Tuesday, 26 December 2017

Ali Choki afunguka Sababu ya mashabiki kupungua kwenye maonyesho ya Muziki



MWANAMUZIKI nguli wa muziki wa dansi nchini, Ally Choky amesema kuwa kukaza kwa vyuma kumesababisha mashabiki wengi kutohudhuria kwenye maonyesho mbalimbali ya muziki.
Choky ambaye ni Mwanamuziki wa Bendi ya The African Stars ‘Twanga Pepeta’, amesema kwa sasa hali ni mbaya katika bendi karibu zote.
“Ukitaka kujua kuwa vyuma vimekaza, wewe angalia shoo nyingi hazina mashabiki kama zamani. Sisi kama Twanga Pepeta tunaendelea kupambana na hali yetu hadi kieleweke maana lazima maisha yaendelee na tuna imani mambo yatabadilika,” alisema Choky.

Aina Ya Virutubisha Vya Vyakula Kwa Mjamzito



Moja kati ya changamoto kubwa ambayo huwakumbuwa wajawazito wengi hata kupelekea watu hao kuweza kujifungua kwa operation ni pamoja na kutokuzingatia lishe ya mama mjamzito, hata hivyo kutokana na changamoto hiyo wengi wa wajawazito wamekuwa wakichagua vyakula vya kula huku wakisahau vile vyakula walivyoviacha ndivyo vinavyosababisha kukosa lishe kamili ifaayo kwa mama mjamzito.
Zifuatavyo na aina ya vyakula na virutubisho vifaavyo kwa mama mjamzito;
Protini
Protini katika chakula cha mama mjamzito inasaidia ukuaji wa tishu za mtoto, hiyo ni pamoja na ubongo pia hata ogani nyingine za mwili. Pia inasaidia matiti na tishu za tumbo la uzazi kukua wakati wa mimba, na pia inachangia usambazaji mzuri wa damu.
Mama anahitajika kula milo 2 hadi 3 kwa siku yenye vyakula vya protini kama vifuatavyo:-
Nyama ya ng’ombe ya steki.
Samaki wa maji baridi au maji chumvi.
Maini.
Nyama ya kondoo
Karanga
Jamii ya mikunde kama maharage.
Kalshamu (Calcium)
Mama mjamzito anahitaji madini ya kalshamu kama miligramu 1000 kwa siku. Madini ya kalshamu yanasaidia kurekebisha viwango vya majimaji mwilini, kujenga mifupa na meno ya mtoto aliye tumboni.
Vyakula vyenye madini haya ni kama:-
Mayai.
Maziwa
Jibini
Maharage meupe
Maharage ya soya
Samaki
Kabichi
Madini ya chuma
Madini ya chuma husaidia kuongeza kiwango cha damu mwilini na kukukinga na upungufu wa damu mwilini (Anemia).
Vyakula vyenye madini ya chuma ni kama vifuatavyo:-
Spinachi
Mchicha
Kabichi
Nyama
Maini
Nafaka zisizokobolewa
Samaki
Mayai
Folic acid
Folic acid acid hupatikana katika vyakula tunavyokula, hii husaidia kujengeka vizuri kwa ogani za mtoto na kumuepusha na ulemavu pamoja na tatizo linalojulikana kitaalam kama mgongo wazi au neural tube defect (NTD). Katika nchi zinazoendelea mara nyingi wajawazito huwa hawapati virutubisho hivi kwa kiasi cha kutosha katika vyakula, kwa hiyo kinamama wajawazito huongezewa virutubisho hivi kama vidonge vya folic acid wanapohudhuria kliniki.
Folic acid hupatikana katika vyakula kama:-
Kabichi
Spinachi
Machungwa
Papai
Limao
Embe
Nyanya
Zabibu
Tikiti
Nafaka
Mkate
Jamii za mikunde kama maharage
Vitamini C
Matunda na mbogamboga huwa na vitamini C kwa wingi. Vitamini C husaidia uponaji wa majeraha kwa haraka, husaidia meno na fizi na kujengeka kwa mifupa, pia husaidia mmeng’enyo.
Vyakula vyenye vitamini C ni kama:-
Machungwa
Limao
Nyanya
Zabibu
Pilipili
Embe
Mboga za majani
Tahadhari
Mama mjamzito anatakiwa kuhakikisha kuwa vyakula vyote hivi, lazima viandaliwe katika mazingira safi kuepuka athari kwa mama na mtoto. Vyakula vingine visipopikwa vizuri vyaweza kuwa na vimelea hatari vya magonjwa kama Salmonella na E coli pia aina nyinginezo za vimelea ambavyo vyaweza kuwa hatari kwa afya.
Mpango wa mazoezi
Mpango wa mazoezi ni muhimu kwa mama mjamzito kwa kuwa mazoezi husaidia maendeleo ya kiafya ya mama na mtoto aliye tumboni.Pia mazoezi humsaidia mama kuwa mwenye nguvu wakati wa kujifungua. Mazoezi ya kutembea huwafaa sana kina mama walio wajawazito. Lakini ni vyema kushauriana na daktari wako kabla ya kujihusisha na aina yeyote ya mazoez

Fahamu Madhara Ya Usukaji Wa Nywele Bandia Na Uvaaji Wa Mawigi



Katika karne ya sasa , uvaaji wa wigi umekuwa fasheni katika sekta ya urembo na hutumika hususan na wanawake. Ingawa uvaaji wa wigi huwafanya wanawake hao kuonekana ni walimbwende zaidi.
Wigi huvaliwa zaidi na kinamama wenye asili ya Afrika au Wamarekani wa asili ya Afrika. Lakini tukiangalia moja ya chimbuko hasa la uvaaji wigi ni ubaguzi uliokuwepo wakati wa utumwa ambapo wale wenye ngozi nyeupe na nywele shombeshombe walipewa kazi za ndani na wale wasio na ngozi nyeupe na nywele zisizo shombeshombe walifanyishwa kazi ngumu za mashambani.
Watumwa waliopelekwa barani Amerika hawakuweza kuzihudumia nywele zao kutokana na hali ngumu, na mabwenyenye waliwashusha hadhi na kuwavunja moyo kwa kuwaambia hawakuwa na nywele bali ni "manyoya".
Lakini sababu nyingine inayodhaniwa kuwaathiri wanawake wa asili ya Afrika ni fikra kuwa mwanamke mwenye nywele ndefu pengine hadi mgongoni ni mrembo zaidi. Pia siku hizi warembo na wanaoshiriki katika mashindano ya urembo hujaribu kurefusha nywele zao ili kuwa na viwango na aina za mitindo ya ughaibuni.
Pamoja na kuwa wanawake wanajaribu kuwa warembo kwa uvaaji wa wigi, zifuatazo ni baadhi ya hasara au madhara kiafya ya uvaaji wigi na usukaji wa nywele za bandia.
1. Uvaaji wa wigi au nywele za bandia waweza kukusababishia mzio(allergy), endapo malighafi au kemikali zilizotumika kutengeneza wigi hiyo zitasisimua mfumo wa kinga ya mwili wa mvaaji.
2. Kupata mba ni tatizo jingine kutokana na uvaaji wigi, hii hutokana na kukosekana kwa hewa ya kutosha ya Oksijeni katika ngozi ya kichwa(scalp hypoxia) na katika tishu za shina la nywele. Kwa hiyo kama utaamua kuvaa wigi uhakikishe imetengenezwa kwa viwango vya ubora unaotakiwa na inapitisha hewa ya kutosha ya Oksijeni.
3. Pia waweza kunyonyoka nywele hata kama una nywele nzuri zenye afya, na kama utachagua kuvaa wigi na unataka kuepuka madhara hakikisha kuwa nywele zako ni safi, usilazimishe kuvaa wigi iliyo ndogo na yenye kubana sana, hakikisha unapata muda wa kupata hewa na nywele zako zinapakwa mafuta kuepuka ukavu wa ngozi ya kichwa na nywele kukatika .
4. Maumivu ya kichwa ni tatizo ambalo laweza kusababishwa na uvaaji wigi au usukaji wa nywele bandia. Wigi iliyo ndogo husababisha mkandamizo kichwani na kusababisha maumivu ya kichwa ya mara kwa mara.
5. Upotevu wa muda na fedha ni dhahiri kwa kuwa ufumaji wa nywele za bandia waweza kuchukua muda mrefu, itamlazimu mvaaji wigi kubadili kwa kununua mpya kila baada ya muda fulani au kuwa na wigi nyingi kwa ajili kubadili kulingana na fasheni.
6. Harufu mbaya huweza kujitokeza endapo mba na jasho vitachanganyikana na hupelekea uwepo wa bakteria au fangasi na kusababisha muwasho mkali, hii yaweza kumkosesha raha mvaaji wigi na mwenye kufuma nywele za bandia hasa pale anapokuwa katika majumuiko ya kijamii.Kama utachagua kuvaa wigi hakikisha nywele zako zinasafishwa na shampoo au sabuni, zinakaushwa vizuri na kupakwa mafuta.
Endapo mwanamama atachagua kuvaa wigi,asisahau kuwa nywele zake za asili zinahitaji matunzo,na azingatie wakati wa kununua wigi au nywele za bandia, ahakikishe ananunua yenye ubora unaotakiwa ili kuepuka madhara ya kiafya anayoweza pata kutokana na uvaaji wigi au anapofuma nywele za bandia.

Kilimo Cha Maharage ya Njano



Kilimo cha maharage ni rahisi na kinalipa sana kikifanyika kwa utaalamu. Gharama nafuu na ushindani wa soko sio mkubwa sana. Huhitaji kusafiri, kinachofanyika ni kuwaita wateja waje shambani kwako na kuchukua mzigo.
Ekari moja ya maharage ya njano kwa maeneo mengi unaweza pata gunia kati ya 8 – 12 au zaidi ila inategemea na eneo unalolimia.
Shamba la maharage kama unalima kwa kumwagilia unaweza lima mara tatu kwa mwaka . Hii ina maana ukilima ekari moja tu utakua na uhakika wa kipato cha uhakika na kikubwa kila baada ya miezi minne.
 Upandaji wa Maharage
1.Mbegu.
Upandaji wa maharage unatakiwa ufanyike katika muda muafaka kutokana na eneo ili kuweza kupata maji ya kutosha (mvua) na wakati wa mavuno kunatakiwa kuwe na ukavu ili maharage yasiharibikie shambani.
Maji mengi yaliyotuama na ukame siyo nzuri kwa maharage na husababishia mmea magonjwa na kuoza au kukauka.
Kuna aina nyingi za maharage ambazo zinaweza kupandwa kwa mfano (Rojo, Mshindi, Pesa, SUA 90 na Canadian wonder) ambazo ni mbegu zilizoboreshwa, lakini pia kuna mbegu za kawaida zilizopo kwa wakulima ambazo huhimili
baadhi ya magonjwa na wadudu.
Inashauriwa kupanda maharage katika umbali wa (50×20) sentimita 50 (mstari kwa mstari) na sentimita 20 (mmea kwa mmea), panda mbegu mbili za maharage katika shimo moja, mbegu zinaweza kupandwa katika umbali wa sentimita 3-6 kwenda chini.
Kama mbegu moja moja katika kila shimo, nafasi itapungua. Kwa maharage yaliyokuwa vizuri kunatakiwa kuwe na idadi ya mimea 150,000-200,000 kwa hekta (maharage mafupi), maharage yatambaayo idadi yake ni nusu ya maharage mafupi kwa hecta. Hekta 1 = ekari 2.471.
2. Mbolea.
Mimea huhitaji virutubisho kutoka kwenye udongo ili kuweza kukua na kuzalisha matunda yenye afya. Maharage huhitaji madini ya ‘phosphorous’ na ‘potassium’ ambayo hupatikana kutoka kwenye mbolea hai kama vile samadi, mboji, majivu, mkojo wa mifugo na mabaki ya mimea.
Ni muhimu kufahamu udongo ambao unatarajia kupanda mimea yako ili kutathmini viwango vya madini yaliyopungua ili kufanya juhudi za kuongeza.
Zaidi ya yote ni vizuri kutumia mbolea hai ambazo zinasaidia viumbe hai huweza kukua na kuendeleza kurutubisha udongo, kwa mfano mizizi ya maharage husaidiana na viumbe hai (nitrogen fixing bacteria) waishio kwenye udongo kutengeneza nitrogen. Mbolea za chumvichumvi huharibu na kufukuza viumbe hai kutoka kwenye udongo.
3.Magugu.
Inashauriwa kupalilia mimea kabla haijatoa maua. Shughuli hii inatakiwa ifanywe kwa uangalifu ili kukinga mimea isiharibike kwenye mizizi kwani uharibifu wa aina yoyote huweza kusababisha magonjwa kwa mmea.
Inashauriwa kupanda mimea kwa kuzunguka (crop rotation) ili kupunguza uwezekano wa magugu na maradhi kuweza kushambulia
mimea.
4.Wadudu na magonjwa.
Maharage hushambuliwa na wadudu na magonjwa. Miongoni mwa njia za kuzuia, kukinga na kufukuza wadudu ni kuhakikisha kuwa mimea ipo katika hali nzuri (imepaliliwa, nafasi ya kutosha na haijaharibika).
Pia kubadilisha aina ya mimea inayopandwa kwenye shamba moja mara kwa mara husaidia kupunguza uwezekano wa wadudu kuongezeka. Kwa baadhi ya wadudu kama vile viwavi (African Ballworm) huweza kufukuzwa kwa kutumia muarobaini au vitunguu saumu.
Maji ya muarobaini ni dawa nzuri sana kwaajili ya kufukuzia wadudu na haina madhara yoyote kwa binadamu.
5.Kukomaa na Kuvuna.
Maharage ya kijani yanatakiwa yavunwe kabla punje za maharage hazijakuwa sana. Hii ni kati ya wiki 7-8 baada ya kupanda. Maharage makavu huvunwa mara tu kiasi cha kuridhisha cha kukomaa na kukauka kinapokuwa kimefikiwa.
Kwa mfano asilimia 80 ya maharage yakishakomaa na kuanza kubadilika rangi (kukauka) au kwa aina nyingine kusinyaa yanakuwa tayari kwa mavuno.
Kwa kawaida mmea wote hung’olewa na kuwekwa juani ili uendelee kukauka kisha maharage hutolewa kutoka kwenye mmea na kuendelea kukaushwa ili kupunguza matatizo wakati wa kuhifadhi.
Baada ya kukauka hadi kufikia angalaua asilimia 12 ya unyevu, maharage yanatakiwa yahifadhiwe kwenye chombo chenye mfuniko kama vile ndoo ya plastiki au pipa na kuendelea kuyaangalia mara kwa mara ili kuhakikisha kuwa wadudu hawajaingia na kisha kuyafunika tena.
6. Kilimo mchanganyiko.
Ni vizuri sana na inashauriwa kupanda maharage pamoja na mimea ya jamii nyingine kama vile mahindi kwani husaidia katika kusambaza madini ya nitrogen na kwa maharage yenye kutambaa, hupata sehemu ya kujishikilia au kutambalia.
Maharage yanaweza yakapandwa katikati ya mistari ya mahindi. Pia viazi huweza kupandwa pamoja na maharage. Inashauriwa kutokupanda maharage pamoja na mimea mingine ya jamii ya maharage (leguminous) kwani husababisha mimea isiweze kukua vizuri kwasababu ya kutokupata virutubisho vya kutosha na huweza kusababisha matatizo kama ya wadudu kama nzi weupe.

Tabia ya kuzoeana. inavyoweza kuathiri maisha yako ya kimahusiano



kuzoeana baina ya wanandoa ni jambo zuri, kwa maana ya kila mmoja kumfahamu mwenzake, lakini kuzoeana huku kunaweza kuzalisha dharau hususani kwa upande wa mwanamke kwa kutojali usafi wake, mavazi anayovaa, chakula anchopika, nidhamu ya nyumba na mpangilio kwa ujumla.
Matatizo mengi ndani ya nyumba yanaweza kusababishwa na moja au baadhi ya tabia hizo, ambazo huenda ikawa hazitokani na dharau, bali kuzoeana, kwa mfano, siku za mwanzo wa ndoa mwanamke huwa anajali sana usafi wa mwili wake, umaridadi wa nguo anazovaa, usafi wa nyumba na nidhamu ya hali ya juu, upishi wa chakula unaozingatia vionjo na ubunifu, mapokezi yenye bashasha na wakati mwingine hata kumkumbatia mumewe arudipo kutoka kazini.
Lakini baada ya kuzoeana yote hayo hubadilika, mwanamke huhisi kuwa hana jipya la kumuonyesha mumewe, hujiona wameishakuwa watu wazima sasa, na mara nyingi utakuta mwanamke huyu anashinda na sare (uniform) moja kuanzia asubuhi hadi anapopanda kitandani usiku, mambo ya Hinna, nguo za fashion, salon, manukato, kujipamba na dhahabu huyafanya pale anapotoka kwenda harusini na sio nyumbani. Huku ndio kuzoena, na tafsiri sahihi ni kudharau.
Hivyo ili kulinda kibarua cha chako cha mahusiano ni vyema ukajifunza kila wakati kutofanya vitu ambavyo vimekuwa havijayajengi mahusiano yako.

Monday, 25 December 2017

Lukuvi, Ummy Mwalimu watajwa tena



Siku 6 kabla ya kufunga mwaka 2017, wasomaji na wafuatiliaji wa habari kupitia mitandao ya kijamii ya Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), wametoa maoni wakiwataja mawaziri watano wa Serikali waliofanya vizuri katika maeneo wanayoyasimamia.
Wametoa maoni hayo takriban wiki moja baada ya gazeti hili kufanya tathmini ya utendaji wa mawaziri watano. Katika orodha hiyo, mawaziri wawili wameingia katika makundi yote mawili ambao ni William Lukuvi wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Ummy Mwalimu anayeisimamia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Wazee na Watoto.
Wananchi wametoa maoni hayo kupitia swali lililoulizwa kwenye akaunti za MCL za mitandao ya kijamii za Instagram, Facebook na Twitter.
Swali hilo lililoambatana na picha ya Rais John Magufuli akiongoza kikao cha Baraza la Mawaziri lililisema, “Ni waziri gani katika Serikali ya Rais Magufuli ambaye amekuvutia kwa utendaji wake mwaka huu? Kwa nini? Toa maoni yako.”
Mbali ya Lukuvi na Ummy, mawaziri wengine waliotajwa kufanya vizuri kwa maoni ya wasomaji hao ni; Selemani Jafo (Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa); Dk Hamisi Kigwangalla (Maliasili na Utalii) na Profesa Makame Mbarawa (Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano).
Kwa maoni yao, Lukuvi ndiye anayeongoza akifuatiwa na Jafo, Dk Kigwangalla, Ummy na Profesa Makame.
Hadi jana jioni, Lukuvi alikuwa akiongoza katika mitandao yote ya Instagram, Facebook na Twitter akimwagiwa sifa na wasomaji zaidi ya 100.
Katika gazeti hili toleo la Desemba 16, mawaziri waliotajwa mbali ya Lukuvi na Ummy walikuwa, Angellah Kairuki wakati huo akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora na Utumishi), Profesa Palamagamba Kabudi (Katiba na Sheria) na Profesa Joyce Ndalichako (Elimu, Sayansi na Teknolojia).
Ingawa waliotoa maoni kupitia mitandao ya kijamii ya MCL waliwataja mawaziri hao watano, wapo ambao walisema hawakufanya vyema.
Wengine waliwataja mawaziri vivuli kutoka kambi ya upinzani akiwamo Tundu Lissu wa Katiba na Sheria huku baadhi wakimtaja aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye aliyeng’olewa katika wadhifa huo Machi 23.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pia ametajwa kama kiongozi anayemudu nafasi yake vyema kwa kuwasimamia watendaji walio chini yake, wakiwamo mawaziri akielezewa kuwa mwaka huu ametimiza majukumu yake vyema.
Akichangia swali hilo, angwisa137 alisema, “Kuanzia mwakani tunatarajia makubwa mno kutoka kwa mawaziri. Watakuwa wamezijua wizara zao vizuri. Ila Lukuvi yuko vizuri mno. Hamisi Kigwangalla namkubali. Ila mawaziri waache kufanya kazi kwa mazoea tunahitaji mabadiliko ya kweli.”
Mwingine alikuwa maseleizengo ambaye alisema, “Waziri Lukuvi ni pekee amefanya kazi ya wanyonge... ameokoa viwanja vingi sana vya wanyonge vilivyokuwa vimeibwa na wenye fedha. utapeli wa ardhi umepungua sana.”
Mtoa maoni mwingine, mikeuswege alisema, “Lukuvi na Jafo ni wahalisia wengine walio wengi wanafanya kwa pressure.’’
Kwa maoni yake, Isaya Wa Yesu alisema, “Majaliwa ni Waziri Mkuu ambaye anajua kuyatumia mamlaka yake vizuri, Lukuvi amerudisha nidhamu kwa maofisa ardhi pia amewapa watu uhuru na amani ya kumiliki ardhi.”
Kareemgriff alisema, “Majaliwa, kubwa kabisa alivyotenganisha utendaji wake na masuala ya kichama, amekuwa si mwongeaji bali mtendaji.”
Katika maoni yake Julius S. Bugarika alisema, “Sauti ya watu wengi ni sauti ya Mungu. Lukuvi comment (maoni) nyingi zinaukubali utendaji wake. Waziri aliyefanya vizuri kiutendaji mwaka 2017 ni William Lukuvi.”
Mtoa maoni mwingine, witnessselestin alisema, “Mh. Lukuvi sababu ametafuna mifupa mingi na migumu iliyowashinda watangulizi wake na waheshimiwa wengine waige kutoka kwake huku edo_de__best akisema ‘’Makame Mbarawa naona anasimamia vizuri taaluma yake.”
Mwingine alikuwa meshackkwila ambaye alisema, “Mh Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu ni mtu mwenye busara anaongea kwa kufikiri sana naweza kusema ni kiongozi bora wa kuigwa.”
France Kavishe alisema, “Dah kwangu waziri aliyefanya vizuri na anayefanya vizuri awamu hii kwangu ni Mh. Dr @HKigwangalla.”
Mchangiaji mwingine, festosimkwayi_sr alisema, “Mheshimiwa Ummy Mwalimu anafanya mambo yake katika kulitumikia Taifa kwa uhakika bila papara wala mbwembwe. Hakika ni waziri wa afya anayetumia elimu na dhamana aliyopewa vyema.”
Akizungumzia maoni hayo ya wasomaji wa MCL, Lukuvi alisema, “Nimefurahi kuona wameridhika na utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano kupitia Wizara ya Ardhi, tutaendeleza ushirikiano huo.”
Waziri Lukuvi alisema moja ya jukumu alilopewa na Rais John Magufuli ni kuhakikisha anamaliza migogoro ya ardhi.
Alisema anafanikiwa kutokana na juhudi zake na ushirikiano anaoupata kutoka kwa watendaji wa wizara.
“Tuliacha watendaji wa Serikali huko nyuma wakatengeneza migogoro, hakuna mgogoro wa ardhi ambao hauhusiki na watendaji au viongozi wa Serikali. Nimeambiwa na Rais ndani ya miaka mitano hii jukumu kubwa liwe ni kutatua migogoro ya ardhi,” alisema Lukuvi.
Akizungumzia hilo, Waziri Ummy alianza kwa pongezi akisema, “Nashukuru kwa ‘feedback’ kutoka kwenu na kutoka kwa wananchi, nawashukuru sana! Hakika mnanitia moyo katika utendaji wangu.”
Alisema sekta ya afya bado inakabiliwa na changamoto nyingi lakini anachopenda kuwaahidi Watanzania ni kuendelea kupambana usiku na mchana ili kutatua changamoto kadhaa.
Waziri Ummy alizitaja changamoto hizo kuwa ni kuendelea kuboresha huduma za mama na mtoto ili kupunguza vifo vya wajawazito na uzazi na kuimarisha upatikanaji wa dawa muhimu katika ngazi zote za kutoa huduma na hasa ngazi ya msingi yaani zahanati na vituo vya afya.
Alitaja mikakati mingine kuwa ni pamoja na kuimarisha hospitali za rufaa za mikoa ili kuziwezesha kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa kuzipatia madaktari bingwa, vifaa na vifaa tiba lengo likiwa ni kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi na kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Jambo lingine ambalo alisema wizara yake itahakikisha inalifanya ni, “Kuongeza idadi ya Watanzania wanaojiunga katika mifuko ya bima ya afya ili kupata huduma za matibabu bila kikwazo cha fedha pindi wakiugua. Hivi sasa ni asilimia 32 tu ya Watanzania wamejiunga na mifuko ya bima ya afya. Ninaamini kwa mwaka 2018, sekta ya afya tutapata mafanikio makubwa,” alisema waziri Ummy.
Waziri Mbarawa akichangia swali hilo kwenye ukurasa wetu wa Twitter alindika ‘’Shukrani kwa wote tuendelee kushirikiana kwa maendeleo ya wananchi wote.”
Juhudi za kuwapata mawaziri wengine waliotajwa na wasomaji ambao ni Dk Kigwangalla na Jafo ziligonga mwamba kwa kuwa simu zao za mikononi ziliita pasipo kupokewa na wengine hazikupatika kabisa.

Hussein Bashe Aomba Radhi





Mbunge wa Nzega Mjini, kwa tiketi ya (CCM) Hussein Bashe amefunguka na kuwaomba radhi baadhi ya wananchi wa Nzega na Watanzania mbalimbali ambao kwa namna moja au nyingine amewakwaza mwaka huu katika utekelezaji wa majukumu yake.
Bashe amesema hayo kupitia mitandao yake ya kijamii ambapo anatuma salamu za heri ya sikukuu kwa wananchi na watanzania na kudai kuwa wamsamehe pale ambapo amewakosea katika utekelezaji wa majukumu yake ya kibunge.

DK. Shein atoa onyo Kali



Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, amewaonya wale waonadhani kuwa yeyeni mpole na kwamba hawezi kuwachukulia hatua viongozi wa serikali na chama wanaovunja nidhamu na kukiuka taratibu za utendaji.
Dk. Shein ambaye pia ni Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ametoa kauli hiyo mjini Zanzibar katika sherehe za kumpongeza baada ya kuchaguliwa tena kushika wadhifa wa Makamu Mwenyekiti wa CCM katika Mkutano Mkuu wa Tisa wa CCM uliofanyika mjini Dodoma hivi karibuni.
Amesema, kiongozi wa nchi anapaswa kutumia taratibu za uongozi na si kukurupuka kwa kuwaadhibu watu bila ya utaratibu.
Amesema yupo madhubuti na imara kwa kuwashughulikia wanaovunja nidhamu ya chama hicho na hatomuonea wala kumuadhibu mtu bila kufuata utaratibu wa maadili ya CCM .

Wizi Wa Miundombinu Ya Umeme, Wananchi Waiomba Tanesco Kukamilisha Fidia



Wananchi wa Kijiji cha Misigiri, Tarafa ya Ndago,Wilayani Iramba,Mkoani Singida wameliomba shirika la ugavi umeme Tanzania (TANESCO) kukamilisha malipo ya fidia kwa wananchi 17 wa Kijiji hicho ambao maeneo yao yamepitiwa na njia kuu ya umeme wa KV 400 kutoka Mkoani Iringa hadi Shinyanga ili waweze kuondoa chuki kati yao na shirika hilo na hivyo kuwa walinzi wakubwa wa miundombinu iliyowekwa kwenye njia hiyo.
Wananchi hao, Kanasi Peter, Boniface Nzenga, Mwita Wilson Makanga na Helena Yuda wamesema vitendo vya uharibifu na wizi wa miundombinu ya shirika hilo vinasababishwa na shirika hilo kutowalipa wananchi hao madai yao ya fidia kutokana na njia kubwa ya umeme kupita kwenye maeneo waliyokuwa wakilima na hivyo kuwafanya waendelee kufanya shughuli za uzalishajimali zilizokuwa zikiwaingizia kipato.
Malalamiko hayo yametolewa na wananchi wa Kijiji cha Misigiri,Tarafa ya Ndago wakati uongozi wa shirika la TANESCO ulipokwenda kutoa elimu kwa wananchi hao juu ya kushirikiana na shirika hilo kulinda wizi pamoja na uharibifu wa miundombinu ya shirika hilo.

Waziri Mpina aagiza kuvvunjwa mkataba Kati ya Ranchi ya Mzeri na Overland



Waziri wa mifugo na uvuvi Luhaga Mpina ameagiza kuvunjwa kwa mkataba kati ya ranchi ya Mzeri na Kampuni ya Overland ambayo ilianzisha kampuni ya OVENCO kutokana na kasoro mbalimbali zilizojitokeza na kutengenezwa mkataba mpya utakaozingatia maslahi ya taifa.
Agizo hilo amelitoa wakati wa ziara yake katika ranchi Mzeri iliyopo wilayani Handeni ambapo baada ya kupokea taarifa amebaini kutokamilika kwa uundwaji wa bodi kampuni OVENCO na kuiacha kampuni ya overland yenye 70% ya hisa kufanya shughuli zake bila usimamizi wa pamoja.
Anesena Mkataba uliopo ambao umedumu kwa zaidi ya miaka miwil uvunjwe ifikapo disemba 31 mwaka huu na kutengeneza mpya ambao utaainisha thamani ya uwekezaji na ukubwa wa eneo kulingana na mahitaji badala ya kuhodhi ardhi kubwa bila ya kuendelezwa
Aidha Waziri Mpina amesema pamoja na kasoro zilizopo kwenye mkataba wa uanzishwaji wa Ovenco ameridhishwa na juhudi za mwekezaji katika kuinua sekta ya mifugo na kwamba wakati mkataba mpya ukiandaliwa maslahi ya uwekezaji huyo yatalindwa
Akizungumzia hatua hiyo ya waziri meneja uzalishaji uendeshaji ranchi za taifa Bwire Kafumu amesema Narco itafanya uhakiki wa thamani halisi wa mali zilizopo na kuishauri serikali.
Kwa upande wake mkurugenzi wa kampuni ya overland Feisal edha amesema ameridhishwa na hatua ya waziri ambayoitatoa fursa na haki kwa pande zote

Muuza bangi aingia kimakosa ndani ya gari la polisi akidhani ni teksi



Mtu anayeshukiwa kuwa muuza madawa ya kulevya alijipa krismasi asiyoitaka wakati aliingia kwenye teksi akiwa na karibu misokoto 1000 ya bangi na kugundua kuwa alikuwa ameingi kwenye gari la polisi nchini Denmark.
Polisi nchini Denmak walisema kuwa mwanamume huyo alikuwa akirudi nyumbani wakati alifanya makosa hayo mabaya.
Makosa hayo yalitokea katika eneo la Christiana, wilaya moja ya mji mkuu Copenhagen iliyo maarfu kwa biashara ya madawa ya kulevya.
Polisi wanasema kuwa mwanamume huyo atafunguliwa mashtaka, Polisi walisema kuwa walifurahi kumuona, kwani alikuwa amebeba misokoto 1,000 ya bangi.
Bangi ni haramu nchini Denmark.
Polisi wamefanya uvamizi mara kadhaa katika wilaya ya Christiana miezi ya hivi karibuni waliwatafuta wauza madawa ya kulevya .

Yanga yavuka kizingiti kombe la FA



Klabu ya Soka ya Yanga imeweza kuibuka na ushindi wa bao 2-0 dhidi Reha FC inayoshiriki Ligi Daraja la Pili katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la FA mzunguko wa pili mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Mchezo huo ambao timu ya Reha ilianza kwa kushambulia upande wa wapinzani wao na kuwashika vilivyo kwani hadi dakika 45 zinamalizika hakuna timu ailiyofunga katika kipindi cha pili timu ya Yanga ikabadilika na kuanza kujaribu kupiga mashuti ambapo dakika ya 82 mchezaji Pius Buswita aliwapatia Yanga bao la kwanza lilodumu kwa dakika tatu na Amiss Tambwe aliweza kuongeza bao lingine lilowafanya kusonga mbele katika michuano hiyo.

Nuh Mziwanda Akanusha Kurudiana na Shilole



Staa wa Bongo fleva Naftal Mlawa ‘Nuh Mziwanda’, amefungukia tetesi za kurudiana na msanii mwenzake wa ambaye pia alikuwa mepenzi wake wa zamani kabla ya kila mtu kushika hamsini zake Zuwena Mohamed ‘Shilole’ kwa kuweka wazi kwamba hana wazo wala hisia zozote za kurudiana na msanii huyo kwa siku za hivi karibuni.
Akizungumzia stori hizo Nuh mziwanda alisema kwamba amekuwa akizisikia tetesi za uwepo wa penzi la chinichini kati yake na Shilole licha ya kwamba mwanamke huyo ni mke wa mtu.
“Siwezi kurudiana na Shilole hata iweje, mimi kurudiana na shilole ni stori tu ambazo watu wanazusha,ukweli siwezi kumrudia mtu huyo. Na sivutiwi kuzungumzia habari zake kwa sasa kwakuwa anamaisha yake ya ndoa takatifu, si vizuri kumwongelea kwa sasa. Siwezi kurudiana na Shishi” alisema Nuh Mziwanda