Thursday, 19 October 2017

Wema Afunguka sababu za kutokwenda kumuona lissu Nairobi

Mrembo wa Tanzania na Kada wa Chadema Wema Sepetu ametoa ya Moyoni kwa nini hakwenda kumuona mapema Mbunge wa Singida Mashariki Tundu Lissu baada ya kupigwa risasi septemba 7 ni kwamba asingeweza kumuona akiwa kwenye maumivu.
Wema ameweka wazi maneno hayo kwenye ukurasa wake wa Instagram ikiwa ni baada ya dakika chache tangu kuachiwa kwa picha za kwanza za Mbunge huyo akiwa hospitali ya Nairobi nchini Kenya.
Wema ameandika "Kisichokuua kinakufanya uwe na nguvuz zaidi....Utarudi tena ukiwa na nguvu kuliko ulivyokuwa awali...Shujaa wetu. ... Picha hii imenifanya nipate hisia. Sasa naweza andaa safari ya Nairobi kuja kukuona.. Awali nisingeweza kuvumilia kukuona ukiwa kwenye maumivu".
Wema Sepetu ametajwa na Chama cha Chadema kama mmoja wa wahamasishaji aliyeweza kuhamasisha watu kutoa michango kwa ajili ya matibabu ya Mbunge Tundu Lissu aliyelazwa Hospitali ya Nairobi baada ya kupigwa risasi na watu wasiojulikana alipokuwa kwenye gari lake nje ya makazi yuke huko mjini Dodoma.

Beka Flavour : Siwezi kurudi yamoto band,,

Msanii wa Bongo Fleva, Beka Flavour amefunguka na kusema kuwa yeye kwa sasa hayupo tayari kurudi kwenye kundi la Yamoto Band na kudai ukweli ni kwamba kundi hili lilishakufa na kila msanii sasa anasimama kivyake.
Beka alisema hayo alipokuwa kwenye kipindi cha Planet bongo na kusema kuwa wakati wanaondoka kwenye kundi hilo hawakuwa na pesa zozote zile kwani enzi zao wakati wanafanya show mbalimbali walikuwa wanapewa fedha za matumizi tu na wao walipendekeza kwa uongozi fedha zinapopatikana wafanyiwe mambo kadhaa ikiwa pamoja na kujengewe nyumba.
"Mimi saizi ukisema nitoke kwenye uongozi wangu mpya nirudi Yamoto Band sidhani kama itawezekana unajua watu hawajui tu lile kundi ndiyo limeshakufa kwa sababu saizi kila msanii yupo na uongozi wake, sidhani kama wanaweza kukubaliana watoke walipo na kurudi kule" alisema Beka Flavour
Mbali na hilo msanii huyo aliweka wazi kuwa anafurahi kuona Aslay msanii ambaye alikuwa naye kwenye kundi moja na yeye saizi anakuwa ni kati ya wasanii wanaozungumziwa sana kwa kazi nzuri.
"Mimi nazidi kumuombea kwani mwenzangu saizi amekuwa ni kati ya wasanii ambao wanazungumziwa sana kutokana na kazi zake, lakini napenda kuwaambia Watanzania kuwa wasanii ambao tulikuwa tunaunda kundi la Yamoto Band Mungu alitupa kitu ndani yetu hivyo muda si mrefu mtakuja kuona haya nayosema kwani kila mmoja ana upekee wake katika kazi zake" alisisitiza Beka

Wednesday, 18 October 2017

Simbaye : sekta binafsi Hali tete,,,,,

Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye
Mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bwana Godfrey Simbeye, amesema sekta binafsi sasa hivi zinapitia kwenye wakati mgumu kutokana na kodi ambazo TRA wameziweka, kitu ambacho kinaweka mazingira magumu ya kazi za uzalishaji.
Bwana Simbeye ameyasema hayo alipokuwa akizungumza kwenye kipindi cha East Africa Breakfast kinachorushwa na East Africa Radio, na kusema kwamba licha ya serikali kuweka jitihada zake za kuimarisha sekta hizo, lakini kumekuwa na changamoto kubwa inakuja kwenye utaratibu usiofaa wa ukasanyaji kodi.
“Serikali kwa juhudi zake imeendelea kutengeneza mazingira mazuri ya biashara, kama kurekebisha njia za usafirishaji ikiwemo reli na viwanja vya ndege, lakini suala la kodi limekuwa ni tatizo, malalamiko mengi ya sekta binafsi yanatoka kwa namna ambavyo TRA wanakusanya kodi, ni kero kubwa, imekuwa kwa mwezi mmoja taasisi binafsi inaweza ikatembelewa na timu ya TRA tatu na zote zikaja na makadirio tofauti, kwa hiyo hilo suala tunatakiwa tuliangalie”, amesema Bwana Simbeye.
Bwana Simbeye ameendelea kwa kusema kwamba changamoto nyingine ambazo sekta binafsi zinapitia kwenye kipindi hiki ambacho uwekezaji unakua, ni pamoja na kukosa mikopo, kutokana na hali ya mabenki ilivyo kwa sasa.
“Uwekezaji mpya unakua Tanzania, hata kwenye kituo cha uwekezaji project mpya zimeongeneka, lakini uwekezaji wa ndani bado haujakuwa sana kwa sababu hali ya kukopesha kwenye sekta binafsi bado haijawa nzuri, bado hatujaona dalili nzuri ya ukopeshaji wa mabenki kwenda sekta binafsi, ingawa serikali imekuwa ikiendelea kutoa dhamana ya serikali, lakini kwa upande wa sekta binafsi bado”, amesema Bwana Simbeye.

TAKUKURU Yawahoji Madiwani Waliojihuzulu CHADEMA

Maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kutoka makao makuu jijini Dar es Salaam, wamewahoji kwa zaidi ya saa sita, madiwani waliojiuzulu Chadema wanaotuhumiwa na Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari kuwa walipewa rushwa.
Waliofika Takukuru ni Catherine Mtui, aliyekuwa diwani wa viti maalumu, Japhet Jackson (aliyekuwa diwani wa Ambuleni) na Bryson Isangya (aliyekuwa diwani wa Maroroni). Baada ya kuhojiwa hawakutaka kuzungumza chochote wakisema wanaacha uchunguzi uendelee.
Pamoja nao, diwani wa Mbuguni, Ahimidiwe Rico anayedaiwa kuwa ndiye alirekodi sauti na picha wakati akishawishiwa na viongozi wa Serikali na wa Halmashauri ya Meru amehojiwa kwa zaidi ya saa tatu jana Jumanne Oktoba 17, 2017.
Rico amesema amewaeleza Takukuru kila kitu ambacho anakifahamu katika sakata hilo, ikiwemo kuwarekodi viongozi ambao walimshawishi kujiuzuru udiwani.
"Msimamo wangu ni kwamba, nachukia rushwa. Nimewaeleza kila kitu na wao waliniuliza kuhusu vifaa nilivyotumia kuwarekodi nikawaambia ni mali ya mbunge, alivitoa nchini Uingereza," alisema.
Rico aliyesindikizwa na diwani wa Nkwanankore, Wilson Nanyaro amesema ana imani na Takukuru kwamba watafanya uchunguzi wa kina na kuchukua hatua.
"Nimewaeleza wazi kuwa hata shauri hili likienda mahakamani nipo tayari kwenda kutoa ushahidi na kuthibitisha sauti za watu ambao niliwarekodi," alisema.
Alisema baada ya mahojiano yaliyoanza saa tatu hadi saa sita mchana, maofisa wa Takukuru walimwambia aondoke na watamuita watakapomuhitaji.
Hakuna ofisa wa Takukuru aliyekuwa tayari kuzungumzia mahojiano hao wakisema wasemaji ni makao makuu ya ofisi hiyo Dar yaliyoko jijini Dar es Salaam.

Kauli ya Lissu Baada ya kutoka ICU

Dar es Salaam. Kaka wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, Alute Mughwai ameeleza jinsi alivyomtoa mdogo wake chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) na kile ambacho alikisema mara tu baada ya kutoka ndani kwa mara ya kwanza.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano, Alute amesema Lissu mara baada ya kutoka si yeye pekee alifurahi hata ndugu zake waliokuwapo walifurahia tukio hilo.
“Manesi walipanga kumtoa nje Jumamosi (Oktoba 14) na kwa kuwa Lissu alijua tunakwenda, aliwaeleza wasimtoe wasubiri ndugu zake tufike, nilikuwa mimi na ndugu wengine,” amesema Alute
“Ilipofika saa 10 jioni tulimtoa na mimi ndiye nilimtoa ICU, alifurahi na sisi tulifurahi kwa hatua hiyo,” ameongeza
Mwananchi lilipotaka kujua, Lissu baada ya kutoka nje alisema nini, Alute amesema, “alifurahi kwa mara ya kwanza kupigwa jua, alisema ni sawa na ukiwa mfungwa huoni jua, mawingu wala hupigwi upepo ule wa kawaida.
Alute amesema Lissu alikaa nje karibu nusu saa kisha akarudishwa wodini ambako ameleeza ingawa si ICU lakini ina ulinzi na ungalizi wa karibu na si kila mtu anaweza kumwona.
“Kama alivyosema Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema- Freeman Mbowe) jana, anaendelea vizuri na ana akili ziko timamu.”
Kuhusu mchakato wa kumpeleka nje ya Nairobi ambao familia itahusika zaidi, Alute amesema: “Mimi nilikuwa Nairobi, ndiyo narudi nitatoa maelezo ya kipi kitafuata baada ya kuwasiliana na ndugu.”
Amesema ndugu wapo sehemu mbalimbali kama Kenya, Australia, Marekani, Canada ambao watabidi wajadiliane kwanza ndipo watatoa taarifa ya kinachoendelea.

Kipa avunjika Mguu Wakati akiokoa Gori

Mwishoni mwa wiki iliyopita katika mchezo wa Ligi Daraja la Pili (SDL) kati ya AFC Arusha na Kitayosce, kipa wa Kitayosce, Mussa Juma alikumbana na majeraha yaliyomsababishia kutolewa nje.
Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Ushirika na AFC kuibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na John Milinye dakika 47, kipa huyo aligongana na mchezaji wa AFC Dickson Kalinga katika harakati za kuokoa hatari iliyokuwa inaelekea langoni mwake.
“Baada ya kuona maumivu makali ndipo uongozi wa timu uliponiwahisha Hospitari ya KCMC kwa matibabu zaidi na hatimaye daktari kugundua nimepata tatizo kwenye mfupa mdogo wa mguu wa kulia,” alisema Juma.
Aliongeza kuwa kwa sasa haruhusiwi kufanya lolote na baada ya wiki mbili atatakiwa kwenda kutazamwa tena hospitalini na hapo ndipo atakapojua mustakabali wake wa kukaa nje kwenye soka.

Waziri Wa maliasili na utalii, Mh. Hamisi kigwangalla Atembelea Meli ya Mfalme Wa Oman

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Dkt.Hamisi Kigwangalla ames
ema Tanzania na Nchi ya Oman wamefanya mazungumzo ya pamoja ya namna ya kukuza sekta ya Utalii baina ya nchi hizo mbili ambapo watashirikiana katika muingiliano wa Watalii watakaokuwa wakitokea moja kwa moja Oman na kuja Tanzania.
“Tumeweza kuzungumzia ushirikiano wa sekta ya Utalii. Hii ni pamoja na kuanzisha soko la pamoja kati ya Oman na Tanzania. Watalii wanaokwenda Oman wanaotaka kuja nchi za Afrika basi waunganishwe moja kwa moja kutoka Oman na kuja Tanzania kwani wenzetu wana watalii wengi kuliko sisi. Hivyo ujio wao hapa nchini ni faida kubwa kabisa na tumejifunza mengi katika sekta hii.
"Pia tumeweza kujifunza namna wenzetu wanavyoitangaza nchi yao na sisi tutatumia uzoefu huo kuboresha sekta hii ya Utalii kama dhamana tuliyopewa” alieleza Dk. Kigwangalla.
Awali Dk. Kigwangalla aliweza kutembelea meli hiyo ya kifahari ya Mfalme wa Oman Mhe. Qaboos bin Said ‘Fulk Al Salamah’ iliyofika mapema jana Jijini Dar e Salaam ikiwa katika msafara wa kitaifa kati ya Serikali ya Oman na Tanzania.
Aidha, katika tukio hilo Mh. Waziri DK. Kigwangalla aliweza kuungana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Mama Samia Suluhu Hassan katika chakula cha mchana ndani ya Meli hiyo ya Mfalme wa Oman Mhe. Qaboos bin Said ijulinakanyo kama ‘Fulk Al Salamah’.
Meli hiyo ya kifahari ya Mfalme wa Oman Mhe. Qaboos bin Said ‘Fulk Al Salamah’ ipo nchini hadi Oktoba 21.2017. ambapo ipo nchini kusambaza ujumbe wa ‘Amani na upendo’ duniani ambapo ikitoka Tanzania inatarajia kuelekea Mombasa Kenya kwa madhumuni hayo hayo.

Hii hapa Orodha ya majina ya wanafunzi watakaopata mikopo ya HESLB

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru
Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema baada ya uchambuzi wa maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2017/2018, orodha ya awamu ya kwanza yenye wanafunzi 10,196 wa mwaka wa kwanza waliopangiwa mikopo imekamilika.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru katika taarifa kwa umma iliyotolewa leo Jumatano Oktoba 18,2017 amesema Sh34.6 bilioni zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi hao 10,196.
Amesema kwa jumla Sh108.8 bilioni zitatolewa kwa wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/2018.
Badru amesema orodha ya awamu ya kwanza inapatikana kwenye tovuti ya Bodi ya Mikopo http://www.heslb.go.tz/ na itatumwa kwa vyuo husika.
Amesema orodha nyingine (batches) zitafuata kwa kadri utaratibu wa udahili na uchambuzi unavyokamilika.
“Lengo ni kutoa majina ya wote waliofanikiwa kupata mkopo kabla ya vyuo kufunguliwa mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba, 2017,” amesema.
Mkurugenzi mtendaji huyo amesema orodha hiyo ya wanafunzi 10,196 imepatikana baada ya kupokea na kuchambua awamu ya kwanza ya majina ya wanafunzi 32,495 waliopata udahili katika chuo kimoja.
“Itakumbukwa kuwa moja ya sifa kuu za kupata mkopo ni mwombaji kupata udahili katika taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa na Serikali,” amesema.
Amesema wanafunzi waliopata udahili katika chuo zaidi ya kimoja na ambao wana sifa za kupata mikopo, watapangiwa mikopo baada ya kuchagua na kuthibitisha chuo watakachojiunga kwa ajili ya masomo.
Wakati huohuo, Badru amesema wanatarajia kuanza kutuma vyuoni fedha za mikopo ya wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao wamefaulu mitihani yao kuanzia leo Jumatano, Oktoba 18, 2017.
Amesema Sh318.6 bilioni zitatolewa kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo kwa mwaka 2017/2018.
“Tayari Serikali imeshatoa fedha hizo na lengo la Bodi ni kuhakikisha zinafika vyuoni kabla ya kufunguliwa kwa vyuo ili kuwaondolea wanafunzi usumbufu,” amesema.
Bodi imewasihi waombaji wa mikopo kuwa na subira wakati ikiendelea kukamilisha maandalizi ya orodha zinazofuata za wanafunzi waliopata mikopo. Hii hapa Orodha ya majina ya wanafunzi watakaopata mikopo ya HESLB

Breakfast news : Kocha Wa Simba ajiuzulu

Kocha Jackson Mayanja ameamua kuachana na klabu ya Simba nrejea kwao Uganda.
Mayanja ambaye bado yuko jijini Dar es Salaam, ameamua kuachana na Simba akidai ana matatizo yake binafsi.
“Ni matatizo ya kifamilia lakini suala hilo siwezi kulizungumzia kwa sasa,” alisema.
Lakini habari kutoka Simba zimeeleza kuwa sasa wako katika hatua za mwisho kuvunja mkataba wake baada ya kukubaliana naye kutokana na uamuzi wake huo.

Moto waacha wanafunzi bila nguo bwenini

PICHA HII HAIHUSIANI NA TUKIO LA KUUNGUA SHULE YA SEKONDARI YA NANDEMBO.
ZAIDI ya wanafunzi 70 wanaosoma katika Shule ya Sekondari ya Nandembo wilayani Tunduru Mkoa wa Ruvuma, wamekosa mahali pa kulala na kuhamishiwa eneo la kanisa, baada ya moto kuteketeza bweni lao.
Wanafunzi hao walinusurika kifo kutokana na kuwa darasani moto huo ulipoanza kuwaka Jumatatu.
Moto huo uliunguza na kuteketeza madaftari, nguo, mashuka na mali nyingine za wanafunzi.
Mashuhuda walisema bweni hilo walilokuwa wakilala wanafunzi wa kiume wa kidato cha kwanza na kidato cha nne lililipuka moto kati ya saa 1:30 na saa 2: 00 usiku.
Mkuu wa shule hiyo, Mary Ndunguru, alisema baada ya kuzuka kwa moto huo, walimu walishirikiana na wanafunzi kuuzima moto huo bila mafanikio.
Alisema wakati wa tukio hilo, wanafunzi walikuwa wakiendelea na masomo ya jioni katika madarasa yaliyopo zaidi ya mita 200, hivyo kuchelewa kubaini kilichokuwa kinaendelea.
Ndunguru alieleza baada ya kuudhibiti moto na kubaini kutokuwapo uwezekano wa wanafunzi kuendelea kulala katika bweni hilo, aliwasiliana na viongozi wa Kanisa Katoliki kijijini hapo na kuomba wanafunzi waende kulala eneo la kanisa kwa muda wakati uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ukiendelea na juhudi za kutafuta ufumbuzi wa kuwajengea bweni lingine.
Kaimu Ofisa Elimu wa Shule za Sekondari wilayani Tunduru, Habiba Mfaume, alisema takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya wanafunzi 72 walikuwa wanalala katika bweni hilo na hakuna aliyepata madhara.
Alisema amemuagiza mkuu wa shule hiyo kuwaita wazazi wote katika kikao kilichopangwa kufanyika kesho, ili kuomba msaada wa awali kwao na kila mzazi ajitahidi kufika na nguo zitakazosaidia kuwasitiri watoto wao katika kipindi hicho cha mpito.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Chiza Marando, alisema ili kuwasaidia wanafuzni wanaojiandaa kufanya mitihani ya kuhitimu masomo ya kidato cha nne inayotarajiwa kuanza Oktoba 30 mwaka huu, ameshawatuma wataalamu kupitia masomo yote waliyosoma, ili kuwasaidia kuwatolea nakala wanafunzi wote kuwasaidia waendelee kujisomea.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru ambaye ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, Kaimu Ofisa Tawala wa wilaya hiyo, Agustino Maneno, alisema amemuagiza Kamanda wa Polisi wa wilaya hiyo kupeleka wataalamu wake kupeleleza chanzo cha moto huo.

Askari Aliyekuwa Akifanya Mapenzi na Mfungwa Ajinyonga.....

Askari mmoja wa Chuo cha Mafunzo ya Wafungwa cha Losperfontein, nchini Afrika Kusini amejinyonga hadi kufa mara baada ya kuzagaa kwa picha zilizomwonyesha akimpiga busu mfungwa kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii .
Taarifa iliyotolewa na Idara ya Magereza nchini humo imesema kuwa ilifahamishwa kuhusu picha zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na kwamba wakati wanafanya uchunguzi wa tukio hilo, tayari ofisa huyo alikuwa ameshajinyonga.
Aidha, Kamishna wa Magereza wa Limpopo‚ Mandla Mkabela amesema katika taarifa yao kwamba wameshtushwa sana na wamehuzunishwa mno na tukio hilo la kujinyonga kwa Askari huyo.
“Tumetuma timu ya mameneja waandamizi na wataalamu wa mpango wa ushauri kwa wafanyakazi kwa ajili ya kutoa msaada wowote muhimu,” amesema Mkabela.
Hata hivyo, Mkabela amelaani tukio la usambazaji wa picha zinazodaiwa kuwa ni za ofisa huyo ambazo zimeweza kumsababishia kuchukua maamuzi ya kujinyonga.

Moto Waendelea kuwaka CCM

Wakati Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole akiwataka wakuu wa wilaya nchini kuwa na hekima ya kuridhika na vyeo walivyonavyo moto umeendelea kuwaka ndani ya chama hicho, baadhi ya makada na wachambuzi wa siasa kukosoa pendekezo lake la wagombea kuwa wakazi wa majimbo husika.
Wiki iliyopita, Polepole alisema katika kipindi cha redio Times kuwa wanachama wanaotaka kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM 2020, sasa watalazimika kuwa wakazi wa eneo wanalotaka kuliwakilisha, sharti ambalo linaweza kuwaondoa takriban nusu ya wabunge wa sasa.
Tamko hilo la Polepole lilizua mjadala mzito jambo lililosababisha Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM Organaizesheni, Pereira Silima alitoa taarifa kueleza kuwa hakuna mahali popote katika mabadiliko ya katiba yao palipoandikwa kuwa wagombea wa udiwani na ubunge watajadiliwa kwa sifa ya kuishi jimboni.
Ukiacha hilo juzi usiku katika kipindi cha ‘Tuambie’ kinachorushwa na televisheni ya TBC, Polepole alizungumzia suala jingine la kuwa kanuni za uchaguzi haziwakatazi wakuu wa wilaya kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wa Taifa wa CCM, wanapaswa kuwa na hekima.
Kauli ya Polepole imekuja wakati tayari kukiwa na wakuu wa wilaya wanne, mkuu wa mkoa na makatibu tawala walioshinda katika chaguzi za chama hicho zilizofanyika hivi karibuni.
Walioshinda ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Halima Dendego ambaye aligombea ujumbe wa mkutano mkuu wa CCM baada ya kupata kura 311.
Mwingine ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Nanyumbu, Salum Palango aliyepata kura 295.
Wakuu wa wilaya walioshinda ni Simon Odunga (Chemba) aliyeshinda kwa kura 432, Christina Mndeme (Dodoma) na Elizabeth Kitundu (Bahi) wote kutoka mkoani Dodoma.
Mkoani Morogoro, walioshinda ni Alhaji Mohamed Utaly (Mvomero) na Seriel Nchembe (Gairo).
Wakuu wengine wa wilaya walioshinda ni Raymond Mushi (Babati) mkoani Manyara, Herman Kapufi (Geita), katibu tarafa wa Makuyuni (Arusha), Paul Kiteleki na mkuu wa Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Alexander Mnyeti.
“Ukienda kwenye kanuni za uchaguzi za 2017 fungu la 25: Nafasi ya uongozi ni kazi ya muda wote (inazitaja hapo), Mkutano Mkuu wa Taifa haujatajwa, lakini mkuu wa wilaya ni kiongozi wetu wa Serikali pia ni kiongozi wetu wa chama,” alisema Polepole na kuongeza:
Mkuu wa wilaya ni mjumbe wa kamati ya siasa ya wilaya ni mjumbe wa halmashauri kuu ya wilaya na ni mjumbe wa mkutano mkuu wa wilaya. Huyu pia ni kamisaa wa Serikali, ‘public officer’ anayefanya kazi zote za chama. Sasa nikasema hekima pale ituongoze, yaani mtu ujiongeze mwenyewe.”
Aliendelea kusema: “Kama wewe una dhamana zote hizi, kwa nini mkutano mkuu tusimwachie mwanachama mwingine asiye na dhama nyingine yeye ashiriki kwenye mkutano wa chama?”
Polepole aliyewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma mkoani Mara na baadaye Ubungo jijini Dar es Salaam alisema kwa sasa kuna wakuu wa wilaya wapatao 166 na kama wote wataomba nafasi hizo, watafurika kwenye nafasi za chama hicho.
“Kama wakuu wa wilaya wote watachukua kwa pamoja wako 166, zamani mkutano mkuu tulikuwa 2400 sasa hivi tumepunguza idadi tumekuwa 1,700, hao ni wanachama walioomba dhamana halafu kati ya hao 166 ni wakuu wa wilaya,” alisema Polepole na kuongeza:
“Upande wa pili ni hekima ya kuwa na kiasi. Wewe una nafasi kadhaa, hizi nafasi nyingine tumwachie mtu mwingine. Hiyo inakuja kutokana na maelekezo yetu kwenye fungu la 22 kwamba; mtu mmoja kofia moja. Ukiwa kiongozi una dhamana tayari basi hii nyingine waachie wengine nao waweke mawazo yao katika kupeleka mbele chama chetu.”
Mbunge wa Nzega Mjini(CCM), Hussein Bashe katika maoni yake alisema dhana ya ukazi imepitwa na wakati pamoja na kuwa inaenda kinyume na Katiba, kanuni na tamaduni za chama hicho.
“Nimeisikia kauli ya katibu wangu nadhani ni kauli ambayo inahitaji mjadala mpana, binafsi naamini chama chetu kina katiba, Kanuni na maadili. Utamaduni huu ndo msingi a chama chetu ambao unatuongoza,” alisema.
Bashe alisema dhana ya aina hiyo ikipewa fursa siku moja itakuja hoja ya kwamba anayetakiwa kugombea uchaguzi ni lazima awe mchaga, ikiwa hoja ya mkazi itakosa uhalali na nguvu kisiasa.
“Fursa aina hii ya mawazo ikipewa uhalali, siku moja hoja ya mkazi ikikosa uhalali na nguvu ipo siku tutatumia ukabila, ikiisha tutasema udini kwa kuwa ukiwa muislamu utayajua sana matatizo ya waislamu,” alisema.
Bashe alisema mbunge anayo majukumu yake nayo ni uwakilishi na kwamba, mbunge kuwa mkazi haiwezi kumfanya azifahamu shida za watu yapo mambo ya msingi ambayo yanatakiwa kutazwa.
“Je Mbunge ametimiza majukumu yake? Ametimiza ahadi zake? Amekuwa muwakilishi mzuri wa wananchi wake? Dhana hii binafsi naiona kama ni dhana ‘aoutdated’ (imepitwa na wakati),” alisema.
Alisema kuwa hoja ya mkazi haimfanyi mtu kuwa mwakilishi mzuri na ifahamike kwamba wabunge wengi wanafanya shughuli mbalimbali ikiwazo zao binafsi zinazosaidia maendeleo ya wananchi wake.
“Mwalimu Nyerere alitengeneza mifumo toka Tanu mpaka CCM ya kumuandaa kiongozi kuanzia Chipukizi, Yuth Legue.Haya ni maeneo ya majaribo na makosa
Alisisitiza kuwa zipo nafasi ambazo kiongozi hatakiwi kutoa kuli yenye Taswira ya kuwagawa watanzania kwa msingi wowote ule hata kama utakuwa na nia njema.
“Tumeona kauli ya Silima, ni kauli sahihi kabisa. Hivi karibuni kumekuwa na matamko controversial ambayo unajiuliza duh hivi Katibu Mkuu yupo wapi? Hata kama tunafanya reform, hii ni njia sahihi? Vitisho vimekuwa vingi sana,”alisema Bashe.
Alieleza kuwa CCM ni wanachama na wanachama
“Leo wana CCM wameanza kuwa wanyonge na hofu ya kukosa ari. Tumeanza kujenga tabaka la watawala na watawaliwa ndani ya chama, ni muhimu sana kila kiongozi aheshimu katiba na kupima kauli zetu,”.
Source: Mwananchi

Audio | Jygga Lo Ft. Becka Tittle – Hawaniwezi | Mp3 Download

Audio | Jygga Lo Ft. Becka Tittle – Hawaniwezi | Mp3 Download

https://hearthis.at/baraka-matara-junior-vu/jyyga-lo-ft-becka-tittle-hawaniwezi/download/