Monday, 20 November 2017

Mahakama ya Kenya kuamua juu ya kesi ya urais leo

Jaji Mkuu wa Mahakama ya juu zaidi nchini kenya David Maraga

Mahakama ya juu zaidi nchini Kenya Jumatatu inatarajiwa kutoa uamuzi katika kesi zilizowasilishwa kwenye mahakama hiyo kupinga uchaguzi wa marudio wa tarehe 26 Oktoba ambapo rais wa sasa Uhuru Kenyatta alitangazwa kama mshindi.

Katika Kesi majaji watatakiwa kutoa uamuzi kuhusu masuala yafuatayo:

Wataamua iwapo tume huru ya taifa ya chaguzi na mipaka (IEBC ) ilifaa kuteuwa upya wagombea urais au la.

Uamuzi pia utatolewa na mahakama hiyo juu zaidi juu ya ya ikiwa kujiondoa kwenye uchaguzi huo kwa kiongozi Muungano wa upinzani Raila Odinga na Makamu wake Kalonzo Musyoka kuliathiri uchaguzi huo.

Majaji pia watatoa uamuzi kuhusu ikiwa baada ya tume ya IEBC kushindwa kuendesha uchaguzi katika ameneo bunge 25 kati ya 290 kunahalalisha ama kubatilisha matokeo ya uchaguzi.

Aidha Mahakama hiyo itawaeleza waKenya ikiwa tume ya uchaguzi (IEBC) ilikuwa na uwezo wa kuandaa uchaguzi wa haki na huru baada ya kugubikwa na mgawanyiko miongoni mwa wajumbe wake.

Kwa upande mwingine Wakenya watasubiri kusikia uamuzi wa mahakama kuhusu kama ghasia zilizotokea kabla na baada ya uchaguzi wa marudio wa urais ziliathiri ama hazikuathiri matokeo ya uchaguzi na kuufanya kuwa usio wa haki na huru au la.

Mahakama itatoa ufafanuzi juu ya dosari ya karatasi za kupigia kura, maarufu kama form 34A ziliathiri matokeo ya uchaguzi.

Hukumu hii inasubiriwa kwa shauku kubwa na raia wa Kenya pamoja na kwingineko duniani, huku wengio wakijiuliza hatma ya Kenya.

Tangu kufanyika kwa uchaguzi wa marudio wa urais tarehe 26 Oktoba, baadhi ya miji mikuu nchini Kenya ukiwemo mji mkuu Nairobi, pamoja na mji wa magharibi wa Kisumu imekuwa ikikumbwa na ghasia za maandamano ambazo zilizosababisha mauaji ya watu na wengine kujeruhiwa.

Kansela Merkel awekwa njia panda



Mazungumzo kuunda serikali ya mseto nchini Ujerumani yamevunjika, hali ambayo inaweka njia panda mstakabali wa Kansela Angela Merkel.

Baada ya wiki nane ya majadiliano chama chenye mrengo wa kati cha Centrist Free Democrats -FDP- kimejitoa kikilalamikia tofauti zisizoweza kusuluhishwa na chama cha Merkel cha Christian Democrats na vyama vingine katika mazungumzo.

Baadaye leo bibi Merkel atakutana na Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier, ambaye ndiye mwenye nguvu kuitisha uchaguzi mpya.

Bibi Merkel ameonya kuwepo kwa magumu katika wiki zijazo, Kiuhalisia makubaliano9 ya muungano huo yanawezekana lakini bado haijawa wazi iwapo kuna uwezekano wowote washiriki kufanya umuhimu wa kupata suluhu

Waliolipukiwa na bomu wapata tatizo la kuona


Ikiwa ni siku moja baada ya mlipuko wa bomu uliotokea Shule ya Msingi Kihinga mkoani Kagera, majeruhi wawili wamerejeshwa hospitali baada ya kupata tatizo la kuona.

Watoto hao wawili ni miongoni mwa majeruhi 43, akiwemo mwalimu, wa mlipuko wa bomu uliotokea Novemba 8 na kuua wanafunzi watano baada ya mmoja wao kuliokota na kwenda nalo shuleni akidhani kuwa ni chuma chakavu ambacho angekiuza.

Mganga mkuu wa Hospitali ya Misheni ya Rulenge, Dk Mariagoreth Frederick alisema jana kuwa watoto hao waliruhusiwa kurejea nyumbani Novemba 10 na walirejeshwa Novemba 14 kutokana na kuathirika machoni.

Aliwataja watoto hao kuwa ni Irene Sherehe na Domina Wabandi (10).

Dk Mariagoreth alisema Domina anafanyiwa utaratibu na Halmashauri ya Wilaya ya Ngara ili apelekwe Hospitali ya Rufaa ya KCMC ili kuwekewa jicho la bandia.

Bomu hilo lililipuka wakati wanafunzi wa darasa la kwanza wakiingia darasani na liliokotwa na mwanafunzi ambaye alilihifadhi kwenye begi lake la madaftari kwa lengo la kwenda kuliuza kwa wafanyabiashara wa vyuma chakavu.

Mbali ya hao, Dk Mariagoreth alisema watoto wengine wawili jana walihamishiwa Hospitali ya Kagondo wilayani Muleba ambako kuna madaktari bingwa wa mifupa.

Pia, alisema leo watawaruhusu majeruhi watano kurejea nyumbani kutokana na afya zao kuimarika, hivyo watabaki watano.

Majeruhi waliohamishiwa Hospitali ya Kagondo ni Emanuel Hilali (13) ambaye anahitaji uchunguzi zaidi wa mguu wa kushoto na ambaye pia alipoteza jicho la kulia lililoondolewa kutokana na kuharibika.

Mwingine ni Simon Boniface (10), mwenye tatizo kwenye kidevu na anahitajiwa kuchunguzwa meno yake. Pia, ana maumivu mguu wa kulia.

Dk Mariagoreth alisema bado wanahitaji dawa na vifaa tiba.

Alisema gharama za matibabu zilizotumika kwa majeruhi 33 walioruhusiwa ni Sh1.827 milioni na kwa waliopo hadi Novemba 14 wamefikisha Sh4.061 milioni.

“Wazazi wa majeruhi hawajiwezi kiuchumi, hivyo uongozi wa wilaya ulishauri watafutwe madaktari bingwa watoe huduma hapa badala ya kuwasafirisha kwenda hospitali za rufaa ili kupunguza gharama,” alisema.

Alisema majeruhi wanne ambao kila mmoja amepoteza jicho moja, hivyo wanatibiwa majeraha na mipango inafanywa ili fedha zikipatikana pia wapatiwe miwani ili kuongeza uwezo wao wa kuona kwa jicho lililobaki.

Dk Mariagoreth alisema wanahitaji dawa za antibiotiki kwa ajili ya kukausha vidonda vya majeruhi.

Jukwaa la Maendeleo ya Wakazi wa Rulenge na Murusagamba wilayani Ngara zlmechangia Sh1.07 milioni kusaidia mahitaji mbalimbali kwa ajili ya majeruhi hao.

Mkuu wa Wilaya ya Ngara, Michael Mntenjele aliyefika hospitalini kuwajulia hali majeruhi mwishoni mwa wiki, aliwataka wazazi na walezi kuwa na imani na madaktari wanaoshughulikia afya za watoto wao.

Alisema Serikali ya wilaya inafanya kila jitihada kuhakikisha huduma muhimu zinatolewa kwa majeruhi na baada ya kupona kutafanyika utaratibu wa kuhakikisha wanaendelea na masomo.

Pia, aliwashukuru wananchi wanaojitokeza kutoa misaada kupitia ofisi yake na kwa uongozi wa hospitali kwa kuonyesha uzalendo na kuwajali wenye shida.

Mwananchi.



Mugabe kushitakiwa

Mugabe kushitakiwa


Mtandao wa Twitter unaofuatilia taarifa za vyombo vya habari nchini Zimbabwe unaripoti kuwa Kiongozi wa chama tawala Cha ZANU PF anaamini mchakato wa kumshtaki Bwana Mugabe utaendelea kama ilivyopangwa Jumanne , wakati ambapo chama bunge linatarajiwa kukaa.

Hii ni kama muda wa makataa uliowekwa wa kujiuzulu kwake ambao ni Jumatatu saa sita adhuhuri utakwisha kabla Bwana Mugabe hajajiuzulu

Halikuwa tangazo ambalo baadhi ya waZimbabwe walilisubiri. Bwana Mugabe bado ni rais na haijawa wazi ikiwa bunge sasa litaanza mchakato wa kumshitaki.

Watu wa Zimbabwe walikuwa wanatarajia kusikia mugabe akijiuzulu kulingana na madai yao.

Baadhi ya wale waliokusanyika kufuatilia hotuba yake kwenye vilabu waliiambia BBC kuwa wamekatishwa tamaa na kutojiuzulu kwa rais Mugabe.

Hata hivyo hali ya imeendelea kuwa tulivu katika maeneo mengi ya Zimbabwe, huku wengi waliendelea kusubiri mchakato utakaofuata.

Duru kutoka ndani ya mazungumzo ya hatma ya Mugabe zimeiambia BBC kuwa Mugabe mwenye umri wa miaka 93 alikuwa amekubali kuondoka madarakani , lakini baadae akabadili mawazo yake
Jeshi linatarajiwa kuwa na mkutano na waandishi wa habari Jumatatu asubuhi pamoja na Muungano wa Wapiganaji waliopigania Uhuru wa Zimbabwe.

Katika hotuba yake ya kwanza kwa taifa tangu jeshi lichukue madarakwa Jumatano, Mugabe hakujiuzulu na alisema kuwa ameazimia kuongoza kongamano lijalo la Zanu-PF.

Hatma yake sasa iko mashakani kwani kulingana na mbunge wa Zanu-PF Terence Mukupe anasema kongamano hilo ni mahala panopofaa kumuidhinisha kiongozi mpya anayependelewa na chama cha Zanu-PF





Mke wa Lissu atamani kuwajua waliomshambulia mumewe



Mke wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, amesema angependa kuwajua watu waliomshambulia mumewe, aliyewaamuru wafanye shambulio hilo na sababu za kufanya uovu huo.

Mke huyo ambaye pia ni wakili, Alicia Magabe anasema kuwafahamu watu hao ni muhimu kwa kuwa familia haijui kwa sasa watu hao wanatafakari na kupanga kitu gani baada ya jaribio la kwanza la kumuua kushindikana.

Lissu, mmoja wa wanasiasa wasio na hofu kusema lolote wanaloliamini, alishambuliwa na watu wasiojulikana Septemba 7 akiwa ndani ya gari lililokuwa limewasili kwenye makazi yake Area D mjini Dodoma akitokea bungeni.

Tangu wakati huo, wakili huyo wa kujitegemea na mwanasheria mkuu wa Chadema, amelazwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya na hadi sasa Jeshi la Polisi halijaeleza kama limeshapata fununu ya waliohusika zaidi ya kujibu kuwa linaendelea na upelelezi kila waandishi wanapotaka kujua maendeleo ya suala hilo.

Na sasa mke huyo wa Lissu na ambaye pia ni wakili, Alicia Magabe anataka kuwajua waliomfyatulia mumewe zaidi ya risasi 30, aliyewatuma na sababu za kuwatuma.

Magabe pia anasema familia yake kwa sasa ipo shakani kwa kuwa hajui hao waliofanya shambulio hilo ambalo linaonekana la kukusudia kumuua, wanatafakari nini na kupanga nini.

Akizungumza na Mwananchi katika Hospitali ya Nairobi, Wakili Magabe alisema Lissu ametumia sehemu kubwa ya ujana wake kupigania masilahi na haki za Watanzania, hivyo angependa kuona haki inatendeka.

“Binafsi nimewasamehe kwa kitu walichokifanya, lakini hiyo haina maana kwamba nisingependa kuona haki inatendeka,” alisema wakili huyo.

“Sitaki kuwe na mkanganyiko baina ya kusamehe na hali ya kutamani kuona haki inatendeka.”

Alisema tukio hilo limemfanya aanze kuamini kuwa kuna watu walitaka kumuua Lissu, lakini hawajafanikiwa na anaamini watu hao wapo, hivyo anahofia usalama wa familia yake.

“Mpaka sasa sijasikia kama kuna uchunguzi wowote umefanyika na sijawahi kusikia watu wamekamatwa,” alisema Wakili Magabe.

“Hivyo nawaza kuwa hayupo salama na mimi kama mke wake sijisikii kama niko salama sana. Nawaza hawa watu watakuwa wanatafakari au wanapanga nini. Hiyo ndiyo hali niliyonayo kwa sasa. Sijui hao watu wako wapi.”

Hata hivyo, Wakili Magabe alisema Lissu yuko imara na shambulio hilo halijamrudisha nyuma katika harakati zake za kupigania haki na za kisiasa.

Alisema hilo alilionyesha mara tu alipopata fahamu.

“I have survived to tell a tale, I have lived to tell a tale (nimeepuka kifo ili nieleze jambo) ndivyo alivyosema baada ya kuzinduka,” alisema Wakili Magabe.

Alisema baada ya fahamu kumrejea sawasawa amekuwa akizungumza maneno yanayoashiria kwamba ana ari zaidi.

“Spirit yake ipo very high (ari yake iko juu sana). Si mtu wa kusema kuwa baada ya tukio amekuwa mnyonge, mwoga au ujasiri wake umepungua,” alisema wakili huyo.

“Sijawahi kupata hata kauli yake moja inayoashiria kwamba sasa atarudi nyuma. Kama mke nataka mume wangu apone, tutoke hospitali turudi nyumbani. Lakini wanapokuja viongozi wenzake kutoka Tanzania; wastaafu na wa sasa na hata hapa Kenya, kauli zake zote zinaashiria amekua zaidi kisiasa.

“Anasema ‘kuna siku nitapona na nitaendelea na kazi zangu’ ili kuwatia moyo wanasiasa na wanaharakati.”

Kuhusu mumewe kuendelea na siasa baada ya kupona, Wakili Magabe alisema Lissu ndiye anaweza kulizungumzia suala hilo.

“Mimi nikiwa msaidizi wake wa kwanza, nitakuwa mtu wa mwisho kusema Lissu asifanye analotaka kwa kuwa hata akiyatamka hayatakuwa na nguvu mbele za Mungu,” alisema.

“Binafsi nasema alikuja duniani kwa makusudi. Mungu alimleta duniani kwa sababu na alijua hata kabla hajazaliwa maisha yake yatakuwaje na atafanya nini hapa duniani.

“Sidhani kama kuna binadamu anaweza kuzuia yale ambayo Mungu amepanga. Sitaki kusema kama ataendelea na siasa, hataendelea nazo, yupo kwa kusudi lake.”

Magabe alisema kuna watu wanapigwa risasi moja na wanafariki dunia, lakini Lissu alipigwa risasi 16 za moto ambazo zilipita kwenye mwili wake na anaendelea kuishi.

Alisema anafarijika kuona Lissu yu mzima kwa kutumia nguvu za watu wote ambao kwa namna moja au nyingine wanapenda aishi, akianzia na waliochanga fedha, waliomtolea damu, walioomba, waliomnyanyua, waliomtibu mara ya kwanza na wanaoendelea kumtibu.

“Hatujawahi kuwa peke yetu na nimegundua kumbe kupigwa risasi kwa Lissu ni tukio ambalo limewagusa Watanzania na mataifa mengi na wapo tayari kusaidia,” alisema mwanamke huyo.

“Hii ni kwa kuwa ametumia ujana wake kupigania masilahi na haki za Watanzania.”

Magabe alisema risasi zilizompata Lissu ziliharibu zaidi mifupa, tishu zilizo karibu na mifupa ya mguu wa kulia na mikono, lakini hakuumia kwenye neva, mishipa mikubwa ya damu, ya fahamu au ogani.

“Madaktari wanasema risasi zilikuwa zinakwepa maeneo muhimu. Ni kitu ambacho hawajawahi kukiona,” alisema.

“Hapa kuna mshipa mkubwa wa damu, lakini risasi imepita pembeni. Walikuwa wanashangaa inawezekana vipi risasi nyingi zikaingia lakini zikakwepa maeneo muhimu.”

Alisema madaktari wamemweleza Lissu kuwa ataendelea kuimarika lakini itachukua muda kabla hajapona na kuweza kutumia viungo vyake vyote kama kawaida.

Mama huyo alisema awamu ya kwanza ilikuwa kumtibu majeraha na ya pili ni kumjengea uwezo wa kutumia viungo vyake ili baadaye aweze kusimama na kurudi katika hali yake.

Magabe alisema ilichukua mwezi mmoja Lissu kutoka ICU na hakuweza kumhudumia kwa ukaribu kutokana na masharti ya chumba cha uangalizi maalumu.

“Kila siku naamka kama nakwenda kazini. Lazima niamke asubuhi kuja hospitali kisha narudi usiku nyumbani. Siruhusiwi kulala hapa,” alisema.

Simulizi ya siku ya tukio

Magabe alisema siku ya shambulio alikuwa ametoka Kerege wilayani Bagamoyo na alipanga kukutana na rafiki yake eneo la Mpiji, Bunju.

“Saa 6:30 nilifika kwake, akaniambia lazima nipate chakula cha mchana, baada ya chakula nilimwambia nipumzike kwenye kochi,” alisema.

“Baada ya dakika 25 akaniamsha akaniambia Alicia amka ukilala sana mchana huu usiku unaweza usipate usingizi,” alisema.

Alipoamka aliwasha simu zake na kukuta ujumbe usemao, “hello sister, kuna taarifa inazunguka sina hakika kama ni ya kweli. Kama kweli pole sana dada yangu.”

Alisema moja kwa moja wasiwasi ulimjia kwamba huenda mumewe amekutwa na jambo baya, alisema alichowaza awali huenda amepata ajali na ndipo akamuomba rafiki yake ampigie mtu huyo simu kujua zaidi kuhusu ujumbe huo.

“Niliingia kwenye magroup ya Whatsapp ya Chadema nikakutana na hiyo taarifa. Nilipiga kelele kwa nguvu, rafiki yangu aliniuliza umeona nini nikamwambia kuna ujumbe huu,” anasema na kumpa rafiki huyo simu asome ujumbe huo uliosema “Tundu Lissu amepigwa risasi.”

“Nilianza kuwaza yupo hai au amekufa. Niliwaza nifanye nini nikamwambia nataka kwenda nyumbani. Huko niliamini kuwa ningewaza kwa utulivu nini cha kufanya.”

Anasema baadaye simu zilianza kuingia mfululizo na ndipo alipoamini kuwa habari hizo ni za kweli.

“Nilimpa jukumu hilo (la kupokea simu) kwa sababu ni rafiki yangu wa karibu tangu sijaolewa,” alisema.

Baadaye waliingia kwenye gari na yeye kuanza kuendesha huku rafikiye akizungumza na waliokuwa wakimpigia simu.

Magabe alisema baada ya kuiingia mtaa wa nyumbani kwake, aliona vijana wanamwangalia katika namna ambayo ilionyesha kuna kitu wanakijua. “Mwonekano wao ulikuwa tofauti wananiangalia kwa huruma, kwa mshangao. Wanatamani waongee,” alisema.

Anasema nyumbani aliwakuta shemeji zake wawili na mtoto wa baba yake mdogo, lakini alishindwa kuingia ndani na badala yake alikaa bustanini.

“Nilipigiwa simu na watu waliokuwepo hospitali na wakaniambia ni kweli amepigwa risasi, lakini yupo hai. Walinitaka nitulie mpaka nitakapopewa taarifa nini cha kufanya,” alisema.

Alisema mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alimweleza nini cha kufanya kwa wakati huo.

Alisema baadaye aliambiwa Lissu angepelekwa Nairobi na hivyo aende uwanja wa ndege kwa ajili ya safari ya Dodoma na baadaye Nairobi.

Aliondoka na kaka yake na marafiki wa karibu, lakini alipigiwa simu na kutakiwa kushuka kwa kuwa muda haukuwa rafiki.

“Nilipanda bodaboda,” alisema.

“Wale vijana walikimbiza sana na ilikuwa ni mara ya kwanza kupanda pikipiki Dar es Salaam. Niliogopa na kusali Mungu anisaidie kufika uwanja wa ndege salama.”

Alipofika Dodoma ndipo alipomuona kwa mara ya kwanza Lissu tangu apate taarifa za shambulio.

“Baada ya dakika chache akaja akiwa kwenye kitanda kutoka chumba cha upasuaji. Kwa kumuangalia nilijua ameumia sana hakuwa anajitambua,” alisema.

Mwananchi.

MAGAZETI YA LEO 20/11/2017

MAGAZETI YA LEO 20/11/2017