Thursday, 28 December 2017

Rais Magufuli akutana na kamati ya uhakiki CCM


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)  John Magufuli amekutana na kamati maalum aliyoiunda kwa lengo la kuhakiki mali za chama hicho, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Rais amekutana na kamati hiyo leo Desemba28 kwa mara ya kwanza tangu alipoitangaza  Desemba 20, Mkoani Dodoma ambayo inaongozwa na Dk. Bashiru Ally.

Katika Mazungumzo hayo  Rais Magufuli amewataka wajumbe wa kamati hiyo kufuatilia na kuhakiki mali zote za chama, kumhoji mtu yeyote ambaye atahitajika kutoa taarifa juu mali za chama na kubaini thamani ya mali, mahali zilipo, makusanyo ya mapato na wanazozishikilia ama kutumia mali hizo.

Rais Magufuli pia ametoa wito kwa wanachama wa CCM na wananchi wengine kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zote zinazohusu mali za chama kwa kamati hiyo, na watakaoitwa kuhojiwa waitikie wito huo.

“Nataka mali za chama zikinufaishe chama, nataka mkamhoji mtu yeyote, awe kiongozi, awe mwanachama, awe mfanyabiashara, mtu yeyote. Mkazihakiki mali zote ili chama kipate haki yake” amesema  Rais Magufuli.

Akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo, Dk Bashiru Ally amesema kamati imeanza kazi rasmi na ametoa wito kwa wanachama, wananchi na wote wanaozitumia mali za chama kutoa ushirikiano watakapoitwa kuhojiwa.

“Tumezungumza na Mwenyekiti kwa karibu saa mbili, katueleza matarajio yake, sababu za kuunda tume hii, kazi zake na faida zake kwa chama na kwa nchi, kwa hiyo ametukabidhi vitendea kazi na taarifa mbalimbali na ametuambia kazi yetu ni kuhakiki mali zote za chama kwa kushirikiana na wanachama na wale wanaoshirikiana na chama kuzitumia hizo mali kama vile wapangaji, wasimamizi, nakadhalika” amesema Dk  Ally.


No comments:

Post a Comment