Thursday, 30 November 2017

Afariki baada ya kunywa sumu mahakamani



Kikao cha kusikiliza rufaa iliyowasilishwa na washtakiwa wa uhalifu wa kivita mjini The Hague, Uholanzi kimesitishwa ghafla baada ya mmoja wa washtakiwa kusema amekunywa sumu baada ya kusikiliza hukumu.

Slobodan Praljak, 72, alikuwa mmoja wa viongozi sita wa zamani wa kisiasa na wa kijeshi wa Bosnia wa asili ya Croatia ambao walikuwa wamefika mahakamani.

Amefariki akitibiwa hospitalini na Umoja wa Mataifa umesema sasa mahakama hiyo ni "eneo la uhalifu".

Alikuwa amehukumiwa kufungwa jela miaka 20 mnamo 2013 kwa makosa ya uhalifu wa kivita yaliyotekelezwa katika mji wa Mostar.

Baada ya kusikiliza hukumu kwamba majaji walikuwa wamedumisha kifungo hicho, alimwambia jaji, "Nimekunywa sumu".

Sita hao walikuwa wanasikiliza uamuzi wa mwisho wa rufaa uliokuwa unatolewa na mahakama maalum ya kimataifa ya UN iliyokuwa inashughulikiwa makosa yaliyotekelezwa Yugoslavia (ICTY).

Ingawa walikuwa washirika dhidi ya Waserbia wa Bosnia wakati wa vita hivyo vya 1992-95, Wacroatia wa Bosnia na Waislamu walipigana wenyewe kwa wenyewe kwa miezi 11.

Praljak alisimama na akainua mkono wake hadi kwenye kinywa chake, kisha anainamisha kichwa chake nyuma na kuonekana kunywa kitu kutoka kwenye gilasi ndogo.

Jaji mwandamizi Carmel Agius mara moja alisitisha shughuli na gari la kuwabeba wagonjwa likaitwa.

"Sawa," jaji alisema. "Tunaahirisha ki...Tunaahirisha...Tafadhari, pazia. Usiondoe gilasi ambayo ameitumia alipokunywa kitu."

Kabla ya pazia kurejeshwa, ukumbi wa mahakama umeonekana kujawa na mkanganyiko, anasema mwandishi wa BBC Anna Holligan kutoka The Hague.

Gari la kuwabeba wagonjwa lilionekana baadaye likifika nje ya ukumbi wa mahakama huku helikopta ikipaa juu angani.

Wafanyakazi kadha wa uokoaji wameingia ukumbini na vifaa vyao.

Uhalifu dhidi ya Waislamu

Praljak, kamanda wa zamani wa wahudumu wakuu wa Jeshi la Walinzi wa Wacroatia wa Bosnia (HVO), alifungwa kwa makosa ya jinai dhidi ya binadamu.

Baada ya kufahamishwa kwamba wanajeshi walikuwa wanawakamata Waislamu Prozor majira ya joto 1993, alikosa kuchukua hatua zozote za maana kuzuia hilo, mahakama hiyo ya UN ilisema.

Aidha alikosa kuchukua hatua hata baada ya kupashwa habari kwamba mauaji yalikuwa yamepangwa, pamoja na mashambulio dhidi ya wafanyakazi wa mashirika ya kimataifa na kuharibiwa wka daraja la kale la mji wa Mostar na misikiti.

Mahakama ya ICTY ambayo iliundwa 1993 itamaliza kati yake mwisho wa mwaka huu.

Wakamatwa kwa kuonyesha makalio hekaluni



Watalii wa Marekani wakamatwa kwa kupiga picha za utupu hekaluni

Raia wawili wa Marekani wamekamatwa nchini Thailand baada ya kuchapisha picha yao mtandaoni wakionyesha makalio yao katika hekalu.

Watalii hao walipiga picha hiyo katika hekalu maarufu nchini Bangkok Wat Arun na kuichapisha katika mitandao ya Twitter na instagram.

Mamlaka ya uhamiaji iliambia BBC kwamba wawili hao Joseph na Travis Dasilva wote wakiwa na umnri wa miaka 38 watapigwa faini na kurudishwa kwao.

Thailand ina sheria kali kuhusu tabia zinazoonekana kutokuwa na heshima na zinazoingilia dini yake ya Buddha.

Watalii hao walikamatwa jioni Jumane wakati walipokuwa wakiondoka nchini humo katika uwanja wa ndege wa Bankok Don Mueang.

Naibu msemaji wa idara ya uhamiaji nchini Thailand, kanali Choengron Rimpadee aliambia BBC kwamba wawili hao walikuwa katika orodha ya watu waliokuwa wakichunguzwa baada ya mamlaka kuona picha hizo zenye utata katika mitandao ya kijamii.

''Wakati watakaposhtakiwa maafisa wa polisi wa uhamiaji wa Thailand watafutilia mbali visa zao na kutaka warudishwe makwao'', alisema.

Pia watapigwa marufuku kurudi nchini Thailand.

Alielezea kwamba wawili hao waliwasilishwa katika kituo cha polisi cha Yai nchini Bangkok ili kushtakiwa kwa kuonyesha utupu katika eneo la umma, makosa ambayo mtu anapopatikana na hatia anaweza kupigwa faini ya dola 153.

Hatahivyo, serikali ya Thai na maafisa wa polisi wameambia vyombo vya habari kwamba mashtaka hayo yanaweza kuwa mabaya zaidi.

Waombolezaji watelekeza jeneza



HALI ya taharuki na hofu imezuka katika Kijiji cha Katani Kata ya Nkandasi wilayani Nkasi mkoani Rukwa na kusababisha waombolezaji kutimua mbio na kuacha jeneza lenye mwili wa marehemu baada ya mvua kubwa kuanza kunyesha na kubomoa nyumba za wakazi wa kijiji hicho.

Tukio hilo lilitokea jana saa 6 mchana baada ya kuanza kunyesha mvua kubwa iliyoambatana na radi na upepo mkali ulioezua baadhi ya nyumba za wananchi hao ambao walikuwa wakiomboleza msiba wa mwananchi mwenzao aliyefariki baada ya kuugua siku chache zilizopita.

Mwenyekiti wa serikali ya kitongoji cha Kaungo, Robert Kanoni, alisema wakiwa wanaelekea kufanya maziko ya marehemu Dismas Kanoni aliyefariki jana, ghafla ilianza kunyesha mvua kubwa ikiambatana na radi na upepo mkali hali iliyosababisha baadhi ya waombolezaji kutimua mbio na kurejea majumbani kutokana na hofu iliyoibuka kufuatia tukio hilo.

Baadhi ya wananchi walivumilia nakurejea na jeneza lililokuwa na mwili wa marehemu nyumbani na kuahilisha maziko kwa muda ili kupisha hali hiyo itulie na walikwenda kuzika baadaye katika makaburi yaliyopo kijijini hapo.

Alisema tukio hilo limezua hisia za kishirikina kwa wananchi wa kijiji hicho kwani miezi miwili iliyopita baba yake na marehemu huyo alifariki baada ya kugongwa na gari la kampuni ya ujenzi wa barabara na walipofanya maziko siku iliyofuata walikuta ngozi ya kondoo juu ya kaburi la marehemu kitendo kilichowashangaza.

Kanoni alisema kutokana na mvua hiyo, nyumba zipatazo 10 zimebomoka kabisa na zinatakiwa kujengwa upya huku makazi licha ya kuwa wamepata hifadhi na misaada ya kibinadamu kwa wenzao. 

Naye Peter Kalale, mkazi wa kijiji hicho akizungumzia tukio hilo, alisema mara kwa mara kijiji hicho kimekuwa kikikumbwa na dhoruba pindi mvua zinaponyesha kwa kuwa kimepitiwa na mkondo wa upepo mkali ambao unasababisha hali hiyo.

Alisema changamoto iliyopo ni tabia ya wananchi kukata miti kwa ajili ya mashamba hivyo kusababisha pepo zinapovuma hazikuti kizuizi chochote na kuwa sababu ya kuezuliwa nyumba zao na wakati mwingine kubomoka kabisa.

Mwenyekiti wa kamati ya maafa ya wilaya hiyo ambaye ni Mkuu wa wilaya  hiyo, Said Mtanda, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutoa wito kwa wananchi kujenga makazi bora kwani miongoni mwa nyumba  hizo zipo ambazo zimeezekwa kwa nyasi.

Alisema sera ya serikali ya awamu ya tano ni kuwahimiza wananchi wajenge nyumba bora na za kisasa ili waepuke majanga yanayotokana na tabianchi kwani bila kufanya hivyo, wananchi wataendelea kupata hasara.

Hizi ndizo sababu za Ngoma kusepa Yanga



MSHAMBULIAJI WA TIMU YA YANGA, DONALD NGOMA

HUKU mshambuliaji wa kimataifa wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, Donald Ngoma, akiwa nje ya kikosi cha timu hiyo kutokana na kuelezwa kuwa ni majeruhi wa goti, imebainika kuwa sababu ni kutokana na kuidai klabu hiyo fedha za usajili.

Akizungumza na Nipashe mmoja wa watu wa karibu na Ngoma (jina tunalihifadhi), alisema Ngoma ni mzima na kwamba yupo katika "mgomo baridi" wa kuitumikia Yanga ambayo inadhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, akishinikiza kulipwa kwanza fedha zake za usajili kama walivyokubaliana.

Chanzo hicho kilisema kuwa kutokana na Yanga kushindwa kutimiza makubaliano hayo licha ya Ngoma kusaini mkataba wa miaka miwili, mshambuliaji huyo amesema kuwa tayari mkataba waliosaini umevunjika rasmi.

Aliongeza kuwa kutokulipwa kwa fedha hizo, kumemfanya mshambuliaji huyo kuchukua uamuzi wa kujiweka pembeni kwa sababu hapati majibu ya kueleweka kuhusiana na madai yake.

"Sababu kubwa ya Ngoma kuikacha Yanga ni kuwa anawadai, anasema wanamzungusha, hilo ndiyo tatizo kuu na si majeruhi kama ilivyokuwa hapo awali, anajuta kwa nini alisaini mkataba mpya ambao bado hajafaidika nao kama walivyokubaliana," kilisema chanzo hicho.

Katibu Mkuu wa Yanga , Boniface Mkwasa, aliliambia gazeti hili jana kuwa wamemwandikia mshambuliaji huyo barua mara mbili za kujieleza, lakini bado hajatoa majibu yoyote kuhusiana na hatua ya kuondoka nchini bila kupewa ruhusa na klabu.

Hata hivyo, Mkwasa, kocha wa zamani wa mabingwa hao watetezi hakuwa tayari kuweka wazi kama Ngoma anaidai au haidai Yanga na kusema kuwa mshambuliaji huyo ni mali yao.

Mkwasa alisema kuwa Ngoma ni mchezaji halali wa Yanga ambaye alisaini mkataba wa miaka miwili Julai mwaka huu na endapo ataendelea kukaa nje ya kikosi, hatua kali dhidi yake zitachukuliwa ili iwe fundisho kwa wachezaji wengine kutofanya kosa kama hilo.

"Kwanza tulikuwa hatujui yuko wapi, tukamwandikia barua kupitia barua pepe ajieleze yuko wapi, hakuijibu, baadaye kupitia mitandao tunaona yuko Zimbabwe, tukamtumia barua nyingine ili aseme kwa nini ameondoka nchini bila ruhusa, amekaa kimya hadi leo (jana), sasa tunashangaa kuona ameitwa katika timu ya Taifa, wamemuona wapi wakati yeye ni majeruhi?" Alihoji Mkwasa.

Katibu huyo aliongeza pia wamefurahishwa na uteuzi alioupata, lakini wanashangaa kusikia mshambuliaji huyo ni mchezaji huru, jambo ambalo si la kweli na klabu yake inafahamu wazi ana mkataba ambao unambana na anatakiwa kuitumikia timu kwenye mechi za ligi na mashindano mengine watakayoshiriki.

Source: Nipashe

Tanzania uso kwa uso na Libya Jumapili hii



Kilimanjaro Stars, ikifanya mazoezi mbalimbali katika Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam

Timu ya Taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), itashuka dimbani siku ya Jumapili ya Desemba 3 huko nchini Kenya kuikabili Libya katika michuano ya Chalenji mwaka 2017.

Kilimanjaro Stars itacheza mchezo huo wa kundi A, katika kuwania kombe la michuano ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA ambayo inatarajiwa kuchezwa nchini Kenya kuanzia Desembe 3 hadi 17 mwaka huu.

Mataifa 10 yanatarajiwa kushiriki katika michuano hiyo mikubwa kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki huku droo ya hatua ya makundi ikionyesha mwenyeji Kenya itacheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Rwanda huku Tanzania ikiikabili Libya siku hiyo.

Kundi A: Kenya, Rwanda, Libya, Tanzania na Zanzibar

Kundi B: Uganda, Zimbabwe, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini.

Michuano hiyo itachezwa katika uwanja wa Bukhungu mjini Kakamega, Afraha Nakuru, Mumias Sports Complex na Moi, mjini Kisumu.

Hata hivyo, kuna wasiwasi michuano hii isifanyika mjinui Kisumu kwa hofu za kiusalama kwa mujibu wa chama cha soka nchini Kenya na sasa uwanja wa Machakos utatumiwa.

Serikali yashindwa pingamizi kesi ya mbunge CUF



Dar es Salaam. Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh ameruka kihunzi cha Serikali mahakamani, baada ya kushinda pingamizi la awali lililowekwa na Serikali katika kesi ya kuhoji uhalali wa wajumbe wapya wa bodi ya wadhamini wa chama hicho.

Saleh ambaye pia ni mwanasheria amefungua kesi Mahakama Kuu akihoji uhalali wa wajumbe wapya wa bodi waliosajiliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

CUF imegawanyika pande mbili; inayomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na inayomuunga  Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye ndiye aliunda bodi inayopingwa.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Ofisa Mtendaji wa Rita, anayewakilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kupitia jopo la mawakili wa Serikali linaloongozwa na Gabriel Malata.

Wengine ni bodi ya wadhamini (mpya) ya CUF, mwenyekiti wa bodi hiyo, Peter Malebo, wanaowakilishwa na wakili Majura Magafu na wajumbe wapya wa  bodi hiyo wanaowakilishwa na wakili Mashaka Ngole.

Wadaiwa wengine ni wajumbe wa bodi waliomaliza muda wao na ambao wengine walipendekezwa tena na upande wa Maalim Seif ambao hata hivyo hawakuidhinishwa na Rita, wanaowakilishwa na mawakili Juma Nassoro, Daimu Halfan na Hashim Mziray.

Serikali kwa niaba ya mdaiwa wa kwanza (Mtendaji wa Rita), iliweka pingamizi la awali ikiiomba Mahakama iitupilie mbali kesi, ikitoa hoja kuwa imefunguliwa kabla ya wakati bila kufuata utaratibu wa kuishtaki Serikali na kwamba mdai amemshtaki mtu asiyestahili.

Saleh anayewakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Fatma Karume, ameshinda pingamizi hilo katika uamuzi uliotolewa na Jaji Wilfred Dyansobera alioutoa jana Jumatano, Novemba 29,2017.

Jaji Dyansobera ametupilia mbali pingamizi hilo la Serikali baada ya kuridhika kuwa hoja za pingamizi hilo hazikuwa na mashiko.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo, wakili Malata alidai mdai amemshtaki mtu asiye sahihi; akidai Rita ni wakala ndani ya ofisi ya Kabidhi Wasihi Mkuu ambaye ndiye aliyestahili kushtakiwa na si mtendaji wa Rita.

Pia, alidai kesi ilifunguliwa kabla ya wakati kwa kuwa ilifunguliwa kabla ya kutoa taarifa ya kusudio kwa Serikali ya siku 90, kama inavyoelekezwa katika sheria ya mashauri dhidi ya Serikali.

Wakili Mpoki alipinga hoja hizo akidai mtu waliyemshtaki ni sahihi na kwamba, kwa aina ya kesi hiyo hapakuwa na haja ya kutoa taarifa ya siku 90 kwa Serikali kwa kuwa hawaishtaki Serikali.

Jaji Dyansobera katika uamuzi wake amekubali hoja za upande wa mdai, kuwa suala la nani ashtakiwe na nani asishtakiwe ni jukumu la mdai kwa kuwa ndiye anaona kuwa nafuu anazoziomba atazipata kwa nani.

Amesema kesi hiyo haikuhitaji kutoa taarifa ya siku 90 kwa Serikali kwa kuwa si Serikali inayoshtakiwa bali kesi hiyo inahusu mgogoro wa ndani ya chama cha siasa, ambako Serikali haipaswi kujiingiza wala kuwa na upande.

Jaji Dyansobera amepanga kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo Desemba 8,2017 kwa kusikiliza hoja za msingi za mbunge Saleh na majibu ya wadaiwa na kisha atapanga tarehe ya kutoa uamuzi.

Majibu ya DNA yapotea katika mazingira ya kutatanisha



Hai. Familia ya binti wa kidato cha pili anayedaiwa kubakwa na kupewa ujauzito mwaka jana na mzee wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania(KKKT)  Kanda ya Usharika wa Nkuu Kiserenyi, wamemuomba mwanasheria mkuu wa Serikali kuingilia kati baada ya majibu ya vinasaba (DNA) kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Mzee huyo aliukana ujauzito huo, hali iliyosababisha hakimu mkazi wilaya ya Hai, Anold Kerekiano anayeisikiliza kesi hiyo kuamuru mtoto afanyiwe vipimo vya DNA ili kujua ukweli.

Hata hivyo, baada ya kufanyiwa vipimo majibu yalichukua mwaka mmoja na yalipotoka hayakuonekana.

Inaelezwa majibu hayo yalitolewa Juni 13, lakini hayakuwafikia wahusika hali ambayo inaitia shaka familia hiyo kuwa huenda yamechukuliwa.

Binti huyo anadai kuwa, baba huyo tangu mtoto azaliwe hajawahi kumpa matunzo mtoto wake.

Alisema anaishi maisha magumu kutokana na familia yake kuwa duni, hivyo anashinda mtoni na mtoto wake kupondaponda mawe ili kupata fedha ya kumnunulia mwanae maziwa.

Naye mama mzazi wa binti huyo, Martha Kweka aliiomba Serkali kuingilia kati suala hilo kutokana na binti yake kuishi kwa shida na ndoto zake zimeharibika.

Martha alisema binti yake ni mtoto wake wa kwanza na alikuwa akimtegemea kwa asilimia kubwa, ili baada ya kumaliza masomo angemsaidia kutokana na maisha duni wanayoishi.

Baba mzazi wa binti huyo, Kulasauko Nyuki alisema anashangaa unyama aliofanya mzee huyo na kuachiliwa wakati  watoto wake wanaendelea kusoma.

“Hii si sawa naomba sheria ifuate mkondo wake mimi nashindwa kuvumilia kuona mtuhumiwa anadunda na kutamba kuwa, hatuwezi kumfanya kitu chochote maana familia yangu ni maskini, naumia sana,” alisema Nyuki.

Hata hivyo, ofisa ustawi wa jamii wa Hai, Helga Njuyui alikiri majibu ya DNA kutumwa Juni  13, lakini inashangaza hayajawafikia.

Pretty ajibu madai ya kutelekeza Ndoa



MSANII wa filamu Bongo, Suzan Michael ‘Pretty Kind’ amefungukia madai ya kuwa, kabla ya kwenda India ‘kudanga’ aliolewa na kuitelekeza ndoa kwa kusema si kweli kama aliolewa.

Akifafanua kuhusu madai hayo yaliyoshika kasi kwenye mitandao ya kijamii, Prety alisema ukweli ni kwamba hakuwahi kuolewa, alikuwa na mwanaume huyo polisi kipindi yupo Mwanza ambaye alikuwa anaishi naye kinyumba lakini waliachana hata kabla ya safari yake ya India.

“Haya ni maneno ya watu wanaotaka kunichafulia CV yangu, huyo mwanaume sikuwahi kufunga naye ndoa ya serikali wala ya kimila, ila niliwahi kuishi naye kinyumba na tulimwagana kabla sijafikiria kwenda India, iweje hayo madai yaibuke leo,” alisema Prety.


Marekani yaitaka dunia kusitisha biashara na Korea Kaskazini



Marekani imetoa wito kwa mataifa mbalimbai kukata uhusiano wake wa kidiplomasia na kibiashara na Korea Kaskazini, ikiwa ni hatua ya kupinga majaribio ya makombora ambayo yamekuwa yakifanywa na taifa hilo.

Balozi wa Marekani Nikki Haley, ametoa pendekezo hilo katika mkutano wa dharura wa baraza la usalama la umoja wa mataifa unaoendelea mjini New York.

Bi. Haley amesema kuwa Rais wa Marekani amemtaka Rais wa China Xi Jinping kusitisha biashara ya mafuta ghafi na Korea Kaskazini, kama sehemu ya kutekeleza hatua ya kuwekewa vikwazo kwa taifa hilo.

Kupitia hatua hii ya kuiwekea vikwazo Korea Kaskazini tunapaswa kusitisha asilimia tisini ya biashara na Korea Kaskazini pamoja na asilimia 30 yamafuta yake.

Mwaka 2003, China ilisitisha kupelekea mafuta Korea Kaskazini ,muda mfupi baadaye taifa hilo likasogea katika meza ya majadiliano.

''Tumefikia hatua ya kuitaka China kuchukua hatua Zaidi katika hili, ni lazima isitishe kuipatia mafuta Korea Kaskazini," alisema Haley.

Wajumbe wa baraza la usalama la umoja wa mataifa wanakutana mjini Ne York kujadili hatua ya Korea kaskazini na majaribio ya makombora ya masafa marefu.

Msemaji wa katibu mkuu wa umoja wa Stéphane Dujarric, amesema kuwa Antonio Guterres, amelaani hatua hiyo Korea Kaskazini na kuongeza kuwa huo ni ukiukaji wa maamuzi ya baraza la usalama la umoja wa mataifa.

Sasha; Naolewa ili kutoa Nuksi


MWANADADA mwenye mvuto wa aina yake Bongo, Sasha Kassim ambaye anatarajia kufunga ndoa mwanzoni mwa mwaka kesho amesema kuwa, ameamua kuolewa ili kutoa nuksi.

Sasha ambaye hujulikana sana mitandaoni kwa picha zake za kihasara, alisema hadi sasa bado hajaenda kutambulishwa ukweni na wala hakuna mpango huo, ila amekuwa akiwasiliana na wakwe zake kwa njia ya simu, baada ya ndoa ndipo ataenda kupata baraka zao lakini makazi yake yataendelea kuwa Bongo.

“Naolewa kutoa nuksi si unajua mwanamke kukaa bila ndoa haileti picha nzuri, wakwe zangu wamenikubali japo hawajawahi kuniona laivu zaidi ya kwenye simu, nimeshaongea na mume wangu mtarajiwa kwamba akinioa nitaendelea kuishi Bongo, sababu napapenda sana huko Italy nitakuwa naenda kwa muda mfupi na kurudi na amekubali,” alisema Sasha ambaye anatarajia kuolewa na Bonphace, raia wa Italy.

VIDEO ya Waziri Mkuu alipokamata Semitrela 44 Bandarini

VIDEO ya Waziri Mkuu alipokamata Semitrela 44 Bandarini



TCRA Mwanza imewapeleka Mahakamani Watu watatu kwa kugushi namba tambulishi za simu



TCRA Mwanza imewapeleka Mahakamani Watu watatu kwa kugushi namba tambulishi za simu



KESI YA C.U.F BADO INAENDELEA



KESI YA C.U.F BADO INAENDELEA