Thursday, 25 January 2018

Mwalimu akamatwa kwa kutumia lugha ya matusi kwenye mtandao


JESHI  la Polisi Mkoa wa Mwanza linamshikilia Mwalimu wa Shule ya Sekondari  Mkolani, Deogratius Kisandu, akidaiwa kutumia lugha ya matusi, kejeli na kudhalilisha katika ukurasa wake wa Facebook.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema  Kisandu alikamatwa jana baada ya kuwapo taarifa kuhusu kuonekana ujumbe wa matusi na lugha zisizofaa  katika ukurasa  wake ya Facebook.

Alisema walimfuatilia mtuhumiwa na kumkamata akiwa na simu yake ambayo huitumia kupeleka na kuandika matusi hayo kinyume na Sheria Namba 4 ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

“Polisi bado wanaendelea na  na mahojiano na upelelezi dhidi ya mtuhumiwa. Utakapokamilika atafikishwa mahakamani kwa mujibu wa sheria.

“Taarifa zinaonyesha kuwa mtuhumiwa amewahi kushtakiwa kwa makosa kama hayo kipindi cha nyuma,” alisema Kamanda Msangi.

Kamanda   amewataka  vijana wanaotumia mitandao ya  jamii kuacha kwa sababu  ni kosa kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015.

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, alisema alipokea  malalamiko kutoka kwa wananchi siku mbili zilizopita kuhusu lugha ya kudhalilisha, matusi na kejeli  inayotumiwa na Kisandu ambaye pia ni mtumishi wa umma, katika  ukurasa wake wa Facebook.

“Tumetumia siku mbili mpaka kumpata Kisandu. Mwanzoni nilifikiri labda haya mambo yanafanywa na mtu ambaye si raia wa Tanzania lakini katika mahojiano amekiri yeye ni Mtanzania.

“Kwa kweli lugha anayoitumia ni ya kudhalilisha, matusi na kejeli na haifai kutumiwa kutokana na utamaduni wetu,” alisema.

Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Kanda ya Ziwa,   Lawi Odiero, alisema sheria ipo na inakataza matumizi mabaya ya mitandao na  kwa kuwa kesi hiyo ipo polisi  atatoa ushirikiano unaohitajika kusaidia uchunguzi.

Akukumiwa Kwa kumwingilia mwanaume kinyume cha maumbile


Mahakama ya Mkoa wa Mwera imemuhukumu mshtakiwa Simai Khamis Salum mwenye umri wa miaka 30 mkaazi wa Uzini wilaya ya kati Mkoa wa Kusini Unguja baada ya kutiwa hatiani kwakosa lakumuingilia mwanamme mwenziwe kinyume na maumbile.
Imedaiwa Mahakamani hapo namuendesha mashtaka Rahima Kheir mbele ya hakimu Muhammed Ali Muhammed kwamba mnamo tarehe 2/3 /2015 huko Uzini bila ya ridhaa kwamakusudi amefanya kitendo hicho kwakijana mwenye umri wa miaka 20 jinalimehifadhiwa na kumsababishia maumivu makali huku akijua jambo hilo ni kosa kisheria.
Akisoma hukumu Hakimu Muhammed amesema Mahakama imeridhika na ushahidi uliotolewa kwa upande wa mashtaka na kumuona nimkosa wakosa hilo ndipo Mahakama hiyo ilipomtia hatiani kutumikia chuo cha mafunzo kwa muda wa miaka saba pamoja na kumlipa fidia mtendewa yashilingi Milioni mbili ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia kama hiyo.

Mawakili wa Sugu wajiondoa kwenye Kesi


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi-Mbeya, Michael Mteite, amegoma kujitoa katika kusikiliza kesi inayowakabili Mbunge Joseph Mbilinyi na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga.

Mapema leo Alhamisi Januari 25,2018 Sugu na Masonga waliwasilisha ombi mahakamani wakimkataa hakimu huyo wakitaka ajitoe kusikiliza kesi kwa maelezo kuwa hawana imani naye.

Hakimu Mteite amesema sababu zilizotolewa na akina Sugu hazipo kisheria na hazimfanyi kujitoa.

Baada ya hakimu kukataa kujitoa, mawakili Boniface Mwabukusi, Hekima Mwasipu na Sabina Yongo wanaowawakilisha washtakiwa walitangaza kujitoa katika shauri hilo.

Sugu, mwenzake wamkataa hakimu Sugu na Masonga wameiomba Mahakama kuwapatia wiki mbili za kutafuta mawakili wengine.

Hakimu Mteite ameahirisha kesi hadi Februari 2,2018 na ameamuru washtakiwa kurejeshwa rumande.

Vijana waigao tamaduni za wageni wawatia Aibu wa zanzibari


Kamati ya utamaduni  ya wilaya ya  Magharib B wachoshwa na Kadhia ya wanaojitia pamba za masikio kudharau utamaduni wao wa asili na kufuata tamaduni zakigeni wawataka wabadilike venginevyo Serikali ya Wilaya iondoe muhali na hali na kuwatia hatiani.
Hayo yamebainika kufuatia baadhi ya vijana kujiingiza katika dimbwi zito la kuiga tamaduni za kigeni ambapo kilio cha baadhi ya Wananchi wakisema.”Vijana tunakunasihini tukimuona mtu hajavaa nguo rasmin lazima ule mtu tumwite, tumuhoji na ipo haja hata yakufungiwa kuwa asifanye lile jambo kwasababu wanatupotosha mila zetu na silka za kizanzibari”
Nae Katibu mtendaji wa baraza la sanaa Zanzibar Omar Abdallah Adam amewataka wananchi kufuata tamaduni na silka zilizomo nchini.
“Vijana kwakeli wameingia katika dibwi ambalo mi silipendi nami ninawaonea huruma sana kwasababu wao ni nguvu kazi ta Taifa, kwamijibu wa tamaduni zetu Silka zetu na desturi zetu tuwe karibu na wazee wetu kuskiliza wanachokisema na wanachokitaka vile wanavyotufahamisha. Sasa bilisi huyu sijui katokea wapi”
Kwaupande wake Afisa mipango kutoka Magharib B Zawadi Daniel Yussuf Amewasisitiza vijana kuwa makini katika kuendeleza utamaduni wao ili kizazi kijacho kiwe na mwenendo mwema.

Lowassa uso kwa uso na Membe msibani



Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Awamu ya Nne, Bernard Membe wamekutaka katika msiba wa mama wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima.

Membe na Lowassa wamekutana leo Alhamisi Januari 25,2018 nyumbani kwa Askofu Gwajima, Salasala wilayani Kinondoni.

Wawili hao walijitosa katika kura ya maoni ya CCM kuwania kupitishwa na chama hicho tawala kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Katika mchakato huo jina la Lowassa lilikatwa mapema, huku Membe akiwa miongoni mwa wagombea watano waliopitishwa na Kamati Kuu ya CCM. Walishindwa na John Magufuli aliyepeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi huo na kuibuka na ushindi.

Ruth Basondole, mama mzazi wa Askofu Gwajima amefariki dunia akiwa na miaka 84

LIVE:Takribani Bilion 660 zimetolewa na Serikali kuboresha Jiji la Dar es salaam


Waziri Mwigulu asimamisha zoezi la utoaji wa hati za kusafiria (Passport)

Waziri Mwigulu asimamisha zoezi la utoaji wa hati za kusafiria (Passport

Tundu Lissu afunguka kutolewa risasi nyingine mwilini


Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akifanya mazoezi akiwa hospitalini nchini Ubelgiji. Picha na Maktaba

 Siku 35 baada ya Tundu Lissu kusema mwili wake bado una risasi moja baada ya kutolewa nyingine 15, jana mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema) amelieleza Mwananchi kuwa madaktari wamemtoa kipande cha risasi kilichokuwa mwilini mwake.

Hata hivyo, mwanasheria huyo mkuu wa Chadema, ambaye alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 akiwa ndani ya gari lililokuwa nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7 mwaka jana, alisema chuma hicho ni tofauti na risasi iliyonayo mwilini, ambayo alielezwa na madaktari wa Hospitali ya Nairobi, Kenya kuwa iko sehemu mbaya, lakini isipotolewa haiwezi kumdhuru.

“Leo (jana) madaktari wamenitoa kipande cha chuma katika sehemu ya makalio ambacho nilipokuwa Nairobi (Kenya) madaktari walikiona lakini kilikuwa ndani ya nyama wakashindwa kukitoa,” alisema Lissu kwa njia ya simu kutoka Ubelgiji ambako alipelekwa Januari 7 kwa ajili ya tiba ya mazoezi.

“Kipande hiki kilisogea na wamekitoa. Ni tofauti na ile risasi ambayo iko mwilini mwangu.”

Akieleza kiundani kuhusu hali yake, Lissu alisema anaendelea vizuri.

“Huu mkono wa kushoto ambao ulikuwa na tatizo, wameunyoosha na kuufanyia mazoezi kweli kweli na huu mguu wa kulia ambao ndio wenye tatizo, unaendelea vyema,” alisema.

“Huku ni mazoezi tu. Kwa siku nafanya mazoezi kwa saa nne, Naingia saa 3:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi, narudi tena saa 5:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana. Mwisho naingia mazoezini saa 8:00 mchana hadi saa 10:00 jioni. Hiyo ndiyo ratiba yangu kwa siku.”

Alisema katika mazoezi hayo anatumia magongo maalumu pamoja na kiti cha magurudumu.

“Mfano, huu mguu wa kulia natakiwa kuukanyagia kwa kilo 20 hadi 25 katika mzani na mimi nina kama kilo 90. Ninapoukanyagia ninaulizwa kama unauma, ikiwa sijasikia maumivu ina maana sijafanya kitu, kwa hiyo ni kazi kwelikweli,” alisema.

Kuhusu muda ambao anatakiwa kufanya mazoezi hayo mpaka atakaporejea katika hali yake ya kawaida, Lissu alisema bado hajajua.

“Ah bwana we, hapa madaktari wamegoma kunieleza hilo, lakini wameangalia katika maungio ya goti la mguu wa kulia kuna mfupa haujaunga vizuri, ni lini utaunga hilo sijajua,” alisema.

Mara baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya siku hiyo usiku.

Desemba 21 mwaka jana wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam, Lissu alisema madaktari wa Nairobi walimueleza kuwa risasi iliyokuwa imesalia mwili haina madhara.

Alisema risasi saba zilitolewa na madaktari hao, jambo lililomaanisha kuwa risasi nyingine nane, zilitolewa na madaktari wa Tanzania, saa chache baada ya kushambuliwa alipofikishwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.   



Dk Kigwangalla kutaja majina wanaotuhumiwa kwa ujangili



Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla anatarajiwa kutaja hadharani majina ya watu wanaotuhumiwa kwa ujangili nchini.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Dk Kigwangalla amesema atazungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Januari 25,2018 mjini Dodoma kuelezea mambo yanayohusu wizara hiyo.

“Pia nitaweka hadharani watu mbalimbali wanaotuhumiwa kwa ujangili nchini,” ameandika Dk Kigwangalla.

Amesema tangu alipoteuliwa na Rais John Magufuli Oktoba 7,2017 kushika wadhifa huo, alijua kuna mambo mawili ambayo ni changamoto katika wizara hiyo.

 “Nilipoteuliwa nilijua kuna mawili, kujiunga na mtandao wa uovu ili nifaidike binafsi au kuukataa mtandao huu; nilijua kabisa mshahara wa dhambi ni mauti, na kwamba dhuluma haijawahi shinda vita dhidi ya haki, na wala uongo haujawahi shinda vita dhidi ya ukweli,” ameandika Dk Kigwangalla.

Nafasi za kazi leo Jan 25

Tausi Mdegela afunguka kuolewa Mke wa pili


Msanii wa filamu wa Tanzania mwenye muonekano wa kipekee na kipenzi cha watoto, Tausi Mdegela, ameutaarifu umma kuwa anatarajia kuolewa kuwa mke halali wa mpenzi wake wa siku nyingi ambaye ni msanii wa muziki wa taarabu, Prince Amigo.

Akizungumza na mwandishi wa www.eatv.tv Tausi amesema suala la ndoa ni mipango lakini ni jambo ambalo lipo, kwani tayari wamekuwa kwa muda mrefu kwenye mahusiano na mpenzi wake huyo ambaye ni mwanamuziki wa taarab, ambaye tayari ana mke wa kwanza.

“Ndoa ni mipango mtuombee Mungu tufike mbali, ni muda mrefu tumeanza tunaishi pamoja, ila Amigo ana mke mkubwa, kwa hiyo mimi nasubiria kuwa mke mdogo, hapa akiongezeka watatu ndio itakuwa mtihani, wawili tushatosha wengi wa nini, hapo ndo tutapigana sasa, na tukigundua kuna wa tatu hapo ndio litakuwa lingine, na mke mkubwa kashakubali”, amesema Tausi.

Tausi ameendelea kwa kusema kwamba yeye hajali maneno ya watu wanayosema kuhusu mahusiano yake hayo, kwani anachoangalia ni maisha yake na sio watu wanasema nini.


Daktari wa timu ya Olimpiki ahukumiwa kifungo


Larry Nasser daktari wa zamani wa timu ya Olympiki ya Marekani

Aliyekuwa daktari wa timu ya Olimpiki Larry Nasser amehukumiwa kwenda jela miaka 175 baada ya kukutwa na makosa ya ukatili wa kingono dhidi wananawake na wana michezo.

Katika kesi hiyo mashahidi 160 wamewasilisha ushahidi wao huku Nasser mwenyewe alikiri makosa kumi.

Alikuwa tayari akitumikia kifungo cha miaka 60 kutokana na kukutwa na hatia ya kumiliki picha ngono za watoto kinyume cha sheria.

Jaji Rosemary Aquilina ameiambia mahakama kuwa amejisikia fahari na furaha kubwa kutoa adhabu hiyo kutokana na kitendo alichofanya Nasser na kwamba anataka iwe fundisho kwa wengine.

'Nataka ukae jela maisha yako yote'. Hata hivyo baada ya hukumu hiyo mmoja wa waathirika amesisitiza kuwa washirika wa daktari huyo wanapaswa kushitakiwa pia.

Muda mfupi baada ya kutolewa hukumu hiyo, mkuu wa chuo kikuu cha jimbo la Michigan (MSU) alikokuwa anafanya kazi Nassar kati ya mwaka 1997 na 2016, amejiuzulu.

Bi Simon alikana taarifa kuwa MSU ilifahamu kuhusu tuhuma hizo za unyanyasaji lakini kilishindwa kuchukua hatua.

Katika taarifa yake alisema: "kwa waathiriwa, samahani yangu haiwezi kutosha, kuwa daktari aliyeaminika, aliyefahamika alikuwa ni mtu muovu kwa kweli, aliyewadhulumu kwa kutumia kigezo cha kuwatibu."

"Ushahidi wa wahanga wa unayanyasaji wa Nassar ni wa kusikitisha, kuvunja moyo na binafsi unaonitia kichefu chefu," aliongeza.

Takriban wasichana 140 wamewasilisha kesi dhidi ya Nassar, taasisi ya USA Gymnastics na chuo kikuu cha MSU, wakidai kuwa taasisi hizo mbili zilipokea tuhuma za unyanyasaji wa kingono dhidi ya daktarihuyo miaka kadhaa ya nyuma.

Taasisi hiyo ya michezo na chuo hicho zimekana kuwa kulikuwa na chochote cha kufichwa.

Hukumu ya Larry Naser inafuatia wiki ya ushuhuda kutoka kwa wanawake takribani mia moja na sitini, wakiwemo washindi wa medali ya dhahabu ya olympiki Biles, Aly Raisman, Gabby Douglas na McKayla Maroney

Arsene Wenger afunguka kuhusu Sanchez


Meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesema kwa sasa mambo ya usajili wa Alexis Sanchez yameshapita ndani ya timu hiyo.

Sanchez amekamilisha dili lake la kujiunga na Manchester United huku likimuhusisha Henrikh Mkhitaryan kuhamia Emirates mwanzoni mwa wiki hii.

Kufuatia ushindi dhidi ya Chelsea katika michuano ya Carabao Cup hapo jana siku ya Jumatano Wenger akizungumza na vyombo vya habari juu ya uhamisho wa Sanchez amesema kuwa “Tumepoteza mchezaji bora lakini kama timu kunahaja ya kuendelea nayale muhimu ili kutopoteza muelekeo wetu,” amesema Wenger.

“Kwa sasa tunafahamu tunapaswa kuendelea mbele sote kwa pamoja kujipatia muda.”

Kikosi cha Wenger kimefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano ya Carabao Cup na kutarajiwa kucheza na Manchester City baada ya kuifunga timu ya Chelsea hatua ya nusu fainali.