Thursday, 30 November 2017

CLOSE MY EYES 02 IMETAFSIRIWA KISWAHILI


CLOSE MY EYES SEHEMU YA 1-IMETAFSIRIWA KISWAHILI

CLOSE MY EYES SEHEMU YA 1-IMETAFSIRIWA KISWAHILI



Rooney afunga bao la mwaka Everton



Everton, Wayne Rooney amesema bao alilofunga dhidi ya West Ham United litabaki katika kumbukumbu yake daima.

Rooney alisema hakuwahi kufunga bao maridadi katika maisha yake ya soka tangu alipoanza kucheza soka Everton, Manchester United na timu ya taifa ya England.

Nahodha huyo wa zamani wa Man United na England aliiongoza Everton kupata ushindi mnono wa mabao 4-0 ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Goodison Park.

Nguli huyo alifunga mabao matatu ‘hat trick’ kwa mara ya kwanza tangu aliporejea Everton katika usajili wa majira ya kiangazi kutoka Man United.

Pia ushindi wa Everton ni ukaribisho wa kocha mpya Sam Allardyce ‘Big Sam’ aliyetua Goodison Park baada ya kuwa nje ya uwanja muda mrefu tangu alipojiuzulu kuinoa England.

Rooney alifunga bao la kwanza kwa shuti kali akiwa katikati ya uwanja dakika ya 66 akimtungua kipa mkongwe Joe Hart umbali wa mita 54.

“Hili ni bao bora zaidi kati ya mabao yangu niliyowahi kufunga. Ni mara ya kwanza kufunga ‘hat trick’ nikiwa Everton ni hili ndilo bao maridadi tangu nilipoanza kucheza soka,”alisema Rooney.

Mbali na kufunga mabao hayo, Rooney mwenye miaka 32 alikuwa nahodha katika mchezo huo na alicheza kwa kiwango bora dakika zote 90.

Pia alidokeza alifunga bao zuri kwa mkwaju wa penalti kwa kuwa anatambua udhaifu wa Hart tangu wakiwa wote timu ya taifa.

“Bao la kwanza lilikuwa muhimu. Nimejifunza sana kupiga penalti nyingi dhidi ya Joe Hart na najua jinsi ya kumfunga kwa kuwa anajua udhaifu wake,” alisema Rooney.

Matokeo hayo yamemuweka David Moyes katika mazingira magumu na juzi alichukizwa na kiwango cha wachezaji wake akidai walicheza ovyo na walistahili kufungwa.

Alikiba awapa mashabiki wake zawadi ya wimbo huu kwenye birthday yake



Msanii wa muziki wa bongo fleva ambaye sasa anafanya vyema na wimbo wake 'Seduce me' Alikiba ameamua kuachia video ya wimbo wake wa zamani ambao ulivuja kama zawadi kwa mashabiki wake katika siku yake ya kuzaliwa.

Alikiba ambaye jana alikuwa anasherehekea kumbukumbu ya mwaka wa kuzaliwa aliamua kuachia video ya wimbo wa 'Maumivu Per Day' kama njia ya kusherekea siku hiyo na mashabiki zake.

"Nashukuru sana watu ambao wamenitakia kheri katika siku yangu ya kuzaliwa, nimejaliwa, kupendelewa na kupendwa pia nashukuru sana kwa jambo hilo, nawapenda wote na nitafanya kazi kwa nguvu zote kuwafanya mjivunie uwepo wangu. Maumivu Per Day ni kati ya nyimbo zangu za zamani zinazopendwa nimeamua kuitoa japo siyo rasmi ili kusherehekea kumbukumbu ya siku yangu ya kuzaliwa na mashabiki zangu" alisema Alikiba

Unesco kuinufaisha Hifadhi ya Ngorongoro




Ngorongoro. Hifadhi ya Ngorongoro inatarajiwa kunufaika zaidi baada ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) kuiweka katika mchakato wa orodha ya maeneo ya kimataifa ya kipekee yanayojumuisha uhifadhi na maendeleo endelevu ya jamii (Unesco Global Geoparks).

Hatua hiyo itaiwezesha hifadhi hiyo kuingia katika orodha ya dunia ya kijiolojia itakayotambuliwa na Umoja wa Mataifa, hivyo kuaminiwa kimataifa na kuwezesha kutembelewa na watu wengi wakiwemo watalii.

Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dk Freddy Manongi amesema hati ya usajili wa kupandishwa hadhi inatarajiwa kutolewa na Unesco hivi karibuni baada ya kukamilika kwa mchakato.

Dk Manongi amesema Hifadhi ya Ngorongoro kwa sasa ipo katika orodha ya Unesco ya maeneo ya urithi wa dunia. Eneo hilo la kijiolojia linaruhusiwa kuishi wanyamapori na kuendeleza mila za watu wa makabila ya Masai, Hadzabe na Barbaig.

Hifadhi hiyo iliyoko katika bonde la ufa la Mashariki lilipata hadhi ya kimataifa ya kuwa katika orodha ya maeneo ya urithi wa dunia mwaka 1979.

Hifadhi ya Ngorongoro ndilo eneo ambalo limeendeshwa kwa mafanikio kwa mtindo wa  kuchanganya matumizi ya binadamu (wafugaji) na uhifadhi. Watu 88,000 wanaishi katika eneo hilo kwa amani na utulivu na wanyamapori.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla amesema hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kujitangaza kimataifa na kuaminiwa zaidi, hivyo kunufaika na idadi kubwa ya wageni watakaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro.

Mkazi ndani ya hifadhi hiyo, John ole Kuyan amesema mchakato huo wa Unesco ni faraja kwao kwa sababu wametambuliwa kuwa ni sehemu ya Ngorongoro.

“Tutahakikisha tunahuisha utamaduni wa Kimasai, Kihadzabe na Kibarbaig kwa sababu ni asili ambayo kama tukiipuuza inaweza kupotea kama ambavyo tamaduni nyingine zilivyosahaulika,” amesema Ole Kuyan.

Mtibwa Sugar yamnyakua beki wa Serengeti Boys




BEKI wa pembeni wa Mtibwa Sugar, Nickson Kibabage amesaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro.

Kibabage aliyekuwemo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys kilichoshiriki fainali za Afrika Mei mwaka huu nchini Gabon, anasimamiwa na akademi ya Cambianso ya Dar es Salaam.

Alijiunga na kikosi cha pili cha Mtibwa Sugar msimu uliopita na baada ya uzoefu mkubwa alioupata akiwa na Serengeti Boys, sasa ameanza kukomazwa kikosi cha kwanza.

Nickson Kibabage (kulia) amesaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea klabu ya Mtibwa Sugar ya Morogoro. Kushoto ni Mratibu wa Mtibwa, Jamal Bayser

Katika hatua nyingine, kipa Abdallah Makangana ambaye yuko nje ya uwanja kwa takribani wiki moja sasa akiendelea na matibabu kutokana maumivu aliyoyapata akiwa anafanya mazoezi, anaendelea vizuri.

“Ninaendelea vizuri, ni jambo la kumshukuru Mungu kadiri siku zinavyokwenda mbele na hali yangu ya kiafya inazidi kuimarika na ninataraji kupewa ruhusa hivi karibuni ya kujiunga na wenzangu kuendelea harakati za kupigania timu,”amesema.

Msimu huu, Abdallah Makangana ametumikia Mtibwa katika michezo mine tu kabla ya kuumia kufanya idadi ya majeruhi kufikia wane, wengine ni wakiwa ni kipa Shaaban Hassan Kado, beki wa pembeni Salum Kupela Kanoni na kiungo Henry Joseph Shindika.

Wachezaji wa Mtibwa Sugar wamepewa likizo ya wiki moja kufuatia Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kusimama kwa wiki mbili hadi tatu kupisha michuano ya CECAFA Challenge inayoanza Desemba 3 nchini Kenya.



Taarifa ya TANESCO kuhusu itilafu katika gridi ya Taifa asubuhi ya leo



MAJIRA ya saa 7:20 leo hii Alhamisi Novemba 30, imetokea hitilafu kwenye Gridi ya Taifa na hivyo kusababisha umeme kukatika takriban kwenye mikoa yote iliyounganishwa kwenye Gridi hiyo.

Kwa mujibu wa Kaimu Meneja Uhusiano wa TANESCO, Bi. Leila Muhaji, mafundi na wataalamu wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO wameanza kufuatilia kujua chanzo chake hasa ni nini na taarifa Zaidi zitatolewa kila baada ya muda ili kuufahamisha umma na watuamiaji wa umeme.

Source: Michuzi

Sikukuu ya Krismasi kuwa chungu kwa Wakazi wanaokabiliwa na Bomoabomoa



Dar es Salaam. Wakati sikukuu ya Krismasi ikikaribia, hali si shwari kwa wakazi wa Ubungo hadi Kimara ambao nyumba zao zimewekwa alama ya X zinazotarajiwa kubomolewa Desemba 21.

Nyumba 450 kati ya 1,200 zilizo ndani ya mita 91 katika hifadhi ya barabara zitabomolewa mwezi ujao kupisha upanuzi wa barabarahiyo ya Morogoro.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wakazi wa maeneo hayo walisema sikukuu ya mwaka huu itakuwa chungu kwao tofauti na miaka mingine ambayo walisherehekea wakiwa kwenye nyumba zao.

Mkazi wa Ubungo eneo la Kibo, Aloyce Chitala alisema sikukuu haitakuwa nzuri kwa upande wake kwa kuwa mwisho wa kuwapo kwenye nyumba yake ni Desemba 20 kwa mujibu wa barua aliyopewa na Wakala wa Barabara (Tanroads).

“Barua inatutaka tuondoke mwezi ujao, kwa hiyo hata ile shamrashamra ya sikukuu mwaka huu itakuwa ngumu, fikiria sasa hivi tumeambiwa tubomoe unafikiri baada ya kubomoa hapa kuna sikukuu tena zaidi ya simanzi?” alihoji.

Chitala alisema wanatambua kuwa ubomoaji huo ni kwa ajili ya maendeleo, lakini bado wanahitaji kulipwa chochote kwa ajili ya kutafuta sehemu nyingine ya kujisitiri bila hivyo yatawakuta kama ya Kimara ya kulala nje.

Alisema wakati wenzao wa Kimara Stop Over wanabomolewa nyumba zao, wao walijua wamepona, lakini hali ni tofauti na hatimaye maumivu yameangukia katika kipindi cha sikukuu.

“Inauma mtu unaishi miaka mingi halafu nyumba inakuja kubomolewa tena kwa kupewa mwezi mmoja pekee, basi wangesogeza mbele angalau hii sikukuu ipite ili na sisi tufurahi kama wenzetu,” alisema.

“Wakati huo nyumba zenyewe zitakuwa zimeshavunjwa na wengine tunaishi nje hivyo hakuna sikukuu tena, wenzetu wenye furaha tunawatakiwa kila la kheri katika sikukuu hii.”

Mkazi mwingine wa hapo, Idd Vagi alisema ni kweli eneo ni la Serikali, lakini awali wananchi hawakushirikishwa kwa kupewa elimu ili wasijenge.

Vagi mwenye umri wa miaka 75 alisema amekuwa akiishi sehemu hiyo tangu mwaka 1970 wakati huo eneo hilo likiwa pori.

“Walikuja hapa mwezi uliopita wakatoa notisi, wakasema tuanze kubomoa ndani ya mwezi mmoja kinyume na hapo inabidi tuwalipe kama wakija kubomoa wenyewe,” alisema.

Mzee huyo alisema wananchi wanaosomesha utakuwa ni mwezi mbaya zaidi kwao kwa kuwa watoto wanahitaji sare za shule na ada huku nyumba zao zitakuwa zinabomolewa.

“Ni kweli mwezi huu sikukuu sio nzuri hasa kwa wenzetu, lakini tutafanyaje hatuna jinsi ndiyo Serikali yetu hii, hatuna pa kwenda na hatuna cha kufanya tupo tu,” alisema.

Vagi aliongeza kwamba suala la kuhama sio gumu, lakini kuhamisha vitu ikiwamo matofali na vifaa vingine ni vyema Serikali ikawapatia fidia kidogo ili wapate fedha za kusafirishia mizigo yao kwenda sehemu nyingine ili kupisha iendalee na ujenzi.

Bernadeta Mushi ambaye ameanza kubomoa nyumba yake, alisema kwa sasa hajui sikukuu itakuwaje kwa upande wake kwa kuwa hadi hafahamu mahali atakakokwenda kuishi baada ya nyumba yake kubomolewa.

Alisema baada ya kupata notisi iliyomtaka kuondoka ndani ya mwezi mmoja alichanganyikiwa.

Hata hivyo, alisema anachokifanya kwa sasa ni kutoa vyombo vyake ili kama nyumba yake itabomolewa visiharibike.

“Yaani dada kwa sasa ukiniuliza kuhusu sikikuu sijui hata nijibu nini kwani navuta picha siku hiyo nitakuwa hospitali au chini ya mti maana sina pa kwenda,” alisema.

Akizungumzia hali hiyo, meya wa Manispaa ya Ubungo, Boniface Jacob alisema hadi nyumba 450 zimeshawekwa alama ya X na mwezi ujao zitabomolewa.

Alisema wananchi wana maumivu kwa kuwa wanatakiwa kuondoka mwezi huu bila malipo, hali inayosababisha hofu miongoni mwao ya kukosa makazi.

“Kwa kweli hivi sasa hali ni mbaya kwa wananchi hawa ambao wanatakiwa kuondoka. Utata ni kwamba kuna wenzao ambao walilipwa, kwa hiyo nao wanadai malipo yao,” alisema.

Akizungumza kwa simu na mwandishi wa habari hizi, meneja wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Julius Ndyamkama alisema ubomoaji utaanza rasmi Desemba kwa wale waliowekewa X mwezi huu.


  1. Hata hivyo, hakutaka kuingia kwa undani kuhusu suala hilo.

Rais Trump amshutumu waziri mkuu wa Uingereza Theresa May



Rais Donald Trump amemwambia waziri mkuu wa Uingereza Theresa May kuangazia ugaidi nchini Uingereza badala ya kumkosoa kwa kusambaza video za kundi la mrengo wa kulia la Uingereza ambalo linaeneza chuki.

''Usiniangazie sana mimi, angazia ugaidi unaotekelezwa na makundi yalio na itikadi kali ambao unatekelezwa nchini humo'', Trump alituma ujumbe wa Twitter.

Rais huyo wa Marekani awali alituma video tatu zenye chuki zilizosambazwa katika mtandao wa Twitter na makundi hayo nchini Uingereza.

Msemaji wa bi May alisema kuwa ni makosa kwa rais kufanya hivyo.

Marekani na Uingereza ni washirika wa karibu na wameelezewa kuwa na ''uhusiano maalum''.

Theresa May alikuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kumtembelea rais Trump katika ikulu ya Whitehouse.


Kanda za video zilizosambazwa na Trump ambaye ana takriban wafuasi milioni 40 awali zilikuwa zimechapishwa na Jayda Fransen, naibu kiobngozi wa kundi la Uingereza la Britain First, kundi lililoanzishwa na wanachama wa zamani wa mrengo wa kulia wa chama cha Uingereza cha BNP.

Bi Fransen mwenye umri wa miaka 31 ameshtakiwa nchini Uingereza mwa kutumia maneno ya kutisha, na matusi katika hotuba alizotoa katika mkutano mjini Belfast.

Wanasiasa nchini Uingereza wameukosoa ujumbe huo wa rais Trump akiwemo, askofu mkuu wa Cantebury Justin Welby ambaye alisema kuwa inakera kwamba rais Trump aliamua kulipatia sauti kundi lenye itikadi kali la mrengo wa kulia.

Hatua hiyo imezua hisia kali huku baadhi ya raia wakitaka ziara ya rais Trump nchini Uingereza kufutiliwa mbali ,ijapokuwa afisi ya waziri mkuu imesema kuwa ziara hiyo bado itafanyika.



Maofisa 2 wa zamani Argentina wahukumiwa kifungo cha maisha



Maofisa wawili wa zamani wa jeshi la maji la Argentina wamehukumiwa kifungo cha maisha kwa makosa ya ukiukaji wa haki za binadamu, waliyoyatekeleza kati ya mwaka 1976 na 1983 chini ya utawala wa kijeshi.

Kaptain Alfredo Astiz na Jorge Eduardo Acosta walikutwa na hatia ya kuhusika katika mauaji ya mamia ya wanasiasa wa upinzani.

Hawa ni kati ya washitakiwa 54, kati yao raia ni wawili, walioshitakiwa kwa makosa ya ukiukwaji wa haki za binadamu,na mauaji ya mamia ya wanasiasa wa upinzani,katika kituo chao cha mateso cha ESMA.

Ukatili huo ulifanyika,hapo ilikuwa ni shule ya ufundi makenika ya wanamaji hao.
Hatua hii inaatajwa na wemngi kuwa itaifanya Argentina kuheshimika zaidi kimataifa.

Zitto aitaka Kilimanjaro Stars kutoshuka dimbani kuikabili Libya



Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo na Mbunge wa Kigoma Mjini Mh. Zitto Kabwe ameitaka timu ya taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) kutoshuka dimbani kuikabili Libya siku ya Jumapili katika michuano ya CECAFA ikiwa ni hatua ya kuonyesha kuchukizwa na vitendo vya biashara ya utumwa vinavyoendelea katika nchi hiyo.

Zitto ameyasema hayo kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Twitter ikiwa zimesalia siku chache  kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania Bara kucheza mchezo wake wa kwanza siku ya Jumapili ya Desemba 3 dhidi ya Libya katika michuano ya Afrika Mashariki na Kati inayofanyika huko nchini Kenya.

Leo @masoudkipanya ameshauri Tanzania isusie mechi yake dhidi ya Libya siku ya Jumapili kuonyesha kuchukizwa na Biashara ya Utumwa. Ninaunga mkono. Tanzania isiingie Uwanjani kucheza na Libya. @SADC_News iagize nchi zake zote zirudishe mabalozi wake kutoka Libya.

Kilimanjaro Stars itacheza mchezo huo wa kundi A, katika kuwania kombe la michuano ya Afrika Mashariki na Kati CECAFA ambayo inatarajiwa kuchezwa nchini Kenya kuanzia Desembe 3 hadi 17 mwaka huu.

Mataifa 10 yanatarajiwa kushiriki katika michuano hiyo mikubwa kwa ukanda huu wa Afrika Mashariki huku droo ya hatua ya makundi ikionyesha mwenyeji Kenya itacheza mchezo wa ufunguzi dhidi ya Rwanda huku Tanzania ikiikabili Libya siku hiyo.



Msando amefunguka kuhusu video yake akiwa na Gigy Money


MWANASHERIA maarufu nchini aliyekuwa Chama cha ACT Wazalendo na hivi karibuni akahamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Albert Msando, kwa mara ya kwanza amefunguka LIVE kuhusu video yake akiwa na mwanamuziki na modo Gigy Money iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii mwezi Mei mwaka huu.

Video hiyo ilimuonyesha Msando na Gigy Money wakiwa ndani ya gari, huku Msando akipitisha mkono wake juu ya mwili wa Gigy, wakati huo Gigy Money akikata kiuno huku anacheza muziki.
Akifanya mahojiano leo  kwenye Kipindi cha Clouds 360 kinachorushwa kupitia Clouds TV, Msando amesema;

“Ile ni moja kati ya sehemu zilizonisaidia katika maisha yangu, ilinisaidia kujua jamii inanichukuliaje na nini inategemea kutoka kwangu. Video ile haikutengenezwa kwa sababu zozote, mimi sikuwa namfahamu Giggy.

“Tukio lile lilitokea wakati nimekunywa kilevi, sikuwa nikitambua kilichokuwa kinaendelea. Zaidi ameeleza kuwa video ile ni funzo kwa jamii nzima kuwa responsible hata kama hujakamatwa, usisubiri uwe ‘caught on camera’ ili uwajibike,” alisema Msando.

Hata hivyo, baada ya video hiyo kusambaa watu mbalimbali walionyesha kuchukizwa na wanavyomfahamu Mwanasheria Albert Msando mtu wanayemwona ana  heshima kubwa na umaarufu katika jamii,  ambapo aliomba msamaha kupitia ukurasa wake wa Instagram

Tutaiangamiza Korea Kaskazini iwapo vita vitazuka: Trump



Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong un na mwenzake wa Marekani Donald Trump

Marekani imeyataka mataifa yote kukatiza uhusiano wa kidiplomasia na ule wa kibiashara na Korea Kaskazini baada ya taifa hilo kufanyia jaribio la kombora lake la masafa marefu.

Akizungumza katika baraza la usalama la umoja wa kimataifa ,mjumbe wa Marekani katika baraza hilo Nikki Haley amesema kuwa rais Trump amemtaka mwenzake wa China kukata usambazaji wa mafuta kwa Pyongyang.

Amesema kuwa Marekani haitaki mzozo lakini Korea Kaskazini itaangamizwa iwapo vita vitazuka.
Onyo hilo linajiri baada ya Pyonyang kufanyia majaribio kombora lake la kwanza katika kipindi cha miezi miwili.

Korea Kaskazini imesema kuwa kombora hilo lililorushwa siku ya Jumatano ambalo inasema liliruka kimo cha kilomita 4,475, ikiwa ni mara kumi zaidi ya kimo cha kituo cha angani.

Madai hayo hayakuthibitishwa na wataalam wametiliashaka uwezo wa taifa hilo kuwa na teknolojia kama hiyo.

Hatahivyo kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un amesema kuwa uzinduzi wa kombora hilo ulikuwa wa kufana.

Jaribio hilo likiwa mojawapo ya majaribio yaliofanywa na taifa hilo limeshutumiwa na jamii ya kimataifa na tayari baraza la usalama la umoja wa kimataifa limeitisha kikao cha dharura.

Bi Haley alionya kuwa kuendelea kwa uchokozi kunalenga kuliyumbisha eneo hilo.

''Tunahitaji China kuchukua hatua zaidi'', alisema.

Rais Trump alimpigia simu rais Xi Jinping mapema siku ya Jumatano , Ikulu ya Whitehouse ilisema kuwa rais Trump alizungumza na Xi Jinping kwa simu akimtaka kuchukua hatua zozote kuishawishi Korea Kaskazini kusitisha uchokozi na kusitisha mpango wake wa kinyuklia.