Serikali imewaonya viongozi wa dini wanaotumia mahubiri yao kuchambua masuala ya kisiasa, ikiwataka kuheshimu msingi wa uanzishwaji wa taasisi zao la sivyo taasisi zao zitafutwa.
Taarifa iliyotolewa leo Desemba 28 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Meja Jenerali mstaafu Projest Rwegasira imesema taasisi za dini zinapaswa kuzingatia sheria na masharti ya kuanzishwa kwake ambayo yapo kwenye Katiba za taasisi husika.
"Baadhi ya jumuiya zimekuwa zikifanya shughuli zao kinyume na malengo yaliyomo kwenye Katiba zao bila kuiarifu Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za kidini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, " amesema na kuongeza,
"Hivi karibuni kumekuwepo na tabia ya baadhi ya viongozi wa jumuiya kutumia mahubiri yao wakati wa ibada kuchambua masuala ya siasa kinyume na Katiba zao. Hakuna jumuiya iliyosajiliwa chini ya sheria ya jumuiya ili kufanya siasa."
Amesema kufanya hivyo ni kwenda kinyume na malengo na ukiukwaji wa Kanuni ya 7 ya Kanuni za Jumuiya zilizoundwa chini ya sheria ya Jumuiya, inayotamka pamoja na mengine kuwa Jumuiya yoyote hairuhusiwi kufanya mabadiliko ya malengo yake bila kibali cha msajili.
“Ofisi ya Msajili inazikumbusha Jumuiya zote kwamba ukiukaji wowote wa Sheria ni kosa ambalo linaweza kupelekea Jumuiya husika kufutiwa usajili wake kama ilivyoelezwa kwenye kifungu cha 17 cha Sheria husika," amesema.
Mwananchi.
No comments:
Post a Comment