio Makubwa.



Mafanikio ni kitu cha lazima sana katika safari ya mjasiriamali. Uwe mjasiriamali mdogo, wa kati au mkubwa kwa vyovyote vile unahitaji mafanikio. Lakini ili kufanikiwa na kufikia mafanikio hayo, yapo mambo ya msingi ambayo unatakiwa kuyazingatia.
Mambo hayo ni kama haya yafuatayo:-
1. Kujiwekea malengo.
Ukiwa kama mjasiriamali unayetakiwa kufikia mafanikio makubwa, suala la kujiwekea malengo ni lazima kwako. Unapokuwa na malengo yanakuwa yanakupa mwelekeo sahihi wa kupata kile unachokitaka. Hiki ni kitu ambacho unahitaji kukizingatia sana kwani ni nguzo kubwa ya kufikia mafanikio makubwa.
2. Kujitoa Mhanga(Take Risks)
Hakuna mafanikio makubwa utakayoyapata bila kujitoa mhanga. Wajasirimali wote wakubwa ni watu wa kujitoa mhanga sana. Wanakuwa wako tayari kutoa kitu chochote ilimradi wafikie malengo yao. Kitu cha kuzingatia hata kwako wewe unalazimika kujitoa mhanga na kulipia gharama ili kufikia mafanikio makubwa.
3. Kutokuogopa Kushindwa.
Wengi wetu tumefundiswa sana kuwa kushindwa ni vibaya. Hali ambayo hupelekea tunakuwa tunaogopa kujaribu karibu kila kitu kwa sababu ya hofu ya kushindwa. Ikiwa wewe ni mjariamali unatakiwa kuwa jasiri na kujua kwamba mafanikio yanataka roho ya ujasiri na kutokuogopa kushindwa. Hiyo ndiyo siri itakayokifikisha kwenye kilele cha mafanikio na sio uoga unaouendekeza.
4. Acha kuridhika mapema.
Ni kosa kubwa sana kujikuta unaridhika mapema eti tu kwa sababu ya faida unayoitengeneza sasa. Ni vizri kujua, safari ya mafanikio bado ni ndefu kwako, hivyo hutakiwi kuridhika kwa namna yoyote ile. Kama kuna jambo umelifanikisha, endelea kwenye jambo lingine hadi kujenga mafanikio makubwa kabisa.
5. Tafuta ‘Mentor’
Acha kujidanganyai kuingia kwenye safari ya mafanikio huku ukiwa peke yako. Ikitokea umekwama kwa sababu huna mtu wa kukuelekeza au kukushauri, huo ndiyo unakuwa mwisho wako. Hivyo ni muhimu kuwa na kiongozi wako ‘mentor’ ambaye atakuongoza kwenye kufikia mafanikio yako.
Kwa kuyajua mambo hayo yatakusaidia wewe mjasiriamali kuweza kuendelea mbele zaidi na kufanikiwa katika safari yako yamafanikio.

Kama unaogopa kufanya kitu hiki, sahau kuhusu Mafanikio katika Maisha yako yote


Fikiria kila unachokijua na kukikumbuka kuhusu mabadiliko unayotaka yawe katika maisha yako, halafu uone ukweli huu kama kweli nawe ni mmoja kati ya watu wanaotaka mafanikio au uko nje ya mstari wa mafanikio na pengine tu wewe hujijui. Kama kweli unataka mafanikio, ni kwanini mara kwa mara umekuwa ukisita au kuogopa kufanya jambo ambalo lingeweza kubadili maisha yako na kukuletea mafanikio mkubwa? Hili ndilo tatizo walilonalo watu wengi wanahofia sana kufanya mabadiliko kwa namna moja au nyingine hata kwenye yale malengo waliojiwekea wao wenyewe kuna wakati huwa wanaogopa pia.
Kimaumbile, kila binadamiu anahofia mabadiliko, lakini hofu ya mabadiliko inapozidi kuwa kubwa na kukuzuia kufanya mambo ya maana kwako, hofu hii sasa hugeuka kuwa ni maradhi yanayokuzuia wewe kufanikiwa. Hebu fikiria tena, ni mara ngapi umekuwa ukitaka kufanya mabadiliko Fulani katika maisha yako, lakini umekuwa ukijikuta ukishindwa kufanya hivyo kutokana na kuogopa kufanya vitu Fulani? Ni mara ngapi umekuwa ukitaka kuingia kwenye biashara lakini umekuwa na hofu nyingi zinakuzuia? Hivi ndivyo ilivyo mabadiliko huogopwa, wakati mwingine bila sababu ya msingi.
Wengi wetu kutokana na kuogopa mabadiliko, hujikuta ni watu wa kutoa sababu ambazo hata hazina mashiko zinazosababisha wao washindwe kutekeleza malengo na mipango waliojiwekea. Utakuta mtu anakwambia hawezi kufanya biashara ni kwa sababu hana mtaji, ukija kuchunguza kidogo utagundua kuwa hiyo ni sababu ambayo amekuwa akiitoa kwa muda mrefu, iweje kila siku mtu huyohuyo awe hana mtaji tu. Kama uko hivi una hofu tu hata kwa vitu vidogo ambavyo ungeweza kuvifanyana , tambua kuwa kuanzia sasa unaye adui mkubwa ndani mwako anayekuzuia kufanikiwa. Na unapoogopa kufanya mabadiliko ambayo unaahitaji sasa ili ufanikiwe, sahau kuhusu mafanikio katika maisha yako yote.
Tatizo kubwa utakalokuwa nalo linalosababishwa na hofu hii ya kuogopa kufanya mabadiliko ni lazima utakuwa mtu wa kutaka mafanikio ya harakaharaka. Watu wengi wenye mawazo ya kutaka kufanikiwa leoleo hata kama wameanza biashara leo, wengi wao huwa wana hofu hii kubwa ya mabadiliko ndani mwao, unaweza kufanya utafiti mdogo utagundua ukweli huu ulio wazi. Hawa ni watu ambao kiuhalisia hawaijui wala kuiamini subira ndani mwao, bali ni watu wakutaka mfumo wa maisha uwe ambao unaanza leo biashara na wiki ijayo uwe tajiri ni kitu ambacho hakiwezekani kabisa.
Hivi ndivyo walivyo watanzania wengi wanaogopa mabadiliko na kuamini katika miujiza, sio katika wao wenyewe kutenda na kuona matokeo. Hebu jaribu kukagua maisha ya walio wengi utakuja kugundua ukweli huu ni watu wanaofikiria sana leo, sasa hivi, siyo baadaye. Hata malengo yao ni ya karibu sana na hawataki shida, wanataka wafanye leo, wamudu leo na kila kitu kimalizike leo. Sijui kesho watafanya kitu gani? Ukimwambia mtanzania aanzishe mradi ili aje faidi baada ya miaka 10 kutoka sasa kwanza atakushangaa, kisha atakucheka we hadi mbavu zimuume. Anataka leo hata kama ni kwa miujiza.
Ndiyo maana wengi kati ya Watanzania hawana malengo, wanaishi tu na kutawaliwa na hofu za mabadiliko. Kuweka malengo siyo sehemu ya maisha yao, kwani malengo yanataka mtu mwenye subira, mtu anayeamini kwamba maisha ni kuanguka na kusimama. Wanachojua kikubwa ni kulalamika na kulaumu, kuponda na kukejeli, kwa sababu wao wamekata tamaa bila kujijua. Ndiyo maana ni watanzania wanne tu kati ya kumi ambao wanafanya kazi, wanatoka jasho na wanaweza kusubiri bila kukata tamaa, wengine waliobaki wanasubiri ujanja ujanja tu ilimradi wafanikiwe hata kama ni kwa kufanya uhalifu wa aina yoyote.
Ni watu ambao wanataka kuishi kihadithi, wawe na pete ambayo wanaweza kuiamuru iwape wakitakacho na wakipate. Maisha ni ya kibunuasi- abunuasi tu, watu hawa kwao mabadiliko ni kitu kigumu sana kwao na kinaogopwa kweli. Kama unataka mafanikio ya kweli yawe kwako, unatakiwa kubadilisha fikra za zako na kuamua kukubali kuwa mafanikio yanahitaji mabadiliko makubwa sana ambayo wewe mwenyewe unatakiwa uyafanye kwa kujitoa hasa. Acha kuwa na hofu zisizo na maana zinazokuzuia wewe usifanikiwe, chukua hatua katika maisha yako, kuyafikia maisha unayoyataka.

Saturday, 16 December 2017

Zaidi Ya kaya 100 zakosa makazi Songea



Zaidi ya Familia 100 hazina mahali pa kuishi kufuatia nyumba zao kubomoka na kuezuliwa kwa upepo uliuoambatana na mvua kali iliyonyesha usiku wa kuamkia leo ambapo nyumba zaidi ya 60 na vyumba vitano vya madarasa ya shule ya msingi Chandamali kata ya Bombambili manispaa ya Songea vimeezuliwa.
Kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Songea chini ya mwenyekiti wake mkuu wa wilaya Pololeti Mgema wamewatembelea wananchi waliokumbwa na kadhia hiyo kwa lengo la kutoa pole kwa wahanga.
Serikali imewataka wananchi kuzingatia kanuni bora za ujenzi kwani nyumba nyingi zilizoezuka zimejengwa bila kuzingatia kanuni za ujenzi, aidha serikali itaelekeza nguvu zake kukarabati vyumba vitano vya shule ya msingi Chandamali hivyo wananchi waanze kukarabati nyumba zao bila kusubiri msaada.
Wakati huo miundo mbinu ya Tanesco nguzo zimedondoka na nyaya za umeme kusambaa hovyo, aidha huko Matimila halmashauri ya wilaya ya Songea nyuma 15 zimeezuka na jengo la utawala la sekondari ya Matimila gharama za hasara iliyotokana na maafa hayo bado haijafahamika serikali inaendelea kukusanya taarifa sahihi.

Simba yafanya Maamuzi Magumu



SIMBA SC imesajili wachezaji watatu wapya wa kigeni, beki Mghana Asante Kwasi, kiungo mshambuliaji Mzambia Jonas Sakuwaha na mshambuliaji Antonio Dayo Domingues kutoka Msumbiji.
Wakati dirisha dogo la usajili linakaribia kufungwa jana, viongozi wa Simba walikuwa wanahaha kukamilisha usajili huo, hususan wa mchezaji Kwasi, ambaye bado ana mkataba na klabu yake ya sasa, Lipuli ya Iringa.
Lakini kwa Sakuwaha na Domingues hakukuwa na tatizo na habari zinasema wachezaji hao watachukua nafasi za beki Mzimbabwe, Method Mwanjali na washambuliaji, Mghana Nicholas Gyan na Mrundi Laudit Mavugo.
Wapinzani wao, Yanga wamesajili wachezaji wawili tu wapya, beki Fiston 'Festo' Kayembe Kanku kutoka Balende FC ya kwao, DRC na mshambuliaji kinda, Yohanna Nkomola ambaye ni mchezaji huru, aliyekuwamo kwenye kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys.
Azam FC imeingiza mmoja tu mpya, mshambuliaji Bernard Arthur kutoa Liberty Professional ya Ghana, baada ya kumuacha Mghana mwenzake, Yahya Mohammed na Singida United imesajili saba wapya; Lubinda Mundia kwa mkopo kutoka Res Arrows ya Zambia, Daniel Lyanga kutoka Fanja ya Oman, Kambale Salita 'Papy Kambale' kutoka Etincelles ya Rwanda, Issa Makamba, Assad Juma, Ally Ng’azi na Mohamed Abdallah wote huru waliokuwa Sereneti Boys.
Singida imewaacha wawili, Atupele Green na Pastory Athanas waliovunjiwa mikataba wakati Mohamed Titi na Frank Zakaria wametolewa kwa mkopo Stand United na Mbeya City imewasajili George Mpole kutoka Maji Maji na Abubakar Shaaban huru, baada ya kuwaacha Emmanuel Kakuti na mkongwe Mrisho Ngassa anayehamia Ndanda FC.

Ronaldo Atimiza ndoto yake



Nyota wa klabu ya soka ya Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo,
amesema anajisikia vyema kutimiza malengo yake kwenye ulimwengu wa soka na anafuraha kushindana na Lionel Messi kwa muda mrefu.
Akifanya mahojiano na tovuti rasmi ya FIFA, Ronaldo amesema ndoto yake ilikuwa kuweka historia na kuacha kumbukumbu kwenye ramani ya soka na hicho kitu kimetimia akiwa ametwaa mataji mengi pamoja na mafanikio binafsi ikiwemo tuzo tano za Ballon d’Or.
“Najisikia vizuri kutimiza malengo yangu, nilitamani sana kuweka historia kuacha jina langu kwenye vitabu vya soka, nimepata mafanikio mengi sana ngazi ya klabu na taifa, nafurahia kuwa mmoja wa wachezaji waliofanikiwa zaidi kama kuchukua tuzo tano sawa na Messi”, amesema Ronaldo.
Ronaldo ameongeza kuwa katika maisha yake amefanya kitu anachokipenda zaidi ambacho ni kucheza soka na amefanikiwa sana na hiyo inamuhamisha kuendelea kufanya vizuri akiwa bado anapenda soka kwasababu utafika wakati hawezi tena kufanya hivyo.
Ronaldo ameshinda taji la Ligi Kuu ya England EPL mara tatu akiwa na Manchester United kabla ya kutua Real Madrid na kushinda ubingwa wa La Liga mara mbili. Pia ameshinda taji la ligi ya mabingwa barani Ulaya UEFA mara nne.

BREAKING NEWS : Mkurugenzi Mkuu NHC Asimamishwwa kazi



Zitto Kabwe ahoji kuhama kwa makada Wa ACT



Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ametumia hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha Kamati Kuu kuzungumzia wimbi la kuhama kwa makada wa chama hicho, akihoji iwapo kimeanza kupoteza mwelekeo.
Katika hotuba yake leo Jumamosi Desemba 16,2017, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini amewataka wajumbe wa kamati hiyo kujiuliza maswali magumu, likiwemo la kwa nini hali hiyo inakikumba chama chao.
Makada wa chama hicho waliojiunga na CCM ni Profesa Kitila Mkumbo aliyeachia nafasi ya ushauri wa ACT –Wazalendo baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho; wakili Albert Msando, Samson Mwigamba na Edna Sunga.
Katika hotuba hiyo, Zitto amesema hamahama hiyo imezua taharuki kwenye chama hicho na kuacha maswali juu ya kinachoendelea katika siasa za Tanzania.
“Ni lazima tujiulize maswali magumu sisi wenyewe na kuzungumza tukitazamana machoni, je hakuna sababu za ndani sisi wenyewe zinazokimbiza wanachama wetu? Kama zipo ni zipi? Je ni sababu ambazo tunaweza kurekebisha na kukiimarisha chama," amehoji Zitto.
Amesema, "Kama ni sababu zilizo nje ya uwezo wetu tunafanya nini ili kuzikabili, je bado sisi tunaamini katika misingi ya chama kwa mujibu wa Azimio la Tabora? Tulikuwa kundi tu tulioumizwa na vyama tulivyokuwamo na tukaamua kuunda chama kupoza hasira zetu tu na sasa hasira zimeisha hakuna sababu ya chama kuwapo."
Amesema kati ya waanzilishi watatu wa ACT, wawili wamekikimbia na kujiunga na CCM na kwamba, jambo hilo huenda likarutubisha hoja kuwa chama hicho kilikuwa mradi wa chama tawala, kwamba sasa hauna maana tena.

Wabakaji Watoto Kuuwawa India



Wabakaji wa watoto wanapaswa kuuawa katika muda wa miezi sita tangu watekeleza uovu huo, mteteaji mkuu wa haki za wanawake India amependekeza.
Swati Maliwal ametoa ombi hilo katika barua aliyomuandikia waziri mkuu Narendra Modi.
Iliandikwa kuendana na kumbukumbu ya mwaka wa tano tangu mwanafunzi Jyoti Singh mwenye umri wa miaka 23 alipobakwa na gengi la wanaume, kifo chake kilichozusha maandamano ya kitaifa.
"Hakuna kilichobadilika kaika miaka mitano iliyopita," Bi Maliwal, ameiambia BBC.
"Delhi bado ndio mji mkuu wa ubakaji. Mwezi uliopita, mtoto wa kike wa mwaka mmoja na nusu alibakwa na gengi la wanaume, na ubakaji wa mtoto wa miaka saba,na mwingine wa kike wa mwaka mmoja na nusu alibakwa."
Kwa wastani, alisema, watoto watatu wa kike na wanawake wasita wanabakwa katika mji mkuu huo kila siku.
India ilifanyia mageuzi sheria zake kuhusu ubakaji kutokana na shutuma miaka mitano iliopita, na ilichukua hatua kuharakisha kusikilizwa kesi na kuwashinikiza maafisa wa polisi kutilia uzito tuhuma za ubakaji na unyanyasaji wa kingono.

Rais Mstaafu CWT anaswa na TAKUKURU



Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU inamshikilia Rais mstaafu wa Chama Cha walimu Tanzania (CWT) Gracian Mkoba kwa tuhuma za rushwa.
Hilo limethibitishwa na Afisa Uhusiano wa TAKUKURU Makao Makuu, Mussa Misalaba, ambaye amesema wanamshikilia Mkoba kwa tuhuma za kugawa fedha kwa baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho ili kuwashawishi wamchague mgombea anayemtaka.
"Mukoba ameshastaafu, lakini kuna mgombea mmoja alikuwa anataka achaguliwe, tumemkamata leo asubuhi akigawa rushwa kuwashawishi wapiga kura kwenye ukumbi wa Chimwaga wamchague huyo mgombea wake," amesema Misalaba.
Misalaba ameongeza kuwa TAKUKURU inaendelea kufanya uchunguzi zaidi dhidi ya Mukoba kabla ya kumfikisha mahakamani.
Mukoba anakuwa mtu wa tatu kukamatwa na TAKUKURU kwa tuhuma za rushwa kwenye uchaguzi ndani ya wiki moja, wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis na mfanyabiashara Haider Gulamali.

Waziri azindua mfumo Wa kieletroniki utambuzi wanamuziki



Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe leo December 16, 2017 amezindua mfumo mpya wa Kieletroniki wa Utambuzi wa Wanamuziki ambao utaanza kutumika nchini kwa ajili ya kulinda maslahi ya wasanii.
Moja ya vitu ambavyo Dr. Mwakyembe amevizungumza ni kuhusu kuibiwa na kutumiwa kwa kazi za wasanii na watu wachache bila ridhaa yao “tulipotoka ni kubaya, mimi nilikuwa DRC nilichoshangaa sana nilipita sehemu nikakuta picha kubwa ya Kanumba kule ni Star, ukija hapa mi nlifikiri kaacha mali za ajabu sana,”
“Vijana wetu wana majina makubwa, mifukoni hawana kitu, mambo mengi yanaudhi ni kwenye sanaa, tutakwenda Mahakamani haiwezekani huu unyonyaji, ngoja tuondoe hii njaa ya mwanzo afu nianze kupambania mambo mengine,” – Dr. Mwakyembe

Waziri Jafo Azuia shule ya Ihunge kuwa Chuo Kikuu



Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,TAMISEMI Selemani Jafo amewasisitiza viongozi wa mkoa wa Kagera kutokubadilisha malengo ya shule ya Ihungo kwa kuigeuza kuwa chuo kikuu baada ya kukamilika kwa ujenzi.
Jafo ameyasema hayo alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo inayojengwa upya baada ya hapo awali kukumbwa na tetemeko la ardhi.
Shule ya Ihungo inajengwa kisasa na itakapokamilika itakuwa shule ya kipekee kwa kuwa na miundombinu ya kisasa hapa nchini.
Amesema Majengo ya shule hiyo kwasasa yanaweza kuwatamanisha baadhi ya viongozi kutaka kubadilisha shule hiyo hapo baadae kuwa chuo kikuu kitu ambacho amezuia jambo hilo.
Amesema amezuia ili vijana wa kidato cha tano na sita ili waweze kupata nafasi kusoma katika shule hiyo yenye mazingira mazuri.
Baada ya ukaguzi wa shule hiyo,Waziri Jafo alielekea na ukaguzi wa shule nyingine ya Nyakato inayojengwa na Suma JKT na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi.

Tani 9 za dawa ya meno Aloe zaangamizwa Zanzibar



Wafanyakazi kutoka Bodi ya Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar wameangamiza Tani tisa za Dawa ya meno aina ya Aloe zilizoharibika katika jaa la Kibele Wilaya ya Kati Unguja
Dawa hizo ziliingizwa nchini na Kampuni ya Bacelona Interprises Limited zikiwa zimeharibika baada ya kontena lilikuwa na dawa hizo kuinga maji wakati wa kusafirishwa kuja Zanzibar .
Mkaguzi Mkuu wa Wakala wa Chakula Dawa Zanzibar Mwadini Ahmadi Mwadini alisema walibaini kuwa dawa hizo zimeharibika wakati wa kuzitoa bandarini na kumshauri mmiliki wa dawa hizo kuzirejesha zilikotoka au kuziangamiza na alikubali ziangamizwe ili kujiepusha na gharama nyengine.
Mwadini alisema Bodi inaendelea kufanya ukaguzi kwa bidhaa zinazoingizwa bandarini na maduka mbali mbali ili kuhakikisha zinakuwa salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
Aliwataka wafanyabiashara kuwa waangalifu wanapoagiza Bidhaa na kujenga ushirikiano wa karibu na Bodi yake kwa kutowa taarifa wanapoona bidhaa zao zinamashaka kuuzwa kutokana na kuharibika au kupitwa na muda wake wa matumizi.
Aidha aliwaomba wananchi wanaponunua bidhaa madukani na kuzigundua kuwa hitilafu watowe taarifa katika Bodi ili hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa kwa usala wao.
“Kama mukigundua kunafanyika udanganyifu kwa bidhaa mnazonunua kama kuharibika au kupitwa na wakati musisite kutoa taarifa kwetu, tupo kwa ajili ya kulinda usalama wa wananchi.” alisema Mkaguzi Mkuu.
Nae mtoa mzigo Bandarini aliesimamia kontena hilo Omar Kombo Sharif alisema mzigo huo uliingia Zanzibar mnamo mwezi wa nane na baada ya kubainika umeharibika walitoa taarifa kwa mmiliki na walikubaliana uzuiliwe kwa ajili ya kuuangamiza.
Wakati huo huo Mkuu wa Uchunguzi wa Chakula na Dawa Zanzibar Mohamed Shadhil alisema wamekamata Nyama ya ngombe kilo 180 iliyokuwa inasafirishwa kinyume na taratibu zilizowekwa na Bodi hiyo.
Alisema bidhaa hiyo imekamatwa wakati inasafirishwa kutoka machinjioni kwa kutumia Baskeli pamoja na vespa bila ya kuwa na kibali cha daktari na nikinyume cha utaratibu. Bidhaa za nyama zinatakiwa kusafirishwa kwa kutumia gari kwa ajili ya usalama wa watumiaji.
Nyama hiyo wameamua kuifukia baada ya kufanyika uchunguzi na kuwaita wamiliki ambao walikubali kuwa wamefanya kosa licha ya kulalamika kuwa utaratibu wa kusafiri bidhaa hiyo kwa kutumia baskeli na vespa umekuwapo kwa muda mrefu.
Mkuu huyo wa uchunguzi aliwataka wananchi wanaochinja nyama kufuata taratibu zilizowekwa ikiwemo kutumia vyombo vinavyotakiwa vyakuchukulia bidhaa hiyo ili kuepuka usumbufu na hasara katika biashara zao.