Saturday, 16 December 2017

Simba yafanya Maamuzi Magumu



SIMBA SC imesajili wachezaji watatu wapya wa kigeni, beki Mghana Asante Kwasi, kiungo mshambuliaji Mzambia Jonas Sakuwaha na mshambuliaji Antonio Dayo Domingues kutoka Msumbiji.
Wakati dirisha dogo la usajili linakaribia kufungwa jana, viongozi wa Simba walikuwa wanahaha kukamilisha usajili huo, hususan wa mchezaji Kwasi, ambaye bado ana mkataba na klabu yake ya sasa, Lipuli ya Iringa.
Lakini kwa Sakuwaha na Domingues hakukuwa na tatizo na habari zinasema wachezaji hao watachukua nafasi za beki Mzimbabwe, Method Mwanjali na washambuliaji, Mghana Nicholas Gyan na Mrundi Laudit Mavugo.
Wapinzani wao, Yanga wamesajili wachezaji wawili tu wapya, beki Fiston 'Festo' Kayembe Kanku kutoka Balende FC ya kwao, DRC na mshambuliaji kinda, Yohanna Nkomola ambaye ni mchezaji huru, aliyekuwamo kwenye kikosi cha timu ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys.
Azam FC imeingiza mmoja tu mpya, mshambuliaji Bernard Arthur kutoa Liberty Professional ya Ghana, baada ya kumuacha Mghana mwenzake, Yahya Mohammed na Singida United imesajili saba wapya; Lubinda Mundia kwa mkopo kutoka Res Arrows ya Zambia, Daniel Lyanga kutoka Fanja ya Oman, Kambale Salita 'Papy Kambale' kutoka Etincelles ya Rwanda, Issa Makamba, Assad Juma, Ally Ng’azi na Mohamed Abdallah wote huru waliokuwa Sereneti Boys.
Singida imewaacha wawili, Atupele Green na Pastory Athanas waliovunjiwa mikataba wakati Mohamed Titi na Frank Zakaria wametolewa kwa mkopo Stand United na Mbeya City imewasajili George Mpole kutoka Maji Maji na Abubakar Shaaban huru, baada ya kuwaacha Emmanuel Kakuti na mkongwe Mrisho Ngassa anayehamia Ndanda FC.

Ronaldo Atimiza ndoto yake



Nyota wa klabu ya soka ya Real Madrid na timu ya taifa ya Ureno Cristiano Ronaldo,
amesema anajisikia vyema kutimiza malengo yake kwenye ulimwengu wa soka na anafuraha kushindana na Lionel Messi kwa muda mrefu.
Akifanya mahojiano na tovuti rasmi ya FIFA, Ronaldo amesema ndoto yake ilikuwa kuweka historia na kuacha kumbukumbu kwenye ramani ya soka na hicho kitu kimetimia akiwa ametwaa mataji mengi pamoja na mafanikio binafsi ikiwemo tuzo tano za Ballon d’Or.
“Najisikia vizuri kutimiza malengo yangu, nilitamani sana kuweka historia kuacha jina langu kwenye vitabu vya soka, nimepata mafanikio mengi sana ngazi ya klabu na taifa, nafurahia kuwa mmoja wa wachezaji waliofanikiwa zaidi kama kuchukua tuzo tano sawa na Messi”, amesema Ronaldo.
Ronaldo ameongeza kuwa katika maisha yake amefanya kitu anachokipenda zaidi ambacho ni kucheza soka na amefanikiwa sana na hiyo inamuhamisha kuendelea kufanya vizuri akiwa bado anapenda soka kwasababu utafika wakati hawezi tena kufanya hivyo.
Ronaldo ameshinda taji la Ligi Kuu ya England EPL mara tatu akiwa na Manchester United kabla ya kutua Real Madrid na kushinda ubingwa wa La Liga mara mbili. Pia ameshinda taji la ligi ya mabingwa barani Ulaya UEFA mara nne.

BREAKING NEWS : Mkurugenzi Mkuu NHC Asimamishwwa kazi



Zitto Kabwe ahoji kuhama kwa makada Wa ACT



Kiongozi wa chama cha ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe ametumia hotuba yake ya ufunguzi wa kikao cha Kamati Kuu kuzungumzia wimbi la kuhama kwa makada wa chama hicho, akihoji iwapo kimeanza kupoteza mwelekeo.
Katika hotuba yake leo Jumamosi Desemba 16,2017, Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini amewataka wajumbe wa kamati hiyo kujiuliza maswali magumu, likiwemo la kwa nini hali hiyo inakikumba chama chao.
Makada wa chama hicho waliojiunga na CCM ni Profesa Kitila Mkumbo aliyeachia nafasi ya ushauri wa ACT –Wazalendo baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.
Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira aliyekuwa mwenyekiti wa chama hicho; wakili Albert Msando, Samson Mwigamba na Edna Sunga.
Katika hotuba hiyo, Zitto amesema hamahama hiyo imezua taharuki kwenye chama hicho na kuacha maswali juu ya kinachoendelea katika siasa za Tanzania.
“Ni lazima tujiulize maswali magumu sisi wenyewe na kuzungumza tukitazamana machoni, je hakuna sababu za ndani sisi wenyewe zinazokimbiza wanachama wetu? Kama zipo ni zipi? Je ni sababu ambazo tunaweza kurekebisha na kukiimarisha chama," amehoji Zitto.
Amesema, "Kama ni sababu zilizo nje ya uwezo wetu tunafanya nini ili kuzikabili, je bado sisi tunaamini katika misingi ya chama kwa mujibu wa Azimio la Tabora? Tulikuwa kundi tu tulioumizwa na vyama tulivyokuwamo na tukaamua kuunda chama kupoza hasira zetu tu na sasa hasira zimeisha hakuna sababu ya chama kuwapo."
Amesema kati ya waanzilishi watatu wa ACT, wawili wamekikimbia na kujiunga na CCM na kwamba, jambo hilo huenda likarutubisha hoja kuwa chama hicho kilikuwa mradi wa chama tawala, kwamba sasa hauna maana tena.

Wabakaji Watoto Kuuwawa India



Wabakaji wa watoto wanapaswa kuuawa katika muda wa miezi sita tangu watekeleza uovu huo, mteteaji mkuu wa haki za wanawake India amependekeza.
Swati Maliwal ametoa ombi hilo katika barua aliyomuandikia waziri mkuu Narendra Modi.
Iliandikwa kuendana na kumbukumbu ya mwaka wa tano tangu mwanafunzi Jyoti Singh mwenye umri wa miaka 23 alipobakwa na gengi la wanaume, kifo chake kilichozusha maandamano ya kitaifa.
"Hakuna kilichobadilika kaika miaka mitano iliyopita," Bi Maliwal, ameiambia BBC.
"Delhi bado ndio mji mkuu wa ubakaji. Mwezi uliopita, mtoto wa kike wa mwaka mmoja na nusu alibakwa na gengi la wanaume, na ubakaji wa mtoto wa miaka saba,na mwingine wa kike wa mwaka mmoja na nusu alibakwa."
Kwa wastani, alisema, watoto watatu wa kike na wanawake wasita wanabakwa katika mji mkuu huo kila siku.
India ilifanyia mageuzi sheria zake kuhusu ubakaji kutokana na shutuma miaka mitano iliopita, na ilichukua hatua kuharakisha kusikilizwa kesi na kuwashinikiza maafisa wa polisi kutilia uzito tuhuma za ubakaji na unyanyasaji wa kingono.

Rais Mstaafu CWT anaswa na TAKUKURU



Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU inamshikilia Rais mstaafu wa Chama Cha walimu Tanzania (CWT) Gracian Mkoba kwa tuhuma za rushwa.
Hilo limethibitishwa na Afisa Uhusiano wa TAKUKURU Makao Makuu, Mussa Misalaba, ambaye amesema wanamshikilia Mkoba kwa tuhuma za kugawa fedha kwa baadhi ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho ili kuwashawishi wamchague mgombea anayemtaka.
"Mukoba ameshastaafu, lakini kuna mgombea mmoja alikuwa anataka achaguliwe, tumemkamata leo asubuhi akigawa rushwa kuwashawishi wapiga kura kwenye ukumbi wa Chimwaga wamchague huyo mgombea wake," amesema Misalaba.
Misalaba ameongeza kuwa TAKUKURU inaendelea kufanya uchunguzi zaidi dhidi ya Mukoba kabla ya kumfikisha mahakamani.
Mukoba anakuwa mtu wa tatu kukamatwa na TAKUKURU kwa tuhuma za rushwa kwenye uchaguzi ndani ya wiki moja, wengine ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Sadifa Juma Khamis na mfanyabiashara Haider Gulamali.

Waziri azindua mfumo Wa kieletroniki utambuzi wanamuziki



Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe leo December 16, 2017 amezindua mfumo mpya wa Kieletroniki wa Utambuzi wa Wanamuziki ambao utaanza kutumika nchini kwa ajili ya kulinda maslahi ya wasanii.
Moja ya vitu ambavyo Dr. Mwakyembe amevizungumza ni kuhusu kuibiwa na kutumiwa kwa kazi za wasanii na watu wachache bila ridhaa yao “tulipotoka ni kubaya, mimi nilikuwa DRC nilichoshangaa sana nilipita sehemu nikakuta picha kubwa ya Kanumba kule ni Star, ukija hapa mi nlifikiri kaacha mali za ajabu sana,”
“Vijana wetu wana majina makubwa, mifukoni hawana kitu, mambo mengi yanaudhi ni kwenye sanaa, tutakwenda Mahakamani haiwezekani huu unyonyaji, ngoja tuondoe hii njaa ya mwanzo afu nianze kupambania mambo mengine,” – Dr. Mwakyembe

Waziri Jafo Azuia shule ya Ihunge kuwa Chuo Kikuu



Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais,TAMISEMI Selemani Jafo amewasisitiza viongozi wa mkoa wa Kagera kutokubadilisha malengo ya shule ya Ihungo kwa kuigeuza kuwa chuo kikuu baada ya kukamilika kwa ujenzi.
Jafo ameyasema hayo alipokuwa akikagua maendeleo ya ujenzi wa shule hiyo inayojengwa upya baada ya hapo awali kukumbwa na tetemeko la ardhi.
Shule ya Ihungo inajengwa kisasa na itakapokamilika itakuwa shule ya kipekee kwa kuwa na miundombinu ya kisasa hapa nchini.
Amesema Majengo ya shule hiyo kwasasa yanaweza kuwatamanisha baadhi ya viongozi kutaka kubadilisha shule hiyo hapo baadae kuwa chuo kikuu kitu ambacho amezuia jambo hilo.
Amesema amezuia ili vijana wa kidato cha tano na sita ili waweze kupata nafasi kusoma katika shule hiyo yenye mazingira mazuri.
Baada ya ukaguzi wa shule hiyo,Waziri Jafo alielekea na ukaguzi wa shule nyingine ya Nyakato inayojengwa na Suma JKT na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi.

Tani 9 za dawa ya meno Aloe zaangamizwa Zanzibar



Wafanyakazi kutoka Bodi ya Wakala wa Chakula na Dawa Zanzibar wameangamiza Tani tisa za Dawa ya meno aina ya Aloe zilizoharibika katika jaa la Kibele Wilaya ya Kati Unguja
Dawa hizo ziliingizwa nchini na Kampuni ya Bacelona Interprises Limited zikiwa zimeharibika baada ya kontena lilikuwa na dawa hizo kuinga maji wakati wa kusafirishwa kuja Zanzibar .
Mkaguzi Mkuu wa Wakala wa Chakula Dawa Zanzibar Mwadini Ahmadi Mwadini alisema walibaini kuwa dawa hizo zimeharibika wakati wa kuzitoa bandarini na kumshauri mmiliki wa dawa hizo kuzirejesha zilikotoka au kuziangamiza na alikubali ziangamizwe ili kujiepusha na gharama nyengine.
Mwadini alisema Bodi inaendelea kufanya ukaguzi kwa bidhaa zinazoingizwa bandarini na maduka mbali mbali ili kuhakikisha zinakuwa salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
Aliwataka wafanyabiashara kuwa waangalifu wanapoagiza Bidhaa na kujenga ushirikiano wa karibu na Bodi yake kwa kutowa taarifa wanapoona bidhaa zao zinamashaka kuuzwa kutokana na kuharibika au kupitwa na muda wake wa matumizi.
Aidha aliwaomba wananchi wanaponunua bidhaa madukani na kuzigundua kuwa hitilafu watowe taarifa katika Bodi ili hatua zinazofaa ziweze kuchukuliwa kwa usala wao.
“Kama mukigundua kunafanyika udanganyifu kwa bidhaa mnazonunua kama kuharibika au kupitwa na wakati musisite kutoa taarifa kwetu, tupo kwa ajili ya kulinda usalama wa wananchi.” alisema Mkaguzi Mkuu.
Nae mtoa mzigo Bandarini aliesimamia kontena hilo Omar Kombo Sharif alisema mzigo huo uliingia Zanzibar mnamo mwezi wa nane na baada ya kubainika umeharibika walitoa taarifa kwa mmiliki na walikubaliana uzuiliwe kwa ajili ya kuuangamiza.
Wakati huo huo Mkuu wa Uchunguzi wa Chakula na Dawa Zanzibar Mohamed Shadhil alisema wamekamata Nyama ya ngombe kilo 180 iliyokuwa inasafirishwa kinyume na taratibu zilizowekwa na Bodi hiyo.
Alisema bidhaa hiyo imekamatwa wakati inasafirishwa kutoka machinjioni kwa kutumia Baskeli pamoja na vespa bila ya kuwa na kibali cha daktari na nikinyume cha utaratibu. Bidhaa za nyama zinatakiwa kusafirishwa kwa kutumia gari kwa ajili ya usalama wa watumiaji.
Nyama hiyo wameamua kuifukia baada ya kufanyika uchunguzi na kuwaita wamiliki ambao walikubali kuwa wamefanya kosa licha ya kulalamika kuwa utaratibu wa kusafiri bidhaa hiyo kwa kutumia baskeli na vespa umekuwapo kwa muda mrefu.
Mkuu huyo wa uchunguzi aliwataka wananchi wanaochinja nyama kufuata taratibu zilizowekwa ikiwemo kutumia vyombo vinavyotakiwa vyakuchukulia bidhaa hiyo ili kuepuka usumbufu na hasara katika biashara zao.

Waziri Lukuvi ampiga STOP mkurugenzi mkuu NHC



Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Nehemia Mchechu amesimamishwa kazi.
Taarifa ya kusimamishwa kazi kiongozi huyo imetolewa leo Jumamosi Desemba 16,2017 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dk Hassan Abbasi akieleza uamuzi huo umetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
Mchechu aliteuliwa kuliongoza shirika hilo Machi Mosi, 2010. Kabla ya uteuzi huo alikuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CBA.
Taarifa ya Dk Abbasi imesema Lukuvi amechukua uamuzi huo kwa mamlaka aliyopewa chini ya kifungu F. 35 (1) cha Kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2009.
Mbali na Mchechu, Lukuvi ameitaka bodi ya shirika hilo kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Huduma za Mikoa na Utawala, Raymond Mndolwa.
"Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Dorothy Mwanyika imesisitiza kuwa uamuzi huo unapaswa kutekelezwa kuanzia leo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazowakabili watendaji hao," amesema.
Desemba 13, wakati Rais John Magufuli akizindua nyumba 300 za shirika hilo alieleza hujuma zinazofanywa na viongozi wa NHC, akiwemo Mchechu na Bodi ya wakurugenzi.
"Visumu sumu ambavyo vinaleta mawazo mengi vipo, unakuwa na shirika la kujenga nyumba wakati wewe ni mkurugenzi na ni shirika lako. Unanunua viwanja kule na wewe unakwenda unanunua maeneo unayaandikia kwa majina fulani, tukichunguza tunakuta vyako, mengine nimeyamezea kwa sababu ya kazi nzuri unayofanya," alisema Rais Magufuli.
Katika hotuba yake, Rais alimtaka Mchechu kuwa makini na watu anaofanya nao kazi kwa maelezo kuwa wapo wanaotaka nafasi yake na kutumia wajumbe wa bodi na wanasiasa kumchafua.
"Wako wanaokupiga vita kwa wivu wao, lakini na wewe saa zingine matumizi yanakuwa ya ajabu," alisema Rais.

Salam Za JK Kikwete baada ya Zanzibar Heroes kufuzu Fainali challenge cup



Baada ya timu ya taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’ kufuzu kucheza fainali ya michuano ya CECAFA Senior Challenge Cup 2017, Rais mstaafu wa serikali ya awamu ya nne Dr. Jakaya Kikwete ‘JK’ ametuma salam za pongezi kwa timu hiyo.
Kupitia ukurasa wake wa twitter JK ameandika: “Nawapongeza Zanzibar Heroes kwa kututoa kimasomaso na kutinga fainali. Nawatakia kila la kheri katika mechi ya fainali waibuke na kombe na watupe raha ambayo Watanzania tumeikosa kwa muda mrefu.”
Zanzibar waliifunga 2-1 timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ kwenye mchezo wa nufu fainali, ikumbukwe Uganda ndio walikuwa mabingwa watetezi wa kombe hilo walilolitwaa mwaka 2015. Mwaka huohuo Uganda waliifunga Zanzibar 4-0 katika mchezo wa hatua ya makundi.
Mchezo wa fainali utachezwa Jumapili December 17, 2017 kati ya wenyeji Kenya dhidi ya Zanzibar.

Zitto Kabwe aiombea uanachama Zanzibar heroes



Mbunge wa Kigoma mjini Mh. Zitto Kabwe ambaye ni mdau mkubwa wa michezo hususani soka amekiombea aunachama wa FIFA chama cha soka cha Zanzibar ZFA.
Hatua hiyo imekuja baaada ya timu ya taifa ya Zanzibar (Zanzibar Heroes) kutinga hatua ya fainali ya michuano ya CECAFA Senior Challenge 2017 inayoendelea nchini Kenya.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook Zitto amefunguka ya moyoni akitaka ZFA iwe mwanachama wa shirikisho la soka la kimataifa FIFA pamoja na lile la Africa CAF angalau kwa miaka mitano na inaweza kupiga hatua ambazo TFF imeshindwa.
“Kama hatutaki Zanzibar kuwa Mwanachama wa FIFA kama ilivyo Scotland. Tuseme kwa miaka 5 ijayo kuanzia mwaka huu ZFA ndio mwanachama FIFA na CAF ili TFF ipate muda wa kujipanga. Ndani ya hiyo miaka 5 nawaambia Zanzibar itakwenda AFCON na hata Kombe la Dunia. #MsemaKweliMpenziWaMungu”, ameandika Zitto Kabwe.
Zitto ametoa mfano kuwa Zanzibar ingepata uanachama kamili wa FIFA kama ilivyo kwa nchi za Scotland pamoja na Wales ambazo pia ni nchi dada za taifa la Uingereza lakini zinatambuliwa na FIFA kama mataifa wanachama huku Uingereza ikitambulika kama England

Mwaijage Ameitaka kampuni ya mbolea kubadili mfumo



WAZIRI wa Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage, ameitaka Kampuni ya Mbolea ya Taifa (TFC) kubadilisha mfumo wa utendaji ikiwa ni pamoja na kutoingia mikataba inayoweza kuisababishia serikali hasara, badala yake kuangalia wabia wanaoweza kuisaidia kujipanua na kupata faida kubwa zaidi.
Waziri Mwijage, aliyasema hayo juzi wakati akiizindua bodi mpya ya Wakurugenzi ya TFC, na kuongeza kwamba serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Dk John Pombe Magufuli, haiko tayari kuona taasisi zake za umma zikiingizwa katika mikataba mibovu na isiyokuwa na tija.
Pia aliagiza kwamba, baada ya kuizindua bodi hiyo, Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Egid Mbofu na wajumbe wake, waanze kazi mara moja na moja ya majukumu yao ya awali ni kuangalia ama kuipitia upya miokataba ambayo awalo iliingiwa na TFC.
Alisema TFC ikifanya kazi kwa uadilifu mkubwa na kujielekeza kwenye kazi zenye faida kubwa, itaweza kusaidia kasi ya kuendeleza sekta ya kilimo nchini, na kufikia malengo ya serikali ya awamu ya tano ya Taifa la uchumi wa kati na wa Viwanda.
"Tunatambua sekta ya kilimo ni nguzo muhimu kwa ajili ya uchumi wa TANZANIA, lakini haiwezi kuleta mafanikio makubwa kwa jamii, ikiwa TFC haitaweza kupewa uwezo na kuwafikia wakulima wengi zaidi", alisema Waziri Mwijage