Monday, 11 December 2017

Papa Francis, Guterres watoa maoni uamuzi wa Trump juu ya Israel



Katibu mkuu wa umoja wa mataifa Antonio Guterres amesema hatua ya rais Trump kuutambua mji wa Jerusalem kama makao makuu ya Israel inaleta wasi wasi katika jitihada za kuleta amani katika mzozo wa Israel na Palestina.
Akizungumza na CNN Guterres ametoa msimamo huo siku ambayo pia msemaji wa makamu wa rais wa Marekani Mike Pence ameishutumu serikali ya Palestina.
Msemaji huyo ameongeza hakufurahiswa na kitendo cha rais wa Palestina Mahmoud Abbas kushindwa kukutana na kiongozi huyo wa Marekani kwa sababu ya mzozo wa mji wa Jerusalem.
Waandamanaji wameendelea kukusanyika mitaani katika nchi za Kiaarabu wakipinga hatua hiyo ya raia Trump.
Naye Papa Francis ambaye ni kiongozi wa kidini wa wakatoliki wapatao billion moja duniani ametoa maoni yake,akisema kuwa Jerusalem ni mji mtakatifu kwa wakristo,Wayahudi na Waislam.
Amesema ni mazungumzo pekee yanayoweza kuleta suluhu katika mzozo huo wa Irael na Palestina.

Sunday, 10 December 2017

Video ya Babu Seya yampiku Diamond kwenye Trending za Youtube



Siku moja baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli kutangaza msamaha wa kumwachia huru Mkongwe wa Muziki wa Dansi nchini Nguza Viking 'Babu Seya'  na mtoto wake Johnson Nguza 'Papii Kocha' video yao wakionekana wanatoka gerezani imeshika namba moja kwenye Trending za Youtube hivyo kuishusha video mpya ya Diamond.

Video ya wimbo mpya wa Diamond aliomshirikisha mkali kutoka Marekani, Rick Ross unaokwenda kwa jina la Waka ulikuwa ukikamata nafasi ya kwanza lakini tangu Mtandao wa Muungwana Blog kuiweka video ya Seya na Papii wakitoka gerezani imejikuta ikifunika video zote.

Babu Seya na mwanae Papii Kocha ni miongoni mwa wafungwa zaidi ya 8000 waliopata msamaha wa Rais Magufuli jana katika sikukuu ya Uhuru ikiwa ni baada ya kukaa gerezani kwa takribani miaka 14 ambapo walikuwa wakitumikia kifungo cha maisha jela.

TAZAMA FULL VIDEO HAPA CHINI....USISAHAU KUSUBSCRIBE

Mamia wauaga mwili wa Mwandishi wa Mwananchi



Mamia ya waombolezaji wamejitokeza kuaga mwili wa aliyekuwa mwandishi mwandamizi wa gazeti la Mwananchi, Joyce Mmasi.

Shughuli za kuaga mwili wa Joyce zimefanyika leo Jumapili Desemba 10,2017 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

Ibada ya kuaga mwili iliongozwa na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Mbezi Luis, Richard Lucas.

Mchungaji Lucas amesema maisha aliyoishi Joyce yawe fundisho kwa waliobaki duniani.

"Binadamu tuna maisha mafupi ya kuishi duniani. Joyce aliyakabidhi maisha yake kwa Yesu, hivyo hakuna shaka kuwa yuko mahali salama," amesema.

Akizungumza katika shughuli hiyo, Mhariri  Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Bakari Machumu kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji, Francis Nanai amesema Joyce alikuwa mwandishi wa habari lakini pia mjasiriamali.

"Hili ni fundisho kwetu kwamba tunahitaji kuishi maisha ya kujiongeza maana Mmasi alikuwa mwanachama mzuri wa Saccos ya Mwananchi na alitoa mawazo ambayo yamesaidia maendeleo ya Saccos na kampuni," amesema.

Baada ya mwili wa Joyce kuagwa umesafirishwa kuelekea kijijini kwao Mbokomu wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika kesho Jumatatu Desemba 11,2017.

Joyce alifariki dunia usiku wa kuamkia  Jumatano Desemba 6,2017 baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Andrew Kamugisha ambaye ni mume wa Joyce alisema mkewe alifariki saa kumi usiku katika Hospitali ya TMJ jijini Dar es Salaam alikokuwa amelazwa kwa matibabu.

Alisema Joyce aligundulika kuwa na saratani ya damu. Alisema kutokana na tatizo hilo, utengenezaji wa damu ikiwemo rojorojo lililoko katika mifupa (bone marrow) na hivyo kusababisha mfumo wa chembe hai kutofanya kazi inavyotakiwa.

Mwananchi

Peter Stoger aula kibarua cha kuinoa Dortmund



Klabu ya Borussia Dortmund leo tarehe 10 Novemba 2017, imeushangaza ulimwengu wa soka baada ya kutangaza kumfukuza kazi kocha wake, Peter Bosz na kumuajiri Peter Stöger.

Peter Bosz amepoteza michezo 12 tangu ajiunge na klabu hiyo na kitu pekee cha kushangaza ni kwamba Dortmund wamemuajili kocha ambaye ametimuliwa na klabu ya inayoshika mkia wa ligi kuu nchini Ujerumani Bundesliga.

Kuchaguliwa kwa Peter  Stöger kumezua gumzo kubwa nchini Ujerumani kwani wadau wengi wa soka wanasema Dortmund wamekosea kumsajili Kocha ambaye mwenye historia mbaya kwenye kufundisha timu za Ujerumani.

Peter Stoger amepoteza mechi 8 na kupata sare 3 kabla ya kutimuliwa na klabu ya FC Cologne ambayo inashika mkia kwenye msimamo wa Bundesliga. Ambapo imeelezwa kuwa ndio kocha wa kwanza kuanza vibaya kwenye tangu ligi hiyo ianzishwe.

Na hii inakuwa ni hatua ya kwanza kwenye historia ya Ligi kuu nchini Ujerumani kwa kocha mwenye karba hiyo kuajiliwa na klabu kubwa nchini humo.

Msuva kucheza dhidi ya Yanga Klabu Bingwa?




Utamu wa vita ni kumjua adui yako, Yanga inajiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoanza mwakani mmoja wa wapinzani wake katika kusaka taji hilo ni mshambuliaji wake wa zamani, Simon Msuva anayecheza Difaa El Jadidi ya Morocco.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) linataraji kutangaza ratiba ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho Afrika Jumatano ijayo Desemba 13 jijini Cairo, Misri kwa michuano hiyo itakayoanza mwanzoni mwa Februari na kumalizi Novemba mwakani bingwa atajinyakulia dola 2.5 milioni.

Yanga chini ya kocha, George Lwandamina imedhamiria kufanya vizuri katika michuano hiyo na tayari imeanza kufanya usajili wachezaji mbalimbali wa kimataifa ili kutimiza lengo hilo.

Mabingwa hao wa Tanzania Bara, Yanga itaanza Ligi ya Mabingwa hatua ya awali kama ilivyokuwa kwa Difaa El Jadidi inayoshiriki mashindano hayo kwa mara kwanza tangu 2010 ilipotolewa katika raundi ya kwanza.

Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani hatua ya makundi itashirikisha timu 16, zitakazogawanywa katika makundi manne, kutokana na mabadilino hayo Yanga inaweza kupata nafasi ya kucheza dhidi ya Msuva katika hatua ya awali, au raundi ya pili kama siyo hatua ya makundi.

Msuva amekuwa katika kiwango kizuri tangu Julai 28, 2017, alipotua Difaa El Jadidi akifanikiwa kufunga jumla ya mabao 15 katika mechi zote. Msuva amefunga mabao tisa katika mechi 13 za kirafiki, mabao mawili katika Kombe la Mfalme katika Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’ amefunga mabao 4, katika mechi 10.

Akizungumzia ratiba hiyo Msuva alisema sitamani tupangwe dhidi ya Yanga hata kidogo, lakini ikitokea hivyo nitawajibika kuipigania Difaa.

“Ukweli ni kwamba Yanga ni timu yangu, imenilea mpaka kufikia hatua ya kuhitajika na timu kadhaa kubwa barani Afrika, lakini Difaa nipo ni kazi si kingine.

“Pamoja na huku, lakini nimekuwa nikiwasiliana mara kwa mara na wachezaji wa Yanga, hii inaonyesha namna gani ambavyo bado ni kama nipo Yanga vile, ndiyo maana nikatangulia kusema sitamani tupangwe pamoja.

“Ila yote kwa yote ya uwanjani yatabakiwa kuwa ya uwanjani na sidhani kama yataharibu mahusiano yangu na Yanga, naipenda sana Yanga na itabaki kuwa timu yangu,” alisema Msuva.

Mbali ya Diffa El Jadidi timu nyingine zitakazokuwa kikwazo kwa Yanga katika kufuzu kwa hatua ya makundi pamoja na ubingwa ni mabingwa watetezi, Wydad Casablanca ya Morocco, mabingwa wa kihistoria Al-Ahly, na Misr Lel-Makkasa (zote za Misri).

Miamba mingine kiboko ya Yanga katika mashindano hayo ni Esperance de Tunis na Etoile du Sahel (Tunisia), kutoka DR Congo ni TP Mazembe na AS Vita Club wakati Algeria imetoa timu za ES Setif na MC Alger.

Afrika Kusini inawakilishwa na Bidvest Wits na Mamelodi Sundowns wakati Sudan watakuwa na timu za Al-Hilal, Al-Merrikh.

Naye kocha wa Yanga, Lwandamina akizungumza na gazeti dada la Mwanaspoti alisema: “Nimeziona hizo timu nazifahamu si kwa kubahatisha ni timu ngumu, lakini ubora wao zaidi unatokana na nguvu ya fedha wanayotumia kufanya maandalizi yaliyobora kabla ya mashindano.

“Najua tutashindana nao japo sijajua tutakutana na timu zipi ila katika maandalizi ni bora tukaangalia kwa ujumla washindani wetu, tunahitaji kuangalia upana na ubora wa kikosi chetu nafikiri hapa ndiyo kwenye kazi,” alisema Lwandamina.

Kama Yanga itapagwa kwenda Ivory Coast itacheza dhidi ya ASEC Mimosas au Williamsville AC.

Kutoka Zambia kutakuwa na ZESCO United na Zanaco wakati Congo kutakuwa na timu za AC Leopards, na AS Otoho. Mali watawakilishwa na timu za Stade Malien na AS Real Bamako huku Nigeria ikiwa na timu za Plateau United, na MFM.

Mbali ya miamba hiyo Yanga anatarajia kupata ushindani mkubwa wa kufuzu kwa hatua ya makundi kutoka kwa Eding Sport ya Cameroon, Al-Tahaddy (Libya), Aduana Stars (Ghana), 1º de Agosto (Angola), Saint George (Ethiopia) na Township Rollers (Botswana).

Rais Magufuli awapa neno UVCCM



Mwenyekiti wa (CCM) Dkt. John Pombe Magufuli amewaonya wajumbe wa Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM) kuwa endapo watachagua viongozi kama waliokuwepo awali watambue watapata shida kwa miaka mingine mitano.

Magufuli amesema hayo leo Disemba 10, 2017 akiwa Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma alipohudhuria Mkutano Mkuu wa tisa wa UVCCM Taifa ambapo amewataka vijana wa chama hicho wasiogope kufanya maamuzi yenye kuleta mabadiliko katika safu ya uongozi wa Umoja huo kwa kuwa viongozi waliokuwepo tayari wameonyesha kuwa na dosari na kuwakosesha nafasi vijana wengi kuweza kupewa nafasi katika serikali ya awamu ya tano.

"Mwenyekiti mtakaye mchagua, Makamu Mwenyekiti na uongozi wote wa vijana mtakaouchagua leo hao ndiyo watakuwa washauri wangu wakubwa ila mkichagua kama wale ambao hawakunishauri hata kwa kuniletea majina ya kuteua kwenye nafasi zenu, mkachagua tena katika mwaka huu mjue mna miaka mitano mingine ya kuumia" alisisitiza Rais Magufuli.

Aidha Rais Magufuli aliwataka vijana hao kutowachagua viongozi wa UVCCM ambao wanatumia fedha kutaka kupata nafasi ndani ya umoja huo wa vijana wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Simba yazidi kuongeza matawi yake nje ya Dar


Klabu ya soka ya Simba SC leo imefanya uzinduzi wa tawi jipya la Kibaha mkoani Pwani, ikiwa ni sehemu ya kuwaweka karibu wanachama wake wa maeneo hayo.

Uzinduzi wa tawi hilo umefanywa na Mkuu wa Idara ya habari ya klabu hiyo Haji Sunday Manara na kuhudhuriwa na wanachama na mashabiki wa Simba wa Kibaha na matawi ya karibu.

Jumapili ya wiki iliyopita Simba iliingia rasmi kwenye mfumo mpya Wa uendeshaji wa klabu kutoka mfumo wa wanachama na kwenda kwenye mfumo wa hisa ambapo zabuni ya kuwekeza alishinda mfanyabiashaaa na shabiki wa klabu hiyo Mohammed Dewji ‘Mo’.

Pia vinara hao wa ligi kuu soka Tanzania Bara wamethibitisha kuwa kocha mkuu wa timu hiyo Mcameroon Joseph Omog atarejea nchini siku yoyote ndani ya wiki ijayo.

Omog alikwenda nchini kwao kwa mapumziko baada ya ligi kusimama ambapo mazoezi ya klabu hiyo yalianza jumatatu ya wiki hii chini ya kocha msaidizi Masoud Juma kwenye uwanja wa Polisi Kurasini.


Jinsi Babu Seya na wanae walivyohukumiwa jela na maisha yao gerezani



Baada ya kusota gerezani kwa miaka 13 na miezi minne, wakitumikia kifungo cha maisha, hatimaye mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi nchini, Nguza Viking ‘Babu Seya’ na mwanae, Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ jana walirejea uraiani kwa msamaha wa Rais John Magufuli.

Babu Seya na na Papii Kocha walitoka katika Gereza la Ukonga saa 12 jioni huku wakishangiliwa na mashabiki pamoja na ndugu zao.

Babu Seya aliyekuwa akipunga mkono akionekana kutoamini kilichotokea alivaa mavazi kitanashati kama ilivyokuwa kwa Papii Kocha ambaye alikuwa akipunga mkono huku akitabasamu na kuzungumza na mashabiki wake.

Pamoja na kuwa wameachiwa lakini haya ndiyo waliyopitia wanamuziki hao katika safari yao kuanzia kushtakiwa mpaka kuhukumiwa na kuachiwa huru.

Mwanzo wa kesi

Safari ya wanamuziki hao ya kuishi maisha ya gerezani ilianza baada ya kutiwa mbaroni na kisha kufunguliwa kesi ya jinai wakikabiliwa na mashtaka ya ubakaji na ulawiti, wakituhumiwa kuwabaka na kuwalawiti watoto 10 wa kike wenye umri kati ya miaka 6 na 8 ambao walikuwa ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, Sinza jijini Dar es Salaam.

Oktoba 12, 2003: Watiwa mbaroni

Babu Seya na wanae watatu walikamatwa Oktoba 12, mwaka 2003 na kufikishwa kituo cha Polisi cha Magomeni jijini Dar es Salaam, wakikabiliwa na tuhuma hizo za ubakaji na ulawiti wa watoto wa kike wenye umri wa chini ya miaka 10.

Waliotiwa mbaroni walikuwa ni Nguza mwenyewe, Papii Kocha, Nguza Mbangu na Francis Nguza ambao wote ni watoto wake.


Kwa mujibu wa kumbukumbu za kesi hiyo mahakamani, Babu Seya na wanae walitiwa mbaroni baada ya mmoja wa watoto hao ambao walikuwa ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Mashujaa, kugunduliwa na bibi yake kuwa alikuwa ameharibiwa sehemu zake za siri.

Baada ya bibi huyo kumhoji mtoto huyo ndipo alipoeleza kuwa amekuwa akifanyiwa vitendo hivyo na Babu Seya na kwamba si yeye pekee bali wapo na wenzake ambao nao hufanyiwa hivyo, huku akiwataja kwa majina.

Kutokana na taarifa hizo ndipo bibi huyo alipotoa taarifa kwenye vyombo vya dola na hatimaye watuhumiwa kutiwa mbaroni.

Oktoba 16, 2003: Wapandishwa kizimbani

Siku nne baadaye baada ya kutiwa mbaroni, Babu Seya na wanae hao watatu pamoja na mwalimu wa kike wa Shule ya Msingi Mashujaa walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mahakamani hapo walisomewa jumla ya mshtaka 21, mashtaka 10 ya ubakaji wa watoto hao na mashtaka mengine 11 ya kuwanajisi watoto hao.

Juni 25, 2004: Kifungo cha maisha jela

Baada ya kuwa wamesota mahabusu wakati kesi yao ikiendelea kusikilizwa, hatimaye Juni 25, 2004 walianza maisha mapya baada ya Mahakama ya Kisutu kuwahukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Addy Lyamuya baada ya kuwatia hatiani kwa makosa 20 ya kuwabaka na kuwalawiti watoto hao.

Pamoja na adhabu hiyo ya kifungo, pia Hakimu Lyamuya aliwaamuru kuwalipa fidia ya Sh2 milioni watoto hao kila mmoja.

Wakati Babu Seya na wanaye wakitiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu hiyo, mshtakiwa wa tano, mwalimu wa shule hiyo aliachiwa huru.

Januari 27, 2005: Ukuta rufaa ya kwanza

Harakati za wafungwa hao kujinasua katika adhabu hiyo zilianza mara moja baada ya hukumu hiyo ya Mahakama ya Kisutu ambapo kupitia kwa wakili wao aliyewatetea katika kesi ya msingi, Hubert Nyange walikata rufaa Mahakama Kuu.

Hata hivyo, Januari 27, 2005 waligonga ukuta baada ya Jaji Thomas Mihayo aliyesikiliza rufaa yao hiyo kutupilia mbali.

Februari 11, 2010: Babu Seya, Papii Kocha wang’ang’aniwa, wenzao waachiwa

Kwa mara nyingine, Babu Seya na wanae mara hii wakiwakilishwa na Wakili Mabere Marando, walikata rufaa Mahakama  ya Rufani wakipinga hukumu ya Mahakama Kuu.

Hata hivyo, matumaini ya Babu Seya na Papii Kocha kurudi uraiani kwa mara nyingine yalitoweka baada ya kushindwa katika rufaa yao ya pili.

Mahakama ya Rufani katika hukumu yake iliyoandaliwa na jopo la majaji watatu; Nathalia Kimaro, Salum Massati na Mbarouk Mbarouk, Februari 11, 2010 ilitupilia mbali rufaa dhidi yao kuwa hoja zao hazikuwa na mashiko na hivyo ikaridhia kuendelea na kifungo hicho cha maisha.

Wakati mahakama hiyo ikiridhia Babu Seya na Papii Kocha kuendelea na kifungo chao, iliwaachia huru Mbangu na Francis ikikubaliana na hoja za Wakili Marando kuwa hapakuwa na ushahidi  wa kuwatia hatiani.

Desemba 22, 2013: Wakwama tena

Licha ya Mahakama ya Rufani kuwang’ang’ania na kuridhia kuendelea na adhabu hiyo, Babu Seya na Papii Kocha hawakukata tamaa kupambana kuwa huru.

Kwa mara nyingine, walifungua maombi ya marejeo wakiiomba mahakama hiyo irejee tena hukumu yake hiyo na hatimaye ione kuwa ilikosea na hivyo iwaachie huru.

Hata hivyo, mara hii tena waligonga ukuta baada ya mahakama hiyo kutupilia mbali maombi yao kuwa hayana mashiko ya kisheria.

Katika uamuzi wake uliosomwa na kaimu msajili, Zahra Maruma, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali maombi hayo ikisema kuwa waomba marejeo hao hawakuwa na hoja za msingi.

Ilisema hoja zilizotolewa katika maombi hayo ya marejeo si tu kwamba hazikidhi kuifanya irejee hukumu hiyo, bali pia hoja hizo zilishatolewa wakati wa usikilizwaji wa rufaa na kutolewa uamuzi.

Wenyewe watoa kauli

Akisindikizwa na askari kuelekea kwenye gari kurejeshwa gerezani, Papii Kocha alisema: “Sasa tunamuachia tu Rais ndiye anayeweza kutoa uamuzi wa mwisho.”

Lakini Babu Seya kwa upande wake, baada ya kupanda katika gari hilo tayari kurejea gerezani alisema bila ya kufafanua: “Kwa binadamu ni makosa, lakini kwa Mungu hakuna makosa.”

 Juni 21, 2014: Wamlilia JK awasamehe

Baada ya kuona kuwa harakati zao mahakamani zimeshindikana, Babu Seya na mwanaye Papii Kocha waliamua kumwangukia Rais Jakaya Kikwete wakimuomba awasamehe na kuamuru waachiwe huru.

Walitoa ombi hilo kupitia wimbo wao wakati wakitumbuiza katika maadhimisho ya Siku ya Magereza yaliyofanyika Chuo cha Magereza Ukonga, Dar es Salaam mbele ya aliyekuwa  Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe ambaye alikuwa mgeni rasmi.

Babu Seya na Papi Kocha walitumbuiza wakiwa na bendi ya wafungwa na katika wimbo huo walimuomba Waziri Chikawe kufikisha ombi lao kwa Rais Kikwete.

 “Waziri Chikawe tunaomba umfikishie Rais Jakaya Kikwete ombi letu, mwambie atusamehe. Hata Petro alimkana Yesu mara tatu, lakini Yesu alimsamehe kwa nini sisi…,” alisikika akiimba Papii Kocha.

Akijibu ombi hilo wakati akiwahutubia wananchi Waziri Chikawe alisema: “Nimesikia maombi yenu, yamefika na nitajitahidi kuyafikisha kwa Rais Kikwete.”

Novemba 2015: Watua Mahakama ya Haki za Binadamu

Baada ya harakati zao kushindwa katika mahakama za ndani ya nchi, Babu Seya na mwanae waliamua kuendelea na mapambano hayo katika mahakama za nje.

Mara hii walitua katika Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika (AfCHPR) ambako walifungua kesi namba 006/2015, wakidai kuwa haki zao zilivunjwa, hivyo walikuwa wakiiomba iwaachie huru.

Miongoni mwa hoja za walalamikaji hao zilizowasilishwa mahakamani hapo ni pamoja na kwamba mwenendo wa shauri lao la msingi haukufanyika kwa kuzingatia haki.

Vilevile, walidai kuwa hati ya mashtaka dhidi yao ilikosewa kuandikwa tarehe ambayo tuhuma za makosa yao zilidaiwa kufanywa hivyo wakashindwa kutayarisha utetezi wao na kwamba mahakama iliyowatia hatiani ilijielekeza katika ushahidi wa upande wa mashtaka pekee usioshirikisha ushahidi mwingine.

Walikuwa wakidai kuwa Serikali kupitia maofisa wake, ilivunja misingi ya haki za binadamu na sheria za kimataifa.

Desemba 9, 2017: Warudi uraiani.

Mwananchi.

Miili ya wanajeshi waliouwawa kuwasili Desemba 12



Serikali inashirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) kuhakikisha miili ya askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliouawa na waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inarejeshwa nchini.

Akizungumzia na waandishi wa habari leo Jumapili Desemba 10, 2017 Mnadhimu Mkuu wa JWTZ, Luteni Jenerali James Mwakibolwa amesema miili ya askari hao itarejeshwa nchini kati ya Jumanne Desemba 12, au Jumatano Desemba 13,2017.

Mwakibolwa amesema askari hao walivamiwa kambini na waasi wa ADF na mapigano yalidumu kwa saa 13.

Amesema askari 14 wa JWTZ waliuawa, 44 wamejeruhiwa na wengine wawili  hawajulikani walipo.

Mwakibolwa amesema tukio hilo lililotokea Desemba 7,2017 katika kambi ndogo iliyopo katika daraja la Mto Simulike, kaskazini mashariki mwa Wilaya ya Beni, Jimbo la Kivu.

Amesema shambulio hilo ni kubwa zaidi kutokea tangu JWTZ ianze kushiriki ulinzi wa amani nchini DRC mwaka 2011.

"Taratibu za kusafirisha miili ya marehemu kuirejesha nchini inafanyika chini ya uratibu wa Serikali na Umoja wa Mataifa. JWTZ na Serikali tunaendelea kuchukua hatua stahiki kufuatilia tukio hili ikiwemo kufanya uchunguzi katika eneo husika," amesema Mwakibolwa.

Amesema tukio hilo halitawavunja moyo JWTZ wala kutetereka kupeperusha bendera ya Tanzania ndani na nje ya nchi bali linawaongezea ari, nguvu, ushupavu na uhodari zaidi katika kutekeleza majukumu yao.

"Ni bahati mbaya mashujaa wetu wameuawa wakiwa wanatekeleza jukumu la ulinzi wa amani nchini DRC. Kwa umoja wetu Watanzania tuwaombee dua roho zao zipumzike kwa amani na majeruhi wapone haraka iwezekanavyo ili warejee kutekeleza majukumu yao," amesema.

 0     

Msando azidi kuwananga wapinzani


Aliyewahi kuwa mshauri wa Chama cha ACT Wazalendo na Wakili msomi wa kujitegemea, Alberto Msando amesema vyama vya upinzani nchini vimekosa nguvu katika kupambana na rushwa ukilinganisha na chama tawala cha CCM.

Msando amesema hayo leo tarehe 10 Desemba 2017, mjini Dodoma kwenye mkutano mkuu wa UVCCM taifa uliohudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Taifa, Mhe Dkt. John Pombe Magufuli.

“Wapinzani siyo tu wanapotezana, bali hadi sasa wameshapotezana, tumeshawapiga 4-0 ugenini na tukirudi nyumbani nako ni 4-0, tunamaliza kazi, CCM Oyee!!” – Alberto Msando

Alberto Msando ni moja ya watu mashuhuri saba waliohamia CCM kutoka kwenye vyama vya upinzani.

Kisa Babu Seya mashabiki wamvaa Zitto


Rais John Magufuli amevunja rekodi kwqa kusamehe wafungwa 8,157 ikiwamo familia ya mwanamuziki wa dansi Nguza Vicking ‘Babu Seya’  na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ jana Jumamosi.

Rais Magufuli alitangaza uamuzi huo wakati akihutubia maadhimisho ya sherehe ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanganyika zilizofanyika mjini Dodoma.

Hata hivyo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe aliandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kuonyesha kutokubaliana na uamuzi huo kwa madai  kwamba  anashaangaa kuachiwa watu waliohukumiwa kwa sheria ya nchi.

Posti hiyo ya zito ilizua mjadala mtandaoni kutokana na watu mbalimbali kumshukia kwa kuonyesha kukerwa na alichokiandika. Baadhi ya wasomaji walimsihi kuachana na jambo hilo kwani Rais ametimiza wajibu wake kisheria.

Kitu JPM ameongea kuhusu Mwenyekiti wa UVCCM aliekamatwa

Kitu JPM ameongea kuhusu Mwenyekiti wa UVCCM aliekamatwa


BREAKING: TANESCO wafunguka kuhusu tatizo la LUKU Tanzania

BREAKING: TANESCO wafunguka kuhusu tatizo la LUKU Tanzania