Sunday, 31 December 2017

BREAK NEWS; Askofu Kakobe azungumzia utajiri wake


Ikiwa yamebaki Masaa machache kabla ya mwaka 2017 kumalizika na kuukaribisha mwaka mpya wa 2018, Askofu Mkuu wa Makanisa ya Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe ameunguruma katika ibada aliyoiongoza Leo kanisani huku akijinasibu kuwa ni Tajiri kuliko Serikali zote duniani

 Askofu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Zacharia Kakobe amesema kwamba yeye sio tu Tajiri kuliko Serikali ya Tanzania, Bali ni Tajiri kuliko Serikali zote duniani ikiwemo ya Marekani na Uingereza'.

" Wanaosema Kakobe amekimbia nchi nawashangaa sana sipo na wala siendi popote, kipindi Fulani walikuja kuchunguza uraia wangu lakini wakaambulia patupu, tutabanana hapa hapa" Askofu Kakobe

" Watu wanasema Niko kimya sana wala sipo kimya tatizo wanataka nizungumze wanayoyataka wao, sasa Mimi sio mtu wa namna hiyo, ukiniona nimesimama katika madhabau Hays basi ujue nina kibali cha Mungu, mtu ukitwa Mbwa kwani wewe ndio itakua Mbwa? Sasa nashangaa unaogopa nini kuitwa Mbwa wakati wewe sio Mbwa" Askofu Kakobe



Dkt. Shika atangaza nia ya kuoa




Dkt. Louis Shika ambaye amejipatia umaarufu baada ya kutangaza dau la kununua nyumba za Lugumi, amefunguka na kutangaza nia ya kutaka kuoa endapo atapata mwanamke ambaye anamuhitaji.

Dkt. Shika amesema kuwa kwa sasa hana mpango wowote wa kurudiana na wanawake ambao amezaa nao watoto nchini Tanzania bali anatafuta mwanamke mwingine mpya ambaye atamuoa

"Nikimpata anayenihitaji na mimi nikamuhitaji nitaoa , saizi nipo tu kwanza nasubiri ila siyo kama sina mpenzi kwani wapenzi huwa hawakosekani mnakutana, mnapendana lakini mjue kuwa mpenzi na mke ni watu wawili tofauti. Siwezi kabisaa kurudiana na wazazi wenzangu kwani hicho kipindi kimepitwa na wakati saizi nataka mpya" alisema Dkt. Shika

Mbali na hilo Dkt. Shika amesema kuwa hawezi kuhama katika nyumba ambayo anaishi kwa kuwa anaishi bure kwenye nyumba hiyo hivyo ataondoka endapo atapata nyumba yake ila kuondoka na kwenda kupanga ni jambo ambalo hataliweza na kuwa hata huyo rafiki aliyempa nyumba hiyo atamshangaa.

Serikali yatoa maagizo kuhusu matumizi ya Fedha za kigeni



Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango ametoa maagizo kuhusu matumizi ya fedha za kigeni katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusisitiza kuwa utekelezaji wake uanze tarehe 1 Januari, 2018.

Maagizo hayo ni kama ifuatavyo: –

i. Bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. Bei hizi zinajumuisha kodi ya nyumba za kuishi na maofisi, bei ya ardhi, gharama za elimu na afya, bei za vyombo vya usafiri na vifaa vya kielektroniki.

ii. Bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Bei hizi zinajumuisha gharama za usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania, gharama za mizigo bandarini kwenda nchi za nje, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa wageni, na gharama za hoteli kwa watalii kutoka nje ya nchi. Walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni.

iii. Viwango vya kubadilishana fedha vitakavyotumika katika kuweka hizo bei katika sarafu mbili viwekwe wazi na visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni mabenki na maduka ya fedha za kigeni tu yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.

iv. Mkazi yeyote wa Tanzania asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yeyote hapa nchini kwa fedha za kigeni.

Aidha Dkt. Mpango ameviagiza vyombo vya dola viwachukulie hatua za kisheria wale wote watakaobainika kukiuka maagizo haya ya Serikali.



PPF wazungumzia kukamatwa kwa mfanyakazi wao na mirungi



MFUKO wa Pensheni wa PPF umesema mfanyakazi wake, Anitha Oswald, wa ofisi ndogo ya Moshi aliyekamatwa wiki hii akiwa na madawa ya kulevya aina ya mirungi huko Moshi, Kilimanjaro, alikuwa kwenye likizo ya dharura na kwamba alikamatwa akiwa kwenye gari lake binafsi na nje ya eneo la kazi.

Kwamujibu wa taarifa iliyotolewa na PPF vyombo vya habari na Meneja Uhusiano  leo, shirika hilo limesema tuhuma hizo zinamkabili mfanyakazi huyo yeye binafsi na si PPF.  Vilevile limelaani vitendo vya aina hiyo na linaunga mkono juhudi za serikali za kupiga vita madawa hayo.

Shirika pia limemchukulia hatua mfanyakazi huyo kwa kuzingatia sera za wafanyakazi wake.


TRA yatoa sababu ya Kakobe kuchunguzwa




Dar es Salaam. Kauli ya Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe kuwa ana fedha  nyingi kuliko Serikali imeiibua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo imetangaza kuanza mchakato wa kufuatilia ulipaji wake wa kodi.

TRA imesema uamuzi huo unatokana na kiongozi huyo wa kiroho kutokuwamo katika kumbukumbu za ulipaji kodi za mamlaka hiyo.

Na kama utajiri wake unatokana na sadaka pekee, Kamishna Mkuu wa TRA, Charles Kichere aliwaambia wanahabari jana kuwa hilo litakuwa jambo la kushtua.

Kanisa hilo kupitia kwa mtendaji kazi wake, Natus Mwita limesema litatoa ushirikiano kwa TRA japo hadi jana mchana lilikuwa halijapokea taarifa rasmi kuhusu kauli hiyo ya TRA.

Kauli ya TRA imetolewa siku tatu tangu kusambaa kwa picha za video zikimuonyesha Askofu Kakobe akiwa katika mahubiri kwenye kanisa lake lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam, akisema  kiwango cha fedha alichonacho si tu ni zaidi ya kile cha Serikali, bali pia anaweza kuwakopesha fedha hata mawaziri.

“Mimi sihitaji hela nina hela kuliko Serikali, si unaona shughuli yenyewe hii, sio pesa hii,” alihoji akionyesha waumini waliohudhuria ibada hiyo ambao nao walisikika wakijibu, “ni pesa.”

Alisema, “Nimewaambia waandishi wa habari hakuna wa kunihonga wala kunipa hela yoyote hata waziri akiwa hana hela aje kwangu nitamkopesha. Lakini neno  hili lazima litapelekwa vilevile lilivyo. Mtawala akifanya dhambi, atajulishwa dhambi yake, hapa umekengeuka, hapa si njia upasayo kuiendea, njia ya kuiendea ni hii.”

Kwa taarifa hiyo ya ukwasi wa Askofu Kakobe, Kamishna Kichere alisema mamlaka hiyo imeipokea kwa furaha na inataka kujiridhisha juu ya vyanzo vyake.

Alibainisha kuwa TRA inafahamu kuwa shughuli za kidini hazitozwi kodi lakini inataka kufahamu kama fedha hizo za Askofu Kakobe zinatokana na sadaka pekee au kuna shughuli nyingine za kiuchumi.

“Tumefuatilia hakuna kumbukumbu za Askofu Kakobe kulipa kodi, sasa tumeona tumfuate ili maofisa wetu wakajiridhishe kama fedha hizo anazozizungumzia zinatokana na sadaka,” alisema.

“Na kama hana shughuli zozote za kiuchumi ikiwa ina maana utajiri huo unatokana na sadaka ni jambo la kushtua kidogo lakini sisi tutaishia hapo.”

Alisema, katika taarifa za mamlaka hiyo wapo watu wengi wenye fedha nyingi na kumbukumbu zao za kodi zipo lakini Askofu Kakobe si miongoni mwao.

Alimwomba Askofu Kakobe kutoa ushirikiano kwa maofisa wa TRA watakaomtembelea kwa ajili ya ukaguzi.

Alipoulizwa kwa nini uhakiki ufanyike sasa na si miaka ya nyuma, Kichere alisema ni baada ya kusikia kwamba ana fedha nyingi kuliko Serikali wakati anafahamika kuwa ni kiongozi wa taasisi ya dini.

Askofu Kakobe alitoa kauli hiyo siku moja baada ya viongozi wengine wa dini kutumia mkesha na ibada ya Sikukuu ya Krismasi kuhimiza amani, upendo, kukemea maovu,  kushauri viongozi wa Serikali kukubali kushauriwa na kutominya uhuru wa watu kutoa maoni.

Wakati maoni ya viongozi hao wa dini akiwamo Askofu Kakobe yakigeuka kuwa mjadala, Serikali kupitia kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali mstaafu Projest Rwegasira ilitoa taarifa ikiwataka viongozi hao kutojihusisha na masuala ya siasa, bali wajikite kuzungumzia mambo yanayoendana na malengo ya kuanzishwa kwa taasisi zao, vinginevyo zitafutwa.

Meja Jenerali Rwegasira alisema viongozi wa dini wanapaswa kujikita kuzungumzia masuala ya dini yanayoendana na malengo ya kuanzishwa kwa taasisi zao na kuachana na ya kisiasa.

Alisema ukiukwaji wowote wa sheria ni kosa linaloweza kusababisha jumuiya husika kufutiwa usajili kama ilivyoelezwa kwenye kifungu cha 17 cha sheria husika.

Hata hivyo, juzi katibu mkuu huyo alisema viongozi hao wa dini wakiisifia Serikali au viongozi wake hawatakuwa wametenda kosa lolote.

Mbali na kuzungumza katika ibada hizo, baadhi ya viongozi hao walitumia mitandao ya kijamii kueleza mambo yanayofanana na hayo.

Miongoni mwao ni Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe mkoani Kagera, Benson Bagonza ambaye alitumia ukurasa wake wa mtandao wa Facebook kuhoji mipaka ya kuzungumzia masuala ya dini na siasa, huku akitaka wananchi kutojengewa hofu ya kutoa maoni yao.

Jana alipoulizwa kuhusu ujumbe mwingine alioutuma katika mtandao huo alisema, “Kwa hiki kinachoendelea sasa, suluhu ni kufanyika kwa mjadala wa kitaifa ili kuwekana sawa.

“Anayezuia watu kuzungumzia siasa huyu anayezuia atakuwa hana historia vizuri, wakati wa Bunge la Katiba, kulikuwa na wawakilishi wa dini tena na wapiga ramli walikuwemo. Kama walitambuliwa na kushirikishwa katika kuandaa Katiba inakuwaje useme tusizungumze siasa, kama tuliingizwa Bunge la Katiba kwa nini sasa tunazuiwa kuzungumza,” alihoji.

Alisema, “Amri za kibabe au nguvu kwa viongozi wa dini sidhani kama zinajenga. Kuna viongozi wa dini wanaona wanajua siasa kuliko wanasiasa na kuna wanasiasa wanaona wanajua dini kuliko viongozi wa dini, ndiyo maana nikasema mjadala wa kitaifa unahitajika.”

Kamishna wa Magereza azungumzia msongamano wa wafungwa



Mbeya. Kamishna Jenerali wa Magereza, Juma Malewa amesema jeshi hilo linakabiliwa na msongamano wa wafungwa kutokana na kuongezeka vitendo vya uhalifu na makosa ya kijinai.

Dk Malewa amesema hayo leo Jumapili Desemba 31,2017 katika Gereza Kuu la Mkoa wa Mbeya akiwa ziarani kukagua magereza na kuzungumza na askari wa jeshi hilo.

Amesema msongamano unatokana na majengo yanayotumika kuwahifadhi wafungwa ni yaliyojengwa enzi za mkoloni.

Hata hivyo, amesema wamejipanga kuendelea kuongeza idadi ya magereza kwa kila wilaya licha ya baadhi ya wananchi kutopendezewa na jambo hilo.

“Wakati tunapata Uhuru watu tulikuwa kama 10 milioni, hadi sasa majengo kama yameongezeka basi ni mawili lakini ni yaleyale; pia kuna makosa mapya ya uhalifu yameongeza ambayo zamani hayakuwepo,” amesema.

Amesema makosa ya dawa za kulevya na utakatishaji fedha yamejitokeza; huku mauaji yakiongezeka.

Pia, amesema msongamano unasababishwa na kesi zinavyoendeshwa mahakamani ambako zipo zinazochukua muda mrefu upelelezi kukamilika.

Wakati huohuo, Dk Malewa amesema katika kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kuongeza uzalishaji wa chakula kwa lengo la kujitegemea ifikapo mwaka 2022 wametenga magereza 10 yatakayotekeleza mpango wa uzalishaji.

Amesema chakula kitakachozalishwa kitatumika ndani ya magereza hayo na kulisha Taifa litakapokabiliwa na uhaba.

“Kwa sasa Jeshi la Magereza linaitegemea Serikali kwa asilimia 100 ilhali ina rasilimali watu ya kutosha kuzalisha chakula. Hivyo, tumeanza utekezaji kwa magereza 10 na lengo ni hadi kufika miaka mitano ijayo tuwe tunajitegemea kwa asilimia 100 bila Serikali,” alisema Dk Malewa.


Kanisa Katoliki yaitisha maandamano ya amani Kongo



Kuna wasi wasi wa kukosekana utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inayokabiliwa kwa sasa na mgogoro wa kisiasa kufuatia kanisa Katoliki lenye ushawishi mkubwa nchini humo kuitisha maandamano ya amani.

Kabila ambaye waandaaji wa maandamano hayo wanamtaka atamke wazi kuwa hatawania muhula wa tatu wa uongozi, amekuwa madarakani tangu mwaka 2001 wakati aliposhika madaraka ya urais baada ya baba yake Laurent Kabila kuuawa.

Kabila alikataa kujiuzulu bada ya kumalizika  kipindi chake cha pili na cha mwisho  Desemba 2016 hatua iliyosababisha maandamano pamoja na machafuko.

Tangu kipindi hicho maanadamano yamekuwa yakipigwa marufuku licha ya wakati mwingine waandamanaji kukiuka amri ya serikali na kuendelea na maandamano hali ambayo pia imekuwa ikisababisha umwagaji wa damu.

Hatua ya kanisa Katoliki kuitisha maandamano  ya leo Jumapili licha ya serikali kuyazuia yasifanyike inawafanya baadhi ya wachambuzi kuonya juu ya uwezekano wa kukosekana utulivu.

“Maandamano ya leo Jumapili nchini Kongo yanaweza kuwa makubwa zaidi kuliko yale ya mwaka jana” ameandika kupitia ukurasa wa twitter Jason Stearns  mchambuzi aliyebobea katika masuala ya siasa za Kongo kutoka chuo kikuu cha New York kinachohusika na mahusiano ya kimataifa.

Anasema vyama vyote vikubwa vya upinzani, asasi za kiraia, makundi ya vijana wanaharakati pamoja na kanisa Katoliki yanaunga mkono maandamano hayo ya leo Jumapili.

Uchaguzi ulipaswa kufanyika mwaka huu

Uchaguzi ulikuwa ufanyike mwishoni mwa mwaka huu chini ya makubaliano yaliyoasimamiwa na kanisa  katika juhudi za kuzuia machafuko kwenye  taifa hilo kubwa lenye utajiri wa madini ambalo halijawahi kushuhudia mabadilishano ya madaraka kwa njia ya amani tangu lijipazie uhuru wake kutoka Ubeligiji mwaka 1960.

Baada ya kuahilishwa mara kadhaa hasa kutokana na vurugu katika mkoa wa  Kasai  uchaguzi huo uliocheleweshwa sasa umepangwa kufanyika  Desemba 23, mwakani.

Kiasi ya makanisa 150 ya kanisa Katoliki yametoa mwito kwa waumini wao kuitikia wito wa kuandamana  leo Jumapili mjini Kinshasa  wakiwa na biblia mkononi ili kushinikiza kutekelezwa kwa makubaliano yaliyotiwa saini mwaka mmoja uliopita  yaliyokuwa na lengo la  kurejesha uthabiti nchini humo ikiwa ni pamoja na kumtaka Kabila kuondoka madarakani.

Si baraza la maaskofu nchini humo au mwakilishi wa serikali ya mjini Vatican  amezungumzia lolote kuhusiana na maandamano hayo.

Gavana wa mji huo Andre Kimbuta wenye watu milioni 10 amesema jana Jumamosi kuwa maandamano hayo  yasiyo na kibali hayawezi kuendelea kwa maelezo kuwa mji huo hauna maafisa wa polisi wa kutosha kusimamia maandamano  ya leo.

Hata hivyo msemaji wa waratibu wa maandamano  Leonie Kandolo alisisitiza kuwa licha ya kauli hiyo ya serikali maandamano ya leo yatafanyika na kuwa maafisa wa mji huo pamoja na polisi wanalazimika kutimiza wajibu wao kuwalinda raia na mali zao.

Waandaaji wa maanadamano  wametoa mwito kwa waumini kukusanyika baada ya misa ya asubuhi kwa ajili ya kushiriki maandamano leo.

Katiba ya Kongo inamzuia Kabila kuwania muhula wa tatu wa uongozi lakini makubaliano yaliyofikiwa yanamruhusu kusalia madarakani hadi uchaguzi mwingine utakapofanyika.

Nikki wa Pili afunguka kuhusu Muziki wa Hip Hop





Msanii wa Hip Hop kutoka Weusi Kampuni, Nikki wa Pili amesema muziki wa sasa wa Hip Hop ushindani wake upo kibiashara zaidi kwa kuangalia jinsi ya kuwakonga mashabiki jukwaani na namna ya msanii mwenyewe anavyoweza kujiweka kibiashara.

Nikki wa Pili amedai kuwa kinachoangaliwa kwa sasa ni kuuza bidhaa yako na bidhaa nzuri ndiyo inayouza sokoni kwa hiyo ndio muziki wa Hip Hop ya sasa ulivyo.

Akizungumzia ushindani wa Hip Hop ulivyo wa kibiashara, Nikki wa Pili amesema ni ushindani ambao Msanii mwenzako akitoa video kali na wewe unatoa video kali zaidi au akifanya show nzuri na wewe unafanya show kali zaidi yake. Msikilize Nikki wa Pili kwenye mahojiano yake na Bongo5 hapa chini


Nape azungumzia kupokewa wanaohama vyama



Dar es Salaam. Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amehoji sababu za vyama vya siasa kuhangaika kupokea wanachama wa vyama vingine, badala ya kushughulika na Watanzania wasio na vyama.

Akizungumza leo Jumapili Desemba 31,2017 katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Azam, Nape amesema siku zote amekuwa na msimamo tofauti na wanachama wanaovihama vyama vyao kwa maelezo kuwa unawajenga wanaohama, si vyama.

"Kama tunataka kujenga vyama viwe vya kitaasisi ni lazima kuhamahama lisiwe suala la kawaida. Yaani mtu mpaka anahama watu waseme kweli huyu alistahili kuhama," amesema Nape.

Amesema, "Watanzania wapo zaidi ya 50 milioni, wenye uwezo wa kujiunga na vyama kikatiba wanaweza kuwa zaidi ya 30 milioni, waliopo kwenye vyama wanaweza wasifike 10 milioni. Kwa nini tunakwenda kuhangaika na wanachama wa vyama vingine badala ya kushughulika na Watanzania wasio na vyama. Tushughulike kuwashawishi hawa."

Katika kipindi hicho, mwenyekiti wa kamati ya uongozi ya Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro na mwanahabari mkongwe, Dk Gideon Shoo waliungana na Nape kukosoa vitendo vya wanachama kuvihama vyama vyao.

Kwa mtazamo wao, hamahama ya wanasiasa ni miongoni mwa kasoro zilizojitokeza mwaka 2017.

"Bora wafute vyama vingi" - Mbowe



Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amefunguka na kusema kama Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na serikali haioni umuhimu na uwepo wa vyama vingi nchini watumie uwingi wao bungeni wavifute vyama hivyo.

Mbowe amesema hayo leo wakati akiongea na waandishi wa habari na kusema toka imeingia madarakani Serikali ya awamu ya tano watu wa upinzani wanaonekana ni maadui

"Tumemwambia Rais mara nyingi na chama chake kama wao wanaamini upinzani ni hasara kwa nchi na hawajaweza kuona faidi ya vyama vingi vya siasa, kama Chama Cha Mapinduzi hakijaona umuhimu vyama vingi vya siasa kwenye nchi hii kwa miaka 25 hii wana wingi wa kutosha bungeni ni bora wafute vyama vingi lakini ku pretend tupo kwenye vyama vingi wakati mnavikandamiza na kuvifunga mikono wakati nyinyi mnafanya siasa wenzenu wasifanye siasa" alisema Mbowe

Mbali na hilo Mbowe amesema kuwa kupitia chama chake cha CHADEMA kwa mwaka 2018 watakuwa na kazi ya kupigania mchakato wa Katiba Mpya pamoja Tume Huru ya Uchaguzi na kusema hilo wanaliweka wazi mapema ili ifahamike.



Msuva Arejea Nyumbani Kwa Mapumziko Baada Ya Kazi Nzuri Morocco



WINGA wa kimataifa wa Tanzania, Simon Happygod Msuva anatarajiwa kurejea nchini Alhamisi kwa mapumziko ya baada ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Morocco, maarufu kama Botola.

Akizungumza na Bin Zubeiry Sports – Online leo, Msuva amesema kwamba Ligi ya Morocco inakwenda mapumzikoni naye anarejea nyumbani kwa mapumziko na kujipanga kwa mzunguko wa pili.

“Natarajia kurudi nyumbani kuanzia Alhamisi kwa mapumziko ya baada ya mzunguko wa kwanza Ligi Kuu huku, na pia kujipanga kwa mzunguko wa pili kabla ya kurudi kambini,”amesema.

Msuva anaweza kuwa kwenye mapumziko marefu, kwa sababu michuano yote nchini Morocco sasa itasimama kupisha Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee zinazotarajiwa kuanza Januari 13 hadi Februari 4, mwakani.

Simon Msuva (kulia) amefunga mabao matano katika mechi 13 za ligi ya Morocco na ametoa pasi za mabao matatu

Msuva anarejea nyumbani akitoka kuifungia bao pekee Difaa Hassan El-Jadidi ikishinda 1-0 dhidi ya Hassania Agadir Ijumaa.

Msuva, mchezaji wa zamani wa Yanga alifunga bao hilo dakika ya 52 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa Ben Ahmed El Abdi mjini El Jadida, Mazghan nchini Morocco na sasa anafikisha mabao matano katika mechi 13 za ligi ya Morocco, akiwa pia ametoa pasi za mabao matatu.

Msuva anazidiwa mabao mawili mawili na Mehdi Naghmi wa Ittihad Tanger na Jalal Doudi wa Hassania Agadir wanaoongoza kwa mabao yao saba kila mmoja, wakifuiatiwa na Mouhcine Lajour wa Raja Casablanca mabao sita sawa na Bilal El Magri, Hamid Ahadad wote wa Difaa Hassan El-Jadidi na Abderrahim Makran.

Mbali na Msuva aliyewahi pia kuchezea Moro United baada ya kupita akademi ya Azam FC, mwingine mwenye mabao matano ni Badr Kachani wa Hassania Agadir.

Ikumbukwe Msuva yupo katika msimu wake wa kwanza Difaa Hassan El-Jadidi baada ya kujiunga na timu hiyo kutoka Yanga SC ya Tanzania.


Mwaka Mpya wa 2018, Watanzania wakumbushwa kudumisha amani


Katika kuelekea mwaka Mpya wa 2018 watanzania wamekumbushwa kuenzi na kudumisha Mshikamano, Amani na Upendo hususani kwa makundi ya wasiojiweza, yatima na wazee kutokana na kwamba, vitendo hivyo vimeendelea kuwa mhimili na kichocheo muhimu katika kufikia Maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.

Haya yanajidhihirisha kwa vitendo baada ya kikosi cha Jeshi la wananchi 313 Monduli kufika katika kituo cha watoto yatima Global Cha Arusha ambapo kwa pamoja wameshiriki katika shughuli za usafi wa mazingira ya kituo hicho, kufua shuka na mablanket ya watoto lakini pia kutoa msaada wa vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni Tatu na fedha taslimu shilingi laki tano ikiwa ni ishara ya Upendo kwa yatima hao .

Mkurugenzi wa kituo hicho Mack Donald Kavishe anasema ni kwa mara ya kwanza kupata ugeni kama huo na kuongeza kuwa kitendo cha kushiriki usafi na kutoa msaada huo ni tiba ya kisaikolojia kwa watoto hao ili wasijisikie upweke.

Baadhi ya msaada wa vitu vilivyokabidhiwa ni Sukari, mchele, mafuta ya kujipaka na kupikia, magodoro, chumvi, vifaa vya usafi, madaftari, unga na maharagwe.


Ajali mbaya ya Barabarani Kenya, Yaua watu 36 na wengine zaidi ya 11 kujeruhiwa



Watu 36 wamepoteza maisha na wengine 11 kujeruhiwa katika ajali mbaya ya barabarani nchini Kenya iliyotokea mapema usiku wa kuamkia leo.

Polisi wameeleza kuwa chanzo cha ajali hiyo ni basi la abiria ambalo lilikuwa linatokea Busia mpani na nchi yaUganda lililokuwa likielekea jijini Nairobi kugongana ana kwa ana lori lililokuwa linatokea mjini Nakuru.

Mkuu wa kitengo cha trafiki katika eneo la Bonde la Ufa, Zero Arijme, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo ambayo amesema ilitokea saa tisa alfajiri katika barabara kuu ya kutoka Nakuru kwenda mjini Eldoret.

Kwa mujibu wa jeshi la Polisi nchini Kenya wamesema mwezi wa Desemba pekee, watu zaidi 100 wamepoteza maisha katika ajali za barabarani zilizotokea katika barabara kuu ya Nakuru kuelekea Eldoret hali ambayo inaashiria hatari kuwa katika eneo hilo ambalo limekuwa sugu kwa kutokea ajali za mara kwa mara.