Msanii wa kiume wa bongo fleva Ben Pol, amewataka wasanii wenzake kuacha uvivu na kufanya kazi kwa bidii, kwani licha ya sanaa kuwahitaji, pia wana majukumu ya kutimiza.
Akizungumza kwenye Planet Bongo ya East Africa Radio, Ben Pol amesema wao kama wasanii wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii, kwani kuna watu wanawategemea, ikiwemo familia zao na mashabiki wao.
“Niwaambie wasanii wenzangu tuache uvivu hii ni kazi yetu, familia zinatutegemea, tuna-teams ambazo zinaishi kupitia sisi, tuna mashabiki wanatuangalia, turudi studio turudi studio tutoe albam, kama kuna changamoto tutakabiliana nazo mbele kwa mbele”, amesema Ben Pol.
Ben Pol hakuishia hapo aliendelea kwa kuitaka serikali kuhakikisha wanasimamia ipasavyo kazi zao za sanaa, kwani na wao tayari wameshaanza kuchangia pato la serikali kwa kukatwa kodi.
“Tushaanza kulipwa kodi, kwenye shows tunakatwa, mtu anakuja pale mlangoni na mashine, kwa hiyo na wao serikali watusaidie kwenye biashara yetu”, amesema Ben Pol.
Ifahamike kwamba Ben Pol ni miongoni mwa wasanii wachache ambao mwaka huu wameachia albam, kitendo ambacho wasanii wengi wanakiogopa.
No comments:
Post a Comment