Simba wanaopanda juu ya miti wamekuwa kivutio cha watalii katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa kuwa ni kitu kipya.
Tabia ya simba imeanza kushangaza watalii na maofisa wanyamapori kwa kuwa si kawaida ya wanyama hao kupanda juu ya miti na kukaa.
Ofisa wa Mamlaka ya Usimamizi Wanyamapori Tanzania (Tawa), Suleiman Keraryo amesema simba wanaopanda miti walizoeleka katika Hifadhi ya Manyara pekee sasa inaonekana inasambaa hivyo kuhitajika utafiti zaidi.
"Hili si jambo la kawaida linaweza kusababishwa na vitu vingi lakini ni geni na kivutio kizuri kwa watalii," amesema leo Jumapili Desemba 17,2017.
Ofisa wanyamapori mkuu na ushirikishwaji jamii kwenye uhifadhi wa Tawa, Seth Ayo amesema hali hiyo si ya kawaida.
Hata hivyo, amesema jambo hilo linaweza kuwa linasababishwa na mabadiliko ya hali ya hewa na ongezeko la joto ardhini.
"Hili ni jambo jipya na linasambaa tumeona simba juu ya miti Grumeti na leo hapa Ngorongoro," amesema.
Idadi kubwa ya watalii walikuwa wakitazama simba katika eneo la Kingo creta ya Ngorongoro ambaye alikuwa amepumzika juu ya mti.
No comments:
Post a Comment