Ili kulima matikiti maji, inakubidi uwe na sehemu ya kutosha, yenye jua la kutosha, maji mengi na ardhi yenye rutuba ya kutosha, matikiti maji hukua haraka kama mimea mimgine ya jamii yake itambaayo mfano Matango, maboga na maskwash.
Kwa mtu ambaye anaanza kilimo yatampa tabu kidogo tofauti na Yule ambaye ana ujuzi kidogo na mambo ya kilimo kwa sababu yanahitaji umakini kiasi.
HALI YA HEWA
Mimea hii haihimili hali ya joto kali sana, mvua nyingi na udongo unaotuamisha maji, magonjwa ya fangasi na wadudu waharibifu, inastawi vizuri kwenye kuanda wa pwani na miinuko kidogo kama DSM,Tanga, Morogoro, Mtwara, lindi na Pwani ambapo kuna jua la kutosha. Muda mzuri wa kupanda ni kipindi cha kipupwe mwezi wa machi mpaka wa septemba .
UPANDAJI
Panda kwa kutumia Mbegu zinazouzwa madukani, ukitumia Mbegu kutoka kwenye tikiti ulilonunua linaweza likawa ni hybrid na matokeo yake matikiti yatakayozaliwa hayatakuwa bora kwa sababu yatakuwa ni kizazi cha pili (F2) Panda Mbegu yako moja kwa moja kwenye shamba, usinunue miche au kupanda Mbegu kwenyemifuko ya plastiki halafu ndi uhamishie shambani, panda Mbegu mbili sentimeta 2 chini ya udongo kwa umbali wa sentimeta 30 kutoka shina hadi shina na mita 2 - 3 kutoka mstari hadi mstari, baada ya siku chache Mbegu zitaanza kuota, baada ya kama wiki 2 katika Mbegu mbili ulizopanda kata moja na uache ule mche wenye afya zaidi, angalizo using’oe mche bali ukate ili kuzuia kusumbua mizizi ya mche uliobaki.
Unaweza kupandishia udongo kwenye mashina na hii itasaidia kupunguza maji yasituame kwenye mimea yako, pia unaweza kuweka samadi badala ya kupandishia udongo ukiwa na nia ileile ya kuzuia maji yasituame na kuongeza rutuba.
Kama una sehemu ndogo ya shamba unaweza kuyawekea matikiti waya wa kutambalia, ila inabidi uwe imara kwa sababu ya kuhimili uzito wa matunda yenye, na wakati wa kuanza kutambaa kwenye waya ni lazima uifundishe mimea kwa kuielekezea kwenye waya na kufungia
MCHE ULIOCHIPUA
UANGALIZI
Miche ikiwa imetambaa kiasi unaweza kuweka matandazo kwenye udongo ili kuzuia upotevu wa unyevu, unaweza kuweka samadi au mbolea za viwandani, mimea ikiwa midogo tumia zaidi mbolea zenye nitrojen na utumie zaidi mbolea za potasiam mara baada ya maua kutokeza hadi matunda kukomaa, matawi yakifikia urefu wa mita 2 kata mbele ilikuruhusu kutoa matawi na hivyo kupata maua mengi zaidi hatimaye mavuno zaidi
MAUA NA MATUNDA
Matikiti hutoa maua dume na jike kwenye tawi moja, maua dume ambayo ni madogo zadi hutoka kwanza yakifuatiwa na maua jike ambayo ni makubwa zaidi, usipoona maua dume na jike kuna tatizo mfano maji kidogo yalimwagiliwa, upungufu wa viritubisho kwenye udongo, hali ya hewa ni joto/baridi sana n.k
Uchavushaji kwenye matikiti hufanyika na wadudu, kama huwaoni wakifanya kazi yao unaweza kufanya mwenyewe, muda mzuri ni wa asubuhi, unakata maua dume kwa kisu na kufanya uchavushaji kwenye maua jike, maua jike ya mwanzo kwenye tawi ndiyo yenye ukuaji bora zaidi, unaweza kukata tawi lisiendelee kukua baada ya matunda kutokeza hii husababisha kuwa na matunda makubwa zaidi
UCHAVUSHAJI KWA MKONO
UVUNAJI MATIKITI
Ili kujua matikiti yamekomaa inahitaji ujuzi kidogo, upande wa chini wa tunda huanza kuwa na rangi ya njano, pia kikonyo juu ya tunda hukauka kabisa na kuwa kijivu, ila njia nzuri ni kuyapiga kwa kiganja na kusikiliza mlio wake kama tunavyofanya kwenye mafenesi, hii nayo ni shule nyingine. Tumia kisu wakati wa kuvuna matikiti, yabebwe na kuhifadhiwa vizuri kwenye makasha tayari kuuzwa au kwa matumizi binafsi
MAGONJWA NA WADUDU
Wadudu wa matikiti wako wanaoshambulia majani na maua, na wengine hushambulia matunda , pia kuna magonjwa ya fangasi ambayo hushambulia mimea, ili kujua dawa za magonjwa ni vizuri kuchukua sampuli na kwenda nayo kwenye duka la dawa na pembejeo za kilimo ili kjupata dawa sahii, dawa aina ya KARATE itasaidia kuua wadudu wa majani, maua na matunda na FUNGICIDE itasaidia kwa mashambulizi ya fangasi.
No comments:
Post a Comment