Tuesday, 26 December 2017

Amana yaongoza kwa idadi kubwa ya watoto waliozaliwa krismas



Dar es Salaam. Watoto 102 wameripotiwa kuzaliwa katika hospitali mbalimbali nchini wakati wa mkesha wa sikukuu ya Krismasi. Dar es Salaam wamezaliwa 50, Kanda ya Ziwa 29, Arusha 18, na Handeni mkoani Tanga watano.
Hospitali ya Amana ndiyo iliyokuwa na idadi kubwa ya watoto waliozaliwa na Ofisa Muuguzi wa zamu, Agnes Simon alisema kati ya watoto 32, watano waliozaliwa kwa upasuaji.
Alisema afya za watoto hao ni njema na baadhi yao huenda wakaruhusiwa kurudi nyumbani.
“Hakuna mtoto mwenye tatizo, wote wana afya nzuri, hata wazazi wao wanaendelea vizuri pia, hivyo tunatarajia kuwaruhusu wakasherehekee sikukuu nyumbani,” alisema Agnes.
Kaimu Mkuu wa Jengo la Wazazi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Mariam Mlawa alisema jana kwamba watoto waliozaliwa hospitalini hapo wana afya njema na wanaendelea vizuri na idadi hiyo haijapishana na waliozaliwa katika mkesha wa Krismasi mwaka jana.
Alisema kina mama sita walijifungua na kati yao, wawili kwa upasuaji na wengine kwa njia ya kawaida. Pia kati yao, wawili wamejifungua watoto pacha.
“Tunashukuru watoto wote wapo vizuri, mama zao pia wapo vizuri na kwa hawa waliojifungua kwa njia ya kawaida huenda wakaruhusiwa muda wowote,” alisema Mlawa.
Ofisa Muuguzi Kiongozi katika Hospitali ya Temeke Rashidi Nyombiage alisema watoto 12 walizaliwa kwa njia ya kawaida na kwamba hakuna aliyejifungua kwa njia ya upasuaji.
“Hatukupata pacha, watoto wote walizaliwa mmojammoja na hakuna mtoto mwenye tatizo lolote wote wanaendelea vizuri na afya zao pamoja na mama zao zinazidi kuimarika,” alisema Nyombiage.
Katika Kanda ya Ziwa, watoto 16 walizaliwa katika Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure. Muuguzi msimamizi wa zamu, Rhoda Lissu alisema kati ya hao wa kike ni 10 na wakiume sita.
“Watoto wawili kati ya hao wamezaliwa kwa njia ya upasuaji, lakini tunamshukuru Mungu wapo salama na afya za mama zao zipo vizuri, “ alisema Rhoda.
Wilayani Serengeti, muuguzi mkuu wa Hospitali ya Teule ya Nyerere, Neema Machara alisema watoto watatu wa kiume walizaliwa kwa njia ya kawaida.
Arusha, watoto 18, walizaliwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru.
Mganga mfawidhi wa hospitali hiyo, Jackline Urio alisema kati yao 12 ni wa kiume.
Akizungumza jana, Mwamvua Barua mkazi wa Mtoni Kijichi aliyejifungua Muhimbili alisema hakutarajia maishani mwake kujifungua katika siku hiyo akisema atamlea mtoto wake huyo aliyempa jina la Emmanuel katika maadili.
“Huyu ni mtoto wa pili na wote nimewazaa mwezi wa 12, ila uzao huu umeangukia kwenye mkesha wa sikukuu,” alisema.

No comments:

Post a Comment