Sunday, 19 November 2017

MAGAZETI YA LEO 19/11/2017

MAGAZETI YA LEO 19/11/201                           


Msuva atemwa kwenye kikosi cha Challenge



KOCHA Ammy Ninje hajamjumuisha winga Simon Msuva wa Difaa Hassan El-Jadida ya Morocco katika kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars kitakachoshiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge kuanzia Desemba 3, mwaka huu Jijini Nairobi, Kenya.

Badala yake, Ninje amemchukua winga wa Fanja ya Oman, Daniel Lyanga kwenye kikosi chake cha wachezaji 20 aliowataja leo mjini Dar es Salaam.

Katika kikosi hicho, Ninje mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ameita makipa wawili tu, Aishi Manula wa Simba na Peter Manyika wa Singida United. 

Mabeki ni Boniphace Maganga, Gardiel Michael, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Kennedy Wilson.

Viungo ni Himid Mao, Hamisi Abdallah, Muzamil Yassin, Raphael Daudi, Jonas Mkude, Shiza Kichuya, Ibrahim Ajib na Abdul Hilal, wakati washambuliaji ni Elias Maguri, Mbaraka Yusuph, Yohana Nkomola na Daniel Lyanga.

Kilimanjaro Stars imepangwa Kundi A pamoja na ndugu zao, Zanzibar, wenyeji Kenya, Rwanda na waalikwa Libya, wakati Kundi B lina timu za Uganda, Zimbabwe, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini.

Kilimanjaro Stars itafungua dimba na Libya Desemba 3, mwaka huu mchezo ambao utafuatiwa na mechi kati ya wenyeji, Kenya dhidi ya Rwanda.

Kili Stars itarudi uwanjani Desemba 7 kumenyana na Zanzibar Heroes, Desemba 9  na Rwanda kabla ya kumaliza mechi zake za Kundi A kwa kumenyana na wenyeji, Kenya Desemba 11.

Mechi za makundi zinatarajiwa kukamilishwa Desemba 12 na Nusu Fainali zitachezwa Desemba 14 na 15, wakati Desemba 16 itachezwa mechi ya kusaka mshindi wa tatu ikifuatiwa na fainali.

CECAFA Challenge ndiyo michuano mikongwe zaidi ya soka barani Afrika ambayo ilianza mwaka 1926 ikijulikana kama Kombe la Gossage hadi mwaka 1966, ilipobadilishwa na kuwa Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati hadi mwaka 1971 ilipobadilishwa tena na kuwa CECAFA Challenge.

Wadhamini tofauti wamekuwa wakiingia na kutoka kwa kipindi chote hicho, lakini taarifa zinasema kuanzia mwaka huu Televisheni namba moja Afrika Mashariki na Kati, Azam TV ndiyo wanakuwa wadhamini wapya ambao pia watakuwa wanarusha moja kwa moja michuano hiyo.

Uganda ndiyo mabingwa wa kihistoria wa michuano hiyo tangu mwaka 1971, wakiwa wamelitwaa mara 14, wakifuatiwa na Kenya mara sita, Ethiopia mara nne na Tanzania mara tatu.

Uganda, The Cranes pia ndiyo mabingwa watetezi wa michuano hiyo baada ya kutwaa taji la michuano hiyo mwaka 2015 nchini Ethiopia wakiwafunga Rwanda 1-0 kwenye fainali mjini Addis Ababa, wakati mwaka jana michuano hiyo haikufanyika kwa sababu ya kukosa nchi mwenyeji.

Alietajwa kufariki ajali ya ndege kumbe yupo hai



Mfanyakazi wa hoteli za kitalii za andBeyond Serengeti, Moses Muhina aliyetajwa kuwa ni miongoni mwa abiria waliofariki dunia katika ajali ya ndege ya Shirika la Coastal Aviation, imebainika alibadili ndege muda mfupi kabla ya safari ili kuwahi kazini.

Muhina ambaye ni mwongozaji watalii katika hoteli hiyo, alikuwa aondoke na ndege ya Coastal Aviation saa nne asubuhi lakini viongozi wa hoteli walimbadilishia ndege, hivyo aliondoka na Air Exel iliyofika salama Serengeti.

Akizungumza na gazeti hili, meneja uendeshaji wa Hoteli ya andBeyond Serengeti Under Canvas, Mussa Matala alisema Muhina ambaye anasomeka kwenye orodha ya ndege kama Maina alikuwa apande ndege hiyo lakini walimbadilishia.

Alisema waliomba aondolewe kwenye orodha ya wasafiri wa ndege hiyo lakini kwa bahati mbaya hadi ndege ilipoondoka jina lake lilikuwapo.

Wakati huohuo, raia watano wa kigeni ambao walifariki dunia katika ajali hiyo, akiwamo rubani Dewald Raubenheimer raia wa Afrika Kusini, ambaye kwenye orodha ya awali ya waliofariki jina lake halikuwapo anatarajiwa kusafirishwa leo.

Mhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya mkoa ya Mount Meru, Francis Costa alisema miili mitatu kati ya 11 imechukuliwa na ndugu zao.

Alisema miili iliyochukuliwa ni ya ndugu wawili waliokuwa wakurugenzi wa Masai Wondering, Nasibu na Shatri Mfinanga.

Mwingine ni wa Joyce Mkama ambaye alikuwa mfanyakazi wa Hoteli ya Serena.

“Uchunguzi wa miili ya wageni kutoka nje ya nchi unaendelea na ukikamilika itasafirishwa kwa mazishi katika nchi za Afrika Kusini, Ujerumani na Italia,” alisema.

Ndege hiyo namba 5H-EGG aina ya Cessna Grand Caravan ilianguka baada ya kugonga kingo za creta ya Empakai, umbali wa mita 3,250 kutoka usawa wa bahari ikitoka Kilimanjaro kwenda Hifadhi ya Serengeti.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema uchunguzi unaendelea kuhusu ajali hiyo.

Chelsea yaitwanga West Bromwich 4-0

Chelsea imeshangilia ushindi mwingine wa EPL kwa kuichapa Wes Borm kwa mabao 4-0.

Wakati inashinda kwa idadi hiyo, kiungo wake Eden Hazard anaonekana kuamka baada ya kufunga mabao mawili.

Wengine waliofunga ni Alvaro Morata na Alonso ambao kila mmoja alifunga bao moja.