Monday, 27 November 2017

MAGAZETI YA LEO 27/11/2017

Yatima ajinyonga




Dar es Salaam. Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Udaktari cha Imtu, Daniel Mabisi (28) anadaiwa kujinyonga kutokana na kufeli mitihani.

Mabisi ambaye ni mkazi wa mtaa wa Mgeninani, Kata ya Kijichi wilayani anadaiwa kukutwa amejinyonga jana saa saba mchana maeneo ya Mgeninani.

Taarifa zilizopatikana zinadai siku mbili kabla ya kujinyonga, mwanafunzi huyo alionekana mtaani hapo baada ya kutoka chuo alikokuwa akisoma.

Inaelezwa kuwa mwanafunzi huyo amefeli mara mbili mfululizo.

Akizungumza kwa simu kutoka Morogoro, baba mdogo wa marehemu, Joseph Lukuba alisema amepokea kwa mshtuko taarifa za mtoto wake.

“Nimepigiwa simu mchana huu nikaambiwa Daniel amejinyonga, nimeshtuka kwa sababu ni juzi tu tulimtumia nauli ili arudi nyumbani Mwanza baada ya kupata taarifa kuwa amefeli kwa mara nyingine,” alisema Lukuba.

Alisema uamuzi aliouchukua unasikitisha kwa kuwa kufeli, isingekuwa sababu ya kushindwa maisha hadi kufikia uamuzi wa kujinyonga.

“Kama familia tumehama na tuko mbali kikazi, tumemuomba jirani asimamie suala hili wakati taratibu za mazishi au kusafirisha mwili zikiendelea,” alisema.

Akizungumzia tukio hilo, mwenyekiti wa Mtaa wa Mgeninani, Khuruka Mwinyimvua alisema baada ya kupata taarifa hizo alifika eneo la tukio na kukuta mwili ukiwa umening’inia juu ya mwembe.

“Kijana huyo alionekana tangu juzi akizunguka mtaani hapa baada kurejea kutoka chuoni anakosoma, alionekana kama mtu asiyekuwa na furaha,” alisema Mwinyimvua na kuongeza: “Hadi sasa mwili umechukuliwa na polisi kwa taratibu nyingine.”

Naye kamanda wa polisi Mkoa wa Temeke, Emmanuel Lukula alithibitisha kupokea taarifa za kujinyonga kwa kijana huyo na kuwaagiza askari walio karibu na maeneo hayo kuchukua mwili huo.

Meya wa Mnanispaa ya Ubungo Boniface Jacob Aachiwa kwa dhamana



Dar es Salaam. Meya wa Ubungo, Boniface  Jacob ameachiwa kwa dhamana baada ya kushikiliwa polisi kwa takriban saa 15 akidaiwa kutaka kupanga njama za vurugu baada ya matokeo ya udiwani wa Kata ya Saranga kutangazwa.

Jacob ambaye pia ni diwani wa Ubungo (Chadema) alikamatwa na polisi jana Jumapili Novemba 26,2017 saa tano asubuhi katika kituo cha kupigia kura cha Mtakatifu Peter, Kimara.

Akizungumza na MCL Digital leo Jumatatu Novemba 27,2017 baada ya kuachiwa na polisi, Jacob amesema alipokamatwa alipelekwa vituo vya Mbezi kwa Yusuf, Mabatini na baadaye Oysterbay alikokaa muda mrefu.

"Nimeachiwa saa 7:40 usiku kwa dhamana, hizi zote zilikuwa ni njama za kutunyima ushindi. Dhamana gani inatolewa usiku?” amehoji Jacob.

Amesema, "Hii ilikuwa mipango ili Chadema isishinde ila wakazi wa Ubungo wasivunjike moyo na haya, wamejionea hali halisi iliyofanyika na huu ni ushindi kwetu."

Jacob ambaye  pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema amesema ametakiwa kuripoti Kituo cha Polisi Oysterbay leo.

Rais Magufuli awahenyesha mawaziri wawili, vigogo wanne



Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana aliwahenyesha mawaziri wawili pamoja na vigogo wakubwa wanne baada ya kufanya ukaguzi wa ghafla katika Bandari ya Dar es Salaam.

Rais alifikia uamuzi huo akionekana kujua uwepo wa magari 53 aina ya Suzuki ambayo ni maalumu kwa kubebea wagonjwa na malori zaidi ya 50 ya Jeshi la Polisi ambayo yaliingizwa tangu mwaka 2015, lakini hayajatolewa bandarini.

Alienda eneo la maegesho ya magari mara baada ya hafla fupi ya kuwaaga mabaharia wa meli ya Peace Arc waliokuwa wakitoa huduma ya matibabu kwa wiki moja bandarini hapo.

Akionekana kama wakili anayewabana mashahidi wa upande mwingine, Rais aliuliza maswali kutoka kwa waziri mmoja hadi mwingine, na mtumishi mmoja wa Serikali hadi mwingine.

Maswali yake yalilenga kutaka kujua aliyeagiza magari hayo, sababu za taarifa kutotolewa kwa takriban miaka miwili, wahusika kutofuatilia magari waliyoagiziwa na vyombo vya dola kutofuatilia suala hilo, huku vigogo hao wakiwa wamekutanisha mikono mbele kuonyesha unyenyekevu.

Waliowekwa katika hali ngumu jana ni Dk Philip Mpango, ambaye ni waziri wa Fedha na Mipango, Profesa Makame Mbarawa (waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano), Valentino Mlowola (mkurugenzi mkuu Takukuru), Simon Siro (mkuu wa Jeshi la Polisi), George Mnyitafu (kaimu kamishna wa forodha wa Mamlaka ya Mapato) na Deusdedit Kakoko (mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Bandari).

Wengi walionekana kupata taarifa za magari hayo wakati huo, kiasi cha kumfanya Rais aonekane kutoridhishwa na utendaji wao wa kutofuatilia vizuri kazi zao na kufanya magari mengine kukaa bandarini kwa takriban miaka kumi wakati sheria inaruhusu siku 21.

“I’m sorry jamani, haya mengine ni frustration zangu. Nisameheni sana,” alisema Rais Magufuli baada ya kueleza udhaifu wa utendaji wa vigogo hao wa kutochukua hatua.

Rais, ambaye alisema ana taarifa za magari hayo na mtu aliyeyaagiza, alitoa siku saba kwa mawaziri na wakuu hao wa taasisi wawe wamempa taarifa kamili ya suala hilo.

Kabla ya kutoa maagizo hayo, Rais Magufuli aliwahoji mawaziri na viongozi hao wa taasisi ambao kila mmoja alipewa kipaza sauti ili majibu yake yasikike.

Alianza kwa kumhoji Kakoko kuhusu uhalali wa magari hayo kukaa bandarini kwa muda mrefu na aliyeyaagiza.

Rais Magufuli: Nataka kujua haya magari ni ya nani?

Kakoko: Haya magari yameingia wakati hujaingia madarakani, ila yameingizwa na Ofisi ya Rais. Jina la aliyeyaagiza ni la Kichina au Kihindi hivi, lakini anwani ya mwingizaji ni Ofisi ya Rais ingawa na lenyewe limeandikwa vibaya vibaya na hata maneno yana utofauti. Magari yapo 50.

Rais: Kwa hiyo yameagizwa na ofisi yangu? Kuna mtu yeyote wa ofisi yangu ambaye aliagiza?

Kakoko: Hili jina si la mtu wa ofisini kwako na anuani si ya ofisi yako, bali ni lile jina la mwanzo tu.

Rais: Lakini wanasema yameagizwa na Ofisi ya Rais?

Kakoko: Ndivyo nyaraka zinavyoonyesha.

Rais: Mmeshafanya juhudi gani kama tangu mwaka 2015 Rais ameagiza magari kwa jina la Kichina na hayajachukuliwa na yamekaa hapa kwa jina la Kichina mpaka leo. Ulifanyaje? Ulimjulisha waziri? Na yeye anasema ndiyo amepata taarifa leo.

Kakoko: Utaratibu wetu baada ya siku 21 huwa unahama kwetu. Kimsingi yanakuwa yamehamia TRA.

Rais: Kamishna wa TRA yupo hapa hebu tueleze kuhusu haya magari ya Rais.

Mnyitafu: Rais ni kweli magari haya yaliingia mwaka 2015 Juni na taratibu zetu za kiforodha ilitakiwa tuyatangaze baada ya siku 21 ili yaweze kuuzwa.

Rais: Mliyatangaza?

Mnyitafu: Bado baada ya kushauriana na uongozi…

Rais: Mlishauriana na uongozi gani? Nataka jibu ndiyo maana nimewaita viongozi wote hapa.

Mnyitafu: Uongozi wa mamlaka wa wakati huo, tukashauriana, lakini sikuwepo wakati huo.

Rais: Nani ulimhusisha kwenye uongozi ule taja tu majina.

Mnyitafu: Sikuwepo.

Rais: Ulijuaje kama walishauriana wakati hukuwepo?

Mnyitafu: Nilivyouliza kwa wenzangu ambao…

Rais: Nani jina lake?

Mnyitafu: Maofisa ambao wapo bandarini.

Rais: Ulimuuliza nani, taja jina lake?

Mnyitafu: Meneja wa bandari ambaye yupo sasa hivi. Hata hivyo yeye ni mgeni anasema aliambiwa.

Rais: Nataka uwe muwazi, wewe si msomi bwana? Mimi mpaka kuja hapa nina taarifa nyingi ndiyo maana nataka uwe wazi ili nijue. Si umemuona mwenzako amesema wazi ofisi yangu ndiyo ilihusika mwaka 2015?

Mnyitafu: Sisi tunaangalia mtu wa kwanza aliyeagiza ambapo inasomeka kama imeagizwa na Ofisi ya Rais.

Rais: Ameshakuja mteja yeyote kufuata magari haya hapa?

Mnyitafu: Hajaja mteja yeyote kuchukua magari haya.

Rais: Ina maana hamjafanya upelelezi wowote kutambua kwamba haya magari ni ya nani?

Mnyitafu: Tuliamini kwamba ni ya Ofisi ya Rais.

Rais: Labda niulize swali jingine. Magari ya polisi yalikuja lini na haya pia yalikuja kipindi gani?

Mnyitafu: Yamekuja mwaka 2015 mwezi Juni.

Rais: Ndiyo maana nauliza magari ya polisi yalikuja mwezi wa sita na haya ya mtu ambaye hajulikani yamekuja Juni huyu hajayachukua? Polisi magari yenu yapo mangapi?

IGP Sirro: Yapo 55.

Rais: Sirro, haya magari 50 ambayo ni ambulance yanawahusu ninyi?

IGP Sirro: Hapana kwa kweli hatuyatambui na hatujui chochote kuhusu magari haya.

Rais: Nani mwingine anayefahamu kuhusu haya magari? Waziri pia hujui chochote.

Profesa Mbarawa: Mimi sijui. Nimepata taarifa leo asubuhi.

Rais: Kwa hiyo tangu mwaka 2015 Juni aliyekuwa mkurugenzi wa pale TPA mpaka ameondoka ndugu (Madeni) Kipande hakutoa taarifa na aliyeingia naye hakutoa taarifa na wewe waziri watu wako wa TRA waliokuwepo na walioko mpaka sasa hivi hawajaeleza kuwa kuna magari hamsini na kitu ambayo yamekaa hapo kwa miaka miwili, ambayo hayana mwenyewe, yameandikwa hapa president’s office wala hata mimi sijaulizwa. Mtu wa PCB, hebu njoo hapa wewe unafahamu kuhusu hili kwa sababu wewe ndiyo mtumiaji na mpelelezi mzuri. Unafahamu chochote kuhusu haya magari?

Mlowola: Kwa sasa sijui chochote mheshimiwa Rais. Ndiyo kwanza nimepata taarifa hii.

Rais: Na wewe ndiyo umepata taarifa hii leo kwa hiyo mtu wako wa PCB anayekaa bandarini naye hajui? Sheria za TRA zinasemaje Mheshimiwa Waziri? Gari linaweza likakaa humu hata miaka 30 mnatunza tu?

Waziri Mpango: Hapana mheshimiwa Rais. Sheria zinaweka ukomo wa muda na baada ya hapo inabidi zinadiwe.

Rais: Sasa kwa nini haya hayajanadiwa wala hayajatangazwa mnada kuanzia mwaka 2015?

Waziri Mpango: Kwa kweli kama nilivyosema sijui labda kamishna wa customs (ushuru) anisaidie kwa idhini yako.

Rais: Kamishna wa customs (ushuru) kwa nini hayajanadiwa au ulipewa rushwa kusudi usinadi ili kusudi siku tutakapokuwa tunatoa magari ya Serikali na haya yatoke?

Kamishna wa Forodha: Hapana mheshimiwa kama nilivyosema kwamba haya magari yaliandikwa ofisi ya Rais na siyo ofisi ya Rais tu kwa Serikali.

Rais: Kwa nini hukuandika barua kuuliza ofisi ya Rais, na Rais yupo.

Mnyitafu: Mheshimiwa tumeunda kikosi kazi kwa sababu ya kupitia magari haya pamoja na mengine. Mengi ambayo yapo bandarini ni matatizo kama haya

Rais: Kwa hiyo yako magari mengi yaliyoandikwa Ofisi ya Rais

Mnyitafu: Hapana, magari ambayo yamepitiliza muda wa kukaa bandarini lakini hayajauzwa.

Rais: Magari ya polisi yamebaki mangapi?

Mnyitafu: Ninayoyafahamu yapo 32 yapo 28 na mengine manne.

Rais: Wewe unayafahamu mangapi?

Kakoko: Yapo ya awamu tatu, ambayo hayajachukuliwa, yaliyochukuliwa zamani, lakini hayo ambayo wamesema wanagawiwa ya awamu tatu yapo kadri 53.

Akatoa maagizo haya

Baada ya kuhoji kwa muda mrefu, Rais Magufuli alitoa maagizo akitaka apate majibu ya magari hayo ndani ya siku saba ikiwa ni pamoja na kumjua mmiliki.

Alisema taarifa aliyonayo hawezi kuisema, bali anataka wamtajie mmiliki ili aweze kulinganisha na kujua kama wanafanya kazi pamoja naye.

“Kuna sababu magari haya yamefichwa kutoka bandarini kule kote yamekuja yakafichwa hapa na yaliagizwa pamoja na magari ya Serikali,” alisema Rais.

“Walipanga siku magari ya Serikali yakitolewa, na haya nayo yatoke na hiyo ninawapa njia. Ila nataka mfanye juhudi wapatikane hawa wote na kama wapo katika Ofisi ya Rais, muwapate kwa sababu hatuwezi kwenda kwa mchezo huu. Matapeli wanakuja na kusema huu ni mzigo wa Rais?

“Wamejua sasa hawawezi wakacheza vyovyote wamekuja wanayaficha hapa na aliyekuja akayatoa yalipokuwa akaja akayaficha hapa nina uhakika TRA na TPA mnafahamu kwa hiyo nataka majibu.”

Akifungua Baraza la wafanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Ndani Mei 9, 2015, waziri wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Mathias Chikawe alisema Serikali ilipanga kununua magari yapatayo 700 kwa ajili ya Jeshi la Polisi na kwamba huo ulikuwa ni mkakati pia wa kujiandaa kwa Uchaguzi Mkuu.

“Kwenye bajeti hii polisi imepata ongezeko zuri tu, hasa kwenye vifaa wametenga fedha za kutosha. Tunakusudia kwa ajili ya kujipanga kwa chaguzi kubwa mbili zijazo kununua si chini ya magari 700,” alisema Chikawe.

Mapema mwaka huo, ununuzi wa magari hayo ukaanza kutia shaka na wabunge ambao ni wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali walihoji sababu za magari hayo kununuliwa bila ya mkataba baada ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kuhoji.

Hata hivyo, wizara ilieleza baadaye kuwa kulikuwa na mkataba wa mwaka 2013 ambao uliisha bila ya kutekelezwa na baadaye kusainiwa mkataba mwingine wa nyongeza ulioonyesha Dola 10 milioni za Kimarekani, kati ya Dola 29 milioni zilishalipwa. Hadi wakati kamati hiyo inahoji suala hilo, magari 181 yalikuwa yameshaingia nchini.

Katika sakata la jana bandarini, Rais alimuagiza mkurugenzi mkuu wa Takukuru kuchunguza magari yote yaliyokwama bandarini hapo baada ya kuagizwa kwa majina ya taasisi za Serikali na kuwabaini wote walioshiriki katika uingizaji.

Baada ya hapo, Rais aliondoka na kutembea umbali wa zaidi ya mita 700 bandarini eneo lenye jua kali kwa ajili ya kwenda kukagua magari ya polisi, ambayo pia yalisemekana kuingizwa na kukaa kwa muda mrefu bandarinl.

Kabla ya tukio hilo, Rais aliwashukuru madaktari wa meli ya Peace Arc kwa kutoa huduma ya matibabu bure kwa Watanzania, akimsifu mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa kufanikisha na kuwataka viongozi wengine waige juhudi zake.

JKCI yafanya upasuaji wa moyo bila kufungua kifua



Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto ya nchini Israel, wamefanya upasuaji wa bila kufungua kifua (Catheterization) kwa watoto 20 wenye matatizo ya moyo.

Upasuaji huo ambao unatumia mtambo wa Cathlab, ulifanyika katika kambi maalumu ya matibabu iliyoanza Novemba 23 na kumalizika leo. Matibabu yaliyofanyika ni kuziba matundu na kutanua mishipa kwenye moyo.

Taarifa kutoka Kitengo cha Uhusiano na Masoko cha JKCI, ilisema katika kambi hiyo watoto 100 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi.

Taarifa hiyo ilisema watoto 60 ambao watakuwa na matatizo, watapelekwa nchini Israel kufanyiwa upasuaji wa kufungua kifua mwakani na watoto 40 watatibiwa nchini.

“Tumepanga kufanya matibabu kwa watoto 25, tunaamini hadi kambi itakapomalizika watoto wote hawa watakuwa wamepata matibabu,” inafafanua taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, watoto 20 waliopata matibabu, tayari wengine wameruhusiwa na waliobaki hali zao zinaendelea vizuri wataruhusiwa afya zao zitakapoimarika.

Tangu mwaka 2015, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ilianza kushirikiana na Taasisi ya Okoa Moyo wa Mtoto na hadi sasa watoto 40 wamefanyiwa upasuaji wa moyo nchini Israel.

Wakati kambi hii inaendelea, baadhi ya wafanyakazi wa JKCI walikwenda mkoani Kagera kufuatilia maendeleo ya mtoto Julius Kaijage (12) mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Green Acres iliyoko Bunazi ambaye alifanyiwa upasuaji wa moyo nchini Israel mwaka 2013.

“Tumekuwa na tabia ya kufuatilia maendeleo ya watoto tunaowafanyia upasuaji, hii inatusaidia kufahamu wanavyoendelea,” inasema taarifa hiyo na kuongeza:

“Tunatarajia kuwa na kambi nyingine ya matibabu ya moyo kwa watoto na watu wazima itakayoanza leo hadi Desemba mosi. Katika kambi hii ambayo tutashirikiana na wenzetu kutoka Taasisi ya Open Heart International ya nchini Australia, tunatarajia kufanya upasuaji wa kufungua kifua kwa watoto 13 na watu wazima 10.”

Papa aizuru Myanmar inayotuhumiwa kwa mauaji ya waislamu wa Rohingya




Papa Francis anaanza ziara ya wiki nzima nchini Myanmar na Bangladesh leo Jumatatu, wakati wasiwasi unaendelea wa kimataifa kuhusu usalama na ulinzi kwa wasilamu wa Rohingya.

Anatarajiwa kukutana na Aung Sun Suu Kyi na mkuu wa jeshi Myanmar.

Hata kabla ya kuondoka Roma, Papa Francis alikuwa anakabailiwana kitendawili cha kidiplomasia: iwapo kuliita kundi dogo la waislamu Myanmar - Rohingya.

Ni jina lisilo tumika na serikali ya kiraia na jeshi - wakieleza kuwa ni wahamiaji haramu kutoka Bangladesh na kwahivyo hawapaswi kuorodheshwa kama mojawapo ya makabila nchinihumo.

Lakini mashirika ya kutetea haki za binaadamu wanamuomba awaite hivyo, yakieleza kuwa nilazima Papa Francis aoneshe huruma kwa watu walionyimwa uraia na tangu Agosti wamekabiliwa na kile kamishna wa haki za binaadamu katika Umoja wa mataifa amekitaja kuwa 'kinachoonekana kuwa mauaji ya kikabila'.


  • Amnesty:Burma yatega mabomu kuwazuia Rohingya
  • Mapungufu ya UN katika mzozo wa Rohingya
  • Wapiganaji wa Rohingya watangaza kusitisha mapigano, Myanmar
  • Myanmar yatakiwa kukoma kuwatesa Waislamu wa Rohingya


Zaidi ya WaRohingya 600,000 wamekimbilia mpakani - na wakimbizi wakielezea kukabiliwa na mauaji, ubakaji na kuteketezwa moto kwa vijiji - jeshi imekana tuhuma zote.

Papa atakutana na kiongozi wa Myanmarr - Aung Sun Suu Kyi - Jumanne - huenda ni jukumu zito kidiplomasia katika miaka yake minne kama kiongozi wa kanisa katoliki.

Ziwa Victoria lipo hatarini kukauka



Wanasayansi wanasema kwamba ziwa kubwa zaidi lenye maji tulivu barani Afrika Victoria linalounganisha nchi za Tanzania, Kenya na Uganda, lipo katika hatari kubwa ya kukauka.

Wanasema kwamba uvuvi haramu na uliopitiliza pamoja na uvamizi wa mazingira kuzunguka maeneo ya ziwa ni sababu kubwa.

Maji machafu pia yanayotiririshwa kuelekea kwenye ziwa yanahatarisha usalama wa viumbe vya majini.

Mwandishi wa BBC anasema jeshi la Uganda limeweka mipango maalum ikiwa ni pamoja na kuharibu nyenzo za uvuvi zinazotajwa kuwa miongoni mwa sababu.



Wema Sepetu kupukutika Siri yake yafichuka



VYUMA vimekaza? Siri ya staa mkali wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu kupukutika imefichuka baada ya picha zake kusambaa zikimuonesha akiwa hana lile shepu aliloliimba Dogo Aslay.

Kufuatia ishu hiyo, mashabiki wa Wema walipigwa na butwaa jinsi mwili wake huo ulivyopukutika. Ili kumaliza ubishi huo, Ijumaa Wikienda lilizungumza na Wema na kumuuliza kulikoni kupukutika mwili ambapo alisema kuwa, huko nyuma alikuwa hapendi kabisa kujihusisha na mambo ya kwenye ‘gym’ kwani alikuwa akiona hawezi kufanya hivyo kwa ajili ya kupunguza mwili, lakini siku zinavyozidi kusonga aliona ni bora kufanya hivyo kwa sababu mwili wake uliongezeka kupita kiasi.


“Unajua nilikuwa nikiangalia kila nguo ninayovaa inanibana. Wakati mwingine ni kubwa kabisa, lakini inakuwa hainitoshi, nikaona nina kila sababu ya kupunguza huu mwili ambao siyo mzuri hata kiafya,” alisema Wema.


Wema ambaye wikiendi iliyopita alikuwa nchini Rwanda kwa ajili ya Shoo ya Instagram Party alisema kuwa, sasa hivi anafanya mazoezi takriban mwezi mmoja, lakini ameanza kuona matunda yake na anajilaumu alikuwa wapi kwa kipindi chote hicho na kushindwa kufanya mazoezi kwani mwili aliokuwa nao usingekuwepo. “Nina mwezi mmoja sasa tangu nianze mazoezi ya kupunguza mwili, lakini ninafurahia maisha haya na najuta kwa nini sikuanza mapema,” alisema Wema.
Stori: Imelda Mtema





Wizara ya Maji Yabomolewa

Wizara ya Maji Yabomolewa



Kazi ya ubomoaji majengo ya Wizara ya Maji yaliyoko eneo la Ubungo mkoani Dar es Salaam imeanza.

Kazi hiyo iliyoanza leo Jumatatu Novemba 27,2017 ni utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli ambaye aliagiza majengo ya wizara hiyo na ghorofa la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuwekwa alama ya X kwa ajili ya kubomolewa.

Novemba 15,2017 akitokea Chato alipokwenda kwa mapumziko baada ya ziara ya Uganda, Rais Magufuli aliagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka alama ya X katika jengo la Tanesco na Wizara ya Maji, sehemu zilizo katika hifadhi ya barabara.

Katika majengo ya Wizara ya Maji, tingatinga limevunja ukuta, huku watu wengine wakiendelea na kazi ya kuondoa madirisha na milango kwenye majengo. Jengo lililoanza kubomolewa ni la ofisi ya Waziri wa Maji.

Wafanyakazi wa wizara hiyo wanaendelea kutoa mali ndani ya majengo waliyokuwa wakiyatumia kwa ofisi.

Mbali ya majengo hayo, Tanraods inaendelea kuweka alama ya X kwenye nyumba za wananchi zilizo katika hifadhi ya barabara ikiwa ni pamoja na kupisha ujenzi wa barabara za juu eneo la Ubungo.

Tayari nyumba takriban 1,200 zikiwamo tano za ibada, vituo vya mafuta na baa katika eneo la Ubungo hadi Kimara Mwisho zimewekwa alama kwa ajili ya ubomoaji.

Kwa mujibu wa Tanroads, ubomoaji katika eneo la Ubungo hadi Kimara Mwisho unahusisha nyumba zilizo mita 91.7 katika hifadhi ya barabara ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Hifadhi ya Barabara ya mwaka 1932.