Thursday, 25 January 2018

Tundu Lissu afunguka kutolewa risasi nyingine mwilini


Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu akifanya mazoezi akiwa hospitalini nchini Ubelgiji. Picha na Maktaba

 Siku 35 baada ya Tundu Lissu kusema mwili wake bado una risasi moja baada ya kutolewa nyingine 15, jana mbunge huyo wa Singida Mashariki (Chadema) amelieleza Mwananchi kuwa madaktari wamemtoa kipande cha risasi kilichokuwa mwilini mwake.

Hata hivyo, mwanasheria huyo mkuu wa Chadema, ambaye alishambuliwa kwa zaidi ya risasi 30 akiwa ndani ya gari lililokuwa nje ya makazi yake mjini Dodoma Septemba 7 mwaka jana, alisema chuma hicho ni tofauti na risasi iliyonayo mwilini, ambayo alielezwa na madaktari wa Hospitali ya Nairobi, Kenya kuwa iko sehemu mbaya, lakini isipotolewa haiwezi kumdhuru.

“Leo (jana) madaktari wamenitoa kipande cha chuma katika sehemu ya makalio ambacho nilipokuwa Nairobi (Kenya) madaktari walikiona lakini kilikuwa ndani ya nyama wakashindwa kukitoa,” alisema Lissu kwa njia ya simu kutoka Ubelgiji ambako alipelekwa Januari 7 kwa ajili ya tiba ya mazoezi.

“Kipande hiki kilisogea na wamekitoa. Ni tofauti na ile risasi ambayo iko mwilini mwangu.”

Akieleza kiundani kuhusu hali yake, Lissu alisema anaendelea vizuri.

“Huu mkono wa kushoto ambao ulikuwa na tatizo, wameunyoosha na kuufanyia mazoezi kweli kweli na huu mguu wa kulia ambao ndio wenye tatizo, unaendelea vyema,” alisema.

“Huku ni mazoezi tu. Kwa siku nafanya mazoezi kwa saa nne, Naingia saa 3:00 asubuhi hadi saa 4:00 asubuhi, narudi tena saa 5:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana. Mwisho naingia mazoezini saa 8:00 mchana hadi saa 10:00 jioni. Hiyo ndiyo ratiba yangu kwa siku.”

Alisema katika mazoezi hayo anatumia magongo maalumu pamoja na kiti cha magurudumu.

“Mfano, huu mguu wa kulia natakiwa kuukanyagia kwa kilo 20 hadi 25 katika mzani na mimi nina kama kilo 90. Ninapoukanyagia ninaulizwa kama unauma, ikiwa sijasikia maumivu ina maana sijafanya kitu, kwa hiyo ni kazi kwelikweli,” alisema.

Kuhusu muda ambao anatakiwa kufanya mazoezi hayo mpaka atakaporejea katika hali yake ya kawaida, Lissu alisema bado hajajua.

“Ah bwana we, hapa madaktari wamegoma kunieleza hilo, lakini wameangalia katika maungio ya goti la mguu wa kulia kuna mfupa haujaunga vizuri, ni lini utaunga hilo sijajua,” alisema.

Mara baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, Lissu alipelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma kwa matibabu ya awali kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya siku hiyo usiku.

Desemba 21 mwaka jana wakati akihojiwa na kituo cha televisheni cha Azam, Lissu alisema madaktari wa Nairobi walimueleza kuwa risasi iliyokuwa imesalia mwili haina madhara.

Alisema risasi saba zilitolewa na madaktari hao, jambo lililomaanisha kuwa risasi nyingine nane, zilitolewa na madaktari wa Tanzania, saa chache baada ya kushambuliwa alipofikishwa Hospitali ya Mkoa wa Dodoma.   



Dk Kigwangalla kutaja majina wanaotuhumiwa kwa ujangili



Dar es Salaam. Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla anatarajiwa kutaja hadharani majina ya watu wanaotuhumiwa kwa ujangili nchini.

Kupitia akaunti yake ya Twitter, Dk Kigwangalla amesema atazungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Januari 25,2018 mjini Dodoma kuelezea mambo yanayohusu wizara hiyo.

“Pia nitaweka hadharani watu mbalimbali wanaotuhumiwa kwa ujangili nchini,” ameandika Dk Kigwangalla.

Amesema tangu alipoteuliwa na Rais John Magufuli Oktoba 7,2017 kushika wadhifa huo, alijua kuna mambo mawili ambayo ni changamoto katika wizara hiyo.

 “Nilipoteuliwa nilijua kuna mawili, kujiunga na mtandao wa uovu ili nifaidike binafsi au kuukataa mtandao huu; nilijua kabisa mshahara wa dhambi ni mauti, na kwamba dhuluma haijawahi shinda vita dhidi ya haki, na wala uongo haujawahi shinda vita dhidi ya ukweli,” ameandika Dk Kigwangalla.

Nafasi za kazi leo Jan 25

Tausi Mdegela afunguka kuolewa Mke wa pili


Msanii wa filamu wa Tanzania mwenye muonekano wa kipekee na kipenzi cha watoto, Tausi Mdegela, ameutaarifu umma kuwa anatarajia kuolewa kuwa mke halali wa mpenzi wake wa siku nyingi ambaye ni msanii wa muziki wa taarabu, Prince Amigo.

Akizungumza na mwandishi wa www.eatv.tv Tausi amesema suala la ndoa ni mipango lakini ni jambo ambalo lipo, kwani tayari wamekuwa kwa muda mrefu kwenye mahusiano na mpenzi wake huyo ambaye ni mwanamuziki wa taarab, ambaye tayari ana mke wa kwanza.

“Ndoa ni mipango mtuombee Mungu tufike mbali, ni muda mrefu tumeanza tunaishi pamoja, ila Amigo ana mke mkubwa, kwa hiyo mimi nasubiria kuwa mke mdogo, hapa akiongezeka watatu ndio itakuwa mtihani, wawili tushatosha wengi wa nini, hapo ndo tutapigana sasa, na tukigundua kuna wa tatu hapo ndio litakuwa lingine, na mke mkubwa kashakubali”, amesema Tausi.

Tausi ameendelea kwa kusema kwamba yeye hajali maneno ya watu wanayosema kuhusu mahusiano yake hayo, kwani anachoangalia ni maisha yake na sio watu wanasema nini.


Daktari wa timu ya Olimpiki ahukumiwa kifungo


Larry Nasser daktari wa zamani wa timu ya Olympiki ya Marekani

Aliyekuwa daktari wa timu ya Olimpiki Larry Nasser amehukumiwa kwenda jela miaka 175 baada ya kukutwa na makosa ya ukatili wa kingono dhidi wananawake na wana michezo.

Katika kesi hiyo mashahidi 160 wamewasilisha ushahidi wao huku Nasser mwenyewe alikiri makosa kumi.

Alikuwa tayari akitumikia kifungo cha miaka 60 kutokana na kukutwa na hatia ya kumiliki picha ngono za watoto kinyume cha sheria.

Jaji Rosemary Aquilina ameiambia mahakama kuwa amejisikia fahari na furaha kubwa kutoa adhabu hiyo kutokana na kitendo alichofanya Nasser na kwamba anataka iwe fundisho kwa wengine.

'Nataka ukae jela maisha yako yote'. Hata hivyo baada ya hukumu hiyo mmoja wa waathirika amesisitiza kuwa washirika wa daktari huyo wanapaswa kushitakiwa pia.

Muda mfupi baada ya kutolewa hukumu hiyo, mkuu wa chuo kikuu cha jimbo la Michigan (MSU) alikokuwa anafanya kazi Nassar kati ya mwaka 1997 na 2016, amejiuzulu.

Bi Simon alikana taarifa kuwa MSU ilifahamu kuhusu tuhuma hizo za unyanyasaji lakini kilishindwa kuchukua hatua.

Katika taarifa yake alisema: "kwa waathiriwa, samahani yangu haiwezi kutosha, kuwa daktari aliyeaminika, aliyefahamika alikuwa ni mtu muovu kwa kweli, aliyewadhulumu kwa kutumia kigezo cha kuwatibu."

"Ushahidi wa wahanga wa unayanyasaji wa Nassar ni wa kusikitisha, kuvunja moyo na binafsi unaonitia kichefu chefu," aliongeza.

Takriban wasichana 140 wamewasilisha kesi dhidi ya Nassar, taasisi ya USA Gymnastics na chuo kikuu cha MSU, wakidai kuwa taasisi hizo mbili zilipokea tuhuma za unyanyasaji wa kingono dhidi ya daktarihuyo miaka kadhaa ya nyuma.

Taasisi hiyo ya michezo na chuo hicho zimekana kuwa kulikuwa na chochote cha kufichwa.

Hukumu ya Larry Naser inafuatia wiki ya ushuhuda kutoka kwa wanawake takribani mia moja na sitini, wakiwemo washindi wa medali ya dhahabu ya olympiki Biles, Aly Raisman, Gabby Douglas na McKayla Maroney

Arsene Wenger afunguka kuhusu Sanchez


Meneja wa klabu ya Arsenal, Arsene Wenger amesema kwa sasa mambo ya usajili wa Alexis Sanchez yameshapita ndani ya timu hiyo.

Sanchez amekamilisha dili lake la kujiunga na Manchester United huku likimuhusisha Henrikh Mkhitaryan kuhamia Emirates mwanzoni mwa wiki hii.

Kufuatia ushindi dhidi ya Chelsea katika michuano ya Carabao Cup hapo jana siku ya Jumatano Wenger akizungumza na vyombo vya habari juu ya uhamisho wa Sanchez amesema kuwa “Tumepoteza mchezaji bora lakini kama timu kunahaja ya kuendelea nayale muhimu ili kutopoteza muelekeo wetu,” amesema Wenger.

“Kwa sasa tunafahamu tunapaswa kuendelea mbele sote kwa pamoja kujipatia muda.”

Kikosi cha Wenger kimefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya michuano ya Carabao Cup na kutarajiwa kucheza na Manchester City baada ya kuifunga timu ya Chelsea hatua ya nusu fainali.


Mwalimu afikishwa Mahakamani baada ya kumuua mtoto wake kwa panga



 Mwalimu wa sekondari Stephen Wachira Wangara mwenye umri wa miaka 43, amefikishwa Mahakamani kwa kosa la kumuua mtoto wake wa miezi 7 kwa kumchinja na panga nchini Kenya.

 Mashahidi watano wa tukio hilo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama Jimbo la Kirinyaga, Maina Muriuki wamemweleza Jaji Lucy Gitari wa Mahakama Kuu ya Kerugoya, jinsi mtuhumiwa alivyoua mtoto wake,

Maina ameieleza Mahakama kuwa mwili wa mtoto huyo ulikuwa umewekwa ndani ya gunia ukiwa na damu, nje ya nyumba ya Wangara na pembeni ya mwili huo kuliwa na panga ambalo lilitumiwa kumuua mtoto huyo.

Shahidi mwingine Joseph Muriithi amesema wakati wa tukio hilo alikuwa shambani kwa Wangara akifanya kibarua na alimwona mtuhumiwa akiwa na madoa ya damu na muda mfupi baadaye alisikia kelele kutoka kwenye nyumba ya mwalimu huyo.

Mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi March 1, 2018, ambapo itasikilizwa tena.

Wangara ambaye ni mtuhumiwa ni baba mwenye watoto wawili na mwalimu katika shule ya Sekondari ya Gituya

Wanaohusika na uteswaji wa Vijana kukamatwa


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dkt Mwigulu Nchemba ameagiza kutafutwa na kukamatwa mara moja kwa watu wote wanaohusika na uteswaji wa vijana wanaopelekwa nje ya nchi kutafuta ajira.

Dkt. Mwigulu amesema hayo leo wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari baada ya kupata taarifa ya mateso wanayopata baadhi ya wananchi wa Tanzania wanaokwenda kufanya kazi tofauti tofauti nje ya nchi na kusema wameshafanya mawasiliano na Wizara zote zinazohusika na wameshakubaliana kila mmoja kuchukua hatua kulingana na wizara yake.

"Wale watu wanaoweka rehani vijana wetu, wamekuwa wakikimbia hapa na pale na ambao bado hawajakamatwa mpaka sasa waendelee kusakwa wote na wafikishwe katika mkono wa sheria ili sheria iweze kufuata mkondo wake kwa vitendo hivyo vya kinyama na kuwapeleka vijana wetu katika vitendo vya kinyama na kusababisha majonzi kwa familia husika",alisema Dkt. Mwigulu.

Pamoja na hayo na Waziri Nchemba amesema matatizo wanayoyapata vijana hao kwa kisingizio cha kupatiwa kazi nje ya nchi mpaka sasa yamekuwa makubwa mno.

"Tumeona vijana wakiwa wamefungwa miguu vichwa chini na mikono yote huku wakitandikwa viboko kwa madai ya kwamba miongoni mwao kuna aliyewapeleka kuwapa kazi nzuri ya kufanya lakini kwa bahati mbaya wakifika huko wanawekwa rehani kwamba hawataondolewa pale walipo mpaka wale waliowapeleka wakiwa wameshamaliza kupeleka fedha za dawa za kulevya", alisisitiza Waziri Mwigulu Nchemba.

Rais wa Simba Fc alazwa Muhimbili


MWENDESHA Mashtaka Mwandamizi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana Rushwa ,(Takukuru) , Leonard Swai ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa Rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva amelazwa Hospital ya Taifa ya Muhimbili akisumbuliwa na Figo.

Aveva ambaye ni mshtakiwa wa kwanza mshtakiwa mwingine katika kesi ya uhujumu uchumi anashtakiwa pamoja na Makamu rais wa klabu ya Simba, Godfrey Nyange 'Kaburu' ambaye alikuwepo mahakamani hapo

Wakili Swai amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Victoria Nongwa kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Amedai, walishachukua maelezo ya mshtakiwa wa pili na kwamba wanaangalia jinsi ya kupata maelezo ya mshtakiwa wa kwanza ambaye kwa sasa ni mgonjwa.Baada ya kueleza hayo Hakimu Nongwa ameaihirisha kesi hiyo hadi February 8,2018 kwaajili ya kutajwa.

Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi, kuwasilisha nyaraka ya uongo na kutakatisha fedha Dola za kimarekani 300,000.


Mwanafunzi atuhumiwa kwa kumnyonga mpenzi wake Gesti




Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Sokoine (SUA) aliyetambulika kwa jina la Mwita Marwa kwenye miaka (30) anatuhumiwa kufanya mauaji kwa kumnyonga mpaka kufa mpenzi wake Kibua Adam (39) mkoani Morogoro.

Akiongea na www.eatv.tv Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa mpaka sasa jeshi la polisi linaendelea kumtafuta mtuhumiwa.

"Mpaka sasa zipo tetesi tu za hapa na pale hatuwezi kujua sababu kubwa iliyopelekea kijana huyo kufanya jambo hilo, kwani yeye alimchukua huyo mwanamke akampeleka guest na kunyonga huko mpaka akafa" alisema Matei

Kamanda Matei anadai jeshi la polisi walipopata taarifa za kunyongwa mwanamke huyo alifika katika guest hiyo na kuukuta mwili wa mwanamke huyo na kuondoka nao, lakini mpaka sasa mwanafunzi ambaye anatuhumiwa kufanya mauaji hayo hajapatikana na jeshi la polisi linaendelea kumtafuta.

Sugu, mwenzake wamkataa hakimu wakidai hawana imani naye


Mbunge wa Mbeya Mjini 'Sugu' na Katibu wa Chadema Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Emmanuel Masonga wamemkataa Hakimu Mkazi Mfawidhi, Michael Mteite wakidai hawana imani naye katika mwenendo wa kesi hiyo.

Sugu na Masonga wanashtakiwa kwa kosa la kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli wanayodaiwa kuitoa Desemba 30,2017.

Washtakiwa leo Alhamisi Januari 25,2018 asubuhi wamefika katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya kwa ajili ya kuanza kutoa ushahidi baada ya upande wa Jamhuri kukamilisha na kufunga ushahidi wao.

Upande wa Jamhuri umewasilisha mashahidi watano mahakamani na vielelezo viwili ikiwamo sauti iliyorekodiwa.

Baada ya utaratibu wa kimahakama kukamilika ili kuanza ushahidi, wakili Boniface Mwabukusi anayewawakilisha Sugu na Masonga alimuomba hakimu Mteite akisema wateja wake wana jambo la kuieleza Mahakama.

Hakimu alipowaruhusu kuzungumza, Sugu ambaye ni mshtakiwa wa kwanza katika kesi hiyo, amesema kutoka ndani ya nafsi yake ameitafakari kesi na mwenendo wake na kufikia uamuzi wa kumkataa hakimu kwa kuwa hana imani naye kwa sababu tatu.

Amesema, “Naomba niitaarifu Mahakama hii kwamba nimetafakari mwenendo wa kesi hii, mimi mshtakiwa wa kwanza Joseph Mbilinyi naona nikukatae wewe hakimu kutokana na mambo yafuatayo: kwanza; sijawahi kuona hakimu yuko biased (wenye upendeleo) kama ulivyo wewe, ulivyoninyima dhamana bila sababu za kisheria na Katiba.”

“Pili, jana nimeshuhudia kielelezo cha tape recorder kikitokea mikononi mwa wakili wa serikali ambacho wakili wangu (Mwabukusi) alikikana na ukamshambulia sana wakili wangu kwamba wakati anakitoa yeye (wakili) alikuwa ametoka wakati mimi nilikuwa hapa sikuona. Sasa kitendo kile naona wewe hakimu una interest (masilahi) dhidi yangu,” amesema.

Sugu amesema, “Lakini pia jana ulikiri kwamba katika kesi hii unapata mateso, hivyo mimi ni Mkristo, sasa ili nisikupe tabu na mateso naomba nikukatae na apangiwe hakimu mwingine atakayeendesha kesi hii kwa uhuru na haki.”

Amesema kwa sababu hizo anaomba amkatae hakimu huyo.

Baada ya ombi hilo la Sugu, hakimu Mteite alimpa nafasi Masonga ambaye pia alimkataa akitoa msimamo unaofanana na wa Sugu.

Katika sababu zake, Masonga amesema, “Mheshimiwa jana ulipotoa uamuzi wa kupokea vielelezo kutoka kwa upande wa Jamhuri, wa tape recorder na register mheshimiwa hakimu ulieleza Mahakama yako kwamba unaruhusiwa kisheria wakati upande wa Jamhuri ulikubali ushahidi upokewe kama Id (utambulisho) lakini register ipokewe kama  kidhibiti. Lakini bado uamuzi wako ulikuja tofauti na upande wa Jamhuri.”

Amesema, “Ulipofanya uamuzi wakati tulipokuomba dhamana, ulisema unakubaliana na hoja za pande zote mbili (utetezi na Jamhuri). Na Jamhuri walisema kwa ajili ya usalama wetu (washtakiwa), wanaomba tusipewe dhamana. Na wewe katika uamuzi wako umezingatia hoja zao lakini umezingatia zetu kwa sababu ni haki yetu kisheria na kikatiba. Na uamuzi wako ulisema unazuia dhamana kwa sababu unataka kesi hii iendee haraka, bila kujadili hoja zilizoletwa mbele yako.”

Hakimu Mteite amesema amezingatia hoja hizo na atatoa uamuzi baada ya saa moja.

KIVURUGE WA TANDALE -01



SAA saba na dakika zake mchana, tumbo la Ashrafu lilikuwa likiunguruma kwa kusakamwa na njaa kali, aliamua kutoka ofisini kwao ndani ya Jengo la Al- Haramain, Mtaa wa Shaurimoyo jijini Dar na kuamua kushuka kwa kuzikanyaga ngazi moja baada ya nyingine.

Kazi yake ya ufundi wa kompyuta na vifaa vya kielektroniki ilimfanya kuwa kijana maarufu sana na hii ilitokana na uwezo mkubwa aliokuwa nao kwenye kazi yake kiasi cha makampuni mengi kugombea kumwajiri lakini mwenyewe akawa hataki. Kwake aliona ni bora ajiajiri lakini kama kuna kampuni inahitaji huduma yake, inamfuata na wanafikia makubaliano kisha kazi inafanyika.

Baada ya kushuka ngazi kwa tabu hatimaye alijisogeza taratibu hadi mgahawani ambapo palijulikana kwa jina maarufu la Kwa Makofia. Hapo alikutana na umati mkubwa hivyo kushindwa kabisa kuagiza chakula alichokuwa akihitaji hivyo aliamua kuhamia kwenye mgahawa wa jirani yake, kabla hajachukua uamuzi wa kuondoka Kwa Makofia, macho yake yalikutana na kitu kilichomfanya ashtuke kidogo.

Mrembo matata mwenye mvuto wa kipekee, mweupe aliyepanda juu, mwenye macho kama anasikia usingizi, alikuwa amekaa kama anayesubiria huduma! “Dah, huyu ni mtu wa kawaida au ni malaika ameshuka kupunga upepo duniani?” Ashrafu alijikuta akiropoka ingawa ni kwa sauti ndogo na ya chini kabisa na hakuna aliyemsikia hata kwa herufi moja. “Nafanyaje jamani kuhusu huyu msichana mzuri hivi?

Naanzaje kumuacha tena amekaa mwenyewe katika mazingira kama haya? Sasa sijui yuko na mwenzake na ametoka kidogo tu au yuko mwenyewe na mbona leo nimekosa kabisa ujasiri ambao nimekuwa nao kwa siku zote?” Ashrafu alijiwazia moyoni huku akiondoka eneo hilo na kujisogeza kwenye mgahawa wa jirani na hapo. Alifika na kuagiza chakula ambapo alichagua moja ya viti vilivyokuwemo ndani na kukaa huku mawazo yake yakibaki kwa msichana aliyekutana naye pale Kwa Makofia.

Katika hali ya kushangaza, wakati anawaza juu ya mwanamke huyo, alishangaa kumuona msichana yule akiingia mgahawani hapo na kukaa kwenye moja ya viti na kisha kuagiza chakula.

Ni hapo ndipo Ashrafu alishindwa kuvumilia na kuamua kutumia ujasiri wake wa asili ambao humuwezesha kumvaa mtu yeyote kwa wakati wowote na kumwambia chochote kwa mazingira yoyote. “Dada, samahani kidogo,” Ashrafu aliita kwa nidhamu zote na kuonesha heshima ambayo hata yeye mwenyewe aliishangaa imetoka wapi. “Mimi…?” Msichana wa watu aliitika kwa mshangao na macho ya kuuliza kama ni yeye aliyekuwa akiitwa. “Yeah…” Ashrafu aliitikia na kumpa ishara ya mkono msichana yule ambaye alionesha kusita… akatingisha bega lake kuonesha kukataa wito wake. “Samahani nakuomba au ni vibaya kukuita? Kataa neno usikatae wito,” Ashrafu alichombeza.
“Samahani kaka! Samahani lakini, mimi kwa watu ambao siwafahamu siwezi hata kuwasogelea…” alisema yule msichana na kuagiza chakula. Ashrafu alishusha pumzi chini…lile tumbo lake lililokuwa likiunguruma safari hii aliona limezidi mara mbili yake. “Hata mimi nikuombe samahani! Naomba nikae hapo karibu na wewe!” Ashrafu alirusha karata nyingine tena huku akimtolea jicho la aibu. Yule msichana alikubaliana na Ashrafu, ilikuwa furaha kubwa kwake kama siyo ushindi kutokana na mazungumzo ambayo alipanga kuyaendesha kwa muda ambao watakuwa wanasubiri chakula, aliamini kabisa hadi zoezi la kula linamalizika, atakuwa ameshaibuka kidedea. “Siwezi kumkosa huyu mtoto, kwanza anaonekana laini na mwepesi kama maharage ya Mbeya,” Ashrafu aliwaza huku akimtazama usoni msichana yule. “Samahani tena kwa usumbufu…” “Bila samahani kaka…” “Naitwa Ashrafu kwa kirefu, sijui wewe mrembo unaitwa nani?” “Kwa nini unaniita mrembo jamani?” Aliuliza yule msichana huku akijiangalia kiunoni hadi miguuni. “Si kama hivi ulivyo mzuri na mrembo au huoni?” “Aaah, kawaida bwana na huwa sipendi kabisa mtu akiniita mrembo…” “Okey, samahani kwa hilo.”
“Wala usijali. “Unaitwa nani?” “Naitwa Nancy, ni mwenyeji wa Morogoro eneo la Kilombero.” Ashrafu aliendelea kumtolea macho na masikio akiwa haamini kama maneno yale yanatoka kwa yule msichana. “Mi mwenyewe mkazi wa Morogoro!” “Weee! Sehemu gani?” Nancy alishangaa, alionekana kubadilika sura na kuwa ya tabasamu mara baada ya kuambiwa kuwa wanatoka mkoa mmoja kumbe ulikuwa uongo wa Ashrafu ili kumnasa. “Mi natokea Morogoro mjini kabisa eneo moja hivi linaitwa Kihonda, unapajua?”

“Ndiyo, sasa mara nyingi huwa nafikia kwa Shangazi sehemu moja inaitwa Mji Mpya nakaa siku mbili tatu ndiyo naelekea Kilombero.” Wakati wanaendelea na mazungumzo ya kufahamiana, mhudumu alileta vyakula kulingana na maagizo ya kila mmoja wao, ambapo kwa pamoja waliamua kutumia meza moja kula. “Hujaniambia lakini kuhusu kazi yako,” Nancy alianza kuchokoza. “Ah, mi mzugaji tu mjini hapa, nabangaiza ilimradi siku ziende. Nakaa mtaa wa tatu kutoka hapa,” Ashrafu alidanganya kwa mara nyingine hali iliyomfanya Nancy ashtuke. “Mh! Hongera, kama kweli unafanya kazi hizo na unaonekana mtanashati hivyo!”

“Asante sana na wewe je?” “Mimi nafanya kazi katika kampuni ya kuuza vifaa vya solar kutoka China, pale karibu na ‘round about’ alimuelekeza Ashrafu kwa kumnyooshea mkono. “Naishi Mikocheni, niko mwenyewe na maisha yanasonga kwa kweli,” alisema Nancy huku akimtazama Ashrafu kwa macho yaliyojaa aibu za kikekike. Kwa ilivyoonesha, Nancy alikuwa mzungumzaji sana maana ndani ya muda mfupi tu, alishayatawala mazungumzo na mbinu kali alizozitumia Ashrafu, zilimfanya ajikute akimzoea haraka utafikiri wamefahamiana miaka kadhaa iliyopita. Walimaliza kula. Nancy akamwambia alikuwa na safari ya kuelekea Posta kufuatilia hundi ya malipo kwenye kampuni moja waliyofanya nayo biashara.

“Okey, basi nakuomba tubadilishane mawasiliano ili tuendelee kuwa karibu zaidi,” Ashrafu alitupa ndoano kimtego kwa Nancy. “Namba za simu tena? Hapana huwa sitoi namba za simu, utanisamehe kwa hilo,” Nancy alisema huku akiinuka, akachukua mkoba wake mdogo na kuanza kutembea kimadaha, akaenda mpaka kaunta na kulipa bili yake, akamgeukia Ashrafu ambaye bado alikuwa amekaa palepale akiendelea kuusifu uumbaji wa Maulana kwa kiumbe yule. Alimpungia mkono kichokozi huku tabasamu pana likiwa limechanua kwenye uso wake, akatoka zake na kumuacha Ashrafu akiwa bado ameganda palepale kama barafu.


“Ndege mjanja hunasa kwenye tundu bovu,” alijisemea huku tabasamu hafifu likichanua kwenye uso wake, akashusha pumzi ndefu na kuinuka kuelekea kaunta kulipa. Je, nini kitafuata? Usikose kufuatilia kwenye Gazeti la Risasi Mchanganyiko siku ya Jumatano. KUTOKA KWA MWANDISHI: Nimeamua kusitisha simulizi ya Bosi wa Kibamia iliyoanza Jumatano iliyopita kweye Gazeti la Risasi Mchanganyiko, hii ni kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wangu. Poleni kwa usumbufu wasomaji wangu na sasa tuungane kwenye simulizi hii mpya itakayokuacha na funzo kubwa la maisha.

Instrumental | Olamide – Science Student (BEAT) | Mp3 Download

Instrumental | Olamide – Science Student (BEAT) | Mp3 Download

Instrumental | Olamide – Science Student (BEAT) | Mp3 Download

DOWNLOAD INSTRUMENTAL