Peter Manyika Jr ambaye ni golikipa wa Singida United amemkalisha golikipa wa Simba Aishi Manula kwa kucheza mechi nyingi bila kuruhusu goli (clean sheets). Mechi ya jana ambayo Singida walishinda 1-0 dhidi ya Lipuli,Manyika alifikisha jumla ya michezo saba bila kufungwa katika mechi 10 za VPL zilizopita.
Manula ambaye ndiye golikipa namba moja wa kikosi cha Taifa Stars, hajaruhusu goli katika mechi tano za VPL kati ya mechi tisa alizocheza hadi sasa. Amezidiwa cleans sheets mbili na Mayika Jr lakini wawili hao wametofauiana katika idadi ya mechi walizocheza. Manyika tayari amecheza michezo 10 wakati Manula akiwa na mechi tisa huku leo akitarajiwa kucheza mechi yake ya 10 VPL wakati Simba itakapokuwa ikicheza dhidi ya Tanzania Prisons uwanja wa Sokoine Mbeya.
Manyika Jr taratibu anarejea kwenye ubora wake baada ya kuondoka Simba alipokuwa ‘anachoma mahindi’ kwa muda mrefu. Uwepo wa magolikipa wa kigeni Vicent Angban na Daniel Agyei kwa nyakati tofauti ulipelekea Manyika Jr kupoteza nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza pale Msimbazi.
Jana Ijumaa November 17, 2017 Manyika Jr ameandika rekodi yake ya kucheza mechi saba bila kuokota mpira ndani ya nyavu zake katika mechi 10 ambazo amesimama langoni, huku mchezo wa jana ukiwa ni wa tano mfululizo bila kufungwa. Hili si jambo dogo kwake amefikia rekodi ya golikipa wa Azam Razak Abarola ambaye hajaruhusu goli katika mechi saba za VPL katika mechi tisa alizocheza.
Clean sheets za Manyika Jr katika mechi 10 za VPL msimu huu
Stand United 0-1 Singida United
Singida United 1-0 Kagera Sugar
Ruvu Shooting 0-0 Singida United
Ndanda 0-0 Singida United
Mtibwa Sugar 0-0 Singida United
Singida United 0-0 Yanga
Singida United 1-0 Lipuli
Clean sheets za Manula katika mechi 9 zilizopita VPL msimu huu
Simba 7-0 Ruvu Shooting
Azam 0-0 Simba
Simba 3-0 Mwadui
Simba 4-0 Njombe Mji
Mbeya City 0-1 Simba
Baba mzazi wa golikipa huyo Manyika ambaye ni golikipa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars alishawahi kuiambia shaffihdauda.co.tz kuwa, kushuka kiwango kwa kijana wake wakati akiwa Simba kulichangiwa na mambo mengi ya nje ya uwanja na kutozingatia miiko ya soka.
Badae Manyika Jr alirudi kwa mzee wake baada ya kugudua amekosa mwelekeo na kipaji chake kimekosa njia, alipokelewa na baba yake kisha kurejeshwa kwenye kituo cha magolikipa kinachomilikiwa na baba yake (Manyika Sr) pale Karume. Alianzishiwa mazoezi maalum ya kupunguza uzito na kuwekwa fit hatimaye akarejea katika hali yake.
Baba yake ambaye ndio meneja wa mtoto wake alisema, mkataba wa Manyika Jr na Simba utakapomalizika hawatakubali kuongeza mwingine badala yake watamtafutia timu nyingine ambayo wataweka masharti ya kimkataba kuhakikisha anacheza mechi nyingi pale anapokuwa fit, hapo ndipo safari ya kwenda Singida United ikawadia baada ya timu hiyo kujiridhisha na ubora aliokuwanao Manyika Jr wakati huo.
Ubora wa Manyika katika milingoti mitatu umemrejesha Stars
Baada ya kufanya vizuri katika mechi za ligi kuu, kocha wa Stars Salum Mayanga alianza kumuita Manyika Jr kwenye timu ya taifa ili kutoa changamoto kwa Aishi Manula. Inawezekana wengi waliamini Manyika ndio basi tena, lakini baada ya kugundua alikosea wapi na anatakiwa kufanya nini amesimama kwa mara nyingine na kuwaamisha watu bado kipaji chake hakijapotea.
Manyika Jr vs Abarola
Wote hawajaruhusu magoli katika mechi saba hadi sasa, Manyika amecheza mechi 10 wakati Abarola amecheza mechi tisa. Abarola ndio wa kwanza kufikisha mechi saba bila kuruhusu goli lakini Manyika ameifikia rekodi hiyo ya golikipa kutoka Ghana baada ya mchezo wa jana Singida United 1-0 Lipuli.
Manyika Jr anampiku Abarola kwa kucheza mechi tano mfululizo bila kufungwa goli, katika mechi tano zilizopita mfululizo Manyika Jr ameidakia Singida United bila kuruhusu wavu wa goli lake kucheza. Abarora aliwahi kucheza mechi nne mfululizo za mwanzo wa ligi bila kufungwa, Abarola aliruhusu goli la kwanza dhidi ya Singida United timu hizo zilipotoka sare ya kufungana 1-1 kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma
Leo Jumamosi Nov 18, 2017 Abarola yupo kwenye nafasi ya kufikisha mechi nane bila kufunga na kumwacha Manyika Jr endapo hatafungwa kwenye mchezo kati ya Njombe Mji dhidi ya Azam kwenye uwanja wa Sabasaba mkoani Njombe