Ukiwa ni mwaka wa pili kwa Rais John Magufuli kuwa madarakani, uelekezo wa siasa za upinzani umekuwa shakani kutokana na mazingira magumu huku baadhi ya makada wa vyama hivyo wakijiunga na CCM.
Awali kulikuwa na katazo la kufanya mikutano ya hadhara na maandamano licha ya Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 1992 kuruhusu. Katazo hilo limedumu hadi mwaka huu.
Mwaka 2017 umeendelea kuwa wa misukosuko kwa vyama vya upinzani kutokana na kuendelea kukamatwa na mara nyingine kushitakiwa.
Miongoni mwa wabunge waliokamatwa ni pamoja na Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda), John Heche (Tarime Vijijini), Esther Matiko (Tarime), Pascal Haonga (Mbozi), Godbless Lema (Arusha) na Freeman Mbowe (Hai).
Licha kukamatwa, Halima Mdee na Ester Bulaya walifukuzwa bungeni kwa kipindi cha mwaka mmoja kwa madai ya utovu wa nidhamu bungeni.
Mbali na wabunge, mjumbe wa kamati kuu ya Chadema Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa aliitwa kuohojiwa Polisi mara kadhaa, kutokana na kauli zake kuhusu viongozi wa kundi la Uamsho waliokamatwa tangu mwaka 2012, huku Waziri Mkuu mstaafu Frederick Sumaye akinyang’anywa shamba lake lenye hekta 83 lililoko wilayani Mvomero Mkoa wa Morogoro.
Novemba 26 mwaka huu Mbunge wa Chadema, Susan Kiwanga (Mlimba) alikamatwa akiwa na makada 41 wa chama hicho, huku mbunge mwenzake Peter Lijualikali wa Kilombero naye akisakwa wakidaiwa kufanya fujo na kuchoma moto ofisi ya mtendaji baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mdogo wa udiwani katika Kata ya Sofi wilayani Malinyi.
Baada ya kukamatwa, wabunge na makada hao walifikishwa mahakamani na kunyimwa dhamana, walirejeshwa mahabusu hadi Desemba 8, kesi iliposikilizwa na kuachiwa kwa dhamana.
Mwaka 2017, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji naye hakusalimika alijikuta akikamatwa akiwa wilayani Mbamba Bay Mkoa wa Ruvuma hivi karibuni akiwa na baadhi ya wabunge wa chama hicho, wakidaiwa kufanya mkusanyiko bila kibali.
Licha ya kukamatwa mara kwa mara na kushitakiwa, Tundu Lissu (Singida Mashariki) ameendelea kupata umaarufu mkubwa, akiibua hoja zinazoitesa Serikali.
Miongoni mwa mambo aliyoibua Lissu ni kukamatwa kwa ndege ya Tanzania aina ya Bombardier Q400 iliyoshikiliwa nchini Canada kutokana na deni la Dola za Marekani 38 milioni (Sh87 bilioni ) ambazo Serikali inadaiwa na kampuni ya Stirling Civil Engineering Ltd baada ya kukatishiwa mkataba wake wa kujenga barabara ya Bagamoyo mwaka 2009.
Lissu pia alitangaza kumpiga Rais Magufuli katika mikakati yake ya kukamata mchanga wa dhahabu (makinikia) bandarini wa kampuni ya Acacia Mining akimtaka Rais kufanya marekebisho ya mikataba ya madini, huku pia akiponda ripoti za uchunguzi wa michanga hiyo akiita upuuzi wa kitaaluma.
Jambo lingine lililompa umaarufu Lissu ni hatua yake ya kuwania urais wa chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ambapo Serikali ilionyesha kupinga.
Awali Rais Magufuli akihutuibia katika siku ya Sheria Februari 4, 2016 aliitahadharisha TLS kutoingiliwa na wanasiasa.
Hata baada ya tahadhari hiyo, ilibainika kuwa Lissu ana mpango wa kugombea uongozi wa chama hicho.
Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria wakati huo, Dk Harrison Mwakyembe pia aliwatahadharisha viongozi wa TLS kutojihusisha na siasa, huku baadhi ya wanasheria akiwamo Godfrey Wasonga wakifungua kesi kumpiga Lissu kugombea urais wa TLS. Hata hivyo Lissu alishinda kesi hiyo.
Siku moja kabla ya uchaguzi wa TLS uliofanyika jijini Arusha, Lissu alishikiliwa na Jeshi la Polisi na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam kesho yake.
Baada ya kusomewa mashitaka alijidhamini na kwenda Arusha kushiriki uchaguzi na kuibuka na ushindi wa kishindo kwa kupata asilimia 85 ya kura zote Machi 18. Tukio la Lissu kupigwa risasi Septemba 7 limefungua ukurasa mpya wa mapambano, huku Chadema, Bunge na Serikali wakisutana.
Lissu alipigwa risasi akiwa mjini Dodoma saa 7:30 mchana ikiwa ni takribani mwezi mmoja tangu alipoeleza kufuatiliwa na watu wasiojulikana huku akitaja namba za gari wanalotumia.
Kabla ya Lissu kubainisha hivyo, Mbunge wa Nzega (CCM) Hussein Bashe alitahadharisha kuwepo kwa wabunge 11 waliohatarini kuuawa huku akidai kuwepo kwa kikundi kinachotekeleza mauaji hayo ndani ya Idara ya Usalama wa Taifa.
Mwezi mmoja kabla Bashe hajatoa tahadhari hiyo, aliyekuwa Waziri wa Habari, Nape Nnauye alishikiwa bastola na watu ambao hadi leo hawajulikani walikotokea, ikiwa ni siku aliyoondolewa kazi ya uwaziri ya Machi 28.
Tukio la kushambuliwa kwa Lissu ambaye bado amelazwa jijini Nairobi nchini Kenya, limetumiwa na kambi ya upinzani hasa Chadema kuieleza dunia jinsi demokrasia inavyokandamizwa nchini.
Walau Oktoba 30, vyama vya upinzani walipumua baada ya aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyaladu alitangaza kujitoa CCM na kuomba kujiunga Chadema.
Hilo lilikuwa pigo kubwa kwa CCM ambayo imeonekana kujibu mapigo kwa kazi kubwa.
Kabla ya Nyalandu, tayari kulikuwa na madiwani sita kutoka jimbo la Arumeru Mashariki waliojitoa Chadema na kujiunga na CCM.
Madiwani hao ni pamoja na diwani wa Ngabobo, Solomon Laizer, Credo Kifukwe wa Kata ya Murieti jijini Arusha, Anderson Sikawa (Leguruki), Emmanuel Mollel (Makiba), Greyson Isangya (Maroroni) na Josephine Mshiu (Viti Maalumu).
Hata hivyo, Mbunge wa jimbo hilo, Joshua Nassari alidai kuwa na ushahidi wa rushwa kwa ajili ya kuwarubuni madiwani hao, ambao aliupeleka makao makuu ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) jijini Dar es Salaam.
Baada ya kuwaonyesha waandishi wa habari video hizo, walizipeleka makao makuu ya Takukuru jijini Dar es Salaam na kukabidhi ushahidi wao.
Madiwani hao walipokelewa na Rais John Magufuli wakati wa sherehe za kukamisheni maofisa wapya wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijiniArusha.
Novemba 21 baada ya vikao vya Kamati Kuu ya CCM, waliokuwa makada wa Chadema akiwamo Lawrence Masha, aliyekuwa mwenyekiti wa Bavicha, Petrobras Katambi na waliokuwa makada wa chama cha ACT Wazalendo Alberto Msando, Samson Mwigamba na Profesa Kitila Mkumbo walijiunga na CCM na kupokelewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli wakati wa mkutano wa Halmashauri Kuu ya Taifa iliyofanyika ikulu, jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Kama hiyo haitoshi, Novemba 22 aliyekuwa kada wa Chadema, David Kafulila alikihama chama hicho na kutangaza kujiunga na CCM.
Siku mbili baadaye alikabidhiwa kadi ya CCM na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole katika mkutano wa kumnadi aliyekuwa mgombea wa udiwani wa chama hicho, Kata ya Mbweni jijini Dar es salaam.
Kafulila ambaye ni mume wa Mbunge wa Viti Maalumu wa Chadema, Jesca Kishoa aliwahi kuwa mwanachama wa chama hicho kisha kufukuzwa, baadaye akajiunga na NCCR- Mageuzi ambapo alifanikiwa kuwa Mbunge wa Kigoma Kusini mwaka 2010-2015 na baadaye kurudi tena Chadema 2016 kabla ya kuondoka kwa madai upinzani hauna nia ya kupambana na ufisadi.
Hata hivyo, Kishoa alipinga madai ya mumewe akimtaka kusema ukweli na kwamba sababu alizozisema sizo zilizomuondoa ndani ya chama hicho huku akiongeza kwamba mume wake hana msimamo.
Baada ya Kafulila, zamu ikaingia kwa aliyekuwa Mbunge wa Kinondoni Dar es Salaam kwa tiketi ya CUF, Maulid Mtulia alijiengua chama hicho na kutangaza kujiunga na CCM akidai kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli. Mtulia alisema amefikia uamuzi huo kwa kuwa mambo yote waliyoahidi tayari yanafanywa vizuri zaidi na CCM, hivyo ni vigumu kuwa mpinzani.
Kama hiyo haitoshi pia Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira naye ametangaza kujiunga na CCM katika mkutano wa Jumuiya ya Wanawake wa CCM (UWT) uliofanyika mjini Dodoma uliofunguliwa na Rais John Magufuli.
Mghwira aliyekuwa Mwenyekiti wa ACT Wazalendo aliteuliwa kuwa mkuu wa mkoa Juni 3, 2017 na kukabidhiwa ilani ya uchaguzi ya CCM, japo awali alisema ataendelea kuwa mwanachama wa chama chake cha awali.
Mbali na wanasiasa, wasanii nao hawakuwa nyuma kwani mwigizaji wa filamu Wema Sepetu naye alitangaza kukihama chama chake na kurudi CCM alikokuweko awali.
Mbunge aliyefunga kazi ni wa Jimbo la Siha, Godwin Ole Mollel Desemba 14, 2017 alitangaza kuihama Chadema na kujiunga na CCM.
Mbali na hamahama iliyoitikisa kambi ya upinzani, kushindwa vibaya kwenye uchaguzi mdogo wa madiwani kwa kupata kata moja kati ya kata 43 zilizokuwa zikishindaniwa Novemba 26, limekuwa pigo kubwa la kufungia mwaka.
Chadema iliambulia kata moja tu ya Ibighi iliyoko mkoani Mbeya, huku ikilalamikia vitendo vya ukatili kwenye kata walizodai kuwa na nguvu ya kushinda.
Ni kutokana na hatua hiyo, vyama vya upinzani vilivyo chini ya mwavuli wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na chama cha ACT Wazalendo wamesusia uchaguzi mdogo wa ubunge na udiwani utaofanyika Januari 13, 2018.
Japo kususia huko kumetafsiriwa na baadhi ya wachambuzi kuwa ni kukimbia ushindani, lakini pia kumepeleka ujumbe wa manyanyaso wanayodai kufanyiwa na chama tawala cha CCM.