Tuesday, 12 December 2017

Kama Unafikiri Mafanikio Utayapata Kwa Njia Hii, Sahau



Kujenga nidhamu binafsi na kuishi maisha unayoyataka wewe sio kitu rahisi kinachotokea tu mara moja.

Kujitoa na kufanya yale yanayotakiwa kufanyika ili kuweza kutimiza ndoto zako, halikadhalika hicho nacho si kitu rahisi.

Kuweza kutimiza ahadi zako na kuwa na mawazo zingativu juu ya ndoto zako pia nacho hicho si kitu rahisi kuweza kukufanikisha kama unavyofikiri.

Kupanga mipango yako na kufanyia kazi ili iweze kutoa mafanikio pia hicho sio kitu rahisi, kuna ugumu fulani unaojitokeza.

Ukiangalia katika maisha karibu kila kitu ambacho unataka kukifanya na kweli kikatoa mafanikio, kina ugumu wa aina fulani hivi.

Ukiona kuna jambo ukilifanya ni mteremko sana kwako na halihitaji wewe  kujibidiisha sana, ujue hapo kufanikiwa si rahisi sana pia.

Utaona mpaka hapo mafanikio yanahitaji nguvu na kujitoa sana kila wakati  na kila siku ili uweze kuyafikia.

Lakini ikiwa utaamua kuyaendea mafanikio kwa mkono wako mlegevu au kwa jinsi unavyotaka wewe kufanikiwa kwako itakuwa ni shida.

Hapa sina shaka unapata picha kamili kwamba hakuna kitu rahisi katika hii dunia. Kila kitu kina ugumu wake katika kukipata.

Ukiona mtu anakwambia mafanikio ni rahisi au wewe mwenyewe unaona mafanikio ya mwingine yamepatikana kama kwa urahisi vile, sio kweli.

Ipo namna yule mtu ambaye labda unamuona kafanikiwa kiurahisi kapigana na kuweza kufanikiwa kwa mafanikio yale.

Lakini ukiwa na ndoto za kufanikiwa huku umelala, na bila kijibiidisha vya kutosha andika utaumia hutaweza kufanikiwa popote.

Amua kwenye maisha yako kutenga muda wa kutafuta mafanikio yako, kubali kupigika kiakili, kimwili lakini usikubali ukashindwa kufanikiwa.

Unajua dunia tunayoishi ina kila kitu cha kukupa mafanikio. Kinachosababisha ukose mafanikio ni juhudi na nguvu zako tu na sio kitu kingine.

Kama unataka mali na pesa hizo zipo, lakini sio rahisi kuzipata, unatakiwa uweke juhudi na kufanya kazi kwa nguvu zote na kuachana na mchezo mchezo.

Kama utacheza na huku unasema unatafuta mafanikio makubwa, nikwambie tu ukweli huo ni uongo, ambao tena labda unajidanganya wewe na kuwadanganya na wengine pia.

Elewa hauna kitu ambacho cha kimafanikio ni rajisi katika maisha yako, ipo nguvu ambayo unatakiwa kuitumia ili kupata kitu chochote kile.

Chochote kile ambacho kinakupa mafanikio au chochote kile ambacho kinabadili tabia au hali yako na kuwa bora si rahisi sana kukipata.

Kama unafikiri mafanikio utayapata kwa njia ya urahisi, sahau. Unatakiwa kuweka juhudi kwa nguvu zako zote.


Mbinu Bora Ya Kuishi Ndani Ya Bajeti Yako


Hivi falsafa juu ya matumizi ya  bajeti ambayo ipo  ndani ya uwezo wako ikoje? Hili ni swali la muhimu sana ambalo kila mmoja wetu anatakiwa kujiuliza kataka maisha yake ya kila siku.

Nasema hivi kwa sababu moja kati ya tabia ya watu wengi huwa wanaishi nje ya bajeti ambayo wanakuwa wamepanga.

Yote hii hutoka na sababu kubwa moja, sababu hiyo ni pale mtu ambapo amepata fedha nyingi kwa wakati mmoja. Kitendo hicho ndicho ambacho humfanya mtu kuweza kuishi nje ya bajeti yake ya kila siku.

Kwa mfano mtu akipokea mshahara hawezi kuishi maisha ambayo alikuwa ameyazoea ukifananisha na alipokuwa hana pesa, unakuta matumizi yanakuwa mengi kuliko pesa aliyonayo. Wapo wengine mara baada ya kutumia pesa yote hujikuta wanaingia kwenye madeni yasiyo ya msingi.

Achilia mbali madeni, wapo baadhi ya watu pindi wapatapo pesa utakuta wananua vitu vingi hata ambavyo hawakupanga kununua, tatizo hili lipo kwa watu wengi sana, siwezi ita tu ni tatizo bali ni ugonjwa wa matumizi ya pesa.

Niliwahi soma kitabu kimoja cha kanuni ya pesa, ndani ya kitabu hicho mwandishi anasema ya kwamba ukimpa mtu maskini pesa basi ndani ya sekunde kadhaa basi jiandae kujua tabia za mtu huyo, hii ni kwasababu ni mtu ambaye mara zote huongozwa na pesa, basi kila kilichopo mbele yake anataka kukimiliki yeye.

Lakini pesa hiyo ukimpa mtu ambaye anaelewa ni nini maana ya pesa,  basi  pesa hiyo huweza kufanya kitendo cha uwekezaji, ili pesa hiyo iweze kujizalisha yenyewe hapo baadae. Kwa nukta hiyo jaribu kutafakari  hivi pesa ambayo huwa unaipata mikononi mwako   unajiona upo kundi gani kati ya hayo niliyoyaeleza?

Kama utaona ya kwamba upo kundi ambalo umekuwa ni mtumiaji mzuri kuliko kuwa mwekezaji basi tambua lipo tatizo kubwa ndani yako, ambalo linakufanya uishi nje ya mstari wa bajeti yako, Hivyo unatakiwa kujua ni kwa namna gani unatakiwa kuishi ndani mstari bajeti yako kwa kuzingatia jambo hili.

Jambo Kwanza kabisa hakikisha pesa isikupelekeshe hasa pale unapoipata ila wewe ndiyo unatakiwa kuipelekesha pesa, kwa kuzingatia ya kwamba pindi utakapo ipa nafasi pesa ikuendeshe  basi tambua fika lolote linaweza kutokea ndani yako.

Lakini pia kwa  kuwa wanasema pesa ina makelele sana hasa pale unapoipata hivyo hakikisha pale unapoipata pesa unaishi kwenye pajeti yako ambayo umeizoa, kwani pindi utapopandisha bajeti yako eti kwa sababu umeipata pesa basi tambua ya kwamba  utaunganaa na wale wanaosema vyuma vimekaza.

Hivyo  pesa isiongeze matumizi yako ya kila siku eti kwa sababu umepata pesa, hivyo kila wakati jifunze kuishi ndani ya bajeti yako.



Rafiki Wa Karibu Wa Kukupa Mafanikio Ni Huyu Hapa



Kama unataka kusonga mbele na kuwa na mafanikio makubwa zaidi, mshirika wa kwanza ambaye unatakiwa kushirikiana naye bila kumwacha hadi akakupa mafanikio hayo ni muda wako ulionao.
Ufanye muda uwe rafiki yako wa karibu sana ili ukupatie mafanikio. Usipoteze muda wako kwa mambo ya hovyo, fanya vitu vyako kwa umakini na mpangilio mkubwa, kila unapotumia muda wako.

Inawezekana maisha yako umekuwa ukiyaona hayafai hasa kwa kuona hujatimiza karibu kila kitu. Hiyo inaweza ikawa ni sawa, lakini wakati na nafasi ya kubadili mambo hayo na kuwa mazuri unayo tena.

Muda ukiutumia vizuri unaweza kukupa uwezo wa kukamilisha mambo ambayo kwa kawaida yalionekana ni magumu kuweza kuyatimiza. Kipi unachokitaka ambacho kitashindikana kwa sababu ya muda.

Je, unataka kuandika kitabu? andika mistari michache kila siku, muda utafika kitabu chako kitakamilika. Je, unataka kujenga biashara yako? anza na biashara yoyote hata kama ni ndogo sana na ikuze kidogo kidogo, muda ukifika itakuwa kubwa sana.

Chochote unachotaka kukifanikisha kwako inawezekana, hata iwe unataka kuongea lugha mpya? jifunze maneno machache kila siku na wakati utafika utafanya kwa ufasaha na kujikuta mzungumzaji tayari.

Kama nilivyotangulia kusema, karibu kitu chochote unachokitaka, kipo ndani ya uwezo wako na unayo nafasi kubwa ya kukifikia ikiwa utaamua kutenga muda wako kufanya jambo hilo na kulifanikisha.

Rafiki wa karibu yako, rafiki ambaye anaweza kukupa mafanikio makubwa sana  ni muda wako. Unatakiwa ukae chini na kujiuliza maswali ya msingi, je muda wako unautumia vizuri au hovyo hovyo.

Kama unatumia muda wako hovyo, utakuwa kwenye wakati mgumu sana wa kuweza kubadili hali ya maisha yako na hadi kuwa nzuri. Kumbuka hata ukiwa na hali mbaya vipi, lakini ukiweka juhudi na kujipa muda utafanikiwa.

Hakuna ambaye ameachwa mtupu, kama matumizi ya muda wake ni sahihi. Kama ulikuwa hujaanza kutunza muda wako kwa ajili ya mafanikio, anza leo. Fanya mambo ya kukua mafanikio hata kama ni madogo sana, baada ya miaka michache utafanikiwa.

Monday, 11 December 2017

Mo kusaini Miaka miwili Simba SC



KLABU ya Yanga imeshindwa kumpa kiungo Mohamed Ibrahim ‘Mo Ibra’ kile anachotaka, hivyo leo Jumatatu mchezaji huyo anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili na klabu yake ya Simba.

Akizungumza na Championi Jumatatu, Meneja wa Mo, Jamal Kisongo amesema kuwa mteja wake huyo anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka miwili na Simba baada ya kushindwana na Yanga ambao nao walikuwa wanamtaka huku Msimbazi wao wakitimiza makubaliano waliyokuwa wanataka.

Alisema walifanya mazungumzo na Yanga lakini kuna baadhi ya vitu kwenye mkataba hawakuridhika navyo na walipozu-ngumza na Simba wakakubali kurekebisha baadhi ya vipengele kwenye ule mkataba wa awali hivyo rasmi mteja wake anabaki Simba na leo atasaini kandarasi baada ya ile ya awali kumalizika.

“Kesho (leo) natarajiwa kwenda kusaini mkataba mpya wa miaka mawili na mchezaji Mohammed pale Simba baada ya ule wa awali kumalizika, hivyo tunaongeza mwingine.
“Yanga nao walionyesha kumhitaji lakini kuna vitu walishindwa kukamilisha na tulipozungumza na Simba wamekubali kurekebisha baadhi ya vipengele, hivyo atabaki huko,” alisema Kisongo.





Kamishna Magereza awapa neno waliopata msamaha wa Rais


Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, Juma Malewa amewataka wafungwa waliotolewa kwa msamaha wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli siku ya uhuru, waheshimu mamlaka iliyowatoa na waende wakawe raia wema huko waendako.

Kamishna Malewa amesema anaamini kuwa wafugwa hao walioachiliwa huru kwa msamaha huo wameshajifunza na kujirekebisha na kuwaomba raia wawapokee na kuwatengenezea mazingira ya kuwaingiza katika kazi ili na wao waende sambamba nao.

"Kwa wafungwa waliobaki gerezani wao nao waishi kwa amani, wafanye kazi warekebishike, kwahiyo kwa sasa hata wale wafungwa wa vifungo virefu ambao tulikuwa hatuwatumii huko nyuma kwa kuogopa mambo mbalimbali lakini sasa hivi watakuwa wamejifunza katika hili kwamba ukiishi gerezani ukirekebishika mheshimiwa Rais yupo atatumia mamlaka yake kama alivyopewa na atawasamehe kama alivyowasamehe wengine", amesema Kamishna Malewa.

Kamishna Malewa pia amemuelezea Nguza Viking (Babu Seya )  na kusema kuwa alikuwa mfungwa mwenye nidhamu sana na alipewa cheo kikubwa gerezani yaani Unyampara mwaka mmoja tu alivyoingia gerezani.

9 Desemba mwaka huu siku ya uhuru kwa mujibu ya ibara ya 45 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Rais John Pombe Magufuli alitoa msamaha kwa  wafungwa 61 waliohukumiwa kunyongwa hadi kufa na wawili Nguza Viking (Babu Seya ) na Johnson Nguza (Papii Kocha ) waliohukumiwa kifungo cha maisha jela.










Kauli ya Roma baada ya Stamina kumvalisha pete mpenzi wake



kumuomba asihishie hapo amuoe kabisa mpenzi  wake huyo.

Kupitia ukurasa wake wa instagram msanii mwenzake ambae wanafanya naye kazi kwa karibu hivi sasa Roma mkatoliki amemtahadharisha kwa kumwambia " Congratulation My Brother @staminashorwebwenzi On Your #Engagement .Im Proud Of You Son....Sasa #Umuoe Sio Uishie Kwenye #Pete Tu!!Nisaidieni #Kumuwish Mdogo Wangu Marafiki!!"

Kheri James ashinda uenyekiti UVCCM



WAZIRI wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, ambaye pia ni mjumbe wa Baraza la Wadhamini la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi CCM Taifa (UVCCM), leo amemtangaza Kheri James kuwa Mwenyekiti mpya atakayeongoza kwa miaka mitano.

Kheri ametangazwa mshindi baada ya kupata Kura 319 kati ya kura 583 zilizopigwa akiwashinda wenzake 6 aliokuwa akichuana nao kuwania nafasi hiyo. Nafasi ya Makamu Mwenyekiti imechukuliwa na Tabia Mwita.

Mkutano wa Uchaguzi wa UVCCM umefanyika mjini Dodoma kwenye ukumbi wa Chuo Cah Mipango. Mbali na wajumbe wa idara hiyo ya vijana wengine walioshuhudia kutangazwa kwa Kheri ni Katibu Mkuu wa CCM Taifa Ndugu Abdulrahman Kinana.

Mkutano huo wa uchaguzi wa UVCCM ulifunguliwa jana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa Dkt. John Pombe Magufuli na unafungwa leo na Rais wa Zanziobar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein.

Wagombea na Kura walizopata.
1. Kheri James 319
2. Tobias Mwesiga 127
3. Simon Kipala 67
4. Kamana Juma 27
5. Juma Mwaipaja 19
6. Seif Mtoro 16
7. Mganwa Nzota 1

Watoto sita wapelekwa Israel kwaajili ya Matibabu



Watoto sita wenye umri wa kuanzia mwaka mmoja hadi  miaka kumi na tatu wamepelekwa nchini Israel kwa ajili ya matibabu ya moyo.

Watoto hao wamepelekwa chini ya ushirikiano wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s  Heart – SACH) ya nchini Israel. Safari hiyo ya matibabu imejumuisha wauguzi pamoja na wazazi wa watoto ambao kwa pamoja wameondoka nchini Disemba 10 mwaka huu.

Baada ya matibabu ya watoto kukamilika, Maafisa Wauguzi wawili watabaki kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo ya mwaka mmoja ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa waliopo katika wodi ya uangalizi maalum (ICU) na chumba cha upasuaji.

Aidha kundi hilo limekuwa ni kundi la tano la watoto kwenda kutibiwa magonjwa ya moyo nchini Israel tangu mwaka 2015 ambapo Taasisi ya Moyo ilianza ushirikiano  na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto (Save a Child’s Heart –SACH) ya kuwapeleka wagonjwa nchini humo. Hadi sasa watoto 46 wameshatibiwa nchini humo na wanaendelea vizuri.


Amber Lulu afunguka mafanikio aliyoyapata mwaka huu


Msanii wa muziki Bongo, Amber Lulu amefunguka mafanikio aliyoyapata kwa mwaka huu.

Muimbaji huyo amesema cha kwanza kabisa ni uhai wake na mambo mengine yanabaki kuwa binafsi na hata mipango ya kujenga pia.

“Maisha yangu siwezi nikayaweka hadharani, sijui nimeingiza au nimetoa shilingi ngapi lakini namshukuru Mungu mwaka huu umekua wa bahati sana” Amber Lulu ameiambia Bongo5.

“Hiyo ni siri yangu, ukifika wakati nitawaambia nimejenga nakadhalika lakini sasa hivi am not ready” amesema.


Msanii Gilad amesema Cinderella ya Ali Kiba ilimfunza kuimba Kiswahili



Msanii wa muziki toka nchini Kenya mwenye asili ya Israel, Gilad amesema wimbo wa Alikiba Cinderella ndio uliomfunza kuimba Kiswahili.

Muimbaji huyo ameiambia FNL ya EATV kuwa ngoma hiyo ndio ya kwanza kuimba kwa lugha ya Kiswahili ndipo na nyingine zikafuata.

“Cinderella ni wimbo wa kwanza kujifunza kuimba, ni wimbo wa kwanza kuinba kwa Kiswahili. Nilikuwa naimba na bendi jukwaani, kwa hiyo ni wimbo wa kwanza kuimba kwa Kiswahili na nilikuwa natumbuiza kila wiki, nikaja nikaimba Kidumu ‘Haturudi Nyuma’, pia Juliana ‘Tawala’ amesema.

Miongoni mwa ngoma alizoimba kwa Kiswahili Gilad ni pamoja na Nakuhaidi, Sema Milele, Unajua na Mapenzi. Pia mwaka huu ameweza kushinda tuzo mbili za Afrima.

Gilad kwa sasa anasikika Bongo kupitia ngoma mpya ya rapper Azma ‘Shubiliga’.

Mwana FA asema hatujaombana msamaha na Jide




Msanii wa muziki wa kizazi kipya ambaye hivi karibuni amemaliza tofauti zake na msanii mwenzake Lady Jaydee baada ya kutokuwa na maelewano mazuri kwa muda mrefu, amesema hakuna mtu aliyemuomba msamaha mwenzake kati yao ili kuyamaliza.

Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Mwana FA amesema ugomvi wake na Jaydee hakuna mtu aliyewakalisha kujaribu kuwapatanisha au wenyewe kuombana msamaha, bali waliumaliza kwa yeye kumpigia simu, na kuzungumza kama ambavyo wengine wanazungumza,

"Hakuna aliyemuomba msamaha mwenzake, mi ndio nilianza, nilimtumia meseji oya vipi, akajibu fresh, nikamwambia FA hapa usiku nilikutafuta, akajibu mimi siku hizi nimezeeka nalala mapema, ndo hivyo tukayamaliza hivyo", amesema Mwana FA.

Mwana FA ambaye kwa sasa ameachia kazi mpya aliyomshirikisha Maua Sama, amesema licha ya kumaliza tofauti zao na Jaydee, watu wasitarajie sana kazi ya pamoja kwani kibinadamu itaonekana wamemaliza tofauti hizo kwa ajili ya kazi.

Askari JWTZ waliouawa na waasi, miili yao kuwasili leo



Dar es Salaam. Miili ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliouawa na waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inarejeshwa nchini leo.

Taarifa ya ofisi ya habari ya JWTZ imesema miili ya askari hao itawasili nchini leo Jumatatu Desemba 11,2017 saa kumi na mbili jioni katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).

Awali, akizungumzia na waandishi wa habari jana Jumapili Desemba 10, 2017 Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali James Mwakibolwa alisema miili ya askari hao ingerejeshwa nchini kati ya Jumanne Desemba 12, au Jumatano Desemba 13,2017 kwa ushirikiano kati ya Serikali na Umoja wa Mataifa (UN).

Mwakibolwa alisema askari hao walivamiwa kambini na waasi wa ADF na mapigano yalidumu kwa takriban saa 13. Alisema askari 14 wa JWTZ waliuawa, 44 wamejeruhiwa na wengine wawili  hawajulikani walipo.

Alisema tukio hilo lililotokea Desemba 7,2017 katika kambi ndogo iliyopo katika daraja la Mto Simulike, kaskazini mashariki mwa Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu nchini DRC.

Tundu Lissu: Madaktari wamesema nitasimama na kutembea


Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA, Tundu Lissu amefunguka na kusema kuwa ameambiwa na madaktari wake kuwa atasimama, atatembea na kurudi tena Tanzania kuendelea na majukumu yake kama kawaida.

Tundu Lissu amesema hayo leo alipofanya mahojiano na DW na kusema kuwa kwa sasa anaendelea vizuri kiafya na kuwa madaktari wamemweleza kuwa atasimama na kutembea tena kama zamani na kurudi nyumbani kwake Tanzania.

Aidha Tundu Lissu amesema hajapoteza matumaini ya kuwapata na kuwatambua watu ambao walishambulia kwa risasi kwa kuwa anaamini sehemu ambayo tukio hilo lilitokea kulikuwa na ulinzi na walinzi wa serikali.

"Matumaini hayajapotea kwa vile nakaa kwenye nyumba za serikali hizi nyumba zinalindwa masaa 24, Je, siku hizo napigwa risasi walinzi walikuwa wapi? Walinzi wa geti kubwa nao walikuwa wapi? Ile sehemu yote tunayoishi imezungushwa ukuta na kuna geti kuu lenye ulinzi masaa 24 nao walikuwa wapi? alihoji Tundu Lissu

Mbali na hilo Tundu Lissu ameelezea jinsi ambavyo tukio hilo lilitokea mnamo Septemba 7, 2017 pale Dodoma msikilize hapa chini akitolea maelezo hilo.