Tanzania\'s leading online News Edition (The National Newspaper). Get access to the most current and latest authoritative news on local issues, politics, events, celebrations, editorial, columnists, features, people and business.
KLABU ya Simba imesema kiungo wake, Said Hamis Juma, maarufu Said Ndemla amefanikiwa kufuzu majaribio yake ya kucheza soka la kulipwa katika klabu ya AFC Eskilstuna ya Sweden. Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba, Hajji Sunday Manara amesema leo katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari kwamba Eskilstuna wamesema wameridhishwa na uwezo wa Ndemla na wako tayari kumnunua.
“Ndemla aliyekuwa nchini Sweden kwa majaribio kwenye klabu ya Eskilstuna ya huko anatarajiwa kurejea nchini siku ya jumatatu inayokuja. Na mara baada ya kurejea. klabu za Simba na Eskilstuna zitaanza mazungumzo ya kimkataba ili kumwezesha kiungo huyo kwenda Sweden kwa ajili ya kucheza Soka huko,” amesema Manara.
Msemaji huyo wa Simba amesema kwamba klabu imefurahishwa na azma ya Ndemla ya kutaka kusonga mbele zaidi. “Na kama ilivyo desturi na utamaduni wa Simba, klabu haitasita kumruhusu mchezaji yoyote anayepata fursa adhimu kama hiyo itakayomsaidia mchezaji binafsi.klabu na Taifa kwa ujumla,”.
Katika hatua nyingine, Manara amesema kwamba kesho klabu ya Simba itakutana na viongozi wote wa matawi . makao makuu ya klabu, Msimbazi, Dar es Salaam kuanzia Saa 4:00 asubuhi7. Amesema mkutano huo ni maandalizi ya mkutano mkuu maalum wa klabu wa Desemba 3, mwaka huu Wakati huo huo: Hajji Manara amewataka wanachama na mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi kesho Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kuishangilia timu yao katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Lipuli ya Iringa.
TIMU ya TP Mazembe imefanikiwa kutwaa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF) baada ya kulazimisha sare ya 0-0 na wenyeji, SuperSport United Uwanja wa Lucas Moripe mjini Tshwane.
Mazembe inatwaa ubingwa wa Kombe hilo dogo la michunao ya klabu barani kwa ushindi wa jumla wa 2-1 ilioupata mjini Lubumbashi kwenye mchezo wa kwanza.
Ushindi huo, unamaanisha The Ravens wamefanikiwa kutetea taji ambalo walilitwaa kwa mara ya kwanza mwaka jana.
Pamphile Mihayo anakuwa kocha wa 10 Mwafrika kutwaa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika ndani ya fainali 14 za michuano hiyo.
Kocha wa SuperSports United ya Afrika Kusini, Eric Tinkler ameshindwa kutimiza ndoto za kutwaa taji la kwanza la michuano ya Afrika.
Mkongwe wa Tunisia, Faouzi Benzarti amebeba taji hilo mara mbili akiwa na Etoile Sahel, mwaka 2006 na 2015.
Ni kati ya makocha watatu walioshinda Kombe la Shirikisho na wakashinda pia Ligi ya Mabingwa, akipata mafanikio akiwa na klabu ya Esperance.
Makocha wengine wawili wazawa waliotwaa mataji yote ya klabu barani AfrikaThe ni Mghana Cecil Jones Attuquayefio, aliyefariki dunia mwaka 2015 na Mmorocco Hussein Amotta.
Attuquayefio alishinda mataji yote akiwa na vigogo wa Accra, Hearts of Oak wakati Amotta alibeba Kombe la Shirikisho akiwa na FUS Rabat na Ligi ya Mabingwa mwaka huu akiwa na Wydad Casablanca.
Kikosi cha SuperSport kilikuwa: Ronwen Williams, Siyabonga Nhlapo/Grant Kekana dk46, Tefu Mashamaite, Clayton Daniels, Aubrey Modiba, Dean Furman, Reneilwe Letsholonyane, Thuso Phala, Sipho Mbule/Kingston Nkhatha dk81, Bradley Grobler na Jeremy Brockie/Dove Wome dk66.
TP Mazembe: Sylvain Gbouhouo, Issama Mpeko, Joel Kimwaki, Chongo Kabaso, Zola Kiaku, Nathan Sinkala, Koffi Kouame, Daniel Nii Adjei/Miche Mika dk64, Adama Traore/Solomon Asante dk74, Ben Malango na Rainford Kalaba/Mechak Elia dk60.
Dar es Salaam. Uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata 43 zilizoko kwenye halmashauri 36 za mikoa 19 ya Tanzania Bara unafanyika leo.
Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), uchaguzi huo unafanyika kutokana na sababu kadhaa, zikiwemo madiwani kufariki dunia, kujiuzulu, kutohudhuria vikao na wengine ushindi wao kutenguliwa na mahakama.
Mkoa wa Arusha unaongoza kwa kuwa na kata nane miongoni mwa hizo ni za madiwani waliojiuzulu kutoka Chadema na kuhamia CCM wakieleza ni kutokana na kumuunga mkono Rais John Magufuli.
Uchaguzi huu ni wa pili tangu kuanza mwaka huu. NEC katika taarifa yake imesema inatakiwa kufanya uchaguzi wa madiwani mara mbili kwa mwaka kwa mujibu wa sheria. Uchaguzi mdogo mwingine wa ubunge na udiwani ulifanyika Januari 22 mwaka huu.
Ratiba ya mchakato wa uchaguzi huo ilianza Oktoba 26 kwa vyama vya siasa kufanya uteuzi wa wagombea wa udiwani na kampeni zilianza Oktoba 27 na kuhitimishwa jana.
NEC katika taarifa kwa vyombo vya habari jana imevitaka vyama vya siasa na wadau wa uchaguzi kuhakikisha unafanyika kwa amani na utulivu na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura.
Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alisema wapiga kura wapatao 333,309 wanatarajiwa kupiga kura katika vituo 884 ambako walijiandikishia kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2015.
Alisema tofauti na chaguzi zilizopita, NEC kwa kuzingatia masharti ya Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa kifungu cha 62 imewaruhusu wapiga kura ambao ama kadi zao za kupigia kura zimepotea, kuchakaa au kufutika kutumia vitambulisho mbadala kwenda katika vituo walivyojiandikisha ili waweze kupiga kura katika uchaguzi huu.
Jaji Kaijage alisisitiza ili kuruhusiwa kutumia kitambulisho mbadala, sharti majina ya mpiga kura yafanane kwa herufi na majina yaliyoko katika kitambulisho mbadala ambayo yako katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Vitambulisho mbadala ambavyo NEC imeruhusu vitumiwe na wapiga kura ni leseni ya udereva, kitambulisho cha uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) na pasi ya kusafiria.
Pia, aliwataka wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu wakati wa kupiga kura, ambayo ni ya walemavu, wajawazito, wenye watoto wachanga, wazee na wagonjwa.
Morogoro. Mgombea udiwani kwa tiketi ya Chadema Kata ya Sofi wilayani Malinyi, Riko Venance amewekwa chini ya ulinzi na polisi wakati akitembelea kituo cha kupigia kura cha Shule ya Msingi Mission.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, Alfonce Mbassa amesema bado hawajaambiwa kwa nini mgombea huyo anashikiliwa na polisi wakati sheria inamruhusu kutembelea vituo.
"Nimepewa taarifa kwamba mgombea wetu anashikiliwa na polisi na hivi ndio naelekea eneo la tukio, bado sijajua kwa nini amewekwa chini ya ulinzi, nitatoa taarifa baadaye," amesema Mbassa. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro hajapatikana kuzungumzia tukio hilo, jitihada za kumtafuta bado zinaendelea.
Kata ya Sofi ina vijiji vitatu ambapo viwili vinaongozwa na Chadema na kimoja hakina uongozi kwani kilishindwa kufanya uchaguzi kutokana na migogoro ya mipaka.
Kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012 kata hiyo ilikuwa na wakazi 12,000 huku waliojiandikisha kupiga kura mwaka 2014/15 wakiwa 8,700.
Rungwe. Ulinzi umeimarishwa kila kona katika Kata ya Ibighi Wilaya ya Rungwe wakati wananchi wakiendelea kupiga kura za udiwani wa kata hiyo.
Katika kata hiyo CCM na Chadema wameweka walinzi wao kwenye maeneo jirani ya vituo vya kupigia kura.
Msimamizi wa Uchaguzi Mbeya, Stevin Mwakingwe amesema hadi sasa upigaji kura unaendelea vizuri huku utulivu ukitawala katika kituo vyote vya kupigia kura.
Mwakingwe amesema vituo vyote 13 vya kupigia kura vimefunguliwa na kuanza kazi saa1:00 asubuhi na watu wanazidi kujitokeza kwa wingi.
“Nashukuru hadi muda huu watu wanaendelea kupiga kura kwa utulivu kabisa kama unavyoona mwenyewe (mwandishi). Sijapokea malalamiko yoyote kutoka kwa wapiga kura, wasimamizi au mawakala," amesema Mwakingwe.
Amesema kata hiyo ina wapiga kura 4,591 ambao wanatarajia kupiga kura leo Jumapili.
Wagombea udiwani Kata ya Ibighi wapo watano ambao ni Suma Fyandomo (CCM), Lusubilo Simba (Chadema), Geoffrey Mwakajinga (UDP), Emmanuel Mwasilembo (DP) na Grace Ngalaba (CUF).