Tuesday, 26 December 2017

Miradi Mikubwa itakayo kumbukwa mwaka 2017



Dar es Salaam. Mwaka 2017 ukielekea ukingoni, miradi mikubwa saba itaendelea kuutaja kila itakapikuwa ikizungumziwa.
Miradi hiyo ni ujenzi wa bomba la mafuta, uboreshaji Bandari Dar es Salaam, upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge) na ujenzi wa Daraja la Furahisa, Mwanza, bandari mpya ya Bagamoyo na mradi wa kuzalisha megawati 2,100 za umeme wa Stiegler’s Gorge.
Ikiwa imetangaza kuzikaribisha taasisi zinazoweza kufanya utafiti wa namna ya kufanikisha azma ya uchumi wa viwanda, Serikali inatekeleza miradi hiyo mikubwa na kati yake ipo iliyofikia hatua za mwisho.
Bomba la mafuta
Agosti 5, Rais John Magufuli pamoja na mwenzake, Yoweri Museveni wa Uganda walizindua ujenzi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima hadi Bandari ya Tanga. Ajira zaidi ya 1,000 zinatarajiwa kupatikana katika mradi huo.
Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,450 litapita katika mikoa minane ya Kagera, Geita, Shinyanga, Tabora, Singida, Dodoma, Manyara na Tanga. Ndani ya mikoa hiyo, bomba hilo litakalogharimu Sh8 trilioni, litapita katika vijiji 184 vilivyomo katika wilaya 24.
Mbali na ajira kwenye mradi huo, kutakuwa na fursa za kibiashara kwa wauzaji na wasambazaji wa vyakula na vifaa vya ujenzi.
Bomba hilo litajengwa na kuendeshwa na kampuni za Total ya Ufaransa, CNOOC ya China na Tullow ya Uingereza kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (Unoc) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Bandari ya Dar
Julai 2, ulifanyika uzinduzi wa kuboresha Bandari ya Dar es Salaam ambao unatekelezwa na Kampuni ya China Harbour Engineering Company (CHEC) utakaogharimu Sh336 bilioni ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Dunia. Kazi hiyo inatarajiwa kukamilika baada ya miezi 36.
Uboreshaji huo unahusisha ujenzi wa gati jipya la kuhudumia magari pekee, uboreshaji wa gati namba moja hadi saba na kuongeza kina cha maegesho ya meli kutoka mita 8.2 hadi 15 na kina cha mlango wa bahari ili meli kubwa na za kisasa ziweze kufika katika bandari hiyo.
Upanuzi huo unatarajiwa kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam hivyo kuiwezesha kuhudumia kiasi kikubwa cha mizigo hivyo kukuza uchumi.
Licha ya kuboreshwa kwa miundombinu, huduma nazo zinatarajiwa kurahisishwa. Mamlaka zote zinazohusika na uondoshaji au usafirishaji wa mzigo zimetakiwa kuwa na ofisi bandarini hapo. Hizo ni pamoja na benki zote zinazopokea fedha za Serikali ambazo ni na tozo za aina tofauti zinazopaswa kulipwa.
Taasisi zote muhimu zimewekwa chini ya dirisha moja ili kupunguza muda wa kukamilisha mchakato huo na kuharakisha biashara kwa waagizaji wa ndani na nchi jirani zinazoitumia bandari hiyo.
Upanuzi JNIA
Katika kuimarisha usafiri wa anga kwa wasafiri wa ndani na kimataifa, Serikali inapanua uwezo wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Bam International ya Uholanzi, kwa gharama ya Sh560 bilioni.
Wakati upanuzi huo ukitarajiwa kukamlika mapema mwakani na kuongeza idadi ya abiria kutoka milioni 2.5 hadi milioni 6.4 kwa mwaka, Serikali pia inaimarisha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Ndege mbili zikiwa zimeanza kutoa huduma, nyingine nne zipo kwenye mpango wa kuwasili. Mpaka mwakani, Serikali imesema ndege zote zitakuwa zimewasili nchini ili kuimarisha usafiri wa anga na sekta ya utalii kwa ujumla.
Bandari mpya Bagamoyo
Baada ya kusuasua kwa muda mrefu, mwaka huu Serikali imekamilisha taratibu za ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo pamoja na eneo maalumu la uwekezaji (SEPZ). Tangu Oktoba 15, 2015 Rais mstaafu Jakaya Kikwete alipoweka jiwe la msingi la utekelezaji wa mradi huu, hapakuwa na uendelezaji.
Lakini Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amesema taratibu zimekamilika na ujenzi utaanza Januari 2018. Utekelezaji wa mradi huo utaifanya Bagamoyo kuwa bandari kubwa zaidi Afrika Mashariki na Kati.
Utekelezaji wake utagharimu Dola 10 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh22.3 trilioni), na waziri Mwijage alisema utafanywa kwa ushirikiano wa Kampuni ya China Merchants Holdings International (CMHI) ya China na State General Reserve Fund ya Oman. Eka 3,000 zimetengwa na viwanda 190 vinatarajiwa kujengwa kabla ya mwaka 2020.
Utakapokamilika, mradi huo utakuwa na viwanda 700 na kuufanya kuwa eneo la kimkakati kwa uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuchangia kuinua uchumi wa Taifa.
Kwa mujibu wa taarifa za ujenzi huo, awamu ya kwanza itahusu meli kubwa zinazobeba hadi makontena 8,000 ya futi 20 hivyo kupunguza foleni ya meli za mzigo katika Bandari ya Dar es Salaam huku kukiwa na uwezekano wa kuitanua zaidi.
Stiegler’s Gorge
Mipango iliyomshinda Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na awamu tatu zilizofuata baada yake imewezekana hivi sasa. Agosti 30 Serikali ilitangaza zabuni ya ujenzi wa mradi mkubwa wa kuzalisha megawati 2,100 za umeme katika maporomoko ya maji ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge).
Zaidi ya kampuni 80 zimejitokeza kuomba kutekeleza mradi huo unaoelezwa kwamba utapunguza uhaba wa nishati hiyo nchini na kuweka mazingira rafiki ya ujenzi wa viwanda. Utakapokamilika, utaifanya Tanzania kuwa na jumla ya megawati 5,000 ifikapo mwaka 2021.
Mradi huo unatekelezwa huku Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) ukiwa unaendelea kusambaza umeme nchini. Mwaka jana, jumla ya vijiji 4,000 viliunganishwa. Pamoja na hiyo, mradi wa Kinyerezi I na II ipo kwenye hatua tofauti. Upanuzi wa Kinyerezi I uliokamilika kwa zaidi ya asilimia 50 unatarajiwa kuzalisha megawati 185 utakapokamilika wakati Kinyerezi II uliokamilika kwa zaidi ya asilimia 86 ukitegemewa kuzalisha megawati 250.
Ujenzi reli ya kisasa (SGR)
Ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge Railway) kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na Mwanza tangu utekelezaji wake ulipoanza mwaka huu, unatarajiwa kuanza kufanyakazi baada ya miezi 36.
Ujenzi wa awamu ya kwanza kutoka Dar es Salaam mpaka Morogoro utakaogharimu Sh2.7 trilioni wa reli hiyo ya mwendo wa kasi ya kilomita 160 kwa saa, umeanza na utaifanya Tanzania kuwa ya pili kwa kasi hiyo baada ya Morocco.
Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (Rahco) imetiliana saini mkataba wa ujenzi wa awamu ya kwanza ya reli hiyo na Kampuni ya Yapi Merkenzi Instant Ve Sanayi A.S ya Uturuki na Mota-Engil, Engenharia E and Construcao S.A ya Ureno kujenga kilomita 205 za njia kuu na kilomita 95 za kupishania.
SGR itakuwa na uwezo wa kusafirisha tani milioni 17 za mzigo ambalo ni ongezeko karibu mara mbili na nusu ya uzani uliopo.
Daraja la furahisha
Licha ya kujenga barabara zenye urefu wa kilomita 1,500 kwa kutumia Sh1.2 trilioni nchini kote mwaka huu, Serikali imekamilisha ujenzi wa Daraja Furahisha lililopo jijini Mwanza kwa kutumia Sh4.7 bilioni. Rais Magufuli alilizindua Oktoba 30.
Daraja hilo lina urefu wa mita 46, upana mita 3.6 na kimo cha mita 5.8 na njia za kuingia na kutoka zenye jumla ya meta 700. Fedha zilizotengwa kwa ajili ya sherehe za Muungano mwaka 2016 zilijenga daraja hilo baada ya kuzibadilishia matumizi.
Kujengwa kwa daraja hilo kumeokoa kwa kiasi kikubwa maisha ya wapita katika eneo hilo kwani lilikuwa na matukio mengi ya ajali.

No comments:

Post a Comment