Wednesday, 6 December 2017

ACT kufanya maandamano


dara ya vijana ya Chama Cha ACT-Wazalendo imesisitiza kuwa itafanya maandamano yake ya amani yenye lengo la kupinga vitendo vya utumwa wanavyofanyiwa vijana wa Afrika nchini Libya.

Pamoja na kutojibiwa barua yao ambayo wameliandikia jeshi la Polisi kwenye mkoa wa kipolisi Kinondoni kwaajili ya kuomba kibali cha maandamano hayo lakini wamesisitiza kuwa watafanya hivyo

“Polisi Kinondoni wanasema barua yetu ya maandamano ya tarehe 8/12/17 imetumwa KANDA na mpaka sasa majibu hawajaletewa, wanasema tuulizie tena kesho tunapenda kuujulisha umma kuwa ratiba ya maandamano yetu haijabadilika”, imesema Taarifa ya hiyo kutoka idara ya vijana ACT-Wazalendo.

Idara hiyo ya vijana imepanga kuandamana siku ya Ijumaa Disemba 8 kuanzia saa 4 asubuhi ambapo wataanzia eneo la Leaders Club jijini Dar es salaam na kuishia ofisi za Ubalazi wa Libya nchini zilizopo Upanga jijini Dar es salaam na watatumia barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Hivi karibuni nchini Libya kumeibuka vikundi vya watu ambavyo vinafanya biashara ya utumwa kwa baadhi ya wageni wanaoingia nchini humo hususani wale wahamiaji ambao hufika nchini humo kwa lengo la kuvuka na kuelekea barani Ulaya.



Nigeria wateua Waziri wa kushughulikia furaha, mahusiano kifamilia



Gavana wa Jimbo la Imo, Rochas Okorocha (kushoto).

Serikali ya Jimbo la Imo nchini Nigeria imeteua waziri atakayeshughulikia masuala ya furaha na mahusiano ya kifamilia.

Uteuzi wa waziri huyo unaelezwa ni mkakati wa kuwasahaulisha wananchi adha za kisiasa na mapigano ya makundi haramu.

Gavana wa jimbo hilo, Rochas Okorocha amesema uteuzi huo ni wa kwanza kufanyika katika Taifa hilo lililopitia kipindi kigumu cha mashambulizi ya wapiganaji wa kundi la Boko Haram na hali mbaya ya kisiasa.

Okorocha amemteua ndugu yake, Ogechi Ololo kuwa waziri wa masuala ya furaha na mahusiano mema ndani ya familia.

Kabla ya uteuzi huo, Ogechi alikuwa msaidizi wa Gavana Okorocha na mshauri wake maalumu wa masuala ya nyumbani. Pia, anahusika na mapambo wakati wa sikukuu ya Krismasi.

Hata hivyo, msemaji wa gavana huyo, Sam Onwuemeodo hakutoa maelezo zaidi kuhusu majukumu ya waziri huyo.

Akizungumza na Shirika la Habari la AFP alisema, “Hakuna kitu kipya zaidi katika uteuzi huo.”

“Gavana ni mtu mbunifu ambaye kila wakati huanzisha vitu vipya serikalini. Jukumu kubwa la waziri huyu ni kuleta ubunifu ambao utaweza kuigwa na magavana wengine. Gavana anataka kuwafanya watu wawe na furaha kila wakati na ndiyo maana ameunda wizara hii kwa lengo hilo,” amesema.

Urusi Imefungiwa kushiriki michuano ya Olimpiki


Kamati ya kimataifa ya Olimpiki, imeifungia nchi ya urusi kushiriki michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi itayofanyika katika jiji la Pyeongchang nchini Korea kusini mwakani.

Rais wa IOC Thomas Bach na bodi yake walitangaza adhabu hiyo jana jioni baada ya kukutana katika mji wa Lausanne nchini Switzerland, maamuzi hayo yamefikiwa baada ya uchunguzi wa miezi kumi na saba.

Serikali ya Urusi ilihusika katika udanganyifu wa kuanda michuano ya olimpiki iliyofanyika nchini humo mwaka 2014 pamoja na udanganyifu kuhusu matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku michezoni.

Uchunguzi huo ulikuwa ukiongozwa na Rais wa zamani wa IOC Samuel Schmid, Licha adhabu hiyo wanariadha wa Urusi wanaweza shiriki michuano ya majira ya baridi kama wanaridha huru ambao watakuwa wakiwakilisha nchi.

Nafasi za kazi leo Dec 6

Chadema hawana hofu jimbo la Kinondoni



Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Jimbo la Kinondoni kimesema hawana hofu juu ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Maulid Mtulia kuhamia CCM kwani wako imara na kusubiri taratibu za kutangazwa siku ya uchaguzi ili waweze kutetea kiti hicho.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano na mwenyekiti wa chama hicho Jimbo la Kinondoni, Waziri Muhunzi alipokuwa akituma salamu kwa wananchi wa eneo hilo kuwataka kuwa wavumilivu.

"Wananchi wa Jimbo la Kinondoni wako salama kwani Mtulia hakuondoka na wanachama hivyo tuko vizuri na hatujasambaratika kama ilivyodaiwa hapo awali," amesema Muhunzi.

Amesema mbunge wa jimbo hili bado ataendelea kutoka Ukawa licha ya usaliti aliyoufanya Mtulia ili hali Chadema ilipigania kila hatua kuhakikisha amepata nafasi hiyo katika uchaguzi wa 2015.

"CCM hawako salama wasifikiri kumchukua Mtulia wamemaliza Wilaya ya Kinondoni, wanachama wapo na wataendelea kuwepo ndani ya Chadema," amesema.

Kwa upande wake katibu mwenezi Wilaya ya Kinondoni, George Mwingura amesema tangu kuondoka kwa Mtulia hakuna mwanachama aliyetoka kufuatana naye.

Kocha wa Simba Omog apewa mapumziko



UONGOZI wa Klabu ya Simba, umempa kocha mkuu wa timu hiyo, Joseph Omog siku zaidi ya siku kumi za mapumziko kabla ya kurejea kikosini kuendelea kuwanoa wachezaji wa timu hiyo wanaoendelea na mazoezi ya kujiandaa na michezo ijayo ya Ligi Kuu Bara.

Baada ya kuwa na mapumziko ya wiki moja, juzi Jumatatu Simba ilianza mazoezi kwenye Uwanja wa Chuo cha Polisi jijini Dar chini ya kocha msaidizi, Masoud Djuma raia wa Burundi.

Meneja wa Simba, Richard Robert, ameliambia Championi Jumatano, kuwa wanatarajia kuungana na Omog baada ya wiki moja na nusu ambazo ni zaidi ya siku kumi kwani likizo yake ni ndefu kuliko wengine.

“Vijana wanafanya mazoezi na kocha msaidizi wakati Omog akiwa mapumzikoni ambapo anatarajia kurejea kikosini baada ya wiki moja na nusu kuendelea kuwanoa vijana,” alisema Robert.

Moto mkubwa wazuka California



Karibu watu 27,000 walilazimishwa kukimbia manyumba yao usiku wa manane wakati moto mkubwa ulisamba kwa haraka kusini kwa jimbo la Carlifonia.

Watu wamehamishwa kwa lazima kutoka makwao katika miji ya Ventura na Santa Paula karibu kilomita 115 Kaskazini mwa Los Angeles.

Wazima moto walionya kuwa moto huo ulikuwa unasambaa kwa haraka na hawangeweza kuuzima.

Ukichochewa na upepo mkali moto uliosambaa ukubwa wa maelfu ya ekari kwa saa chache.

Gavana wa California Jerry Brown ametangaza hali ya tahadhari katika kaunti ya Ventura akiihaidi kukukabili moto huo kwa vyoyote vile.

Mapema iliripotiwa kuwa mtu mmoja alifariki kwenye ajali ya barabarani akijaribu kuukimbia moto huo, lakini idara ya wazima moto kaunti ya Ventura imesema kuwa hakuna mtu aliyepatikana kwenye gari hilo lilikuwa limepinduka.

Maafisa walisema kuwa mzima moto alijeruhiwa. Pia walisema kwa nyumba 150 zilikuwa zimeharibiwa na watu 260,000 walikuwa hawana umeme.

Zari aweka kambi Madale



Wakati kukiwa na figisufigisu kuhusu uhusiano kati ya wadada wawili waliozaa na mwanaume mmoja, Zarina Hassan ‘Zari’ na Hamisa Mobeto, mwanamke huyo mama wa watoto watano anayeishi Afrika Kusini, anadaiwa kutua jijini na kuweka kambi maalum kulinda kitumbua chake, Risasi Mchanganyiko limeambiwa.

Kwa mujibu wa chanzo chetu kilicho karibu na Zari, inadaiwa kuwa mjasiriamali huyo alikuwa jijini Dar es Salaam ambako alihudhuria shughuli mbili za watu wake wa karibu, lakini inadaiwa kuwa hiyo ilikuwa ni geresha tu, kwani ziara yake ya kushtukiza ilikuwa na lengo maalum.

“Unajua kuna mambo kidogo kama hayaeleweki ambayo Mobeto anafanya, sasa Zari amepiga hesabu na kuamua kujiongeza, amekuja mjini na kupiga kambi Madale kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa, katika matukio yote mawili alihudhuria na mzazi mwenzake, kitu ambacho kilimnyima kabisa nafasi Mobeto ya kusogelea,” alisema mtoa habari wetu.

Kumekuwa na uvumi kuwa Mobeto ameongea na kumalizana na mzazi mwenzake nje ya vyombo vya kisheria na baadhi wakidai kuwa wamerejesha hata uhusiano wao, kitu ambacho kinamfanya Zari kuishi kimachalemachale.

Katika video vilizowekwa katika mitandao mbalimbali ya kijamii, ilimuonyesha Zari akiwa na furaha tele, tofauti na mzazi mwenziye aliyeonekana kama kuna jambo ambalo hafurahishwi nalo. Zari raia wa Uganda, anaishi Afrika Kusini pamoja na watoto wake watano, wakiwemo watatu aliozaa na mumewe, Ivan Ssemwanga aliyefariki mapema mwaka huu.

Source: Global Publisher

Yanga yampiga ‘stop Ngoma


Huku wachezaji wenzake wakianza mazoezi ya pamoja kwa ajili ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbao, mshambuliaji wa Yanga Mzimbabwe, Donald Ngoma yeye amepigwa ‘stop kuungana nao.
Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu mshambuliaji huyo aliporejea nchini akitokea nyumbani kwao Zimbabwe alipokwenda kujitibia bila ya ruhusa ya viongozi.

Timu hiyo, imeanza mazoezi hayo juzi Jumatatu kwenye Gym ya City Mail iliyopo Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam chini ya kocha msaidizi, Shadrack Nsajigwa.

Taarifa zinaeleza, mshambuliaji huyo amezuiwa kuanza mazoezi hadi pale itakapotolewa hukumu ya adhabu yake kutokana na kosa la kinidhamu alilolifanya.

Mtoa taarifa huyo alisema, kamati ya utendaji ya timu hiyo hivi sasa inafanya vikao vyake kwa ajili ya kujadili adhabu ipi anayotakiwa kupewa mshambuliaji huyo baada ya kutenda kosa hilo.
 “Ngoma tumemzuia kwa hivi sasa kujihusisha na chochote katika timu ikiwemo kufanya mazoezi ya pamoja na wenzake walioanza gym, juzi Jumatatu asubuhi.

“Hivyo, mshambuliaji huyo tumemzuia kuanza mazoezi ya gym ambayo alitakiwa kuanza na wenzake kwa ajili ya kujiandaa na mechi ijayo ya ligi kuu dhidi ya Mbao FC.

“Tunataka nidhamu katika timu na kamwe hatutasita kutoa adhabu kwa mchezaji yeyote atakayekwenda kinyume na nidhamu kama ilivyokuwa kwa Ngoma ambaye yeye ligi kuu ikiendelea aliondoka kimyakimya nchini na kuelekea nyumbani kwao Zimbabwe,”alisema mtoa taarifa huyo.

Taarifa nyingine za mshambuliaji huyo za kukabidhi ripoti ya daktari wake aliyekuwa anamtibia Zimbabwe inayomtaka kupumzika nje ya uwanja kwa muda wa wiki sita.

Katibu Mkuu wa Yanga, Boniface Mkwasa amethibitisha kurejea kwa mshambuliaji ambaye aliondoka bila kutoa taarifa na amesema kwamba, maelezo na ripoti aliyokuja nayo bado hayajitoshelezi.


“Bado maelezo hayajitoshelezi kwa maana ya kwamba, ripoti imeandikwa na daktari wake lakini baada ya kutafakari tunahitaji tupate ripoti kamili kutoka kwa daktari wetu.

SOURCE: CHAMPIONI

Maandalizi sherehe ya miaka 56 ya Uhuru yakamilika


Maandalizi ya maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru yamefikia hatua za mwisho huku Serikali ikieleza kuwa sherehe hiyo itapambwa na gwaride la mkoloni litakalofanywa na Jeshi la Polisi.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge alisema

itakuwa ni mara ya kwanza kwa gwaride hilo la mkoloni kufanyika katika sherehe hiyo ambayo mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli.

“Maandalizi muhimu ikiwa ni pamoja na marekebisho ya uwanja na mahitaji mengine muhimu yapo katika hatua za mwisho,” alisema DK Mahenge.

Alifafanua kuwa maonyesho hayo yatakayofanyika Desemba 9 yatajumuisha gwaride maalumu la heshima lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama nchini na onyesho la makomandoo.

Nyinginie ni kwata ya kimya kimya iliyoandaliwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Onyesho la Jeshi la mkoloni kutoka Jeshi la Polisi.

“Watoto 225 kutoka shule za sekondari watashiriki katika gwaride hilo,” alisema.

Alisema lengo la Serikali kuwashirikisha ni kuwafundisha na kuwaridhisha tunu ya uhuru, uzalendo, umoja, mshikamano na utaifa.

Pia, kutakuwa na vikundi vya ngoma za asili kutoka Ruvuma, Kigoma, Zanzibar pamoja na kwaya kutoka Chunya mkoani Mbeya.

DK Mahenge aliwasihi Watanzania kumuunga mkono Rais Magufuli kupiga vita rushwa na kufanya kazi kwa bidiii kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Pia, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika maadhimisho hayo na kutoogopa mizinga itakayopigwa katika sherehe hizo kwasababu haina madhara.

Tetemeko la Ardhi latokea Dodoma



 Wataalamu wa jiolojia wamesema kuwa tetemeko la ardhi limetokea Kata ya Aneti wilayani Chamwino usiku wa kuamkia jana lina ukubwa wa 5 katika kipimo cha richter.

Tetemeko lenye ukubwa wa 5.1 kipimo cha richter lilitokea Julai mwaka juzi katika kata hiyo na kusababisha nyumba zaidi ya 60 kupata nyufa.

Ofisa Mwandamizi wa Jiolojia katika Wakala wa Jiolojia Nchini (GST), Gabriel Mbogoni alisema tetemeko hilo limetokea katika maeneo lilipotokea mwaka jana Kusini

Mashariki wa mji wa Aneti.

Alipoulizwa kama tetemeko hilo lililotokea saa 9 limeleta madhara yoyote, Mbogoni alisema hajapata taarifa.

“Ukubwa wa 5 siyo la kawaida. Unakumbuka la Bukoba lilikuwa na ukubwa gani? Ni kama 5.7 tetemeko linaweza likawa na ukubwa wa tano hadi saba lakini lisilete madhara,” alisema.

Mbogoni alisema tetemeko linaweza likawa na ukubwa mdogo lakini likaleta madhara kutegemea na mpasuko wa miamba umetokea katika kina gani.

“Inategemea pia na eneo ambalo mawimbi yanapita, ile miamba iko namna gani,” alisema Mbogoni.

Alifafanua kuwa tetemeko hilo lilipiga kati ya sekunde nne na tano na kwamba likipiga kati ya sekunde 20 hadi 30 madhara yake ni makubwa sana.

Mbogoni alisema madhara hayo yanatokana na jengo kutikiswa kwa muda ambazo tetemeko linadumu.

Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga alisema hadi jana mchana kulikuwa hakujaripotiwa madhara yoyote.

“Nimewasiliana na viongozi wa kule, diwani na mwenyekiti wa kitongoji wanasema ni kweli lilitokea lakini hadi sasa hakujaripotiwa madhara yoyote,” alisema.

Tetemeko kubwa la ardhi kutokea nchini lilitokea miaka tisa iliyopita katika eneo la Oldonyo Lengai ambalo lilikuwa na ukubwa wa 5.9 kwa kipimo cha richter.

Maji, Vyoo nichangamoto katika Vituo vya Afya Vijijini


Hali ya upatikanaji wa majisafi na salama pamoja na vyoo katika vituo vya huduma za afya maeneo ya vijijini bado ni changamoto, huku asilimia 44 pekee ndio vina huduma hiyo.

Kati ya hizo, asilimia 34 ya vituo hivyo vimebainika kuwa bado vinatumia maji kutoka katika vyanzo ambavyo si salama, ambavyo ni mito, maziwa, visima visivyofunikwa na mabwawa, huku asilimia 56 zikikosa kabisa uwapo wa huduma hizo muhimu.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa utafiti wa tathmini ya upatikanaji wa huduma muhimu katika vituo vya afya wa mwaka 2014/15 uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na wadau wengine.

Ili kukabiliana na hali hiyo, jana Serikali imezindua Mwongozo wa Taifa wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira katika vituo vya afya.

Mwongozo huo umezinduliwa na Mkurugenzi wa Uratibu wa Kisekta wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Dk Andrew Komba kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Mpoki Ulisubsya.

Akizungumza kuhusu mwongozo huo, Mratibu wa Kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira, Anyitike Mwakitalima alisema umeandaliwa kuboresha utoaji huduma katika vituo vya afya nchini.

“Sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi kwa muda mrefu kutokana na kutokuwapo kwa mwongozo wa Taifa ambao utasaidia kusimamia ubora wa utoaji huduma katika vituo vya afya ikiwamo ujenzi wa vyoo bora na upatikanaji wa maji safi.

“Tulibaini pia asilimia 42 ya vituo havina sehemu maalumu za kunawia kwa ajili ya watoa huduma za afya kunawa mikono katika vyumba vya kujifungulia, hali hii ni mbaya ikiwa hatutachukua hatua, kuna uwezekano wa watoto wanaozaliwa kupata athari mbalimbal,” alisema.

Awali, Dk Komba alisema mwongozo huo utasaidia Serikali na wadau wa maendeleo kusimamia na kutekeleza masuala ya usafi wa mazingira.

“Mwongozo unatoa maelekezo stahiki namna ambavyo vituo vya afya katika ngazi zote vinavyopaswa kufanya katika upangaji mipango na uandaaji wa bajeti zitakazotumika katika usimamizi wa usafi wa mazingira,” alisema.

Mkurugenzi wa Mipango wa Shirika la WaterAid, Abel Deganga alisema kutokana na kukosekana kwa mwongozo kwa muda mrefu unaopima hali ya upatikanaji maji katika vituo vya afya nchini, utendaji kazi wa Serikali na wadau ulikuwa ukisuasua.

Hizi ndizo sababu za ongezeko la watu




NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO DK. FAUSTINE NDUNGULILE

IMEELEZWA kuwa kasi ya ongezeko la watu nchini inatokana na jamii kutokuwa na elimu ya  afya ya uzazi inayochangiwa na umaskini ambapo mwanamke aliyefikia umri wa kuzaa anazaa watoto zaidi ya nane.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndungulile

“Takwimu za utafiti wa hali ya afya na idadi ya watu mwaka 2015/2016 inaonyesha kasi ya ongezeko la idadi ya watu ni 2.7 na hali ya uzazi ni wastani wa watoto watano kwa kila mwanamke aliye kwenye umriwa kuzaa,’’ alisema Ndugulile.

Alisema wastani wa idadi ya watoto kwa mwanamke asiye na elimu ni watoto saba, wakati kwa mwanamke aliyefikia elimu ya sekondari ni watoto wanne na wale walio na hali ya umaskini mama anazaa watoto nane ikilinganishwa na yule mwenye uchumi mzuri anayezaa watoto watatu.

Alisema serikali ya awamu ya tano inahakikisha mtoto anayetakiwa kwenda shule kwa ngazi ya msingi na sekondari inagharamia elimu yao .

Aliongeza serikali inasisitiza ujenzi wa viwanda ili vijana wanaomaliza masomo ngazi mbalimbali wapate  ajira.Mwakilishi mkazi wa UNFPA  nchini, Jacqueline Mahon, alisema kumekuwapo na ongezeko kubwa la kutokuwa na usawa duniani la kipato, rasilimali na haki.

Alisema katika nchi nyingi zilizoendelea ikiwamo Tanzania, wanawake wengi wanakosa nguvu katika kufanya maamuzi juu ya masuala ya afya ya uzazi, ikiwamo juu ya maamuzi ya muda na wakati gani wa kushikaujauzito.

“Usawa na ustawi wa watu wote ni msingi wa malengo ya maendeleo endelevu ya dunia ili kuyafikia, tunahitaji kuwajengea uwezo wale ambaowanaonekana wako nyuma hasa wanawake na watoto wa kike,” alisema.

Cristina Kwayu, kutoka UNFPA, alisema  kila mwaka idadi ya watu inaongezeka ambapo kwa sasa Tanzania inakadiliwa kuwa na watu zaidi ya milioni 50.

Aliongeza kuwa changamoto ya kasi ya idadi ya watu imechangia watoto kutopelekwa shule, mtoto kuzaa mtoto hata madarasa kutojitosheleza kutokana na kila mwaka watoto kuongezeka.