Thursday, 8 February 2018

Wednesday, 7 February 2018

Hizi ndizo Njia tatu za kupunguza foleni Dar

Wakati Serikali ikiendelea na utekelezaji wa miradi mbalimbali kukabiliana na changamoto ya foleni jijini Dar es Salaam, Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Japan (Jica) limekuja na mwarobaini wa tatizo hilo.

Timu ya wataalamu wa shirika hilo imefanya utafiti ulioonyesha njia mbalimbali zinazoweza kutumiwa kukabiliana na foleni kubwa, ikiwamo ujenzi wa reli.

Akizungumza wakati wa uwasilishaji wa mpangilio wa sekta ya usafirishaji katika Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka 2018 hadi 2040, mwakilishi wa Jica nchini, Toshio Nagasa alisema kufikia mwaka 2040 wakazi wa jiji hilo watakuwa wameongezeka kutoka milioni sita hadi 12. Kutokana na ongezeko hilo Nagasa alisema ni muhimu kwa Serikali kuweka mazingira wezeshi ya usafiri ili kuwezesha sehemu zote za jiji kufikika kwa urahisi huku shughuli za uchumi zikiendelea.

“Kukabiliana na msongamano utakaojitokeza katika kipindi hicho ni muhimu Serikali ikafikiria kujenga miradi ya reli, ambayo inaweza kusafirisha watu wengi kwa pamoja, hii itasaidia kupunguza magari binafsi kuingia barabarani,” alisema.

Licha ya reli, mpango huo umeshauri kuwapo kwa barabara za juu katika makutano ya Morocco, Chang’ombe na Mwenge.

Kingine kilichoelekezwa katika mpango huo, ni uwapo wa miji midogo maeneo ya pembezoni ili kupunguza msongamano katikati ya jiji.

Kauli ya Serikali

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Spora Liana alisema wataalamu hao wameshauri miji hiyo midogo iwekewe huduma zote za msingi ili watu wengi wasiende mjini. Alisema utekelezaji wa mradi huo utagharimu Sh19.1 bilioni ukihusisha ujenzi wa miundombinu.

Wakati huohuo, mkurugenzi wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam mhandisi Patrick Mfugale alimweleza waziri wa Ujenzi na Usafirishaji wa Lesotho, Lehlohonolo Moramotse, kuwa mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Mandela na Nyerere (Tazara) wenye thamani ya Sh95 bilioni, unatarajia kukamilika Mei na kutumika rasmi mwishoni mwa Oktoba. Waziri huyo yupo nchini na wataalamu wa wizara yake kujifunza namna ambavyo wenzao wanasimamia ujenzi, ukarabati na utunzaji wa barabara.

Serikali yaahidi kuboresha mishahara

Serikali ya Tanzania imeahidi kuanza kuboresha maslahi ya watumishi ya walimu ikiwemo mishahara yao kipindi hiki kutokana na kumaliza zoezi la muda mfupi la uhakiki wa wafanyakazi hewa katika sehemu mbalimbali za ajira.

Hayo yamewekwa wazi na Naibu Waziri Ofisi ya Rais-TAMISEMI George Joseph kakunda leo (Jumatano) katika mkutano wa 10 kikao cha saba cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma wakati alipokuwa akijibu swali la nyongeza kutoka kwa Mbunge wa Karagwe Innocent Bashungwa alipotaka kujua ni lini serikali itawapandishia mishahara walimu.

"Utaratibu huu ambao ulikuwa umesimama kwa kipindi kifupi cha miaka kama miwili hivi kupisha uhakiki wa watumishi ambapo ni zoezi lililofanywa kwa umahiri na ueledi mkubwa, baada ya kuwa tumelikamilisha sasa tutaingia kwenye awamu ambayo ni ya kuboresha maslahi ya watumishi ikiwemo mishahara yao", amesema Kakunda.

Kwa upande mwingine, Mhe. kakunda amewatoa hofu walimu wote ambao hawakupandishwa madaraja yao kutokea mwaka 2016 hadi 2017 na kudai katika mwaka huu wa fedha wameshafanya matayarisho wa kupandisha madaraja hayo.

Askari Magereza 11 wasimamishwa

Jeshi la Magereza Tanzania limewasimamisha kazi askari wake kumi na moja waliofikishwa mahakamani kwa tuhuma za mauaji ya mwanakijiji, Aloyce Makalla (41) wiki iliyopita.

Taarifa kutoka ndani ya jeshi hilo zinasema askari hao walisimamishwa kazi na Kamishna Jenerali wa Magereza, Dk Juma Malewa juzi.

Mkuu wa Magereza Mkoa wa Tanga, John Masunga alithibitisha kusimamishwa kwa askari hao lakini hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani zaidi akisisitiza kuwa msemaji wa jeshi hilo ni Kamishna Jenerali pekee.

Askari waliosimamishwa ambao walishafikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Korogwe mwishoni mwa wiki mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kassim Mkwawa ni Jonas Makere, Shadrack Lugendo, Lazaro Stephen, Mussa Zuberi, Ramadhan Yusuf, Robert Alfred, Fhidirish Osmas, Alfonce Revocatus, Mbesha Naftari, Hamis Msola na Michael Elias.

Taarifa hiyo inaeleza kuwa hatua ya kuwasimamisha kazi askari hao imechukuliwa ikiwa ni kupisha vyombo vya sheria kufanya kazi yake kwa uhuru zaidi na kwamba hatima yao itategemea uamuzi wa mahakama hiyo.

Askari hao wa Wilaya ya Korogwe walifikishwa katika mahakama hiyo wakikabiliwa na shtaka la kumuua, Makalla, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kerenge wilayani humo.

Ilidaiwa mahakamani hapo na mwanasheria mwandamizi wa Serikali, Saraji Iboru kuwa Januari 22 saa 9.30 katika kitongoji cha Mapangoni Kijiji cha Kerenge, washtakiwa hao kwa pamoja walimuua mwanakijiji huyo.

Iboru ambaye alikuwa akisaidiana na mwendesha mashtaka kiongozi, Shosa Naiman alidai kwamba siku ya tukio, washtakiwa hao walikwenda nyumbani kwa Makalla wakimtuhumu kwamba Januari 15 alimjeruhi askari mwenzao aitwaye Sajenti Stephen.

Washtakiwa hao hawakutakiwa kujibu chochote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo kisheria wa kusikiliza kesi za mauaji. Hakimu Mkwawa aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 15 itakapotajwa tena.

Hii ndio gharama aliyotumia Vanessa Mdee kuandaa albamu yake mpya ‘MoneyMonday’

Msanii wa muziki, Vanessa Mdee amedai ametumia gharama kubwa katika kuiandaa albamu yake mpya MoneyMonday.

Muimbaji huyo amesema kuwa albamu ya MoneyMonday mpaka kukamilika imemgharimu zaidi ya shilingi za Kitanzania Milioni 100.

“Nimetumia fedha nyingi lakini kwangu sioni tatizo lolote, niliangalia zaidi jinsi gani watu watatambua Vanessa kafika wapi katika kukua kimuziki, fedha hiyo nililipa idara zote kuanzia wasanii walioshiriki matangazo, video nk na bado naendelea kutoa kwa kuwa matangazo bado yanaendelea ,” Vanessa aliuambia mtandao wa Dar 24.

Ameongezea kuwa hajutii matumizi ya kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa kuwa lengo lake hasa ni kutoa kazi itakayomwongezea heshima kwenye muziki wake sambamba na kuhakikisha inawifikia watu wa aina zote.

Hivi karibuni Vanesa ameachia albamu yake katika ukumbi wa Mlimani City.

Vanessa ni kati ya wasanii wachache ambao wanajaribu kurudisha utamaduni wa kutengeneza Albamu katika muziki wa Bongo fleva jambo ambalo kwa siku za nyuma limekuwa likififia na kupotea.

Naye Diamond Platinum anajipanga kuaachia albamu yake ya Mtoto wa Tandale ambapo juzi alitaja baadhi ya sababu zilizomfanya acheleweshe kutoka kwa albamu hiyo.

Waziri Nchemba aongoza oparesheni ya kuteketeza ekari sita za bangi

Waziri wa mambo ya ndani nchini, Mwigulu Nchemba leo ameongoza oparesheni ya kuteketeza jumla ya ekari sita za bangi zilizokuwa zimelimwa katikati ya msitu ndani ya kijiji cha Engalaoni wilayani Arumeru mkoani Arusha.

Mwigulu akishirikiana na kamanda wa jeshi la polisi mkoani Arusha,(RPC)Charles Mkumbo pamoja na vikosi vya askari wa jeshi la polisi mkoani hapa walilazimika kuacha magari yao njiani na kutembea umbali wa kilomita 5 milimani kufika katikati ya msitu huo ambapo wamiliki wa mashamba hayo walitokomea kusikojulikana.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa zoezi hilo Mwigulu alisema kwamba serikali itaendelea na oparesheni pande zote za nchi na haitasita kuwakamata wahusika wote na kutaifisha magari yatakayotumika kusafirisha bangi.

Akizungumza na askari waliokuwa wakishiriki katika zoezi hilo Mwigulu mbali na kuwapongeza kwa kazi wanayofanya lakini aliwambia kwamba pamoja na kufanikiwa kuteketeza madawa ya kulevya yanayolimwa mashambani lakini waongeze juhudi pia katika kupambana na madawa ya kulevya yanayotengenezwa viwandani.

“Niwapongeze sana songeni mbele na kazi ya kukamata madawa yote ya kulevya mmefanya kazi kubwa sana ya kukabiliana na madawa ya kulevya yanayolimwa mashambani ongezeni bidii kukamata na yale yanayozalishwa viwandani,” alisema Waziri Mwigulu.

Hata hivyo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Arusha(RPC),Charles Mkumbo alisema kwamba jumla ya ekari sita za mashamba ya bangi zimeteketezwa na kusisitiza kwamba oparesheni hiyo ni endelevu katika mkoa wa Arusha na wilaya zake.

Aidha Kamanda Mkumbo alifichua mbinu mpya wanayotumia wamiliki wa mashamba hayo kwamba kwa sasa wameamua kulima mashamba hayo katikati ya misitu kwa lengo la kujificha ili kukwepa mkono wa sheria.

“Walidhani kulima bangi katikati ya misitu hatutawakamat sisi tuna mbinu nyingi na hatutakubali kuona vijana wetu wanaharibikiwa kwasababu ya bangi.”

Vanessa Mdee atoa ufafanuzi kuhusu ngoma zake na Diamond kuchezwa Nigeria



Msanii wa muziki Bongo, Vanessa Mdee ametolea ufafanuzi kauli yake iliyodai alipofika Nigeria alikuta ngoma za wasanii toka Bongo zinazochezwa ni zake na za Diamond.

Baada ya kauli hiyo Vanessa amekuwa akishambuliwa na mashabiki hasa wa team Kiba kuwa kauli yake ni yenye upendeleo kwa upande mmoja. Kupitia Instagram Vanessa ameamua kumjibu shabiki aliyehoji kuhusu hilo.

vanessamdee @ze_masta my love hiyo issue nilikuwa nazungumza kitu kikubwa zaidi lakini wenye akili zao wamegeuza imekuwa hivyo. Na Ukiangalia lengo la jibu langu ilikuwa kuwahamasisha waTanzania wathamini na waPromote zaidi mziki wa home maana wenzetu ndivyo wanavyofanya.

Sasa wapi hapo nimemdiss kaka? Kaka anajua mimi shabiki yake sasa tutafika kweli kila neno linageuzwa kuwa negative when in truth I was just shedding light on what I was seeing. Jamani.

Hapo Jux Vanessa aliiambia Clouds Fm alipoenda Nigeria kwa ajili ya kutangaza albamu yake ‘Money Mondays’ katika moja club alizopita alikuta ngoma zinazochezwa kutoka Bongo ni ya Patoranking na Diamond ‘Love You Die’ na ile aliyoshirikiana na Reekado ‘Move’.

Msigwa amfungukia Kigwangalla Bungeni

Mbunge wa Iringa Mjini kwa tiketi ya CHADEMA, Mhe. Peter Msigwa amefunguka na kumchana Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala na kudai kuwa anafanya kazi kwa mizuka na mihemko na kuisumbua sekta ya Utalii na Maliasili nchini.

Msigwa amesema hayo wakatii alipokuwa akichangia bungeni taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii na Kamati ya Kilimo, Mifugo na Maji, mjini Dodoma na kudai kuwa Mawaziri vijana wamekuwa na mihemko.

"Niwashauri hawa Mawaziri vijana fursa 'opportunity is atrracted by talent, skills, perfomance and abillity. Show your talent and abillity people will love you' hawa Mawaziri wa zamani hawa kwa mfano Lukuvi, Tizeba tunawaona wakijibu hoja wanajibu hoja siyo za kimihemko kiasi kwamba unaridhika hata Waziri akikujibu unapenda lakini Mawaziri vijana wengi mnaonekana mnayofanya katika Serikali hii kiasi kwamba Serikali ijayo muonekane hamna tija" kwa sababu mna mihemko sana"

Mbali na hilo Msigwa alikwenda mbali zaidi na kumnyooshea mkono Waziri wa Maliasili na Utalii na kudai amekuwa na maamuzi ya ajabu jambo ambalo linapelekea kiongozi huyo kuivuruga Wizara hiyo.

"Utalii huu umejengwa kwa muda mrefu sana na akitokea mtu mmoja anaamua kufanya tu kwa kutafuta umaarufu atauvuruga kwa muda mfupi sana, Utalii kwenye pata la taifa unaingiza asilimia 20 na forex ni kubwa inatokana na utalii kwa hiyo hicho si kitu kimoja mtu anaweza kuamka leo anasema nimeharibu na hii diplomasia ya kiuchumi inategemea sana na kutabirika, wawezekaji huko nje wanataka kuona kunatabirika wao kufanya biashara zao. Haiwezekani huyu Waziri anatoa amri mpaka mapolisi wanamkataa anashindwa hata kuwasiliana na Waziri wake wa Mambo ya Ndani, huyu huyu Waziri anatoa amri anapingana na Waziri wa Ardhi, huyu huyu Waziri mmoja anapingana na Waziri wa Uvuvi hatuwezi kuwa na Mawaziri ambao wanakuwa na mizuka na kufanya kazi kwa mizuka wote kama tunalipenda taifa letu tufanye kazi kwa kupendana" alisisitiza Mchungaji Msigwa

. Nassari: katika Jimbo langu kumeanza kuibuka migogogro juu ya michango

Arusha. Mbunge wa jimbo la Arumeru Mashariki (Chadema) Joshua Nassari, ameitaka Serikali kutoa tamko moja juu ya michango ya chakula shuleni kama ni halali ama la ili kuzuia migogoro ambayo imeanza kuibuka.

Akizungumza na Mwananchi leo Februari 7 Nassari amesema  katika jimbo lake kumeanza kuibuka migogoro juu ya michango ya chakula kwani kuna wazazi ambao walikuwa wamechangia mara baada ya shule kufunguliwa na sasa wanataka warejeshewe michango yao.

‘’Hili  suala limeleta utata mkubwa na mgongano baina ya walimu, Kamati za shule na wazazi, kwani  baadhi ya wazazi wameaminishwa kuwa Serikali imetoa fedha kugharamia mahitaji yote ya shule," amesema

Amesema  ni muhimu kuwepo na tamko moja ni michango gani, ambayo ni marufuku na ipi ambayo inakubalika na hivyo kuwekwa utaratibu mzuri wa kuikusanya.

Alisema anachofahamu ni kuwa Serikali, haijapiga marufuku michango ya chakula, bali kinachotakiwa ni wazazi kutoa kwa hiari yao baada ya kukubaliana katika vikao lakini jambo hili linapaswa kuelimishwa.

Waraka namba 3 wa mwaka 2016 juu ya suala la elimu bure, pia umeeleza jukumu la chakula cha wanafunzi kwa shule za kutwa na sare za shule ni la wazazi.

Diwani wa kata ya Imbaseni, Gabriel Mwanda alisema katika kata yake, kuna wazazi walichanga chakula shuleni, lakini kutokana na tamko la serikali la kuzuia michango wameanza kuidai.

"Hili ni tatizo, tumejaribu kuwaeleza wazazi juu ya umuhimu wa michango baadhi wameelewa na wengine bado hawajaelewa" amesema

Mwanda amesema ni ukweli ni kuwa fedha ambazo zinapelekwa shuleni, hazitoshi mahitaji yote lakini sintofahamu iliyopo sasa isipopatiwa ufumbuzi itaathiri sekta ya elimu.

"Suala la chakula kwa watoto  shuleni ni muhimu sana hivyo tumekuwa tukishauri wazazi kuchanga kwa hiari lakini watoto wasirejeshwe nyumbani kwa wazazi wao kwa kushindwa kuchangia chakula," amesema.

Katika shule nyingi wilaya ya Arumeru, kamati za shule zilikuwa zimepitisha mchango wa debe mbili za mahindi na kilo tano za maharage kwa ajili ya chakula na tayari shule zilipofunguliwa wazazi walichanga.

Hata hivyo, kutokana na kuibuka utitiri wa michango shuleni, hivi karibuni Rais John Magufuli alitangaza kupigwa marufuku walimu kupokea michango mashuleni na akawataka wazazi ambao wanataka kujitolea kupeleka michango yao kwa  wakurugenzi.

Wakulima wa Mahindi watoa kilio chao kwa Serikali

Wakulima wa mahindi mkoani Njombe wamedai kuwa bado hawajaanza kuona manufaa ya kufunguliwa kwa mipaka kutokana na wafanyabiashara kutochukua mahindi waliyonayo licha ya bei ya zao hilo ikiwa ni chini ya kawaida.

Wakulima hao wamesema kuwa kufunguliwa kwa mipaka hakuna faida kwao kwa kuwa mazao hayanunuliwi kutokana na wafanyabiashara wanaotoa mazao nje ya nchi tayari wana mahindi ya kutosha.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mkoani Njombe wakulima hao wamesema kuwa zao hilo sasa halina soko la uhakika na bei yake imekuwa ni ya chini mpaka shilingi 4500 kwa debe moja la kilo 20 ambazo pamoja na kushuka hakuna mteja anaye fika kununua.

Halmashauri ya wilaya ya Njombe nayo inalalamika kwa kutonunuliwa kwa mazao hayo ambayo ni moja ya chanzo chake cha mapato ambapo awali ilitegemewa wakala wa hifadhi ya chakula (NFRA), watanunua mazao hayo.

Kambale wa Singida United aiomba radhi klabu yake



Nyota wa kimataifa wa Singida United Kambale Salita gentil ameiomba msamaha klabu hiyo baada ya kumsimamisha kwa muda usiojulikana kutokana na utovu wa nidhamu uwanjani.

Taarifa ya klabu hiyo iliyotolewa leo na Mkurugenzi mtendaji Festo Richard Sanga imeeleza kuwa kiungo huyo aliyesajiliwa kwenye dirisha dogo ametambua kosa lake na kuomba kupunguziwa muda wa adhabu.

Sehemu ya taarifa hiyo pia imenukuu maneno ya Kambale ambaye amesema, ''Naomba sana mnisamehe, mimi ni mtoto wenu, mimi ni kijana wenu na mimi ni mfanyakazi wenu, naomba wachezaji wenzangu wanisamehe pamoja na uongozi wa klabu yangu, tukio hili halitajirudia tena''.

Kambale alimpiga mchezaji wa timu ya Green Worriors kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho kitendo kilichopelekea kuoneshwa kadi nyekundu. Singida United ilishinda mchezo huo na kusonga mbele.

Singida United leo jioni inashuka kwenye dimba la CCM Kirumba kukipiga na wenyeji Mbao FC kwenye mchezo wa ligi kuu. Singida United inashika nafasi ya nne ikiwa na alama 30.

Luis Enrique akubali kurithi mikoba ya Antonio Conte?

Habari kutoka Hispania zinaeleza kuwa meneja wa zamani wa klabu ya Barcelona, Luis Enrique ameonekana kukubali kurithi mikoba ya kocha Antonio Conte ndani ya Chelsea.

Nafasi ya Conte ndani ya kikosi cha Blues imeonekana kuwa mashakani tangu wiki iliyopita baada ya kupata matokeo mabaya ya kufungwa 3 – 0 dhidi ya Bournemouth na yale ya 4-1 mbele ya Watford siku ya Jumatatu.

Kufuatia mwenendo wa kusuasua kwa kikosi cha Chelsea mmiliki wa timu hiyo Mromania Abramovich anampango wa kumpatia mkataba wa miaka miwili na nusu kocha Enrique mwenye umri wa miaka 47 ambao atakuwa the blues hadi mwaka 2020 hii ni kwa mujibu wa chombo cha Sports.

Chadema yasema mgombea Udiwani wa Chama hicho alipewa fedha ajitoe

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji amesema mgombea udiwani wa chama hicho Kata ya Buhangaza Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, Athanas Makoti (28) alilazimishwa kupokea rushwa ya Sh8milioni na watu waliomteka na kumjeruhi ili ajitoe kwenye uchaguzi.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 7, 2018 makao makuu ya Chadema, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Dk Mashinji ameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kuchukua hatua.

Makoti alitekwa Februari 2, 2018 katika mazingira ya kutatanisha na kupatikana Februari 5, 2018 saa moja asubuhi akiwa ametelekezwa na watu wasiojulikana jirani na Hospitali ya Kagando iliyopo Wilaya ya Muleba. Mgombea huyo amelazwa katika hospitali hiyo mpaka sasa.

Dk Mashinji amesema Makoti alikuwa anatoka kwenye maandalizi ya uchaguzi, akaita bodaboda ili arejee nyumbani lakini likatokea gari nyuma yake na kumchukua kwa nguvu.

“Watekaji hao walimfunga kitambaa usoni akapoteza fahamu. Walimzungusha maeneo mbalimbali na alipozinduka hakujua aliko. Walimtaka akubali kupokea Sh8 milioni na ajitoe kwenye uchaguzi, hata hivyo alikataa ndipo wakaanza kumtesa,” amesema Dk Mashinji,

“Hizi ni njama za kisiasa kutaka kuvuruga uchaguzi katika kata ya Buhangaza,” amesema.

Amesema kwa mujibu wa maelezo ya mgombea huyo, alitekwa kwa madhumuni ya kisiasa.

“Tunalaani  kitendo cha mgombea wetu kutekwa, kuteswa na kulazimishwa kupokea fedha ili ajitoe kwenye uchaguzi,” amesema.