picha ya mtandao
Wakati wafanyakazi wa Wakala wa Barabara (Tanraods) wakiendelea kuweka alama kwenye nyumba zinazotakiwa kubomolewa kupisha upanuzi wa Barabara ya Morogoro, wakazi wanaoishi kati ya Ubungo na Kimara wamelalamikia kitendo hicho.Baada ya kutekeleza ubomoaji wa nyumba kati ya Kimara na Kiluvya zilizo ndani ya mita 121.5 kutoka katikati ya barabara hiyo, ubomoaji mwingine utazikumba takriban nyumba 1,200 zilizo ndani ya mita 90, zikiwemo tano za ibada, vituo vya mafuta na majengo ya biashara nyingine kama za starehe.Ubomoaji huo pia utalikumba moja ya majengo maarufu ya makao makuu ya Shirika la Umeme (Tanesco) lililopo Ubungo.Eneo hilo na mengine ndiyo yaliyozua utata mwaka 2011 baada ya kutangazwa ilani ya kubomoa nyumba zote zilizo ndani ya hifadhi ya barabara bila ya kulipa fidia na kumsukuma aliyekuwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutangaza kusimamisha ubomoaji ili kusubiri uamuzi wa Baraza la Mawaziri.Rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete pia alisema bila ya kutaja eneo kuwa ubomoaji ni lazima uzingatie historia ya eneo husika na haki za binadamu kwa kutoa muda wa kutosha kwa wakazi ikiwa nyumba zao ni lazima zibomolewe kutokana na mipango ya Serikali.Mpango huo ulisimama na sasa, miaka saba baadaye, ubomoaji huo umefufuliwa na wafanyakazi wa Tanroads wanapita maeneo hayo kuweka alama ya “X”.Wakizungmza kwa nyakati tofauti, wananchi wa maeneo hayo waliiambia Mwananchi kuwa kitendo cha kubomoa nyumba zao kitawasababishia machungu kwa kuwa hawajui pa kwenda.“Kubomoa nyumba kutanizidishia msongo wa mawazo. Mume wangu alifariki mwaka juzi na nimebaki na watoto watatu. Nategemea nyumba hii kama njia ya kuniingizia kipato,” alisema mkazi wa Kimara Baruti aliyejitambulisha kwa jina la Furaha Nassoro ambaye ameishi eneo hilo kwa miaka 12.“Nimeweka wapangaji vyumba sita. Hii ndiyo ajira yangu, sina kazi wala biashara ngingine.”Alisema wakati Tanroads wanakwenda kuweka alama, walimtaka awe ameondoka ndani ya mwezi mmoja, hali iliyompa wakati mgumu kwa kuwa hautoshi.“Watoto wangu wote wanasoma kwa uhamisho wa harakaharaka hivi nawezaje kumudu gharama hizi? Mwezi ujao kama watakuja kubomoa, itabidi wanangu wasiende shule hadi hapo nitakapopata pesa kwa ajili ya kuhama,” alisema.Alisema kinachofanyika ni kwa ajili ya maendeleo, lakini alidai kuwa maendeleo hayawezi kuja wakati wananchi wana machungu ya kubomolewa nyumba na badala yake kulala nje. Mkazi mwingine wa Ubungo, James Haule alisema alipokea kwa huzuni taarifa ya nyumba yake kuwekwa alama ya kutakiwa kubomolewa kwa kuwa alimaliza ujenzi wa nyumba hiyo mwishoni mwa mwaka jana.Haule aliiomba Serikali kuongeza miezi mingine miwili.“Mwezi mmoja dada hautoshi. Tuna watoto, tunasomesha, maisha yenyewe ya sasa kama unavyoyaona. Mwezi huu mmoja napata wapi pesa ya kupanga au Serikali inataka tuaibike?”alihoji.Katika eneo jingine, Mwananchi ilimkuta mzee aliyejitambulisha kwa jina la Onesmo Mwinuka akiwa nje ya nyumba yake huku akitazama alama ya “X”, usoni akionekana kupoteza matumaini.“Hivi si walishabomoa Kimara? Huku tena wanataka nini? Kwani eneo lote la Kimara halitakiwi kuishi mtu? Sisi ni wanyonge, Rais atuonee huruma,” alisema Mwinuka.Alisema kwa kuwa lengo la Serikali ni kuleta maendeleo ya nchi, lakini pia iangalie namna ya kuwasaidia wazee kwa vile maisha yao yatakuwa hatarini watakapobomolewa.Diwani wa kata ya Kimara, Pascal Manota alisema alishaongea na wananchi kuwataka wajiandae kulipokea suala hilo kwa kuwa haliwezi kuepukika.Alisema kwa sasa anawashauri wananchi hasa wapangaji kulipa kodi ya muda mfupi ili kuepuka hasara baadaye kwa kuwa muda wowote huenda Tanroads wataanza kubomoa nyumba hizo.“Wametoa notisi ya mwezi mmoja, kwa hiyo huenda mwezi ujao zoezi la kubomoa likaanza kwa hiyo nini cha kufanya ni kuwashauri tu wananchi wajipange na kuzoea hii hali,” alisema. Akizungumza na Mwananchi, meya wa Ubungo, Boniface Jacob alisema amewaambia wananchi wapeleke suala hilo mahakamani ili wapewe haki zao na atawatafutia mwanasheria.Alisema kitendo cha kutoa mwezi mmoja ni kuwanyima haki kwa kuwa ilibidi wananchi wafuatilie kwanza kujua hatima yao.Meneja wa Tanroads wa mkoa, Julius Ndymukama alisema uwekaji alama utafuatiwa na ubomoaji.“Tumetoa notisi ya mwezi mmoja na baada ya hapo tutaanza kubomoa,” alisema.
Dodoma. Jumla ya wakazi 1,172 wanaoishi katika vijiji vitano vilivyopojirani na Ikulu Chamwino mkoani hapa wamenufaika na mafunzo yakuwaongezea ujuzi ili washiriki vyema katika upanuzi wa makazi yaRais.Neema hiyo imefuatia utekelezaji wa agizo la Rais John Magufulialilolitoa Julai mwaka jana mjini hapa la Serikali kuhamia mkoani hapakabla ya awamu ya kwanza ya uongozi wake kukamilika.Tayari Waziri Mkuu, mawaziri, manaibu, makatibu wakuu, manaibumakatibu wakuu na baadhi ya watumishi wameshahamia mjini hapa ikiwa niutekelezaji wa agizo hilo.Akizungumza katika mahafali ya tisa ya Chuo cha Veta mkoani hapa, Mkuuwa chuo hicho Ramadhan Mataka amesema kuwa mafunzo hayo yaliendeshwachini ya mfumo wa Competent Based Education and Training (CBET).“Tumeshirikiana na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambaotumeshirikiana nao katika kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa baadhi yawashiriki 1,172 kutoka katika vijiji vitano kwa lengo la kuwaongezeaujuzi ili washiriki vyema katika upanuzi wa Ikulu ya Chamwino,” amesemaMataka.Mataka amesema pia chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Kazi Ajira,Vijana na Watu wenye Ulemavu wamewatambua wanagenzi 260 ambao kati yahao 241 wamefaulu baada ya kupimwa mkoani Dodoma.Akizungumzia kuhusu programu hiyo ya wanagenzi, Naibu Waziri katikaOfisi ya Waziri Mkuu Kazi, Ajira, Vijana Antony Mavunde amesema chiniya programu hiyo wanawachukua wakufunzi wa Veta na kwenda nao mtaanikwa ajili ya kubaini mapungufu waliyonayo vijana na kuyaziba.“Baadaye vijana hao tunawapa vyeti vya Veta bila kusoma Veta. Hawa nivijana 3,900 ambao wako mitaani,”amesema
Tanzania imeiomba Mahakama ya Jimbo la Columbia kutupilia mbali ombi la Stirling Civil Engineering la kutaka kusajili hukumu mbili za Mahakama ya Kimataifa Usuluhishi ili kampuni hiyo ya Uingereza ikamate mali nyingine za Serikali zilizopo nchini Marekani.Stirling, ambayo ni kampuni ya ujenzi iliyokatishwa zabuni ya kujenga Barabara ya Bagamoyo kutoka eneo la Wazo Hill kutokana na kutekeleza mradi huo chini ya kiwango, ilishinda ksi iliyofungua kupinga kitendo hicho msuluhishi akaagiza ilipwe dola 38 milioni za Kimarekani.Kampuni hiyo ilisajili uamuzi huo wa msuluhishi nchini Uingereza na Uholanzi na kufanikiwa kushikilia ndege aina ya Bombardier Q400 iliyonunuliwa na Serikali na sasa inataka mahakama isajili hukumu mbili za mwaka 2015 na 2016 zisajiliwe Marekani ili ipate nguvu ya kushikilia mali nyingine.Lakini Serikali ya Tanzania imeamua kupambana na kampuni hiyo mahakamani kuizuia isiendelee kukamata mali zake.Kwa mujibu wa tovuti ya Law360, ambayo ni maalum kwa ajili ya habari za kisheria, Tanzania imewasilisha pingamizi, ikitaka mahakama hiyo isisajili hukumu hiyo ya Mahakama ya Kimataifa ya usuluhishi.Katika hoja yake, Tanzania imesema mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kushughulikia ombi hilo la Stirling.Serikali inasema ina kinga dhidi ya hukumu mbili zilizotolewa na mahakamani nchini Uingereza na Uholanzi ambazo kampuni hiyo inaomba zitambuliwe pia Marekani, ikisema kuwa ondoleo hilo la kinga linalotolewa na Sheria ya Kinga ya Mataifa ya Kigeni, haiwezi kutumika.Kwa mujibu wa tovuti hiyo, Sheria ya Kinga ya Mataifa ya Kigeni inasema taifa la kigeni halitakuwa na kinga dhidi ya mamlaka ya mahakama ya Marekani katika mashauri yanayowasilishwa kwa ajili ya kuthibitisha tuzo za mahakama ya usuluhishi zinazoongozwa na makubaliano yaliyoidhinishwa na nchi yanayotambuliwa nchini Marekani.Serikaloi inasema Stirling inataka kutambuliwa kwa hukumu za mahakama ya nje ili ziwe na nguvu, badala ya kuomba kutekelezwa kwa hukumu hizo.“Kuna tofauti inayotambulika vizuri kati ya kuthibitisha tuzo ya msuluhishi, kwa upande mmoja, na kutambua hukumu ya mahakama ya nje, kwa upande mwingine,” tovuti hiyo inakariri hoja hizo za Serikali.“ingawa tuzo ya msuluhishi na hukumu ya mahakama zinalingana kwa kiasi kikubwa, hata hivyo zina tofautiana.”Kwa hiyo, Serikali inasema Stirling haiwezi kutumia mwanya huo, kuomba utekelezaji wa hukumu hizo.Kampuni hiyo inadai kuwa kitendo cha Serikali ya Tanzania kukubali kwenda kwenye Mahakama ya Usuluhishi, kiliondoa kinga hiyo na kuipa yenyewe haki ya kulipwa fidia hiyo.Mwaka 1999 Serikali iliipa kandarasi kampuni ya Impresa Ing. Fortunato Federici SpA (IFF) ambayo baadaye ilinunuliwa na Stirling, kukarabati barabara ya Wazo Hill-Bagamoyo, lakini baadaye ikatimuliwa.Mwaka 2004 kampuni hiyo ilifungua kesi Mahakama ya Usuluhishi wa Kimataifa na hukumu ilitolewa mwaka 2009 na 2010, lakini Serikali haikulipa fidia iliyopendekezwa na kuilazimu kukazia hukumu Uingereza na Uholanzi.Novemba 2015, mahakama nchini Uingereza iliridhia utekelezaji wa hukumu hiyo na Uholanzi ilifanya hivyo Desemba 2016.source: Mwananchi
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Abdalah Malela amemvua madaraka Mwalimu Mkuu Masunga Ng’waya wa Shule ya Msingi Mwashagata, iliyopo kijiji hicho kata ya Ihusi kwa kosa la ukosefu wa maadili.
Akizungumza na mwandishi wa gazeti Habarileo, mkurugenzi huyo alisema tukio hilo lilitokea hivi karibuni la baada ya mwalimu mmoja wa shule yake kumrubuni mwanafunzi wake kwa kufanya mapenzi naye tena kwenye nyumba yake, kitendo ambacho ni cha kukosa maadili.“Imebainika hili ni tukio la nne kwa mwalimu huyo kutuhumiwa kufanya mapenzi na wanafunzi tofauti tofauti lakini amekuwa hachukuliwi hatua, lakini mimi kwa mujibu wa sheria nimemvua madaraka mwalimu mkuu huyo ili awe mwalimu wa kawaida, sababu amekosa maadili ya kuendelea kushika wadhifa huo,” alisema mkurugenzi huyo.Aidha, alisema kesi hiyo tayari imefikishwa polisi na wakati wowote mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani. Katika hatua nyingine, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga alisikitishwa na kitendo hicho na kumtaka mkurugenzi wa halmashauri hiyo kumchukulia hatua na kuwashauri wazazi wamuache mwanafunzi huyo aendelee na masomo yasije yakampita huku hatua za kisheria kwa mtuhumiwa zikiendelea.Mlezi wa mwanafunzi huyo, alisema mwanae alisimama masomo kwa muda wa wiki mbili kutokana na tukio hilo. Mwalimu Ng’waya alipozungumza na mwandishi wa habari kwa njia ya simu alikiri kuvuliwa madaraka na kueleza amekuwa mwalimu wa kawaida huku akiendelea kufundisha katika shule hiyo
Jackson Makundi, baba mzazi wa mwanafunzi aliyeuawa wa Shule ya Scholastica, amemuomba Rais John Magufuli kuingilia kati tukio la kifo cha mwanaye ili haki itendeke.“Ninamuomba Rais ambaye ni wa wanyonge alisimamie suala hili ili haki itendeke. Nina uchungu na mwanangu kuuawa kikatili na kuzikwa bila kusitiriwa,” alisema jana wakati yeye na wanafamilia wenzake wakizungumza na waandishi wa habari.Alisema wanashangazwa ni sababu za Wizara ya Elimu kutosema lolote kuhusu tukio la kuuawa kwa mwanaye Humphrey.“Ninaamini Rais wangu tunayempenda na mtetezi wa wanyonge atatenda haki na ukweli wa tukio hili na waliolitenda wajulikane,” alisema Makundi. Pia, aliziomba taasisi zinazojishughulisha na utetezi wa haki za binadamu kuingilia kati suala hilo alilosema ni la kijamii na linatakiwa kuchukuliwa hatua kali kwa kuwa kukaa kimya kunaweza kuendelea na kumtokea kwa mzazi mwingine.Wakati huohuo, mmiliki wa Shule ya Scolastica iliyopo Himo, Edward Shayo amesema hahusiki kwa namna yoyote na kifo cha mwanafunzi huyo aliyekuwa kidato cha pili.Alisema iwapo anajua chochote, basi damu yake isibakie duniani na kwamba anaumizwa na maneno ya uongo dhidi yake.Wakati akisema hayo, taarifa zinadai mmoja wa walinzi wa shule hiyo ametoa maelezo polisi akikiri kumpiga na kusababisha kifo cha mwanafunzi huyo. Hata hivyo, kamanda wa polisi wa mkoa, Hamis Issah amekuwa hazungumzii suala hilo kila anapoulizwa kwa madai kuwa waandishi wanaingilia upelelezi.Akizungumza na gazeti hili akiwa wodi namba 16 katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC alikolazwa, Shayo alisema walifanya kila lililo ndani ya uwezo wao kumtafuta mtoto huyo.Awali Kamanda Issah alisema mtoto huyo alitoweka shuleni Novemba 6. Hata hivyo, uongozi wa shule unadai alitoweka asubuhi ya Novemba 7 na mwili wake uliokotwa Mto Ghona Novemba 10 na kuzikwa Novemba 12 na Halmashauri ya Manispaa ya Moshi kabla ya kufukuliwa kwa amri ya Mahakama.Shayo alisema baada ya kupokea taarifa za kutoweka kwa mtoto huyo, walimjulisha mzazi wake Jackson Makundi na baadaye taarifa zilitolewa Kituo cha Polisi Himo.Kuhusu madai kuwa mmoja wa walinzi wake amekiri kumpiga mtoto huyo wakati akitaka kumrejesha shuleni baada ya kuruka ukuta, alisema haelewi mlinzi huyo ametoa wapi hadithi hiyo aliyoitaja kuwa ya uongo.“Namuachia Mungu. Kuna maneno mengi yanaongewa lakini ukweli siku zote haufichiki na kama kweli mimi Shayo ninajua lolote kuhusu hiki kilichotokea, basi damu yangu isibaki duniani,” alisema.Katika hatua nyingine, daktari wa Hospitali ya Rufaa ya Mawenzi aliyeuchunguza mwili wa mtoto huyo na kushauri uzikwe, anahojiwa na Polisi.Habari za uhakika zinaeleza kuwa daktari huyo alikamatwa Novemba 19 baada ya uchunguzi mpya wa mwili huo kubaini haukuwa wa mtu mzima kama ilivyoelezwa awali na kwamba hakufa maji kama alivyoandika awali.Gazeti hili lilimshuhudia daktari huyo akivalishwa pingu nje ya chumba cha kuhifadhia maiti cha KCMC, kwa tuhuma za kutoa taarifa za uongo za sababu ya kifo na umri wa mwili aliouchunguza Novemba 12.Habari zinadai taarifa za daktari huyo na polisi wa Himo kuwa mwili uliookotwa ulikuwa wa mtu aliyekufa maji mwenye umri kuanzia miaka 35 na umeharibika, ndiyo zilichangia mwanafunzi huyo asitambuliwe.
Flora Mtegoa.
MAMA wa aliyekuwa nguli wa filamu Bongo marehemu Steven Kanumba, Flora Mtegoa amemkingia kifua mwanadada Hamisa Mobeto, baada ya mrembo huyo kuonekana mnafiki kwa kumsikitikia muigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ kisha kuonekana akiwa beneti na mama huyo.
Mwanadada Hamisa Mobeto.
Hivi karibuni, Mobeto alionekana kwenye uzinduzi wa filamu ya Zero Player aliyoshirikiana na mdogo wa Kanumba, Seth Bosco akiwa na mama huyo ndipo watu mitandaoni walipoanza kumnanga kwa kumuita msaliti wakidai ni hivi karibuni tu, aliposti picha ya kumsikitikia Lulu aliyehukumiwa kifungo cha miaka miwili jela ambaye hapatani na mama Kanumba.Ishu hiyo ilimuibua mama Kanumba ambapo alimtetea Mobeto: “Sioni haja ya watu kumsema vibaya Hamisa, wote ni watoto wangu tatizo liko wapi, wasimuite mnafiki bwana,” alisema mama Kanumba.
Kuoa au kuoelwa ni jambo ambalo watu wengi hutamani kwani ni miongoni mwa hatua kubwa katika maisha ya kila mmoja. Ukifanya utafiti kwa watu ambao hawajaoa wengi watakwambia wanatamani siku moja wawe na familia bora na yenye furaha, kwani kila mmoja anaamini hayo ni mafanikio kwenye maisha.Licha ya kuwa kuolewa au kuoa ni jambo jema, baadhi ya watu huwa hawaoi au hawaolewi. Kutokuoa au kuolewa kunaweza kuelezewa na sababu nyingi sana.Leo tutazungumzia suala la mwanamke kuolewa, na tutaweka bayana baadhi ya tabia chache ambazo zinaweza (zinachangia kwa kiasi kikubwa) mwanamke kuto kuolewa.1. Utumiaji mbaya wa mitandao ya kijamii.Hili najua si kwa wanawake tu, lakini kwa sababu leo wao ni walengwa wa mada, tutazungumzia upande wao tu. Baadhi ya wanawake hutumia vibaya mitandao ya kijamii ambapo huchati tangu asubuhi hadi jioni, wakiinua macho basi wanaangalia Tv na akimaliza channel hii atahamia nyingine, akimaliza mtandao huu atahamia mwingine.Kutwa nzima unakuta anafuatilia staa huyu alifanya nini usiku, huyu alipiga picha gani, kikapanda kikashuka.Mwisho wa siku mwanamke kama huyu atakuwa hana cha maana alichojifunza kwenye mitandao au kutazama Tv zaidi ya kuanza kuiga yale aliyoyaona. Na hakuna mwanaume muoaji anayetaka mwanamke ambaye akili yake imetawaliwa na mitandao ya kijamii hakumbuki hata kufanya usafi ndani.2. Kutokupenda kufanya kazi za nyumbani.Wanawake wengi wa ki-Afrika kwa vile wamekwenda shule wakatambua mambo ya haki sawa kwa wote na wengine kuona kwenye filamu wanaume wakifanya kazi ambazo mara nyingi hufanywa na wanawake, basi na wao ndio wameweka nukta kufanya kazi za nyumbani.Kutokana na hali hii, wanawake wamekua wakujiremba tangu mawio hadi machweo, ukitazama kucha zao zilivyondefu unajiuliza huyu anafua kweli?Wengine wameamua kuajiri watu wa kuwafulia hadi nguo za ndani. Kwa hali hii usitarajie mwanaume akuoe kwa sababu anajua ni matatizo anapeleka nyumbani.3. Kujipodoa hadi sura yako ya asili inasahaulika.Ni kweli wanaume hupenda mwanamke mrembo na mwenye kupendeza. Lakini hii haimaanishi ndio ujipodoe hadi uchukize. Kila kitu kwa kiasi chake kwa sababu kitu chochote kikizidi huwa ni sumu.Jirembe kwa kiasi, hili litavutia watu walio-serious kutaka kukuoa, lakini ukiwa ni wa kujiremba hadi ukapindukia, hakuna muoaji atakaye kuta. Tena ikumbukwe kuna baadhi ya wanaume wao hupenda mwanamke asiyejiremba (wenyewe huita natural)Hizi ni baadhi tu, na wewe unaweza kuongezea ili kuwakumbusha wasichana wanaotaka kuolewa.
1. Wanaojiona Kama Wafalme (King Husband).HIi ni aina ya wanaume ambao hutaka kusujudiwa kama wafalme na hupenda kuwafanya wake zao kuwa kama watumwa. Hawafanyi chochote ndani ya nyumba kazi yao ni kutumatuma hata kama mke anaumwa atapaswa kuamka na kupika, wanataka waheshimiwe wao tu na mwanamke akikosea kidogo ni maneno au kipigo. Mwanamke hana kauli ndani na mume akiingia nyumbani ni kama bosi anavyoingia ofisini, wote kimya hakuna hata kuongea.
2. Wanaume Wanaojihisi Bado Hawajaoa (Bachelor Husband).Hii ni aina ya wanaume ambao hawawashirikishi wake zao kwa chochote. Hufanya mambo kama vile bado hawajaoa, hutumia muda wao mwingi na marafiki zao wakifanya mambo ambayo mke hata hayajui mke anaweza kustukizia tu mume kanunua gari bila kumshirikisha na mume haonyeshi hata kujali kuweza kumshirikisha. Hajali kama ana mke na mda mwingi huutumia akiwa na marafiki kufanya mambo yasiyo na msingi ambayo hayana mnanufaa yoyote katika ndoa yake.3. Wanaume Wenye Gubu (Acidic Husband). Hawa hukasirika kila mara tena bila kua na sababu ya misngi, mambo hayaishi, kosa la mwaka juzi anaweza kukukasirikia leo. Wamemuudhi kazini hataki kusemeshwa na mnanuniwa nyinyi, mwanamke akiomba hela ya chakula ni shida ni kununa kutwa nzima, wanahasira na nirahisi kumpiga mke.4. Mume Wa Kila Mtu (Genarel Husband). Hawa wanajifanya wasamaria wema, wanajali kila mwanamke, wanajali marafiki wakike wa mke na wakwao kuliko wanavyowajali wake zao. Mke anaweza kuwa na shida akasema hana hela lakini rafiki akampa. Wana marafiki wengi wakike na mara nyingi huwa hawaachani kabisa na ma X wao, wakiwalalamikia wanawasaidia kuliko hata wanavyowasidia wake zao wakati wakiwa na shida.5. Wanaume Wanaojifanya Wagumu (Dry Husband).Hawa wanajifanya wagumu sana, hawana yale mambo ya kimahaba na wao hujua kuwa ndoa ni kuleta chakula tu na kushughulika kitandani. Hakuna kuongea na hawajali hata hisia za mke, mke akiongea kwao wala hawajali wanajifanya ni vidume sana na wanaona mambo kama vizawadi, kupiga simu, kutuma sms, kusema nakupenda, kununua maua ni mambo ya kike, yaani hawaonyeshi juhudi yoyote kuwafurahisha wekea zao.6. Wanaume Wanaopenda Kutumia Wake Zao (Panadol Husband).Hawa huwa wanaume pale tu wanapokuwa na shida, wanakuwa na wake wazuri wanaowajali lakini wao wala hawajali. Wanapomhitaji mwanamke, wanapotaka mwanamke awafanyie kitu flani basi huja na maneno mazuri na hata kuleta vizawadi, wanajua udhauifu wa wake zao na huutumia kuwalaghai kuwatimizia mahitaji yao lakini wanapotimiziwa tu basi husahau hata kama wanawake, hawajali tena.7. Wanaume Ambao Hawataki Kukua (Baby Husband). Bado wanatabia za kitoto, hawawezi kufanya maamuzi yao wenyewe mpaka kuuliza kwa ndugu zao, mtu kaoa lakini kila siku humpigia simu Mama yake kuuliza hiki na kile. Yaani wakiongea kitu na mke nilazima aulize ndugu kwanza ndiyo kipitishwa na mke akifanya kosaa kidogo kazi nikulinganisha mke na ndugu zake, mbona flani alifanya hivi, flani anaweza fanya zaidi na mambo kama hayo. Kwakifupi hawawezi kufanya maamuzi na mkewe, ndugu zake hasa Mama yake anakuwa kama shemeu ya ndoa.8. Mume Mtalii (Visiting Husband). Hawa wanakuja nyumbani kama wageni vile, mume ataihudumia familia yake kwa kila kitu lakini hawezi kuipa muda wake. Akirudi mke na watoto wamelala ni kugonga na hana sababu za msingi za kuchelewa, hata mwisho wawiki hupenda kutumia na marafiki au ndugu lakini si na mke. Hakuna kitu cha pamoja ambacho anafanya na mkewe au watoto wake, kila akiingia tu anakua na safari ya kutoka yaani hata atoke akakae nnje tu lakini si kukaa na mke au watoto.9. Wanaume Wanaofuatilia Kila Kitu (Stalking Husband). Hii ni aina ya wanaume ambao hufuatilia kila kitu, huchunguza kila kitu mwanamke anachofanya na hawampi pumzi. Akienda sehemu atachunguza anaenda na nani na alikutana na nani, huwa na wivu wa ajabu ajabu na kila saa huhisi wake zao ni wasaliti. Kila mtu mwanamke anayeongea naye wa jinsia tofauti huhisi ni mchepuko na hata marafiki wa mke wakike pia huhisi wanamkuwadia, kwakifupi hampi pumzi mwanamke.10. Mwanaume Mbahili (Miserly Husband). Huyu anaweza kuwa na hela lakini mbahili ajabu. Akimpa mwanamke hela atafuatilia matumizi yake mpaka senti ya mwisho, anafuatilia mpaka mambo ya jikoni. Sukari ikiisha naataka ajue iliisha ishaje na kila mara huhisi mke anamuibia hela labda akajenge kwao, huwa msumbufu sana na mgumu kutoa hela. Mwanamke akifikiria mchakato wa kuomba hela kwa mume hukata tamaa na wakati mwingine kuamua tu kukaa kimya na matatizo yake.
KATIKA harakati zako za kutafuta mpenzi, unaweza kukutana na mwanamke ambaye kwa sababu moja au nyingine anakwondolea uwezo wako wa kufikiri, kutumia mantiki na pia kutumia akili yako ya kuzaliwa. Si lazima awe amekufanyia kitu, lakini inaweza kuwa ni ulevi wako tu unaosababisha ufanye mambo yasiyo ya kawaida. Pengine ndiyo maana baadhi ya wasanii huzungumzia suala la “kudata” kutokana na mapenzi.Ni jambo jema kudhani kuwa wewe na mpenzi wako mnapendana kwa dhati na kwamba kila mmoja amefika kwa mwenzake, lakini kama mojawapo ya mambo haya kumi yaliyoelezwa hapa chini litajitokeza, basi fahamu kuwa yamkini umependa kuliko kawaida, yaani ni kama umenyweshwa sumu ya penzi. Kumbuka kupenda ni kuzuri, lakini kupenda kupindukia kunaweza kukutumbukia nyongo, kwani katika kila jambo kinahitajika kiasi.1. WIVU WA KUPINDUKIANi jambo jema kwa mwanamume kumtakia heri mpenzi wake na kufanya kila awezalo kuhakikisha kuwa hapati madhara, lakini iwapo utakuwa mtu wa wasiwasi na mashaka pale unapomwona mpenzi wako akizungumza na mwanamume mwingine, au anapotoka na marafiki zake wa kike, au anapovaa nguo inayomfanya atamanishe, basi fahamu kuwa tayari umekunywa sumu ya mapenzi.Katika uhusiano wa kimapenzi, kuaminiana ni jambo muhimu sana. Kama kweli unataka mpenzi wako akupende kwa dhati, mwoneshe kuwa unamwamini na unaheshimu maamuzi yake, ikiwa ni pamoja na maamuzi ya kutoka na marafiki zake wa kike na kuwa na marafiki wa kawaida wa kiume. Ondoa hofu na acha kabisa kumpeleleza, maana wapo wanaume ambao hutumia muda wao mwingi kuwapeleleza wapenzi wao ikiwa ni pamoja na kuwategeshea kamera na rekoda za simu.
2. KUTOMWACHIA NAFASI MPENZIKama huishi na mpenzi wako ni jambo la kawaida kuwa na hamu ya kumwona mara kwa mara, lakini kumbuka kuwa mpenzi wako naye ana maisha yake na anahitaji nafasi ya kuwa peke yake kwa ajili ya mambo yake binafsi.Hisia za kutaka kuwa na mpenzi wako muda wote zinaweza kudhaniwa kuwa ni za mapenzi ya dhati, lakini kwa hakika hiyo si ishara njema ya mapenzi ya kudumu. Hebu jiulize kama unaweza kuendeleza hali hiyo maisha yako yote. Ni wazi kuwa utachoka. Kwa hiyo, mpe mpenzi wako fursa ya kupumua. Namna hii mpenzi wako atajenga hamu ya kutaka kukutana nawe lakini ukiwa naye muda wote hamu hiyo itaisha.3. KUMWAMULIA MPENZI MAMBO YAKEUnaweza kujikuta ukisukumwa kumwambia mpenzi wako awe anavaa nini wakati gani, akutane na nani na kwa wakati gani au ale nini. Ukiona hivyo, fahamu kuwa hayo si mapenzi, bali umepitiliza na pengine mwisho wa uhusiano wenu unanukia.Hata ukiachilia mbali suala zima la usawa wa jinsia, hakuna mwanamke ambaye angependa apangiwe kila kitu kuhusiana na maisha yake. Kama ilivyodokezwa hapo juu, kila mtu ana maisha yake na kilichowaunganisha ni mapenzi tu. Kama utataka kumpangia kila kitu ni wazi kuwa utaishia kuishi peke yako.4. KUMUULIZA MPENZI MASWALIIwapo utajikuta ukimuuliza mpenzi wako maswali mengi yanayoonesha wasiwasi wako kuhusiana na mwenendo wake, fahamu kuwa kuna tatizo na tatizo hilo lisipopatiwa ufumbuzi utakuwa mwanzo wa mwisho wa uhusiano wenu.Mwanamke angependa umuulize maswali ya kawaida kuhusiana na jinsi siku yake ilivyokuwa na kama marafiki zake hawajambo au la, lakini kila jambo lina mpaka wake. Mwanamke hatarajii kuwa kila mnapokutana atakuwa kama ameingia kwenye chumba cha mtihani au usaili wa kazi.5. KUTOAMINI ANACHOKWELEZA MPENZIWakati mwingine watu hushindwa kuwaamini wenzao, lakini kwa sababu ambazo ni za msingi, lakini kuna wakati ambapo mtu hushindwa kumwamini mwenzake bila sababu yoyote ya msingi, au kwa sababu zisizo sahihi, kisingizio kikiwa ni mapenzi.Kuna tatizo la kisaikolojia la kujishuku au kuwashuku wenzako. Hili ni jambo ambalo linaweza kukuharibia mustakabali wako katika mapenzi, maana husababisha kujengeka kwa mazingira ya kutokuaminiana. Ili uweze kwenda sanjari na mpenzi wako, amini kila anachokweleza hadi pale utakapokuwa na sababu za msingi za kutokumwamini. Na hata unapokuwa umelithibitisha jambo, endelea kuwa katika uhalisia wako.
6. KUACHA HOBI, MARAFIKIMahusiano ya kimapenzi mara nyingi huhusisha kila mmoja kuacha baadhi ya mambo yake kwa ajili ya mwenzake. Hata hivyo, lengo ni kuweka tu uwiano wa mahitaji, si kuacha kila kitu ulichokuwa nacho kwa ajili ya mwenzako, ama kwa shinikizo, au kwa kulewa penzi.Iwapo utabaini kuwa marafiki zako sasa wamekuwa ni marafiki zako wa zamani na hobi zako zimebaki tu katika kumbukumbu japo kwa hakika bado unahisi mapenzi katika hobi hizo, basi tambua kuwa huyo mrembo wako amekunywesha sumu ya penzi na sasa huwezi hata kuitumia vema mantiki yako.Mbaya zaidi, iwapo utabaini kuwa marafiki zako wapya ni marafiki wa siku zote wa mpenzi wako na hobi zako ni zile za mpenzi wako, basi tambua kuwa huna tena nafsi yako, bali umejisalimisha mzima mzima kwa mpenzi wako. Lakini msemo mmoja wa hekima unatwambia usiweke mayai yako yote kwenye kikapu kimoja. Yamkini unaelewa.7. KUKUBALI KUPELEKESHWAPengine unakumbuka kuwa kuna nyakati ambapo ulikuwa na uwezo wa kujikita katika jambo moja na kulifanya kwa umakini, huku ukiwa pia mwerevu, mjanja na unayejisimamia, lakini leo unayeyuka kirahisi tu kama barafu iliyowekwa juani! Hii ni hatari kwa mustakabali wa maisha yako.Mbaya zaidi ni pale utakapoiacha kazi yako inayokulipa vizuri na kufanya kazi nyingine kwa ajili ya kumfurahisha mpenzi wako. Ukifika hali hii ujue wewe mwenyewe kuwa hapo hakuna mwanamume.
8. UTAYARI WA KUFA KWA AJILI YAKEUmewahi kujisikia kuwa na utayari wa kufa kwa ajili ya mpenzi wako? Kama jibu ni “ndiyo”, basi fahamu kwa hakika kuwa hayo uliyo nayo si mapenzi bali ni upumbavu. Pengine huku ndiko kunywesha sumu ya mapenzi. Kwa hakika, hakuna mwanamke ambaye anastahili kumfanya mwanamume yeyote kufa kwa ajili yake.Yamkini wanaume wanaolengwa katika makala haya si wavulana wanaosoma sekondari, waliobalehe majuzi, ambao wakipenda au kupendwa hujiona kama wako katika sayari yao. Mwanamume aliyepevuka hujiamini na hayaweki maisha yake yote mikononi mwa mwanamke, hata kama mwanamke huyo angekuwa ndiye mrembo wa dunia.Iwapo, ama kwa ujinga au kwa kufahamu umewahi kumwambia mpenzi wako: “Ukiniacha nitajiua,” na ukawa unaamini hivyo kabisa, basi yamkini unahitaji kutafuta msaada wa ushauri nasaha, maana kwa hakika umepotoka.
9. MUDA WOTE UNAWASILIANA NAYEVijana wa siku hizi ni watumiaji wazuri sana wa simu, lakini iwapo utabaini kuwa asilimia kubwa ya muda wako unautumia ama kwa kuongea au kuwasiliana kwa ujumbe mfupi na mpenzi wako, basi fahamu kuwa kuna tatizo ambalo linahitaji ufumbuzi wa haraka.Kumbuka kuwa mapenzi hayachukui nafasi ya kila kitu. Yamkini huyo mpenzi wako amekukuta unaishi na kuna mambo ya muhimu ya kufanya. Hebu achana na simu kwanza ufanye mambo ya muhimu kuhusiana na maisha yako. Kama mpenzi wako hakwelewi katika hili basi hakufai.
10. NDUGU ZAKE WANAKUFUATILIAIwapo utabaini kuwa marafiki, ndugu na jamaa za mpenzi wako wanamtonya mpenzi wako kuhusiana na kile wanachokiita mwenendo wako mbaya, usipuuze hali hii. Kuna uwezekano mkubwa kuwa watu hawa wanayo sababu ya kuwa na wasiwasi na mwenendo wako, kwa hiyo jichunguze na kuangalia jinsi unavyoenenda.Hata hivyo, jambo hili si ishara njema ya mustakabali mwema wa uhusiano wenu. Iwapo mpenzi wako ataweka watu wake wakufuatilie, maana yake halisi ni kwamba hakuamini. Katika hali kama hii, haitarajiwi kuwa mustakabali wa uhusiano wenu utakuwa mzuri, kwani kutakuwa na uingilizi mwingi wa ndugu, jamaa na marafiki zake. Unaweza kukubali kuendelea kuishi katika hali hii kwa kisingizio cha mapenzi, lakini ukweli ni kwamba hayatakuwa mapenzi bali karaha.KUWA MAKINIKama unavyoona, hizi ni baadhi tu ya dalili kuwa mapenzi yako kwa mwanamke sasa yanaelekea katika ulevi, mithili ya ule wa dawa za kulevya. Jambo moja la kukumbuka ni kwamba kweli mapenzi ni kitu kizuri, lakini pia mapenzi yanahitaji kuwa jambo linaloashiria mustakabali mwema kwa wahusika wawili. Yakiwapo mambo haya kumi hauwezi kuwapo mustakabali mwema katika mapenzi.