Thursday, 23 November 2017

Kinachosababisha Mahusiano Mengi ya Kimapenzi kufa Ni Hiki



Tumekuwa ni mashuhuda wazuri tukishuhudia mahusiano ya kimapenzi yanapoanza, huwa yaanaanza kwa mbwembwe nyingi sana, lakini yanapokuja kufa huwa ni kimya kimya, wale wale ambao tuliwashuhudia wakitembea kwa pamoja mara baada ya mahusiano hayo kufa, tumekuwa tukiona kila mtu yupo kivyake.

Licha ya kuendelea kushuhudia hivyo, ukichukunguza kwa umakini sababu ya kufa kwa mahusiano hayo utakuja kugundua kitu kimoja kikubwa ambacho kimesababisha kufa kwa mahusiano hayo ni; uwongo unapobadilika kuwa ukweli.

Hii ni sababu kubwa sana ambayo husababisha mahusiano mengi kufa, na sababu hii ndiyo husababisha mtafaruko mkubwa katika mahusiano yaliyo mengi. Hii ni kwa  sababu watu wengi ambao wanaingia katika mahusiano hutumia njia ya kudanganya ili aweze kumpata fulani, kwa sababu katika sayari ya leo bila uongo mapenzi hayaendi.

Hii ipo wazi, ya kwamba mapenzi ni uongo ambao hufanana na ukweli. Wakati mwingine kabla hujaanza mahusiano na mpezi wako, huwa kunakuwapo na ahadi nyingi sana ambazo zipo baadhi huwa ni za ukweli na zipo nyinginezo ambazo huwa ni za uongo.

Na hizo nyinginezo za uongo pale ambapo inakuja kugundulika ya kwamba zilikuwa za uongo ndipo unakuwa mwanzo wa mahusiano hayo kufa, unakuta mtu wakati wa kumtongoza msichana fulani anamuahidi vitu vingi vya uongo msichana huyo, na msichana huyo pasipo kujua anajikuta anakubali huku akitegemea  kwamba ahadi zote alizoahidiwa na mpenzi wake zitakuja kuwa ukweli, mwisho wa siku ahadi hizo zinabaki kuwa stori mwisho wa siku msichana huyo anaamua kuachana na mwanaume huyo.

Kwa mfano unakuta mtu anamwambia mtu ukiwa na mimi nitakupa nyumba, gari, fedha lakini baada ya muda kadhaa kupita vitu hivyo vinaishia kwenye maneno tu.

Na sababu nyingine ambayo husababibisha mahusiono mengi kufa ni kitu ambacho kinaitwa matarajio. Na matarajio hayo huwa katika ahadi ambazo zilikuwepo wakati awali. Unakuta mtu kabla hajaingia katika mahusiano na mtu fulani  anakuwa anatarajia kupata  kitu fulani kutoka kwa mtu huyo, mwisho wa siku kitu hicho ambacho alikuwa anatarajia anakuta hakipo.

Hivyo akikuta hakipo mwisho wa siku anaamua kuachana na mtu huyo na kwenda kwa mtu mwingine. Hivyo mambo makubwa ambayo hubomoa mahusaiano ya kimapenzi ni hayo ambayo nimeyaeleza.

Mambo yatakayokusaidia Kudumisha Mahusiano ya Mapenzi




Kuna nukuu inayosema “Uhusiano mzuri hautokei tu peke yake bali huchukua muda, uvumilivu, na watu wawili ambao kikweli wanataka kuwa pamoja.”

Japo inasemwa kuwa mapenzi hayana njia moja ya kufuatwa lakini kuna vitu ambavyo vinajulikana kuchangia katika kuboresha mahusiano baina ya wapenzi.

Mahusiano ya mapenzi yenye kudumu ni sharti yapandwe katika udongo wenye rutuba kama ulivyo mmea, yatahitaji maji ya kumwagilia na mbolea ya kukuzia.  Na zaidi ya yote yanahitaji muda wa kukua kabla matunda kuonekana.

1. Uaminifu
Kumwamini mwenza wako ni jambo la msingi sana katika kudumisha mahusiano. Usimshuku mpenzi wako kuwa si muaminifu bila ushahidi wowote. Kushukiwa kukosa uaminifu pasipo ukweli inasononesha sana na kumkosesha raha mpenzi wako.

Imesemwa na wanafalsafa wa mawazo ya binadamu kuwa “Unachofikiri na kuamini kinatokea” hivyo unashauriwa kutofikiri vibaya juu ya mpenzi wako kwani haileti afya katika mahusiano. Hali kadhalika na wewe uwe mwaminifu na mwenye kusema kweli mara zote. Ongeeni juu ya mipango na mawazo yenu bila kufichana.

Watambulishe kwa mpenzi wako ndugu ,jamaa na marafiki wakaribu ili kumpa mwenza wako amani.

2. Weka muda kwajili ya Mwenza wako
Mahusiano mazuri kati ya wapenzi yanahitaji muda wa wapenzi hao kukaa pamoja. Wapenzi wasio na muda wa kukaa wana hatari ya kupoteza mvuto wa mahusiano yao na hivyo kuhatarisha uhai wa mapenzi kati yao.

Kama wapenzi wapo mbali mbali basi wanahitaji kuweka muda wa kuongea kila inapowezekana. Tafuta muda wa kutoka pamoja, hata kama mtaenda mgahawani kunywa chai au juisi tu inatosha sana na inawaweka karibu zaidi.

3. Mawasiliano
Mawasiliano ni muhimu sana baina ya wapenzi. Hata kama umebanwa na kazi pata dakika chache za kuongea na mpezi wako na kumtaka hali. Andika hata ujumbe wa maneno au barua pepe. Mwambie mpenzi wako ulipo kila mara inapobidi ili kumjengea imani na wewe na kumpa amani moyoni. Tuma ramani ya mahali ulipo kama unatumia simu ya “Smart” (Tuma location kwenye whatsapp)
Mawasiliano ni ufunguo wa kudumisha upendo.

Wakati kuwasiliana na mpendwa wako, kumbuka kwamba upendo ni muhimu. Ongea toka moyoni na si kwa ajili ya kutimiza wajibu tu, kwani mpezi wako atajua tu kama hakuna mahaba katika mawasiliano yenu hivyo kutoleta faida ile inayotegemewa.

Mawasiliano mengine ni yale ya kuelezana yaliyo moyoni. Mweleze mwenza wako linalokusibu ili kupata ufumbuzi wa pamoja. Wapenzi wanaoongea kwa utulivu siku zote watakuwa pamoja.

4. Zawadi
Tafuta kitu cha kumpa mpenzi wako. Si lazima kiwe na thamani kubwa. Inaweza ikawa pipi au matunda tu. Mnunulie zawadi kila inapowezekana hasa unaposafiri au katika siku yake ya kuzaliwa.

5. Onyesha Upendo Wako 
Kila mtu anajinsi yake tofauti ya kuonyesha upendo, lakini vyovyote itavyokuwa ni jambo la muhimu sana kuonyesha hisia zako kwa mpenzi wako. Mara nyingi wapenzi wa muda mrefu wanasahau juu ya hili.

Maneno kama “Nakupenda”au majina ya mahaba kama “Mpenzi” au ”La-azizi” yanachangia sana kuonyesha mapenzi na kumfanya mwenza wako kujisikia vizuri. Maneno haya yanaposemwa kwa hisia halisi na toka moyoni yana mchango mkubwa katika kuboresha mahusiano.

Mama kuwa makini House Girl Yaweza Kuwa Mke Mwenzio




Ivi ni vibaya House girl kuolewa na baba mwenye nyumba?

Ndugu msomaji wa Muungwana Blog, karibu kwenye makala hii maalumu, nimeamua kuandika habari hii ili kujaribu kupunguza mifarakano kwenye familia zetu especially familia zenye wafanyakazi wa ndani wanaojulikana kama house girl.

Katika mada hii nimekuwa nikikutana na maswali mengi sana ambayo mda mwingine yalikuwa yakituchanganya hata sisi wenyewe katika kuwajibu wahusika, maswali haya malanyingi yalikuwa yakiulizwa na akina mama.

Na kwa upande wa akina baba maswali yao sio mengi ukilinganisha na akina mama, sasa napenda nianze kwa kusema mambo yafuatayo ili wote twende sawa.

WAJIBU WA MWANAUME KATIKA FAMILIA: 
Mwanaume anawajibu wa kutimiza mahitaji yote ya msingi katika familia yake, moja ya majukumu hayo ni pamoja na kutoa pesa za matunzo ya familia yake kadri ipasavyo, kuonyesha upendo wa dhati kwa mama pamoja na watoto wake, na mambo mengineyo nk.

WAJIBU WA MWANAMKE KATIKA FAMILIA: 
Mwanamke ndiye mtendaji mkuu wa familia kwa upande wa nyumbani ukiachilia mbali ya kwamba baba ndiye kichwa cha familia, mwanamke anamajukumu mengi kwa upande wa nyumbani moja ya majukumu yake ni pamoja na kupika chakula cha familia, kufua nguo za mumewe pamoja na nguo za watoto, kuakikisha nyumba pamoja na eneo linaloizunguka nyumba ni safi, kuonyesha upendo wa dhati kwa mumewe pamoja na watoto wake, nk.

Ndugu msomaji wa makala hii, nadhani mpaka hapo tayari umeisha anza kupata mwanga kuhusu jibu la swali la makala yetu, sasa twende kuona wajibu wa mfanya kazi wa ndani kama house girl.

House girl wajibu wake ni kuakikisha anafanya usafi wa kuizunguka eneo la  nyumba kwa nje na kufanya usafi huo kwa upande wa ndani kwa baadhi tu ya maeneo ya nyumba hiyo pamoja na kuwaogesha watoto, kufua nguo za watoto, na kufanya kazi ndogo ndogo za nyumbani.

House girl hatakiwi kufanya usafi chumbani kwa mume wa mama mwenye nyumba, house girl hatakiwi kufua au kupiga pasi nguo za mume wa mama mwenye nyumba, house girl hatakiwi kumuandalia chakula au chai mume wa mama mwenye nyumba, nk.

Sasa ukiona house girl anafanya kazi zote nilizosema kuwa hatakiwi kuzifanya pindi awapo nyumbani kwako, ukiwa kama mama mwenye akili timamu jua kabisa tayari umeamua kumuletea mumeo mke mdogo na pia usipige kelele wala kulaumu maana jitihada zote za kumuandaa mke mwenzio umezifanya wewe mwenyewe.

Ushauri wangu kwenu akina mama na akina dada nikwamba, hatukatai kuwa wafanyakazi wa ndani hawafai, ila jitaidi mfanyakazi wako awe na mipaka ya kazi, mwanaume anaamua kumuoa house girl kwa sababu yeye amechukua majukumu yote ya mama mwenye nyumba, sasa wewe mama usianze kumtupia maneno mtoto wa watu pamoja na mumeo maana yote hayo umeyataka wewe mwenyewe.

Mambo ambayo Mwanamke hawezi kuyaweka wazi katika Mahusiano



Unapoanzisha mahusaino na mwanamke yeyote yale fahamu fika yapo baadhi yavitu hawezikukkwambia na baadhi ya mambo hayo ni;

1. Idadi ya wapenzi wake wa zamani
Wanaume wengi hupenda kujua wao ni wangapi kuwa na mwanamke Fulani. Lakini mwanamke kamwe hawezi akakwambia wewe ni wa ngapi. Kumuuliza jambo hili kunamkera sana mwanamke na ndio maana mara nyingi hawezi akakwambia ukweli.

2. Anakulinganisha na mpenzi wa zamani
Mwanamke mara nyingi anakulinganisha na mpenzi wake wa zamani japokuwa hawezi kukwambia waziwazi. Wakati mwingine tabia hii huwafanya wanawake kuwatamani wapenzi wa zamani na hata kurudiana nao endapo watakosa mtu aliye bora kuliko mpenzi wake wa zamani.

3. Kasoro zako
Mwanamke kamwe hawezi kukwambia kasoro zako. Wanawake wanajua kumfichiaa mpenzi wao mambo wasiyotaka yajulikane kwa wengine na kwa mpenzi wake. Wanajua njia za kiujanja za kutumia ili kufichua siri zako zote. Mwanamke hawezi kukwambia kasoro zako kwa kuogopa kukuumiza.

4. Mapungufu yake
Mwanamke hawezi kukwambia mapungufu yake labda kwa kuhofia kusheshwa thamani. Wanawake ni wasiri sana kwa mapungufu yao. Wanajua vyema hofu zinazomuandamana, vitu vinavyowakosesha usingizi na mambo yanayowalemea maishani japo sio rahisi kuonyesha. Kwa nje anaweza akaonekana yuko vizuri na hana tatizo kumbe ndani ana matatizo au mapungufu. Anaweza kufanya yote kufunika upungufu wake!

5. Huwa unampagawisha mpaka anakosa la kusema.
Hili halisemi kabisa mwanawake kwa sababu anaona haya kutumia maneno ya wazi kueleza raha unayompa. Maneno ya kuzuzua ni himaya ya wanaume, lakini wakati mwingine wapo wasioweza kuficha.

6. Hauhumridhishi katika tendo la ndoa.
Wanawake wengi hawapendi kusema kama hawaridhiki Kwenye tendo la ndoa. Wanawake wanahitaji kuandaliwa vilivyo kwa dakika 10, 20 ama nusu saa. Mara nyingine wanaume huwahi kabla mwanamke hajawa tayari na hivyo kushindwa kuridhika lakini hawezi kusema. 

Sababu za wanawake kukosa uaminifu katika mahusiano




Yamkini umeshawahi kusikia kwamba wanaume hukosa uaminifu kwa sababu za kimwili zaidi wakati wanawake nao hukosa uaminifu kwasababu za kihisia.

Nikweli kuwa upo ukweli katika hilo, ingawa katika utafiti huu wanawake mbalimbali walipoulizwa kwanini walijiingiza katika mahusiano yasiri mbali na wapenzi wao walikuwa na sababu tele zakuelezea, wako walioelezea kuwa walikuwa wanafurahisha hisia zao tu na wengine walikuwa kwenye mkakati wakulipiza kisasi kwa kile walichowahi kufanyiwa na wapenzi wao, na sababu nyingine nyingi zilielezwa.

Jaribu kusoma kwa umakini ili ufahamu nini walikisema na kilichowafanya kujiingiza katika majaribu hayo. Ni matumaini yangu kwamba utakutana na sababu nyingine ninazokusibu au zilizowahi kukusibu wewe, na yamkini pia ukapata kufahamu kwanini mambo fulani yanaendela vile yalivyo.

Kukosekana kwa mvuto
Mmoja wa waliohojiwa anasema “Nilikuwa na mpenzi wangu kwa muda wamiaka mitatu, alikuwa kijana mzuri sana na nilifurahia sana ninapokuwa naye lakini tatizo nikwamba hakukuwa na chembe ya mvuto baina yetu. Wengi wa marafiki zetu walikuwa wameshachumbiana na kuvishana pete lakini kila mchumba wangu alipojaribu kuanzisha hoja ya kunivisha pete nilijitahidi sana kubadilisha mazungumzo ili tu tusiklizungumzie hilo.

Ipo siku nilisafiri kikazi na huko nikakutana na na kijana mfanyakazi mwenzangu ambaye taratibu nilijikuta naanza kuvutiwa nae. Kwakweli ulikuwa wakati mzuri sana, labda kwasababu niliitarajia safari hii kwa muda na nilikuwa sijasafiri kwa muda pia na ukizingatia nimekutana na mtu ninaevutiwa nae basi mambo yalikuwa mazuri zaidi.

Wakati wa kurudi ulipofika nilirudi nyumbani nikatengana na mchumba wangu na kujikuta sasa naanza mahusiano rasmi na yule kijana niliyefanyanae kazi kule nilikoenda. Ingawa siwezi kusema najisifia kwa nilichokifanya, lakini namshukuru Mungu kwamba mambo yaliendelea kuwa mazuri upande wangu kwa sababu mimi na yule kijana tuliamua kuoana na hadi sasa tunaishi kwa furaha na mapenzi mazuri”.

Kuchelewesha kitendo cha kuachana
“Kabla tu sijaenda kuachana na mwanaume aliyekuwa mpenzi wangu, niligundua kuwa alikuwa na hali mbaya sana kihisia, hakuwa tayari kabisa kusikia kwamba tunaachana nahii ikanifanya kukosa ujasiri wa kumtamkia kuwa tuachane. Kwahiyo nikasubiri kama mwezi mmoja hivi ili haliyake irudi kuwa njema ndiyo nimwambie.

Mara tu haliyake ilipokuwa sawa na wakati na mimi nimeshaanza kupata ujasiri wa kumwambia mara akafukuzwa kazi, nikajihisi tena nimerudi katika hatua ya kwanza. Wakati huo sasa tayari nilishakutana na kijana ambaye nilishatamani sana kuanza naye mahusiano, na kwa kushindwa kujizuia na kwahali niliyokuwa napitia kimahusiano nikajikuta nimemruhusu awe mpenzi wangu, pasipo hata kumhusisha mpenzi wangu wa awali kuwa sasa nipo katika mahusiano mengine.

Nahisi nilijipamoyo kwamba siwezi kumwambia sasahivi wakati hali yake yakihisia haikuwa nzuri”. (Binti aliyehojiwa hapa alikuwa na miaka 30, wakati yule wa kwanza alikuwa na miaka 33)

Madhara ya kuwa mbali na mpenzi wako
“Mimi na mchumba wangu tuliamua kuendelea na mapenzi yetu tukiwa mbalimbali mara tu nilipopata nafasi ya kwenda chuo kikuu mbali na nyumbani. Miezi michache ya kwanza haikuwa na shida, kila kitu kilikuwa sawa na tuliwasiliana bila shida.

Lakini kila muda ulipokuwa ukienda nikajikuta naanza kuvutiwa na kuwa karibu na kaka mmoja aliyekuwa mwanafunzi mwenzangu na mara kwa mara nilikutana naye maabara za sayansi. Baada ya masomo kumalizika nilirudi nyumbani na nilimkuta mchumba wangu akinisubiri kwa hamu sana. Kwakweli kukaanae kipindi hiki haikuwa rahisi kabisa ingawa sikuweza kuachana nae wakati huu sababu bado nilivutiwa nae.

Ziko nyakati hapa katikati nilimtembelea yule mwanafunzi mwenzangu niliyevutiwa nae tukiwa chuoni na nikagundua kuwa kilichokuwa baina ya mimi na yeye kilikuwa ni hisia zaidi nasio penzi haswa, ingawa tulishajikuta tukiingia katika penzi, nahisi hii yote ilisababishwa tu na upweke na kuwa mbali na mwenzangu, basi nikaamua kuacha kabisa kuwasiliana na yule mwanafunzi mwenzangu na kuweka mawazo yangu yote kwa mpenzi wangu kwasababu nilijua kuwa yeye ndio alikuwa wangu wa maisha, nasikitika kwamba sikuwahi kumwambia kilichoendelea wakati nikiwa chuoni, ingawa maranyingine najihisi kushtakiwa moyoni. Maranyingine najipa moyo kwamba ule ulikuwa utoto na ujinga tu. Sasa mimi nayeye tunaendelea vema na ni miaka mine sasa tangu nimemaliza chuo kikuu”.

Kuepukana na kuwa mpweke
Binti huyu mwenye miaka 28 anasema “Nilianza tu kuhusiana kimapenzi na kijana niliye naye sasahivi mara baada ya kuachwa na mpenzi niliyekuwa naye kwa miaka miwili.

Kwakweli ilikuwa ngumu sana kwangu na huyu mpenzi wa sasa kweli aliniokoa katika maumivu hayo, baada ya mimi nayeye kuwa katika mahusiano kwa miezi mitano hivi, mpenzi wangu wa kwanza akarudi na kuomba nimruhusu na kumpa nafasi tena na kuahidi kuwa hayatotokea tena. Ukweli ni kwamba bado nilihisi kumkosa sana moyoni mwangu, kwahiyo tukaanza kuonana mara kwa mara ingawa sio kwamba nilikuwa nimeachana na huyu niliyekuwa naye sasa.

Najihisi nilikuwa nimemuweka huyu kijana wa sasa karibu ili kujihakikishia usalama zaidi maana sikuwa nikijiamini sana kuwa na yule wa awali, nilihofia kama ataniacha tena angalau ninamtu pembeni yuko tayari kwa ajili yangu, ingawa sio kwamba nilimpenda kiukweli kama mpenzi wangu wa mwanzoni.

Kwa bahati mbaya mimi na mpenzi wangu wa awali hatukuweza kuendelea vema hata baada ya kumpa nafasi ya pili aliyoiomba, mbaya zaidi nikwamba mpenzi wangu wa sasa alipogundua kuwa nilikuwa ninaonana mara kwa mara na yule wa kwanza na yeye akasema hatoweza kuendelea na mimi. Kweli nilijifunza somo hapa kuhusu kuhusiana na wanaume wawili wakati mmoja, na pia kujifanya najaribu kulea nakubembeleza penzi lililokwisha kufa”.

Kutafuta pumziko baada ya mahusiano mabaya
“Nilipokuwa binti mdogo (sasa hivi nina 30) nilikuwa katika mahusiano na kijana mmoja ambaye kwakweli alikuwa akinipinga katika kila ninachokifanya, alinikejeli sana kuhusu maumbile yangu na uzito wangu, mara aseme mimi mjinga, mara sijui kitu, mara mi mshamba na mambo mengine mengi mabaya.

Pamoja na mabaya yote haya bado niliamua kuwa naye tu ingawa marafiki zangu wote na wazazi na ndugu zangu walimchukia. Siku moja nikiwa kwenye sherehe nikakutana na kijana mmoja na gafla tulijikuta tumezama kwenye maongezi ya mapenzi na hisia zetu kuvaana. Yani huyu alikuwa ni tofauti kabisa na mpenzi wangu, wametofautiana kilakitu kuanzia maneno hadi matendo, yani ni kijana mpole, mzuri wa tabia, mkarimu na ananitia moyo badala ya kunivunja moyo.

Mara kwa mara tulikuwa wote tukifurahia siku za mwisho wa wiki,na moyoni mwangu ikawa kama vile taa ya yule wa kwanza ndiyo imezima kabisa. Kwa mara ya kwanza nilimbusu usiku kabla hajaondoka kurudi nyumbani kwao, na nilipoenda kuonana na yule wa kwanza nilimwambia tuachane. Niliamua kuendelea sasa rasmi katika mapenzi na mpenzi wangu mpya na baada ya miaka mitatu tukaamua kuoana”.

Jitihada za kutafuta kile unachohisi kukikosa
“Mimi ni binti niliyekulia katika mikoa ya pwani kwahiyo napenda sana kwenda fukweni kukaa, kuogelea na kupunga upepo. Kwa bahati mbaya mpenzi wangu amekulia zaidi bara kwahiyo mambo ya fukweni kwake sio kitu kabisa na hapendi, mara kwa mara tumekuwa na ushindani na mikwaruzano kuhusu wapi twende tukapumzike na mara zote yeye ndio anashinda.

Baada ya kuwa kwenye mahusiano kwa muda wa miezi nane, kuna wakati nilisafiri mimi na rafikizangu na tulitumia boti kwa muda mrefu wa safari, nahodha wa boti hii alikuwa kijana mzuri, mtanashati na anaonekana ni mtu wa maisha ya fukweni zaidi, kweli nilivutiwa nae, Tulipofika tuliahidiana kuonana usiku ule na tulikuwa na wakati mzuri sana pamoja, sikuwahi kumwambia mpenzi wangu kuhusu yaliyoendelea katika safari yangu, na wala sijihisi kushtakiwa moyoni mwangu, tena kuna maranyingine najihisi ndani yangu kuwa kile ndicho kilikuwa chema kumfanyia huyu mpenzi wangu kwasababu ya utukutu wake.

Bahati mbaya sana mimi na mpenzi wangu hatukuweza kuendelea sana, tuliachana baada ya mimi kushindwana naye na niliamua kuhakikisha kwamba kila kijana nitakayeamua kuhusiana naye basi lazima ayajue maisha ya fukweni”.

Jitihada za kumuadabisha (kumkomesha)
“Mpenzi wangu wa mwisho alikuwa na tabia za wanawake sana kabla hatujaamua kuanza neye mahusiano, nilidhani ningeweza kumbadilisha tabia yake hiyo lakini nilijidanganya, mara kwa mara nilisikia tetesi kuwa alikuwa anaonana na wasichana wengine wakati bado tuko naye katika mahusiano, lakini kila nilipomuuliza marazote alikataa katakata.

Usiku mmoja nilipata simu kutoka kwa msichana ambaye walikuwa wamehusiana naye kwa miezi mitatu na akaniambia kuhusu msichana mwingine pia ambaye na yeye amegundua kuwa anamahusiano na huyu mpenzi wangu. Nilikuwa na hasira sana usiku ule, niliamua kutoka na marafiki zangu nikiwa nimevalia mavazi ya kumvuta kila mwanaume ambaye aliniona, na nikaamua kuwa na muda na kijana fulani mzuri sana niliyekutana naye katika mtoko ule.

Ndani yangu nilipata kupumua kidogo nikajihisi kuwa angalau hicho ndiyo alichostahili mpenzi wangu huyu, nilitamani na nilifurahia kuuona uso wake jinsi anavyokuwa wakati nikimpa taarifa ya nilichokifanya usiku ule na ninayoyajua kuhusu yeye na wanawake zake na hatimaye nikamwambia kila mtu achumue muda wake, na tukaachana”.

Jifunze Jambo hili ili kudumisha mahusiano Yenu



Unapokuwa katika mahusiano ya kimapenzi lipo jambo kubwa sana ambalo unatakiwa kulizingatia katika mahusiano hayo, haijalisha mahusiano hayo yamedumu kwa kiwango gani.

Wapo wapenzi ambao mahusiano yao yalianza tangu wakiwa wadogo mpaka sasa hivi wapo pamoja , wapo wengine ambao wamekutana wakiwa masomoni na sehemu nyinginezo.

Hivyo narudia  tena kukwambia lipo jambo la muhimu la kuweza kulikumbuka, Jambo hilo si jingine bali ni jambo la kuweza kutekeleza malengo yenu kwa pamoja. Jambo la muhimu ambalo mnalotakiwa kulifanya ni kuhakikisha mnapanga malengo yenu kwa pamoja na si kupanga tu bali hata kuyatekeleza.

Nasema hivyo kwa sababu yapo baadhi ya mahusiano hayadumu kwa sababu wapenzi wengi wamekuwa hawashirikishan masuala ya kimaendeleo unakuta kila mmoja anafanya vitu kivyakevyake, kitendo cha kufanya hivtyo ni kinyume na mapenzi ya Mungu pia ni kuyasua mahusiano yako bila wewe kujua.

Hivyo kila wakati na kila muda jifunze kutekeza malengo ya maisha yenu kwa pamoja na sio kila mtu afanye kivyake vyake.

Kabla ya kufunga ndoa hakikisha mmepima haya magonjwa 4 ya kuambukizwa


1. Ugonjwa wa kaswende.
Kitaalamu kama syphilis, huu ni ugonjwa hatari sana ambao umeharibu maisha ya watu wengi bila wao kujifahamu. Ugonjwa huu ambao huambukizwa kwa njia ya kujamiana huanza kidogo na kidonda ambacho hakiumi sehemu ambapo wadudu wamepita mfano mdomoni au sehemu za siri.

Kidonda hicho hupona, upele usiowasha hutokea na baadae vyote hivyo hupotea. Ugonjwa huu baadae huingia ndani ya mwili na kuuanza kuharibu viungo vya ndani. Mwisho kabisa ugonjwa huu huahamia kwenye ubongo na kumfanya mtu kua kichaa.

2. Ugonjwa wa hepatitis B.
Ugonjwa huu ni hatari na unaua haraka kuliko ukimwi, virusi vya ugonjwa huu huambukizwa kwa njia ya kujamiana na kugusana kwa damu au majimaji ya mwili kama ukimwi lakini ni rahisi zaidi kuambukizwa ugonjwa huu kuliko kupata ukimwi.

Ugonjwa huu hushambulia maini na kuacha makovu, Mgonjwa hupata macho ya njano, homa, maumivu ya kichwa na kadhalika. Ugonjwa hii mwishoni hupelekea kansa ya ini ambayo inaua ndani ya miezi sita.

3. Ugonjwa wa ukimwi.
Huu ni ugonjwa unaofahamika kwani unatangazwa sana hasa kwenye vituo vya Radio, Tv, Magazeti na sehemu mbalimbali.

Ugonjwa huu uligundulika karne ya 20 na mpaka sasa umeshaua watu wengi sana na zaidi ya 95% ya wagonjwa waliambukizwa kwa kushiriki ngono bila kinga.

4. Ugonjwa wa gonorea.
Huu ni ugonjwa wa zinaa ambao unashambulia jinsia zote yaani Wanaume na Wanawake, mara nyingi Mwanaume hawezi kujificha na ugonjwa huu kwani dalili za ugonjwa huo kama kutoka na usaa kwenye njia ya kukojolea zitamuumbua lakini kwa wananwake ugonjwa huu huweza kukaa kimya na mwana mke hujikuta akisambaza ugonjwa huo bila kujua. Mwishoni ugonjwa huu hushambulia kizazi na kusababisha ugumba.


Mambo ambayo ni sumu katika mahusiano yako ya mapenzi



Katika harakati zako za kutafuta mpenzi, unaweza kukutana na mwanamke ambaye kwa sababu moja au nyingine anakwondolea uwezo wako wa kufikiri, kutumia mantiki na pia kutumia akili yako ya kuzaliwa. Si lazima awe amekufanyia kitu, lakini inaweza kuwa ni ulevi wako tu unaosababisha ufanye mambo yasiyo ya kawaida. Pengine ndiyo maana baadhi ya wasanii huzungumzia suala la “kudata” kutokana na mapenzi.

Ni jambo jema kudhani kuwa wewe na mpenzi wako mnapendana kwa dhati na kwamba kila mmoja amefika kwa mwenzake, lakini kama mojawapo ya mambo haya kumi yaliyoelezwa hapa chini litajitokeza, basi fahamu kuwa yamkini umependa kuliko kawaida, yaani ni kama umenyweshwa sumu ya penzi. Kumbuka kupenda ni kuzuri, lakini kupenda kupindukia kunaweza kukutumbukia nyongo, kwani katika kila jambo kinahitajika kiasi.

1. Wivu kupindukia.
Ni jambo jema kwa mwanamume kumtakia heri mpenzi wake na kufanya kila awezalo kuhakikisha kuwa hapati madhara, lakini iwapo utakuwa mtu wa wasiwasi na mashaka pale unapomwona mpenzi wako akizungumza na mwanamume mwingine, au anapotoka na marafiki zake wa kike, au anapovaa nguo inayomfanya atamanishe, basi fahamu kuwa tayari umekunywa sumu ya mapenzi.

Katika uhusiano wa kimapenzi, kuaminiana ni jambo muhimu sana. Kama kweli unataka mpenzi wako akupende kwa dhati, mwoneshe kuwa unamwamini na unaheshimu maamuzi yake, ikiwa ni pamoja na maamuzi ya kutoka na marafiki zake wa kike na kuwa na marafiki wa kawaida wa kiume. Ondoa hofu na acha kabisa kumpeleleza, maana wapo wanaume ambao hutumia muda wao mwingi kuwapeleleza wapenzi wao ikiwa ni pamoja na kuwategeshea kamera na rekoda za simu.

2. Kutompa nafasi mpenzi wako.
Kama huishi na mpenzi wako ni jambo la kawaida kuwa na hamu ya kumwona mara kwa mara, lakini kumbuka kuwa mpenzi wako naye ana maisha yake na anahitaji nafasi ya kuwa peke yake kwa ajili ya mambo yake binafsi.

Hisia za kutaka kuwa na mpenzi wako muda wote zinaweza kudhaniwa kuwa ni za mapenzi ya dhati, lakini kwa hakika hiyo si ishara njema ya mapenzi ya kudumu. Hebu jiulize kama unaweza kuendeleza hali hiyo maisha yako yote. Ni wazi kuwa utachoka. Kwa hiyo, mpe mpenzi wako fursa ya kupumua. Namna hii mpenzi wako atajenga hamu ya kutaka kukutana nawe lakini ukiwa naye muda wote hamu hiyo itaisha.

3. Kumuingilia mpenzi katika mambo yako.
Unaweza kujikuta ukisukumwa kumwambia mpenzi wako awe anavaa nini wakati gani, akutane na nani na kwa wakati gani au ale nini. Ukiona hivyo, fahamu kuwa hayo si mapenzi, bali umepitiliza na pengine mwisho wa uhusiano wenu unanukia.

Hata ukiachilia mbali suala zima la usawa wa jinsia, hakuna mwanamke ambaye angependa apangiwe kila kitu kuhusiana na maisha yake. Kama ilivyodokezwa hapo juu, kila mtu ana maisha yake na kilichowaunganisha ni mapenzi tu. Kama utataka kumpangia kila kitu ni wazi kuwa utaishia kuishi peke yako.

Namna Ya Kuishi Na Watu Wenye Tabia Ngumu



Ni ngumu na kamwe siyo rahisi kumbadilisha mtu mwenye tabia ngumu awe rafiki. Badiliko hili lawezekana ikiwa mhusika (mwenye tabia ngumu) atadhamiria na kuwatayari kushughulika ili kubadilika.

Kwa hiyo kama ni ngumu au haiwezekani kumbadilisha basi jaribu kubadili mtazamo wako na jinsi unavyoishi naye au nao, kwasababu mara nyingi wewe ndiye unaye kwazika au kuumizwa wakati yeye (yule anayekuudhi) anafanikiwa na anaendelea na furaha yake tu.

Mawasiliano baina yetu na watu wengine yanajumuisha jinsi tunavyowafanyia wengine na jinsi wao wanavyotufanyia sisi (reaction and counter reaction). Kwa kubadili jinsi sisi tunavyowatendea wengine inaweza kubadili jinsi wao wanavyotutendea sisi. Hata kama ni kwa muda au kitambo kidogo tu. Hata kama hali hii haibadili hali kwa kudumu ila inaweza kurahisisha mazingira ya kuishi na mtu au watu wenye tabia ngumu.

Kila wakati lazima uwe na akili sana katika kuishi na watu wenye tabia ngumu, kama hutoweza kujizuia, na ukaanza kuwabwatukia basi itakuwa unaleta tatizo hasa pale ambapo mwenye tabia hii ngumu ni bosi wako. Je, utaropoka au kutukana kama ulivyozoea?
Hata kama mtu au watu wenyetabia hii wako ndani ya familia na yamkini ni wadogo kwako kiumri, bado kuropoka na kuwapayukia siyo suluhisho, hali hii yaweza kukugharimu.

Najua kila mmoja wetu anajinsi anavyofanya kwa mtu au watu wenye tabia ngumu. Wote hatuna namna moja, mmoja anaweza kuwa ni mkimya na mwenye ujasiri hata anapoudhiwa, mwingine hupayuka na kumjibu yule anaye muudhi, mwingine anaamua kulia tu anapoudhiwa, wako wanaozira na kuamua kutozungumza tena na aliyewaudhi, wapo ambao husambaza habari mbaya kuhusu huyo mwenye maudhi, wako ambao huamua kumwambia uso kwa uso jinsi walivyo kwazika, sijui staili yako ni ipi.

Ni rahisi sana kuumizwa au kuudhiwa na maneno au matendo ya mwingine, na mara mtu huyo anapojua kuwa unaumia yeye hupata nguvu, hii huwa ndiyo silaha yake muhimu pale mnapopambana.

Unachotakiwa kufanya ni kuwaachia wakati wote wao wawe washindi, kamwe usitafute kushindana nao, utaumia mwenyewe. Njia pekee ni kujitahidi kuwa mjanja na mwenye akili kuliko yeye na pia kuwa na ushawishi katika yale wanayotaka kuyatenda hata pasipo wao kugundua.
Je, unawajibu vipi watu hawa (How do you react?)
Ni jambo jema kuanza kujitazama jinsi unavyowatendea wengine na jinsi tunavyoshughulika na wale wanaotukwaza. Kumbuka kuwa jinsi unavyoikabili hali hiyo katika mazingira fulani inawezekana isiwe hivyo katika mazingira mengine.

Watu wenye tabia ngumu na zinazotatiza mara nyingi huweka mitego ya maneno au matendo na kwa kiasi kikubwa unaweza kunaswa na kuwaruhusu wakuchezee jinsi watakavyo, na kati ya vitu wanavyo vipenda na kuvitamani ni kukuona unalia na kuumia na kuchanganyikiwa. Kwahiyo fikiri kwanza kabla hujafanya chochote mbele yao.

Watu watabia hii mara zote huwachukulia na kuwatendea watu wote sawa kwa hiyo usifikiri kila alichosema au alichofanya kwako ni cha kibinafsi sana na alikikusudia kwako. Angeweza kufanya au kusema hivyo hivyo hata kwa mwingine aliye karibu naye wakati ule. Kwa kufahamu hili itakusaidia kupunguza maumivu yanayoletwa na hisia zako kwake.

Hembu jiulize ni jinsi gani umewahi kukabiliana na mtu au watu wa jinsi hii, na je ilikuwa ni kwa jinsi ya kuumiza au kuelemisha? Fahamu kwamba kujibu kwa kupayuka, kutukana au kubishana haisaidii, bali kunakushusha chini ya miguu ya yule aliye kusababishia maumivu hayo, na sasa atakuwa anafurahia na kukuona wewe mjinga.

Ni chaguo lako, la ni jinsi gani utakabiliana na mtu au watu wa aina hii, ingawa unaweza kuchagua njia bora itakayoweza kukusaidia kukuimarisha na kupunguza udhaifu wako, zaidi ya kuamua kuchagua njia ambayo itakuacha umeumia, umechoka, umekatishwa tamaa na umejeruhika moyo.

Hii haimaanishi uwe mtu wa kusema ndiyo tu kwa kila kitu na kila mtu, na haimaanishi kuwa hutakiwi kukasirika HAPANA, hasira ni asili na haina tatizo lolote hapa, ila tu matokeo ya hasira hiyo ndiyo yanayoweza kuleta shida. Je ni jinsi gani unakabiliana na hasira yako na unaionyeshaje? Kwa fujo, kupayuka kubishana, kulia, kuvunja vitu, kunyamaza n.k.

Ili Kujua jinsi watu wenye tabia ngumu wanavyokuathiri. Jiulize maswali yafuatayo:
Je, ni unataka kutawaliwa na wengine?
Najua jibu ni kwamba hakuna nayetaka kutawaliwa na mwingine, na ndiyo maana unaweza kujikuta unabishana au kushindana na huyo anaye kukwaza.

Tatizo ni kwamba mwisho wewe ndiyo unaumia na yeye anabaki kufurahia kwa kukushinda mfano; tazama fujo za madereva barabarani hususan wale wa daladala.
Nikweli unahasira naye, lakini je hiyo ni njia muafaka ya kumkabili? kumbuka mwishoni atakayeumia ni wewe.

Fikiri kama unatatizo la shinikizo la damu kama utakubali kuyumbishwa kihisia na tabia mbovu za mwingine wewe ndiyo utabaki unaumia na siyo tu kama hutoweza kufanya vile moyo wako utakavyo bali pia utaachwa ukijihisi kuchoka, kuumizwa kwa hisia zako mwenyewe na kukatishwa tamaa na tabia yako wewe mwenyewe.

Nini Mwitikio wako pale unapoudhiwa? (Haswa na yule mwenye hasira na wewe)
Je, unalipa hasira kwa hasira?
Je, unajitetea na kuukimbia ukweli (being defensive)
Au unajificha kutoroka au kumkwepa?
Njia zote hizi hapa juu siyo nzuri.

Hata kama una haki ya kukasirika, lakini bado atakayeumia unabaki kuwa ni wewe. Na siyo tu utaumizwa na kukasirishwa kwa tabia yake mwenye kukuudhi bali utaumizwa moyoni mwako kwa vile wewe ulivyotenda, dhamiri itakushtaki zaidi (guilty conscious).

Je, unajizumgumziaje wewe mwenyewe, vibaya au vyema?
Mfano: Ukweli mimi najichukia haswa ninapofikia kipindi cha mitihani au usaili.
Hivi mimi nikoje?
Hivi kwa nini nimeumbwa hivi?
Kamwe mimi siwezi kufanya lolote jema!
Wakati wote mimi ni mtu wa bahati mbaya tu!

Wala huhitaji kujichukia unapofikia wakati wa mitihani au usaili, unachohitaji kufanya ni kujiandaa mwenyewe vizuri na kuwahi mapema katika eneo la tukio.
Hisia potofu na zisizojenga ambazo tunajiwazia wenyewe mara nyingi hutupotezea muda na mara tunapoziruhusu hutuharibia siku yetu nzima.

Unafanya nini unapopingwa? (what do you do when you are criticized)
Wako watu wanaopendelea kupinga wengine katika kila kitu, hata katika vile visivyostahili kupingwa,hakuna chochote chema kinachoweza kusemwa na yeyote, bali yeye peke yake. Hata kama kilichosemwa kina ukweli kwa asilimia kubwa basi mtu huyu atajitahidi walau kurekebisha hata lugha tu, ili mradi kisipite hivihivi bila yeye kukipinga japo kidogo (hawa ndiyo wale wenye tabia ngumu).

Hali hii huwapa kufurahi na kujijengea nguvu kwa jinsi wanavyopinga wengine.
Ni kweli upinzani mwingine ni wa ukweli na unajenga lakini hapa nakazia wale wanaopinga ili tu kujifurahisha nafsi zao na kuwafanya wale wanaowapinga waumie mioyo.

Je, unapopigwa, unajibuje? Je, unajitetea au unajishusha na kukubali kila kinachopingwa kwa kuamini kwamba anayekupinga yuko sawa na kwa hiyo unayameza maoni yako yote, bila kuchambua kwa kina mapingamizi hayo.

Kuna jinsi ambavyo unaweza kumkabili au kumjibu anayekupinga na ikawa kama umeweka petroli kwenye moto, upinzani utawaka na hata kuleta ugomvi, lakini pia iko njia ambayo unaweza kumjibu mtu huyu na ukanyamazisha fukuto lote.

Je, una mtazamo hasi (mtazamo usiofaa) na wa kudumu katika kitu fulani?
Mfano; Labda unasema “Mambo yangu hayaendelei tangu nihamie katika nyumba hii, au mambo yangu yanakwama tangu nimuoe au niolewe na huyu, ni matatizo tu tangu tuoane, watoto hawa hasara tupu.” n.k.

Mtazamo huu hasi, waweza kukugharimu siyo tu kukunyima raha bali pia waweza kuharibu hisia zako na za wengine pia.
Ukijikuta katika hali hii ni vyema kujifahamu na kujitahidi kuelewa nini tatizo husika na jitahidi kubadilisha mtazamo wako.

Tafuta vile vitu ambavyo unaweza kuvitazama katika mtazamo chanya hata kama ni vidogo. Tafuta kuviongelea vile unavyovipenda zaidi ya vile usivyovipenda.
Je, unazimeza hisia zako zote, nzuri na mbaya?

Je, unaona ni ngumu sana kusema “nakupenda” “umependeza” “umeniudhi” n.k. labda unaweza kusema neno moja tu na siyo lingine. Wengi wetu tumekuzwa katika mazingira ambayo tunahofu kusema chochote ili tu tusije tukamkwaza mtu, hata kama tunaumizwa au tunajisikia vyema kusema kitu fulani, lakini tunajizuia.

Badala yake tunakwenda kusemea pembeni. Yamkini kunyamaza kunaweza kuwa na faida katika baadhi ya mazingira lakini siyo hata katika kukubali vitu visivyofaa. Hakuna ubaya wowote katika kuelezea jinsi unavyojisikia moyoni mwako ili mradi tu unaeleza kila unachokihisi kwa hali njema na siyo kwa hasira au shari. Katika hali hii kamwe hutowapoteza marafiki zako, na kama kuna yeyote aliye rafiki atasumbuliwa na hili basi usihofu, kubali tu kumpoteza kwa kuwa hakuwa wa muhimu au wa msaada sana kwako.

Hali ya kujifanya hujaumia au hujakwazika na wakati umekwazika na unalia ndani kwa ndani inaumiza na kufanya ujisikie vibaya sana. Inakufanya uzidishe mazingira ya msongo wa mawazo (stress) hasa pale unapojiwazia wewe mwenyewe zaidi ya kushughulika na wale waliokuudhi. Mtazamo wako jinsi unavyojiona wewe mwenyewe huathirika sana, na pia waweza kujisababishia tatizo hasa pale wale wenye tabia ngumu watakapo kugundua kuwa huwezi kusema chochote hata ukiumizwa na hii itawafanya wakugeuze mpira wa kuchezea.

Je, wewe ni kati ya wale wanaojiamini kusema chochote wanachokifikiri bila kujali matokeo yake?

Hebu fikiria jinsi unavyojisikia pale ambapo mtu au watu wengine wangefanya hivyo hivyo kwako. Je, unataka kuwasababishia wengine maumivu ya moyoni? Kusema chochote kinachoshuka toka kichwani mwako kupitia kinywani mwako bila kufikiri juu ya matokeo au athari zake kwa wale wanaokusiliza au waliokuzunguka kunaweza kukupotezea marafiki na kuishusha hadhi yako kwa urahisi sana.

Mara nyingi mtu wa jinsi hii huweza kujikuta akiwa pweke na anayepingana na ulimwengu (kila mtu anamchukia). Hii ni kati ya hisia za kuhuzunisha na kuumiza sana muda wote, lakini pia huumiza zaidi pale unapogundua kuwa ni maumivu uliyojitakia mwenyewe. Peke yako unajikuta umetengwa na mtego wa kihisia na kukuzamisha usipoweza kujikwamua tena.

Jinsi ya kuwazuia marafiki wasingilie mahusaiano yenu ya kimapenzi



Sio mbaya kwa marafiki wa karibu au ndugu na jamaa kufahamu kushirikiana nanyi katika mapenzi yenu kama vile wakati wa sherehe au msiba. Pia sio mbaya kujuliana hali na kutambulisha mambo ya msingi yanayoendelea katika mahusiano yako wewe na mpenzi wako.

Hata hivyo kuna wakati watu wengine wa pembeni, wawe majirani, ndugu, wazazi au marafiki wanaweza kuwa ‘sumu’ ya mahusiano yako, hasa pale unapowategemea sana kutoa msaada, maoni au maelekezo katika maisha yako ya mapenzi. Makala hii inaeleza mambo ya msingi unayoweza kufanya ili kupunguza uwezekano wa rafiki, ndugu, jamaa, au wazazi kuwa ‘sumu’ ya mapenzi yako.

1. Udhibiti wa taarifa kwa wengine
Kadri unavyoelezea mahusiano yako kwa watu wengine ndivyo unavyowapa nafasi watu kutoa maoni, na hata kudhani kuwa wana dhamana ya kukuelekeza unavyotakiwa kuishi na mwenza wako. Hivyo basi, chukua muda wa kutosha kutafakari na kufanya uchunguzi kuhusu maswala yako ya mahusiano kabla haujaanza kutafuta maoni, ushauri kwa watu wengine. Ni bora ukasoma vitabu, na makala mbalimbali, hususani zihusuzo tabia na maisha ya mahusiano, zitafakari vema ili kuona zinahusiana vipi na unayokumbana nayo katika mahusianao yako.

2. Upekee wa mambo.
Tambua kuwa tabia ya mpenzi wako inaweza kuwa ni ya kipekee, mazingira pia ya tukio linalokufanya utake ushauri au maoni kwa wengine yanaweza kuwa ni ya kipekee, hivyo ushauri au maoni utakayopokea yanaweza yasikusaidie moja kwa moja katika suluhisho lako. Ukitambua hili, utafanya bidii ya kujenga uwezo binafsi wa kuchambua tatizo unalokumbana nalo katika mahusiano na kutafuta suluhisho kabla ya kutegemea watu wengine.

3. Mwenye maamuzi ni wewe.
Ni kweli kuwa kuna nyakati ni muhimu kupata ushauri kutoka kwa watu wengine, na zaidi sana watu wenye uelewa sahihi na unaowaamini, hakikisha kuwa unatambua kuwa wewe mwenyewe ndio mwenye kubeba lawama ya maamuzi utakayochukua.

4. Kuwa na subira.
Usichukue maamuziya haraka katika mahusiano hususani uamuzi wa kuamua kuwashirikisha watu wengine habari ya mambo yahusuyo uhusiano wako. Unapofanya uamuzi wa kuwashirikisha wengine kwa haraka  unajinyima nafasi ya kulichunguza jambo kwa ufasaha hususani madhara yanayoweza kutokea kwa kuwaeleza wengine, au kama ni tatizo, basi kufikiria njia sahihi ambazo ungeweza kuzitumia kupata suluhu ya tatizo.

5. Fungua njia za mawasiliano kati yenu: 
Pengine chanzo cha wewe kutaka kuzungumza mambo ya ndani yanayohusu mahusiano yenu kwa watu wengine ni kwakuwa umekosa nafasi ya kuzungumza kwa ufasaha na mwenzi wako. Tafuteni nafasi za kutosha, jengeni mazingira ya kuzungumzia mambo yenu kabla ya kutaka kuwashirikisha watu wengine.

6. Nenda ‘darasani’ : 
Kumbuka mahusiano yanahitaji sana uelewa mkubwa wa jinsi ya kufanya mawasiliano fasaha, kuelewa hisia za mwenzi wako, kutambua mbinu za kusuluhisha migogoro, na zaidi sana kufanya mipango ya muda mrefu ya uhusiano wenu. Jizoeshe kusoma makala na vitabu mbalimbali vyenye kuboresha ufahamu wa mambo ya msingi kama hayo tuliyoeleza hapo juu. Mfano wa makala unazoweza kusoma ni kama vile.

Kukumbatiwa na umpendaye wakati wa maumivu kuna nguvu zaidi ya dawa Paracetamol




Kumbatio kutoka kwa mtu umpendaye, linaweza kuwa na nguvu zaidi ya Paracetamol pale unapokuwa na maumivu, kwa mujibu wa utafiti.

Wanasayansi wamebaini kuwa hisia za ukaribu tunazozipata kupitia mtu anayetushika, kunaweza kusaidia kupunguza maumivu. Lakini kushikwa na mtu usiyemjua, kunaweza kusiwe na matokeo yale yake, kwasababu hatuna hisia nao.

Utafiti huo unaonesha nguvu ya ubongo kuzuia hisia za maumivu. Utafiti huo ulifanywa na wataalam katika chuo kikuu cha Haifa, Israel na ulihusisha wanawake kadhaa ambao waliwatengenezea maumivu kwa kuwaunguza na chuma chenye moto kiasi.

Katika jaribio la kwanza, mtu wasiyemjua aliwashika mkono akijaribu kuwaliwaza kwa maumivu hayo. Kwenye la pili waliwaita waume na wapenzi wao kukaa karibu nao na kugusanisha ngozi.

Katika jaribio la mwisho, wapenzi wao waliruhusiwa kuwashika mkono wakati chuma hicho cha moto kikigusishwa kwenye ngozi zao. Wanasayansi walibaini kuwa mguso wa mtu wasiyemjua pamoja na kuwa na mpendwa wao karibu hakukuwa na tofauti katika jinsi walivyosikia maumivu.

Lakini pale mtu wanayempenda alipowagusa kwenye ngozi, maumivu yalipungua.
Walibaini pia kuwa kadri mpenzi wa mwanamke alivyoonesha huruma na support kwake wakati wa zoezi hilo, alipata afueni zaidi.